Hekaya Za Bahlul Mwenye Busara

Author(s): 

Katika kuona haja ya kupata nasiha na mawaidha nimeonelea vyema kutumia mbinu hii ya kuchapa nasiha na mawaidha katika sura ya hekaya za Bahlul. Kwani maisha yake yanatuchekesha na kutu furahisha papo hapo tunapata mafundisho ndani mwake. Vile vile nimekikusanya na kukitarjumu kitabu kimoja chenye masimulizi na hadithi zilizopo katika Qur’an Tukufu. Hivyo ni matumaini yangu kuwa vitabu hivi na vingine vitatusaidia sisi sote katika kulenga maisha yetu vile ipasavypo.

Category: 
Topic Tags: 
Person Tags: 

Hekaya Za Bahlul Mwenye Busara

Katika kuona haja ya kupata nasiha na mawaidha nimeonelea vyema kutumia mbinu hii ya kuchapa nasiha na mawaidha katika sura ya hekaya za Bahlul. Kwani maisha yake yanatuchekesha na kutu furahisha papo hapo tunapata mafundisho ndani mwake. Vile vile nimekikusanya na kukitarjumu kitabu kimoja chenye masimulizi na hadithi zilizopo katika Qur’an Tukufu. Hivyo ni matumaini yangu kuwa vitabu hivi na vingine vitatusaidia sisi sote katika kulenga maisha yetu vile ipasavypo.

Topic Tags: 
Hekaya
Khalifa
Historia

Katika Kumtaarufisha Bahlul

BAHLUL ni kumaanisha kwa ujumla wa kucheka,uwema na pendeza.

Majibu haya yanaweza kuwa mafunzo kwa watu wa kila aina hadi katika zama zetu na mbeleni.

Watu wengi waliweza kutokezea kwa jina hilo, lakini mashuhuri ni lile la Bahlul aliyekuwapo katika zama za Harun al-Rashid. Bahlul alikuwa ni mmoja wa wanafunzi bora wa Imam Jaafer as-Sadiq a.s. na vile vile alikuwa mpenzi wa Ahli-Bayt a.s. ya Mtume s.a.w.w.

Vile vile inasemekana kuwa Bahlul alikuwa na undugu wa Harun Rashid kwa upande wa mama yake na riwaya nyingine imesemwa kuwa alikuwa jamaa wa karibu wa Harun.

Qadhi Nurallah Shushtary anasema katika kitabu chake Majalis al-Muuminin Bahlul alikuwa ni mtu mwenye akili mno ambaye kwa sababu fulani fulani alijegeuza mwendawazimu.

Bahlul alizaliwa Kufa na jina lake la asili lilikuwa Wahab bin Umru. Kwa mujibu wa riwaya moja, Harun Rashid alimwona Imam Musa bin Jaafer a.s. kama tishio kubwa kwa kubakia utawala wake. Hivyo alijishughulisha katika mbinu za kutaka kumwua. Na aliweza kutafuta hila moja ya kumwua. Hivyo alimzulia dai la kuasi na hivyo aliwataka hukumu wacha Mungu ya kumwua Imam, ambamo Bahlul pia alikuwamo. Wote walitoa fatwa ya kuuawa kwa Imam a.s. lakini Bahlul aliipinga. Bahlul alimwendea Imam a.s. na kumjulisha yale yaliyokuwa yakitokea, na alimwambia Imam a.s. ampatie ushauri na njia za kuyakabili hayo. Imam a.s. alimwambia kuwa ajigeuze na awe mwenda wazimu.

Hii ndiyo sababu ya yeye kuwa mwenda wazimu kwa matakwa ya Imam a.s. na hivyo aliweza kuepukana na adhabu na maangamizi ya Harun Rashid, aliyekuwa Khalifa wakati huo. Na hivyo bila ya woga wowote akijifanya mwenda wazimu, aliweza kukabili, kumsuta hata Khalifa na mawaziri wake na papo hapo aliwatetea wanyonge na wale wote waliokuwa wamedhulumiwa. Pamoja na hali yake hiyo, watu walimpenda kwa mioyo yao, hadi leo hekaya zake zinasimuliwa katika vikao na kujifunza mengi kutokana hayo.

Kwa mujibu wa riwaya ya pili - ambayo inasadikiwa zaidi. Masahaba na wapenzi wa Imam a.s. walikuwa wametingwa na udhalimu wa Khalifa na watawala wake. Hivyo wote walimwomba Imam a.s. uongozi kuhusu swala hilo. Imam a.s. aliwajibu kila mmoja kwa herufi moja tu. "Jim" kwa hivyo walielewa kuwa hapakuwapo na haja ya kuulizia ziada.

Kila mmoja alielewa hilo herufi tofauti tofauti. Mmoja alielewa "Jila Watan" yaani kutoka nyumbani, mwingine alielewa 'Jabl yaani 'Mlimani' na Bahlul alielewa kuwa ikimaanisha 'Junuun' Yaani "Uenda wazimu" na hivyo alijigeuza hivyo na kwa hayo, wote waliweza kunusurika na janga hilo la kuteketezwa na udhalimu wa Khalifa.

Bahlul alikuwa akiishi maisha ya starehe na bora kabisa lakini baada ya ishara hiyo ya Imam a.s. aligeuzia uso dunia na kuziacha starehe zote hivyo akaishi maisha ya utawa na akawa na mavazi yaliyokuwa yamechakaa. Yeye alipendelea kuishi uwanjani kuliko majumba ya Wafalme, vile vile aliishi kwa kipande kikavu cha mkate kuliko kutegemea misaada ya hisani ya Khalifa kwani alikuwa akijiona yu bora kuliko Khalifa Harun Rashid, mawaziri wake na Baraza lake zima.

Bahlul kwa hakika, alikuwa mcha Mungu na mpenzi wake, mwenye akili sawa na Aslim kamili. Yeye alikuwa ni mtu mwenye akili sana na fahamu zaidi na mwenye kutoa majibu ya papo hapo na mtatuzi wa masuala katika zama zake. Jina lake halikuwa mashuhuri tu miongoni mwa watu wenye akili tu bali kwa amri ya Imam a.s. alijifanya mwenda wazimu na hivyo aliweza Din na Sharia na kuelezea uhakika na ukweli wa Ahli Bayt a.s.

Katika zama hizo hapakuwapo na njia nyyingine ila yeye kujifanya mwenda wazimu amasivyo Harun Rashid angalimwua. Kama vile Harun Rashid alisikiliza uthibitisho wa Uimam Musa ibn Jaafer a.s. kutoka mwanafunzi mmoja wa Imam Jaafer as-Sadiq a.s. Hisham bin Hikam, na akamwambia Waziri wake Yahya ibn Khalid Barki: "Ewe Yahya! Maneno ya mtu huyu, Hisham, kwangu mimi ni sawa na tishio la mapanga laki moja, lakini jambo la kushangaza ni kule kubainika kwake hai wakati mimi natawala!"

Harun alibuni kila aina ya mbinu za kutaka kumwua Hisham. Na alipopata habari hizo, alitorokea Kufa ambako aliishi nyumbani (mafichoni) mwa rafiki yake, na katika kipindi kifupi alifariki.

(1). Bahlul Na Chakula Cha Khalifa

Siku moja Harun al-Rashid alimpelekea Bahlul sinia iliyojaa kwa vyakula mbalimbali. Mfanyakazi alipomwakilishia Bahlul vyakula hivyo, alimwambia: "Hivi ni vyakula makhususi vya Khalifa na amekutumia wewe uvile."

Bahlul alimtupia mbwa aliyekuwa ameketi karibu, vyakula vyote alivyoletewa.

Alipoyaona hayo, mfanyakazi wa Harun al-Rashid alighadhabika mno na kusema kuwa hiyo ilikuwa ni kumvunjia heshima Khalifa na angalimjulisha hivyo.

Hapo Bahlul alimjibu: "Ewe kaa kimya! Iwapo na mbwa atafahamu kuwa vyakula hivyo vinatoka kwa Khalifa, naye pia ataacha kuvila!

Fundisho: Inatupasa kukatalia zawadi kutoka kwa waonevu na wadhalimu ili visituathiri sisi kutotimiza wajibu wetu wa ukweli na haki.

(2). Bahlul Kukalia Kiti Cha Khalifa

Siku moja Bahlul aliingia katika Qasri ya Khalifa na kukuta kiti chake tupu aliona hakuna mtu wa kumzuia, hivyo alikwenda moja kwa moja akaketi juu ya kiti cha Khalifa.

Walipotokezea maaskari wa Khalifa, walijaribu kumwondoa Bahlul, lakini alikataa, hivyo waliweza kumwondoa kwa kumpiga. Hapo Bahlul alianza kulia kwa sauti, na alipotokea Harun Rashid alimwona Bahlul akilia kwa sauti na aliwauliza maaskari wake sababu. Wao walimwelezea yote yaliyotokea. Hapo Khalifa aliwakemea maaskari hao na kumpa pole Bahlul.

Kwa hayo, Bahlul alisema: "Mimi sikililii kile kilichonipata, bali ninakulilia wewe Khalifa, kwani mimi nimeteswa kwa kuketi punde tu, je wewe utateswaje kwa kukikalia kiti hiki kwa miaka yote hiyo kwani kiti hiki cha Ukhalifa ni kwa ajili ya watu wengine na wewe umewadhulumu hao, na kukikalia kwa mabavu!"

(3). Bahlul Na Mfanya Biashara

Siku moja mfanya biashara wa Baghdad alimwendea Bahlul kwa kutaka ushauri wake. Alimwambia:
"Ewe Sheikh Bahlul! Naomba ushauri wako katika ununuzi wa bidhaa ambazo zitanipatia faida nyingi."

Bahlul alimjibu:
"Chuma na Pamba" (mapokezi mengine yanataja tende na pamba).”

Mfanyabiashara huyo aliyafuata mashauri hayo, na akapata faida kubwa sana katika kipindi kifupi. Ikatokea tena kukutana na Bahlul. Hapo alirudia ushauri wake kwa kusema:
“Ewe Bahlul Mwehu! Je ninunue bidhaa zipi ili nipate faida nyingi?"

Safari hii Bahlul alimjibu:
“Vitunguu na matiki maji."

Hapo mfanya biashara huyo alitumia fedha zake zote kwa kununulia bidhaa hizo akitarajia kupata faida zaidi. Baada ya kupita siku chache, bidhaa hizo zikaanza kuoza na hivyo kusababisha hasara kubwa mno. Hapo alitoka kumtafuta Bahlul na alipomwona alimwambia "Nilipokutaka ushauri mara ya kwanza ulinishauri kununua chuma na pamba (tende na pamba) kwa hiyo nilifaidika mno lakini mara ya pili, umenishauri kununua vitunguu na matiki maji, maboga yote yameoza kwa hivyo nimefilisika kabisa........."

Bahlul alimkatiza na kumwambia
"Mara ya kwanza wewe uliniita "Ewe Sheikh Bahlul!" na kwa kuwa uliniamini mimi ni mtu mwenye akili hivyo nilikupatia mashauri ya akili. Na kwa kuwa mara ya pili uliniita 'Ewe Bahlul mwehu' na kwa kuwa uliamini mimi ni mwehu, basi nilikujibu kiwehu.....!.

Hapo mfanya biashara alibung'aa kwa majibu hayo na alielewa maana na kujiondokea kimya kimya.

Fundisho: Islam inasisitiza ushauri kama alivyosema Mtume s.a.w.w.:- "Ushauri ni kinga dhidi ya tubu na usalama wa kutolaumiwa na watu...... na Atakaye ushauri husaidiwa......"

(4). Bahlul Amshauri Harun:

Siku moja Bahlul alimtembelea Harun al-Rashid, na aliombwa atoe nasiha.

Hapo Bahlul alianza:
"Ewe Harun! Iwapo wewe utakuwapo porini ukashikwa na kiu ya maji ambayo hayapatikani, huku ukikaribia kufa. Je utalipa kiasi gani kwa kiasi cha kikombe kimoja cha maji?"

"Sarafu za dhahabu (Dinar)!" alijibu Harun.

"Iwapo mwenye maji asiporidhia sarafu hizo, je utampa nini badala yake?" aliendelea kusema Bahlul.

"Nitampatia nusu ya dola yangu" alikatiza Harun kwa haraka.

"Naam, baada ya kumalizia kiu chako, ukashindwa kupata mkojo (ukaziba) nawe usiweze kujitibu, je utampa nini yule atakaye kutibu huo ugonjwa?" Alisema Bahlul.

"Nitampatia sehemu ya nusu ya dola yangu iliyobakia"Harun akanena katika hali ya bumbuwazi.

Basi hapo kwa kupumua, Bahlul alisema: "Ewe Harun! Usijivunie Ukhalifa wako ambao unajua uthamini wake ni sawa na kikombe cha maji na uponyaji wa ugonwa wako. Hivyo, ni kheri yako iwapo utawatendea watu wako kwa upole na haki!"

(5). Bahlul Na Faqihi

Faqihi mashuhuri kutoka Khurasan alifika Baghdad, alialikwa na Harun Rashid katika Baraza lake na akimkalisha ubavuni mwake.

Wakati alipokuwa akizungumza na Harun, alitokezea Bahlul ambaye naye alikaribishwa aketi karibu nao. Huyo mtu alimwona Bahlul yu kama mwehu na hivyo alimwambia Harun: "Nimestaajabishwa na heshima na mapenzi yako Khalifa, kwa kuwa unawastahi hata watu waliwehuka hadi kuwakaribisha karibu nawe?"

Alipoyasikia hayo Bahlul, alielewa kuwa alikuwa akisemwa yeye tu na hapo akajikaza akamwambia: "Kwa nini waringia ilimu yako hiyo kidogo, usinidharau kwa udhahiri wangu bali jitayarishe kwa mabishano ili nami nimdhihirishie Khalifa kuwa wewe haujui lolote!"

"Mimi nimesikia kuwa wewe u - mwehu na hivyo siwezi kubishana na wehu!" Aliyasema huyo Faqihi.

Hapo Bahlul alimjibu akiwa ameghadhabika, "Mimi ninaukubalia uwehu wangu lakini wewe unakataa kuukubalia ujahili wako na kutokuwa na ilimu kamili."

Harun alipoyasikia hayo, alijaribu kumtuliza Bahlul, lakini ilishindikana huku akidai kuingia mabishano na huyo Faqihi, iwapo anajiamini kwa ilimu kamili."

Basi Harun alimgeukia huyo Faqihi na kumwambia: "Je kuna kipingamizi gani katika kumwuuliza maswali?"

Hapo huyo Faqihi alijibu: "Mimi nipo tayari kubishana naye iwapo atakubaliana na shuruti langu moja nalo ni, iwapo ataweza kunijibu basi nitampa Dinar elfu moja za dhahabu na akishindwa itambidi anilipe hivyo."

Bahlul alimjibu: "Kwa kweli mimi huwa sina mali za kidunia na wala sina Dinar wala dhahabu, lakini nipo tayari kuwa mtumwa wake iwapo nitashindwa kumjibu, na iwapo nitamjibu basi nipatiwe hizo Dinar elfu moja za dhahabu ambazo nitazigawa miongoni mwa mafukara."

Kwa hayo, huyo mtu alianza kumuuliza swali hivi: "Katika nyumba moja yupo mwanamke aliyeketi na mume wake halali kisheria na humo humo wapo watu wawili ambao mmoja wao anasali na mwingine yupo katika hali ya saumu. Ghafla anatokezea mtu kutokea nje na kuingia ndani ya nyumba hiyo. Kutokezea huku kwa mtu huyo, wale bibi na bwana wanakuwa haramu baina yao na sala na saumu za wale wawili zinakuwa batili. Je unaweza kuniambia huyo mtu aliyotokezea ni nani?"

Bahlul bila ya kusita anamjibu: "Huyo mtu aliyeingia nyumbani kwa ghafla alikuwa ndiye bwana wa kwanza wa yule bibi kwani alikwenda safari na baada ya muda mrefu kupita, ilijulikana kuwa amefariki na hivyo huyo mwanamke akaolewa na bwana wa pili (aliyekuwa nyumbani) baada ya kupokea idhini ya hakimu sharia. Wale watu wawili walikuwa wamelipwa kwa ajili ya kusali na kufunga saumu zilizo za qadhaa za bwana wake aliyesadikiwa amekufa safarini.

Na kurejea kwake kutoka safari ndefu aliyosadikiwa amekufa, imebatilisha ndoa ya mke wake na yule bwana kwani yu hai bado, vile vile saumu na sala pia zinabatilika kwani kumsalia mtu aliye hai pia ni batili."

Kwa hayo, Harun na wanabaraza wake wote walivutiwa na majibu ya Bahlul na walimsifu sana.

Baada ya hapo, ilikuwa ni zamu ya Bahlul kuuliza swali: "Je niulize?" " Uliza tu!" alijibiwa.

Bahlul aliuliza: "Iwapo ninayo kasiki moja ya siki (vinegar) na nyingine ya urojo wa sukari, na kwa ajili ya kutengeneza Sikanjabin (kinywaji cha Siki) nimeweka ili kuchanganya katika kasiki ya tatu na hapo tunakuja kumkuta panya amefia humo. Je unaweza kutuambia kuwa huyo panya alitokea kasiki ya Siki au Urojo wa Sukari?

Hapo huyo mtu alijaribu kwa uwezo wake wote kumjibu Bahlul, lakini alishindwa.

Kwa kuona hali hiyo, Harun alimwambia Bahlul "sasa wewe mwenyewe tujibu hayo."

Bahlul alimwambia Harun: "Nitafanya hivyo iwapo huyu mtu atakiri kutoelewa majibu yake."

Kwa masikitiko na aibu kubwa huyo Faqihi alikubali kushindwa kwake kwa kuling'amua hilo fumbo.

Alianza Bahlul kulijibu: "itabidi sisi kumtoa huyo panya na kumwosha vizuri kwa maji safi halafu tupasue tumbo lake na humo iwapo tutakuta siki au urojo wa sukari, basi itatubidi tumwage kile kitakachothibitika kuwamo tumboni mwake."

Wote waliokuwa wamehudhuria, walifurahishwa mno na majibu ya Bahlul na Faqihi alilazimika kutoa Dinar elfu moja za dhahabu ambazo Bahlul alizigawa miongoni mwa mafuqara wa Baghdad.

(6). Bahlul Na Mtumwa Aliyeogopa Maji

Mfanya biashara mmoja alikuwa akisafiri katika jahazi pamoja na mtumwa wake kuelekea Basrah. Kwa bahati na Bahlul alikuwamo humo pamoja na watu wengineo. Mtumwa huyo alianza kulia palipotokea machafuko hapo majini. Wasafiri wote walikerwa na sauti za kilio cha mtumwa huyo. Hapo Bahlul alimwomba ruhusa mfanyabiashara huyo ili atumie mbinu za kuweza kumkomesha mtumwa huyo, basi bila ya pingamizi alipewa ruhusa. Na hapo Bahlul alitoa amri ya kutupwa majini kwa utumwa na ilitekelezwa hivyo. Alipofikia wakati wa kutaka kufa, alitolewa nje. Baada ya kutolewa nje, mtumwa huyo aliketi kimya akitulia katika kona moja ya jahazi.

Hapo baadaye, Bahlul alielezea: "Huyu mtumwa alikuwa haelewi raha na usalama wa jahazi inapokuwa majini. Pale alipotupwa majini ndipo alipotambua kuwa jahazi ni mahala pa raha na usalama."

Fundisho: Amesema mtume s.a.w.w.: "Safirini na mutajitajirisha (kwa uzoefu na uelewano)."

(7). Swali Kutoka Harun.

Siku moja Harun alikuwa katika Qasri yake akiangalia mandhari iliyokuwa ikimzunguka na sauti ya mbubujiko wa maji ya mto Tegris. Na mara hapo akatokezea Bahlul, na Harun alimwambia Bahlul: "Ewe Bahlul! leo hii nakuuliza fumbo, iwapo utafumbua vyema basi nitakupa dinar elfu moja na iwapo utashindwa basi nitatoa amri ya kukutosa majini."

Bahlul alimwambia Harun: "Mimi sihitaji dinar hizo, bali ninakubali kwa sharti moja."
Na alipokubali Harun, Bahlul alisema: "Iwapo nitaweza kulijibu vyema basi itakubidi kuwaachia marafiki zangu mia moja - kutoka Gereza lako, na iwapo nitashindwa basi unao uhuru wa kunitupa majini."

Alianza Harun kulielezea fumbo lake: "Iwapo mimi ninayo mbuzi mmoja, mbwamwitu, na fungu la majani.Je nitawezaje kuvivusha vyote hivyo, kwamba majani hayataliwa na mbuzi na wala mbuzi kuvamiwa na mbwamwitu?"

Bahlul alianza kumjibu: "Kwanza utamvusha mbuzi kwenda ng'ambo ukimwacha mbwa mwitu na majani. Baadaye utachukuwa majani uyavushe huku ukirudi na mbuzi upande huu. Utamwacha mbuzi upande huu na utamchukua mbwamwitu ng'ambo.Mwishoni utampeleka mbuzi. Kwa hivi majani hayataliwa na mbuzi wala mbuzi kuvamiwa na mbwamwitu."

Harun alifurahishwa mno kwa majibu ya Bahlul. Na hapo Bahlul alimpa orodha ya majini mia moja ya wafuasi na wapenzi wa Ali bin Abi Talib (a.s. ). Lakini Harun alimgeuka Bahlul. Lakini Bahlul aliendelea kusisitiza, na hatimaye aliwaacha huru watu kumi tu na akimwamwuru Bahlul kuondoka.

(8). Bahlul Auza Pepo

Siku moja Bahlul alikuwa ukingoni mwa mto akicheza kwa udongo kwa kutengeneza nyumba na bustani. Hapo alitokea Zubeidah, mke wake Harun, akipita hapo. Alipomkaribia Bahlul, alimwuliza: "Ewe Bahlul! Je wafanya nini?"

Bahlul alimjibu: "Najenga Pepo (Jannat) ."
Zubeidah alimwambia: "Je wauza hizi Pepo ulizozijenga?"
Bahlul alimjibu: "Naam ninaziuza!"
Zubeidah alimwuliza: "Je kwa Dinar ngapi?"
Bahlul alimjibu "Kwa Dinar mia moja tu!"

Kwa kuwa Zubeidah alikuwa akitaka kumsaidia Bahlul, hivyo aliona hapo ndipo pahala pa kumsaidia na alimwamuru mfanyakazi wake amlipe Bahlul hizo fedha. Nao walimlipa hizo dinar mia moja.

Usiku ule Zubeidah aliota ndoto akiwa Peponi ambamo kuna Qasri nzuri mno iliyopambwa mno na wapo wajakazi wamesubiri amri, wao walimwambia hiyo ndiyo Qasri aliyoinunua kutoka kwa Bahlul.

Zubeidah alipoamka siku ya pili, akiwa amejawa na furaha, alimwelezea mume wake, Harun. Harun alimwita Bahlul, alipofika, Harun alimwambia, "Ewe Bahlul, chukua hizi Dinar mia moja na uniuzie Pepo mojawapo ya Pepo kama ile uliyomwuzia Zubeidah."

Bahlul alicheka na kumwambia:
"Zubeidah alinunua bila ya kuona ambapo wewe unataka kununua baada ya kujua ya kuwapo kwake. Hivyo sitakuuzia!"

(9). Harun Rashid Amkasirikia Bahlul

Harun alimwajiri jasusi makhususi kwa ajili ya kuchunguza na kuripoti kwake juu ya imani na akida sahihi za Bahlul. Baada ya siku chache huyo jasusi alikamilisha uchunguzi wake na kuripoti kwa Khalifa kuwa Bahlul alikuwa ni mpenzi wa Ahl-al-Bayt ya mtume (s.a.w.w.) na alikuwa mfuasi wa Imam Musa al-Kadhim (a.s.).

Harun alimwita Bahlul na kumwambia: "Ewe Bahlul! Mimi nimepata habari za kuaminika kuwa wewe ni mmojawapo wa wapenzi na wafuasi wakubwa wa Musa ibn Jaafar na hivyo unafanya kila jitihada za kudhihirisha na hivyo umejidhihirisha u - mwehu ambapo sivyo ulivyo!"

Bahlul alimjibu: "Iwapo hivyo ndivyo ilivyo, je utanifanya nini?"

Kwa majibu hayo, Harun alighadhibika mno na kumwamuru Masrur, mfanyakazi wake, amvue nguo Bahlul akalishwe juu ya punda na kuzungushwa mjini na hatimaye kukatwa kichwa mbele yake Harun.

Masrur, alitekeleza vile alivyoamrishwa na hatimaye kumleta mbele ya Harun katika hali hiyo ili aweze kuuawa.

Mara, hapo akatokezea Jaafer Barmaki ambaye kwa kuiona hali hiyo ya Bahlul alimwuliza sababu ya hali yake hiyo:
"Ewe Bahlul! Je umetenda kosa gani?"
Bahlul alimjibu: "Kwa kuwa mimi nimesema ukweli, kwa hivyo Khalifa akanizawadia mavazi yenye thamani."

Harun Rashid, Jaafar, na wote waliokuwepo walichekeshwa mno kwa majibu ya Bahlul, na papo hapo Harun alimsamehe Bahlul na kutoa amri ya kufunguliwa na apewe mavazi mapya na mazuri.

Lakini Bahlul hakukubali hayo bali yeye alichukua kifurushi cha nguo zake kuukuu na kuondoka.

(10). Bahlul Na Harun Kwenda Kuoga Pamoja

Ilitokea siku moja Bahlul na Harun Rashid kukutana katika Hammam (majumba ya kuogea).

Khalifa alimfanyia mzaha kumwuliza Bahlul:
"Je iwapo ningalikuwa mtumwa, ningalikuwa na thamani gani?"

Bahlul alimjibu:
"Dinar hamsini."

Harun Rashid katika kughadhabika alisema:
"Ewe Mwehu! itawezekanaje hivyo? Mavazi yangu tu yamezidi thamani hiyo!”

Hapo Bahlul alimwambia:
"Kwa hakika mimi nimesema kuwa hiyo ni thamani ya nguo zako tu ama Khalifa hana thamani yoyote!"

(11). Mabishano Pamoja Na Abu Hanifa

Abu Hanifa alikuwa akiwafundisha wafuasi wake na Bahlul alikuwa ameketi katika kona moja akisikiliza masomo hayo, baina ya mafunzo, Abu Hanifa alisema kuwa yeye hakukubaliana na mambo matatu yaliyoelezwa na Imam Jaafer Sadiq (a.s.), nayo ni:

Kwanza: Imam Jaafer Sadiq a.s. amesema kuwa sheitani ataadhibiwa katika Jahannam (motoni). Kwa kuwa sheitani ameumbwa kwa moto sasa moto utamuumizaje moto huo?

Pili: Yeye amesema kwa sisi hatutaweza kumwona Allah s.w.t. ambapo twajua kuwa kile kilichopo ni lazima kionekane. Hivyo Allah anaweza kuonwa kwa macho.

Tatu: Yeye amesema kila mtenda tendo ndiyo mhusika mwenyewe atawajibika kujibu kwani ametenda mwenyewe. Ambapo sisi (wakina Abu Hanifa) twaamini kuwa kila kitendo kitatokana na Allah na wala mtu hawajibiki.

Abu Hanifa alipoyamaliza kuyasema hayo, Bahlul alichukua rundo moja la udongo na kumlenga Abu Hanifa. Alipoutupa, ulimpiga Abu Hanifa juu ya uso wake, ulileta maumivu makubwa mno. Na hapo ndipo Bahlul alipotimua mbio, lakini wanafunzi wa Abu Hanifa waliweza kumshika Bahlul. Kwa kuwa Bahlul alikuwa akipatana mno na Khalifa, alipelekwa mbele yake, ambapo Khalifa alielezwa hali yote.

Bahlul alisema:
"Aletwe Abu Hanifa ili niweze kumjibu!"

Alipoitwa Abu Hanifa, Bahlul alimuuliza,
"Je, dhambi gani nililokufanyia?

Abu Hanifa alisema:
"Kichwa changu chaumwa sana kwa sababu ya wewe kunipiga rundo la udongo."

Bahlul alimjibu:
"Je waweza kunionyesha maumivu hayo?"

Hapo Abu Hanifa alimwambia:
"Je na maumivu pia yanaweza kuonyeswa?"

Basi Bahlul alianza kumjibu kwa busara: "Wewe mwenyewe umedai kwa kila kitu kilichopo lazima kionekane na umekuwa ukimpinga tena Imam Jaafer Sadiq (a.s.) na vile vile unadai kuwa itawezekanaje kwa Allah kuwapo na asiweze kuonekana?

"Pili madai yako hayafai, kwani inatahidi kuwa kitu cha jinsi moja hakiwezi kukiumiza kitu cha jinsi hiyo (sheitani hana dhambi wala kuchomwa moto) kwani wewe umeumbwa kwa udongo na udongo niliokupiga ni vitu vya jinsi moja."

Tatu, kila tendo linalotokana na Allah, hivyo kwanini wewe unilaumu na kunishtaki mbele ya Khalifa na kudai kisasi kwani umwalumu Allah aliyenisababisha mimi kukupiga ?"

Kwa hayo, Abu Hanifa aliaibika na hakuwa na chaguo lolote isipokuwa kuondoka hapo.

(12). Bahlul Na Waziri

Siku moja Waziri mmoja wa Harun alimwambia Bahlul, "Ewe Bahlul, Khalifa amefanya wewe uwe mtawala na Hakimu wa ufalme wa mbwa, kuku na nguruwe wote."

Bahlul alimjibu: "Basi kuanzia hivi sasa, wewe hauna budi kuzitii amri zangu kwani wewe pia upo miongoni mwa raia wangu."

Wote waliokuwa pamoja na Waziri walicheka mno na kulimfanya aondoke kimya kwa kuaibishwa.

(13). Bahlul Amsihi Abdulla Mubarak

Siku moja Abdulla Mubarak alimwendea Bahlul kwa kutaka nasiha. Alipomfikia Bahlul, alimkuta kichwa wazi na miguu wazi akisema Allah! Allah..... Alimwendea na kumtolea salaam na Bahlul alimjibu.

Baadaye Abdulla alisema: "Ewe Sheikh! Naomba unipatie nasiha na naomba unionyeshe njia itakayonionyesha vile niishi maisha yangu pasi na madhambi kwani mimi ni mtu mwenye madhambi ambayo nafsi yangu potofu imenighalibu.Hivyo nionyeshe njia hiyo mwokovu."

Bahlul alimwambia Abdullah: "Mimi mwenyewe nimehangaika mno, sasa wawezaje kunitegemea? Iwapo ningelikuwa mwenye akili, basi watu wasingaliniita mwehu na wewe watambua kuwa maneno ya mwehu hayana athari yoyote yakuweza kukubaliwa na watu. Kwa hivyo, nakuomba umtafute mtu ambaye ni mwenye akili ili akushauri vyema."

Abdullah akasema: "Ewe Sheikh mara nyingi wehu wanatokezea kusema mengi yenye busara."

Kwa hayo Bahlul alinyamaza. Hapo tena Abdullah akaanza kumwomba kwa kumbembeleza. "Ewe Sheikh, tafadhali sana usinivunje moyo kwani nimekuja kwa matumaini makubwa."

Bahlul alimjibu: "Ewe Abdullah! Tafadhali sana kwanza kabisa kubali sharti zangu nne ili usiyageukie maneno ya mwehu, ndipo hapo nitakupa nasiha zangu ambazo zitakuokoa.

Abdullah akasema: "Je masharti hayo manne ni yapi ili niweze kuyakubali."

Bahlul akasema: "Sharti la kwanza ni lile, iwapo utatenda dhambi lolote lile, na kupinga hukumu ya Allah, basi uache kula riziki itokayo kwa Allah."

Abdullah akamwambia: "Nisipokula riziki ya Allah, je nitakula riziki ya nani?

Bahlul akasema: "Wewe ukiwa mtu mwenye akili umedai kuwa unafanya ibada ya Allah na kula riziki yake Allah na pepo hapo unafanya maasi ya kutozitii amri zake. Tafadhali sana jaribu kuamua mwenyewe iwapo hii ndio haki ya ibada?"

Abdallah akasema: "Ewe Sheikh wewe umesema kweli na yaliyo sahihi na sharti la pili ni ipi?"

Bahlul akasema: Sharti la pili ni kwamba, unapotenda dhambi lolote, basi jitoe katika milki ya Allah."

Abdullah akasema: "Ama kusema ukweli sharti hili la pili ni gumu kuliko hata lile la kwanza, kwani kila mahala pana ardhi ya Allah na utawala wake, sasa nitakwenda wapi?"

Bahlul alimwambia: "Kwa kweli hili ni jambo baya mno kwani wewe unakula riziki yake na kuishi katika milki yake na papo hapo unakana kutii kwa amri yake. Fanya maamuzi yako wewe mwenyewe kuwa hiyo ndiyo sharti ya ibada?"

Hapo Abdullah aliuliza: "Je sharti la tatu ni lipi?"
Bahlul alijibu: "Sharti la tatu ni kwamba iwapo wewe wataka kutenda madhambi yoyote, basi uende ujifiche mahala pale ambapo Allah hataweza kukuona, wala kuona hali yako, na hapo ndipo utende vile upendavyo."

"Sharti hilo ni gumu zaidi!" alisema Abdullah, kwani Allah anafahamu na kuona kila kitu, yupo kila mahala. Chochote kile akitendacho mja, Allah hukiona na kukielewa."

Bahlul alisema: "Wewe mwenyewe u - mtu mwenye akili. Inakubidi wewe uelewe kuwa Allah yupo kila mahala na kumwona kila mtu. Hivyo ni jambo la kustaajabisha ni kule kutumia riziki yake kuishi katika milki yake na vitendo wazi katika utawala wake ambavyo yeye anakuona na kufahamu. Baada ya yote hivyo unadai kufanya ibada yake.

Abdullah alisema: "Kwa hakika umesema ukweli kabisa. Na sharti la nne ni lipi?"

Bahlul alimwambia: "Wakati utakapoijiwa na Malakul Maut (Malaika atoae roho) ili kuitoa roho yako, basi umzuie asifanye hivyo hadi hapo utakapokuwa umekwisha agana na ndugu na rafiki zako wote na kuweza kutenda matendo mema ambayo yatakusaidia hapo baadaye."

Abdullah alijibu: "Lo! Sharti hili ni gumu zaidi kuliko masharti yote. Huyo Malakul Mauti hatanipa hata fursa ya kupumua!"

Hapo ndipo Bahlul alipomjibu: "Ewe mtu mwerevu! Wewe watambua vyema kabisa kuwa mauti hayana hila yoyote, na hauwezi kamwe kujitenga nayo na hautapatiwa muhula wowote ule. Na inawezekana pia ikatokea mauti katikati mwa hali ya madhambi na hautapata hata muhula wa kupumua kama vile Allah (s.w.t.) alivyosema.

Kwa hiyo ewe Abdullah! Pokea nasiha hata kwa mwehu na uamke kutoka usingizi wako!"

Jihadhari na ghururi na ulevi wako na uwazie akhera kwani safari yako ndefu ipo mbele yako na umri wako upo mdogo kabisa. Kazi ya leo usiiweke kesho kwani kesho hiyo labda hautaiona. Muda huu uliopo uthamini. Kazi za Aakhera usizicheleweshe kwani usichokitenda leo utakijutia hapo kesho na kujuta kwako hakutakufaidisha."

Abdullah alipoyasikia hayo alianza kuwaza huku akiwa amekiinamisha kichwa chake.

Mara Bahlul alianza kusema: "Ewe Abdullah! Wewe umenitaka nikusihi ili uweze kufaidika nayo kesho, sasa baada ya kuyasikia hayo mbona wainamisha kichwa chini?"

Siku ya Qiyama, katika uwanja wa Hisabu na Kitabu, utawajibu nini Malaika watakao kuhoji. Yeyote yule atakayekuwa na hisabu yake safi humu duniani, hatakuwa na khofu yoyote ile hapo Aakhera!

Hatimaye,Abdullah alikiinua kichwa chake na kusema: "Ewe Sheikh! Mimi nimeyasikia yote uliyoyazungumza. kwa moyo wangu wote na nimelikubali hili sharti la nne pia, naomba unisihi zaidi na kunifanya niwe mmoja wenu.

Bahlul alisema: "Ewe Abdullah! Mwanadamu afanyalo lolote inambidi aweke mbele maamrisho yake Allah s.w.t. na hata katika hali ya kusema au kusikiliza, kwani kwa kila hali yu mwumba wa Allah s.w.t."

Bahlul alikuwa ni mtu ameelimika kwa Imam Jaafer as-Sadiq a.s.

(14). Bahlul Amsihi Harun.

Harun Rashid alikuwa akipita njia moja na alimkuta Bahlul akicheza mbio na watoto, hapo alimpigia sauti ya kumwita.

Bahlul alipofika alisema: "Je una kazi gani?"
Harun alimwambia, "Nataka nasiha zako!"

Hapo Bahlul alimwambia: "Tazama kwa makini mno majumba ya Wafalme yaliyokuwa ya fahari na sasa yalivyo na vile vile makaburi yao. Hayo pia yanatosha kukutanabahisha. Wewe waelewa vyema kabisa vile wafalme hao walivyokuwa wakiishi katika majumba hayo kwa starehe na fakhari na kiburi chao, lakini leo walipo (makaburini mwao) hawana la kufanya ila wao wanajuta kwa yale waliyoyafanya wakiwa na uwezo. Uelewe vyema kabisa kuwa nasi pia karibuni tutaungana nao." (tutakufa).

Kwa hayo, Harun alitetemeka, na hakusita kuuliza: "Sasa, je nifanyeje ili mola aniwie radhi?"

Bahlul alimjibu, "Watendee matendo mema viumbe vya Mwenyezi Mungu kwa hayo utaweza kupata radhi yake Mwenyezi Mungu."
Harun aliuliza, "Je ni kama matendo gani?"

Bahlul alimjibu: "Utawale kwa haki na uadilifu. Chochote kile ukionacho kibaya kwako ndivyo hivyo hivyo kiwe kwa ajili ya wengineo. Kilio cha aliyedhulumiwa na maombi yake uyasikilize vyema na kuyajibu kwa utukufu na uyafanyie uchunguzi kwa makini na utoe maamuzi na hukumu zako kwa haki na uadilifu."

Harun alisema: "Hongera ewe Bahlul! Kwa hakika umenipatia nasiha nzuri mno. Mimi natoa hukumu kuwa deni zako zote zilipwe."

Bahlul alimjibu: "Deni haliwezi kamwe kulipa deni. Chochote kile ulichonacho wewe ni mali ya Umma,uwarejeshee mali yao. Usinifanyie hisani kwa mali iliyodhulumiwa."
Harun alimwambia: "Fanya ombi lako lingine."

Bahlul alimjibu: "Ombi langu ni kuwa wewe ujaribu kutimiza nasiha zangu, lakini nasikitika mno kuona kuwa roho na nafsi yako imeshakuwa ngumu kutokana na tamaa na starehe za dunia na hivyo nasiha zangu hazitakuathiri chochote."

Kwa hayo, Bahlul akipeperusha kifimbo chake na kusema: "Sogea, kwani farasi wangu hupiga teke pia." Kwa maneno hayo, alijiondokea na safari yake.

(15). Bahlul Amsihi Fadhil Ibn Rabi'i

Siku moja Waziri wake Harun Rashid, Fadhil ibn Rabii alikuwa akipita njia moja hapo alimkuta Bahlul ameketi akiwa ameinamisha kichwa chini akiwa anawaza. Fadhil alisema kwa sauti, "Ewe Bahlul! Je, wafanyaje?"

Bahlul alikiinua kichwa na alipomwona Fadhil, alisema: "Nimekuwa nikiwazia yatakayokupata kwani yaliyompata Jaafer Barki ndiyo hayo hayo yatakayokupata wewe."

Kwa hayo, moyo wake Fadhil ulitingisika, na akasema: "Ewe Bahlul! Mimi nimeweza kusikia hali hiyo kutoka watu tofauti lakini sijawahi kukusikia wewe, hivyo nitapenda kukusikia, juu ya kuuawa kwa Jaafer."

Bahlul akaanza kuelezea:"Katika zama za Ukhalifa wa Mahdi, mwanamke Mansur, mwanamke Khalid Barki, Yahya, aliteuliwa kuwa Katibu na mshauri wa Harun Rashid. Katika kipindi kifupi, Harun, Yahya na Jaafer walishikamana mno. Harun na Jaafer walipendana mno hadi Harun dada yake Abbasa, kuolewa na Jaafer. Lakini pamoja na ndoa hiyo, alimpa sharti la kutomwingilia dada yake. Lakini Jaafer alimwingilia kimwili, na hapo Harun alipopata habari hizo aligeuza urafiki wake katika uadui na upingamizi. Kila wakati alikuwa akibuni mbinu za kumwua na kuuteketexa ukoo wao mzima. Usiku mmoja alimwambia mtumwa wake Masrur: "Mimi nataka usiku wa leo uniletee kichwa cha Jaafer."Kwa hayo, Masrur alishtushwa na kukiinamisha kichwa chake chini. Hapo Harun alimwambia: "Je kwa nini umenyamaza na wawaza nini?"

Mansur alimjibu: "Loh! Kazi hii ni kubwa mno, lau ingeliniijia mauti kabla ya kuamriwa kazi kama hii."

Harun alimjibu: "Iwapo hutaitekeleza amri yangu hii, basi utanaswa na ghadhabu na adhabu zangu na utambue wazi wazi kuwa nitakuua vile hadi wanyama pia watakuhurumia."

Masrur kwa khofu ya mdhalimu huyo aliingia nyumbani mwa Jaafer na kumwelezea vile hukumu ilivyokuwa.

Jaafer alimwambia: "Labda hukumu hii ameitoa akiwa katika hali ya ulevi na kutakapokucha atajuta, hivyo nakuomba uende kwa Khalifa na umjulishe kuuawa kwangu. Iwapo utakuta hakuna athari zozote za kujuta na kusikitika hadi asubuhi basi, utambue kuwa nitakuwekea kichwa changu tayari kwa upanga wako."

Masrur hakuweza kusadiki maneno ya Jaafer, na alimwambia: "Nataka wewe ufuatane nami hadi kwake Harun Rashid, labda inawezekana akakusamehe kwa upendo wako alionao."

Jaafer aliyakubalia maneno ya Masrur na alijitolea kwa maangamizi yake. Basi Masrur alitokezea mbele ya Harun akiwa anatetemeka.

Harun aliuliza: "Masrur, je umetekeleza?"
Masrur alimjibu:"Nimemleta Jaafer, yupo nyuma ya pazia amesimama."

Khalifa akawa amekasirika, alisema: "Iwapo utachelewa hata punde kutekeleza amri yangu, basi nitahakikisha kuwa wewe uuawe kwanza."

Baada ya mazungumzo hayo, hapakuwapo na fursa ya kupoteza. Masrur alimkimbilia Jaafer, kijana mrembo, na mwema, na kumkata kichwa na kukileta mbele ya Harun.

Khalifa huyu aliyekosa huruma, hakukomea hapo tu, bali aliamrisha kuuangamiza ukoo mzima na mali na vitu vyao vyote kuchukuliwa. Mwili wa Jaafer usio na kicwa ulininginizwa katika jumba la Khalifa na baada ya siku chache ukachomwa moto.

Sasa ewe Fadhil! Mimi nahofia matokeo yako. Nahofia matokeo yako pia yasiwe kama yale yaliyompata Jaafer."

Fadhil alishtushwa mno kwa mazungumzo ya Bahlul, na alimwambia Bahlul kuwa "Niombee usalama wangu!"

(16). Kisa Cha Kujenga Msikiti

Fadhil ibn Rabii aliujenga Msikiti katika mji wa Baghdad. Ilipofika siku ya kubandika kibao, aliulizwa kitu gani kiandikwe juu yake. Naye alishauri kuwa jina lake liandikwe kwani yeye ndiye aliyeugharamia ujenzi wake. Wakati hayo yalipokuwa yakitokea, Bahlul pia alikuwapo hapo, naye hakusita kumwuliza: "Je umejenga msikiti huu kwa ajili ya nani?"

Fadhil alijibu: "Kwa ajili ya Allah s.w.t."
Bahlul alisema: "Iwapo ni kwa ajili ya Allah s.w.t. basi usiandikishe jina lako."

Kwa hiyo, Fadhil alikasirika na akatamka: "Kwa nini nisibandike jina langu? Je watu watamjuaje mtu aliyejenga?"

"Je kwa nini usiandike jina langu?" Akasema Bahlul.
"Loh! Hayo kamwe hayawezi kuandikwa." akamjibu Fadhil.

"Iwapo umejenga huu Msikisti kwa ajili ya kujionyesha kujifaharisha, basi utambue wazi kuwa thawabu zako kwa Allah s.w.t. zimepotea."
Hayo ndiyo aliyoyasema Bahlul.

Kwa hayo, Fadhil aliaibika na akanyamaza na kusema: "Fuateni lile alisemalo Bahlul."

Hapo Bahlul akawaambia "andikeni Aya moja ya Quran tukufu na kuitundika mlangoni mwa Msikiti."

(17). Bahlul Na Mwizi Wa Viatu.

Siku moja Bahlul alikwenda Msikitini akiwa amevaa viatu vipya, na huko alimuona mtu mmoja akiviangalia mno viatu vyake, hivyo akaelewa kuwa ataweza kuviiba.

Basi Bahlul akavichukua viatu vyake na kuviweka mbele yake huku akisali.
Yule mwizi akamwambia: "Sala haisihi katika hali hiyo!"
Bahlul akamjibu: "Iwapo sala itanitoka basi viatu vitabaki."

(18). Bahlul Na Rafiki Yake.

Siku moja rafiki yake Bahlul alichukua ngano kwenda kusaga, na baada ya kusagiwa alipakia juu ya punda na kuondoka. Alipokaribia nyumba ya Bahlul, yule punda alianza kufanya machachari na akajibwaga chini. Hivyo huyo mtu alimwita Bahlul na kumwomba msaada wa punda wake ili aweze kuufikisha mzigo wake nyumbani.

Bahlul alikuwa ameishakwisha kula kiapo cha kutomwazima mtu yeyote punda wake, na hivyo alimwambia rafiki yake: "Mimi sina punda!"

Ikatokea kuwa punda akalia kwa sauti. Na hapo rafiki yake akamwambia:"Kumbe punda wako yupo nyumbani na wewe waniambia kuwa hauna punda!"

Bahlul akamwambia: "Loh! wewe rafiki wa kiajabu kweli! Sisi tupo marafiki kwa muda wa miaka hamsini, lakini nashangaa kuona kuwa hautaki kuamini nikuambiayo na huku unayaamini yale akuambiayo punda."

(19). Bahlul Na Mganga Wa Harun.

Harun Rashid alimleta mganga kutoka Ugiriki Khususan katika Baraza lake. Alipowasili Baghdad, alipokelewa na kupewa heshima za kila aina.

Kila mtu wa mji wa Baghdad walikwenda kumuona mganga huyo, na siku ya tatu Bahlul pia alikwenda kumuona pamoja na watu wachache. Wakati mganga akiwa anasifiwa na kutukuzwa, mara Bahlul akamwuliza swali : "Je unafanya kazi gani?"

Kwa kuwa mganga alikwisha kuelewa vile Bahlul alivyo na uwehu wake, hivyo akataka kuleta kichekesho kwa kumjibu: "Mimi ni mganga wa huisha wafu."

Bahlul akamjibu: "Tafadhali usiwaue hai na kumhuisha maiti ni fidia yake."
Kwa majibu hayo ya Bahlul, Harun Rashid pamoja na watu wote katika Baraza lake waliangua kicheko hadi yule mganga akauhama mji wa Baghdad kwa aibu.

(20). Bahlul Aulizwa Swali

Siku moja Bahlul alikwenda katika Baraza la Harun Rashid na akaketi mbele yake. Kwa hayo, Harun aliudhika mno na alitaka amuaibishe Bahlul mbele ya wote waliokuwapo hapo. Alimwuliza: "Je Bahlul yu hadhiri? Nataka jibu la fumbo langu."

Bahlul alisema: "Ni lazima kwanza uniambie sharti lako na utoe ahadi ya kutonigeuka katika kutimiza ahadi hiyo."

Kwa hayo, Harun alisema: "Iwapo utanijulisha jawabu papo hapo basi nitakupa Ashrafi elfu moja na iwapo utashindwa kunijibu basi nitatoa amri ya kunyolewa kwa ndevu na masharubu yako, kisha utembezwe katika mitaa na vichochoro vya Baghdad kwa kuaibishwa na kudhalilishwa."

Bahlul alimjibu "Ah! Mimi sijali wala sihitaji hizo Ashrafi zako, bali ninalo sharti moja iwapo nitaweza kulijibu fumbo lako."

Hapo Harun akasema: "Je sharti lipi hilo?"
"Iwapo nitaweza kukujibu basi nitataka uwatolee amri inzi wasinisumbue" alisema Bahlul.

Harun alifikiri kwa kitambo, kisha akasema: Hili jambo haliwezekani kwani inzi sio katika utii wangu."

Kwa hayo Bahlul aliangusha kichekesho na kwa mshangao akasema: Je kunaweza kutegemewa nini kutoka mtu ambaye hawezi hata kudhibiti kitu kidogo mno kama inzi?"

Kwa hayo, Bahlul aliwaacha wote katika hali ya mshangao. Kwa majibu hayo, uso wa Harun ulianguka na Bahlul alipoyaona hayo, alisema: "Nipo tayari kujibu swali lako bila sharti lolote."

Basi Harun alijikaza, na kuuliza: "Je ni mti upi ule ambao umri wake ni mwaka mmoja na unao matawi kumi na mawili na majani thelathini ni siku ambazo sehemu moja ni usiku na wa pili ni mchana."

Harun alistajabishwa kwa majibu. Na wote waliokuwapo pia walifurahishwa mno kwa busara ya Bahlul.

(21). Sadaka Ya Khalifa

Siku moja Harun Rashid alimpatia Bahlul kiasi fulani cha fedha ili awagawie masikini, mafukara na wenye mahitajio. Bahlul alizipokea fedha hizo, na baada ya kitambo, alimrejeshea Khalifa fedha hizo.

Harun Rashid alistaajabishwa kwa hatua hiyo ya Bahlul na hivyo alitaka kujua sababu.

Bahlul alimjibu katika hali ya kumhurumia Khalifa: "Ewe Khalifa! Mimi kwa hakika nimejaribu mno kumtafuta mustahiki wa sadaka yako hiyo, lakini nimeona kuwa hapa mjini petu hakuna mtu mwingine isipokuwa ni wewe tu! Kwani nimewaona wanaokukusanyia kodi wewe, wakiwa wanawapiga mijeledi raia ili kukukusanyia fedha wewe ambazo unazihitaji katika hazina yako. Hivyo nimefikia uamuzi huo wa kukupa fedha hizo wewe tu unayestahiki mbele ya macho yangu kuliko raia yoyote yule

(22). Neema Bora Ya Allah S.W.T.

Siku moja Harun Rashid alimwuliza Bahlul: "Je ni neema ipi ya Allah s.w.t. iliyo bora?'

Bahlul alimjibu: "Neema bora kabisa ya Allah s.w.t. ni Akili (Agl). Khawaja Abdullah Ansari pia amesema katika munajat: "Ewe Allah! Kwa yule aliyepewa nawe Akili je ni kipi tena ulichomnyima na yule asiyepewa akili umempa nini?"

Imepatikana katika riwaya moja kuwa Allah SWT amepata kumwondoshea mja wake neema zake, basi humwondoshea akili yake. Akili (Agl) inahisabiwa katika kikundi cha riziki.

(23). Bahlul Na Mwizi

Bahlul alikuwa akiishi katika nyumba iliyokuwa tupu. Mbele ya nyumba yake kulikuwa na duka la mshona viatu ambaye dirisha lake lilikuwa likifunguka mbele ya nyumba ya Bahlul alikusanya fedha kidogo na akazifukia ardhini na kila alipokuwa akipata dharura, alikuwa akifukua kiasi alichokuwa akikitaka na kufukia kiasi kilichobakia. Siku moja alipopata dharura ya fedha, alikwenda kufukua, na akakuta hakuna chochote shimoni, na hapo aling'amua kuwa fedha hizo zimeibiwa na mshona viatu tu kwani dirisha lake lilikuwa likifungukia mbele yake.

Basi yeye bila ya kuonyesha dalili zozote zile alikwenda dukani mwa mshona viatu na akaketi kimya, na alianza mazungumzo ya kila aina hadi mshona viatu akafurahi na kuvutiwa. Hapo ndipo Bahlul aliposema: "Ewe rafiki mpenzi! Hebu naomba unijumlishie hesabu yangu!"

Mshona viatu akasema: "Haya anza nami nitakujumlishia."
Bahlul alianza kutaja majumba mengi na pamoja na kila jumba alikuwa akiisemea na fedha.

Hadi kutaja na nyumba anamoishi kuwa ameficha kiasi fulani cha fedha. Mwishowe, mshona viatu akamwambia kuwa jumla ya sarafu alizozitaja ni dinar elfu mbili.

Bahlul akawaza kwa kitambo, na akaanza kusema: "Ewe rafiki mpenzi! Mimi na kuomba ushauri mmoja."

Mshona viatu akasema: "Ndiyo sema tu!"
"Mimi nafikiri kuwa dinar hizo elfu mbili nizilete hapo kwangu na kuzifukia shimoni."

Mshona viatu alimjibu "Loh! wazo zuri kabisa. Ndiyo, kusanya fedha zako zote kutoka kote ulikoficha na uzifukie hapo unapoishi."

"Kwa hakika mimi nasakiki maneno yako tu! Na nakwenda kuzichukua fedha zote zilipo ili nizifukie humu mwangu! "Alimjibu Bahlul. Baada ya kusema hayo Bahlul aliondoka.

Baada ya kuondoka kwake, yule mshona viatu akawaza kuwa itakuwa vyema iwapo hizo fedha kidogo alizoziiba akazirudishe mahala pake ili atakaporudi Bahlul kufukia zingine azikute zipo na hivyo asiingiwe na shaka ya kuibiwa. Hivyo ataweza kupata fedha zaidi kwa mara moja. Hivyo yeye alikwenda kurudisha zote alizokuwa ameziiba.

Baada ya masaa machache, Bahlul alirudi nyumbani mwake na akazikuta zile fedha zake zilizokuwa zimeibiwa na mshona viatu. Basi alizifukua zote na kumshukuru Mwenyezi Mungu, na aliacha nyumba hiyo akahamia mahali pengine. Mshona viatu alikuwa akimsubiri kwa hamu lakini hakuweza kumwona tena. Na baada ya kupita kipindi fulani, hivyo aliweza kung'amua kuwa Bahlul alimdanganya kwa hayo ili aweze kuzirudisha fedha zake!.

(24). Bahlul Na Amir Wa Kufa

Ishaq bin Mohammad bin Sabah alikuwa Amiri wa mji wa kufa.
Mke wake alizaa binti mmoja. Kwa kuzaliwa kwa binti, alihuzunika na kuaibika mno na hatimaye akaamua kuacha kula wala kunywa.

Bahlul alipouyasikia hayo, alimwendea na kumwambia:"Ewe kiongozi! Je huzuni na majuto yote hayo ni ya nini?"

Amiri alimjibu: "Mimi nimekuwa nikitarajia kuzaliwa kwa mtoto wa kiume lakini mke wangu amezaa mtoto wa kike badala yake."

Bahlul alimjibu: "Je ungalipendelea kuzaliwa kwa mtoto wa kiume mwenye kasoro za kimwili au mwehu kama mimi badala ya binti huyu ambaye yu salama na mrembo?"

Kwa kuyasikia hayo Ishaq alifurahi na kucheka na alitoa shukrani zake kwa Allah s.w.t. na akaanza kula na kunywa na aliwaruhusu watu kuja kumpa hongera!"

(25). Bahlul Kupwewa Zawadi

Siku moja Harun Rashid alitoa amri kuwa Bahlul apewe zawadi.Na Bahlul alipozawadiwa alirejesha na akasema:"Hii mali uliowanyang'nya uwarejeshee wenyewe. Na usipowarejeshea wenyewe hii mali, basi itafika siku ambapo Khalifa atatakiwa alipe vyote ambapo hapo ndipo atakapokuwa Khalifa katika ufukara, basi ataibika na kujuta tu."

Harun Rashid Kusikia hayo akatetemeka na aliangua kilio huku akisadikisha aliyoyasema Bahlul.

(26). Kuathiri Kwa Dua

Ngamia wa Mwarabu mmoja alipatwa na ugonjwa wa kujikuna. Watu walimshauri ampake mafuta ya mbarika. Basi huyo Mwarabu alielekea mjini kwenda kununua mafuta hayo. alipoukaribia ule mji, alikutana na Bahlul. Kwa kuwa alikuwa ni urafiki wa Bahlul, hivyo alimwelezea "Ngamia wangu anao ugonjwa wa kujikuna. Na watu wameniambia kuwa ninunue mafuta ya mbarika ndiyo yatakayomtibu. Lakini ni akida yangu kuwa kumpulizia kwako kunaweza kumtibu. Hivyo naomba umuombee dua ngamia wangu apone."

Bahlul alimwambia: "Na kubaliana nawe. Lakini uatmbue kuwa Dua na dawa ndizo zitakazomponya. Hivyo nunua mafuta ya mbarika nami nitamuombea dua na ujue kuwa dua bila matendo na juhudi haifaidii.

Hivyo huyo mtu alinunua mafuta na kuyaleta. Bahlul aliyasomea dua. Baada ya kumpaka kwa siku chache, Ngamia alipona.

(27). Ubora Na Sifa Za Imam Ali A.S.

Siku moja Bahlul alimtembelea Harun Rashid, aliyekuwa ametulia kwake. Alimwuliza Bahlul: "Je ni ali a.s. yu bora kuliko Abbass, mjomba wake mtume s.a.w.w. au je Abbass ni bora kuliko Ali?"

Bahlul alimjibu: "Iwapo utanihakikishia usalama wa maisha yangu ndiyo nitakaposema yaliyo ya kweli."

Harun alijibu: "Ndiyo unayo amani."
Bahlul alisema: "Baada ya Mtume s.a.w.w. Ali a.s. alikuwa ni mbora kuliko Waislamu wote, kwani Ali a.s. alikuwa ni shakhsiya ambayo ilikuwanayo sifa za kila aina. Imani yake madhubuti ya Islam haina swali. Ushujaa wake katika vita vya kuinusuru Islam haina mfano. Yeye hakujitolea mhanga pekee yake katika kuinusuru Islam bali hata ukoo wake mzima ulijitolea mhanga. Katika vita vyote vya Kiislam vya kujihami, yeye daima amekuwa mstari wa mbele na kamwe hakuupa mgongo au kukimbia kwa kuwacha uwanja wa vita. Na wakati Ali a.s. alipoulizwa: "Je kwa nini hautazami nyuma wakati wa mapambano kwani unaweza kushambuliwa na maadui kwa nyuma?"

Ali a.s. aliwajibu: "Kupigana kwangu ni kwa ajili ya vita vya Allah s.w.t. Huwa sina woga wa aina yoyote na wala tamaa yoyote, kwani hujitolea kikamilifu kwa ajili yake Allah s.w.t. Iwapo nitauawa basi itakuwa ni kwa amri yake allah s.w.t. na katika njia yake. Je kutakuwa na upendo mwingine wowote zaidi ya kuuawa katika njia ya allah s.w.t.? ama kama nitauawa hivyo basi mtu ataajiliwa kukaa pamoja na wale watenda haqi!"

Zaidi ya hayo, wakati Ali a.s. alipokuwa Khalifa wa Waislamu yeye kamwe hakupumzika kwani alikuwa akishughulika usiku na mchana.

Yeye kamwe hakukubali mbadhirifu au utumiaji ovyo wa dola ya Umma na kamwe haqi za waombaji na masikini hazikupuuzwa au kusahauliwa.

Siku moja Aqil, ndugu yake, alimjia akiomba apatiwe mali kutoka hazina ya Umma lakini aliaibika kuomba hivyo kwani alimkuta Khalifa alivyokuwa akiishi, pamoja na hayo Imam Ali a.s. alimkatalia katakata.

Yeye daima alikuwa Khalifa aliyeongoza kwa haki na uadilifu na kamwe hakuwateua magavana ambao walikuwa wadhalimu na wala hakuwavumilia. Mfano Ibn Abbas, wakati alipokuwa Gavana wa Basra, alitumia wakati mmoja kiasi cha fedha kutoka hazina ya Umma, Ali a.s. alimtaka arejeshe haraka sana na alimkanya vikali mno.

Vile vile alimpatia tarehe ya kurejesha hizo fedha, lakini Ibn Abbas alishindwa kurejesha, hivyo Ali a.s. alimwamrisha afike kufa badala yake alikwenda Makka ili aweze kupata amani, kwani alitambua wazi wazi kuwa Ali a.s. alikuwa ni mtu afuataye sheria na kanuni kwani yu mtu mwenye msimamo thabiti.

Harun Rashid alipoyasikia hayo, alishikwa na aibu na hivyo akataka kumwulimiza roho Bahlul, aliuliza swali: "Je pamoja na kuwa na sifa zote hizo bora, kwanini aliuawa?"

Bahlul alimjibu:
"Wengi wa wale walio juu ya njia ya haki wamekuwa wakiuawa. Hata Mitume ya Allah s.w.t. pia imekuwa wakiuawa katika zama zao."

(28). Utetezi Wa Bahlul Mahakamani

Katika mji wa Baghdad kulikuwapo na mfanyabiashara aliyekuwa mtu mwema na mwadilifu katika biashara yake. Yeye alikuwa akiagiza mali kutoka mbali na kuuza kwa bei nafuu, na kwa hayo, alikuwa maarufu na alipendwa na wakazi wa mji huo.

Vile vile kulikuwapo na mfanyabiashara mmoja Myahudi ambaye alikuwa akiuza mali yake kwa bei ghali mno na vile vile alikuwa akiendesha shughuli za kukopesha fedha kwa riba. Alikuwa akiwapa watu fedha kwa kutaka riba kubwa na alikuwa akitoa masharti magumu mno.Ikatokea kuwa yule mfanya biashara mwema na hivyo alimwendea huyo Myahudi na kumtaka deni. Kwa kuwa Myahudi alikuwa na uadui wa siku nyingi, basi alimwambia kuwa atampa kwa sharti moja nayo ni iwapo atashindwa kulipa kwa tarehe maalum basi akubali kukatwa nyama mwilini mwake kiasi cha kilo moja, sehemu yoyote ile. Kwa hayo mfanyabiashara huyo alikubali sharti hilo na hivyo akafanya mapatano hayo katika njia ya maandishi.

Ikatokea huyo mfanyabiashara akashindwa kulipa deni lake kwa tarehe ya mapatano, hivyo, Myahudi akapeleka mapatano yao kwa Hakimu kwa kupatiwa hukumu ya kutekeleza kukatwa kwa nyama. Naye alikuwa amekwisha panga kukata nyama sehemu ile ambayo itamfanya huyo mtu afe tu. Lakini Hakimu amekuwa daima akiichelewesha hiyo kesi au Myahudi akaghairi mawazo yake.

Lakini Myahudi akawa anamwendea kila siku kutaka kuharakishwa kwa hukumu. Kesi hiyo ikawa mashuhuri hapo Baghdad, na siku ya kesi ilipotolewa, watu walijazana Mahakamani kusikiliza kesi na yatakayotokea.

Siku hiyo Bahlul pia alifika kujionea. Aliweza kusikiliza kwa makini mno maneno ya pande zote mbili.

Hakimu alisoma karatasi ya mapatano na mwishoni alimwambia Mfanyabiashara:"Kwa mujibu wa waraka huu, wewe unatakiwa kumlipa Myahudi kwa mjibu wa mapatano, nyama ya sehemu yoyote ile aitakayo yeye. Sasa je unalo lolote la kusema au kujitetea?

Mfanyabiashara akasema:"Ewe Mwenyezi Mungu! Wewe ndiye uelewaye zaidi. Basi!"
Na hapo Bahlul akasema kwa sauti: "Ewe hakimu! Je inawezekana kwangu mimi kumtete binadamu mwenzangu katika kesi hii kama wakili wake?

Hakimu alimjibu: "Naam inawezekana. Hivyo tutolee dalili zako za utetezi."
Bahlul alijitosa baina ya mfanyabiashara na Myahudi na akasema: "Kwa mujibu wa mapatano haya Myahudi anayo haki ya kumkata nyama huyu bwana lakini atakapokata nyama ya huyo mfanyabiashara basi kusidondoke hata tone moja la damu na anapomkata nyama aikate kwa kipimo tu - yaani isizidi wala kupungua. Na iwapo huyo Myahudi atakiuka masharti hayo mawili basi ahukumiwe adhabu ya kifo, mali na milki yake yote itaifishwe!"

Hakimu kwa maneno ya Bahlul, alibakia kimya huku akifurahi. Na Myahudi yule ilimbidi achukue fedha alizomkopesha bila ya riba yoyote."

(29). Mbinu Za Bahlul.

Siku moja Bahlul alikuwa akipita njia moja na akamkuta mtu mmoja akilia, ambaye alionekana kama mgeni hapo mjini.

Bahlul alimwuliza: "Ewe ndugu! Je kitu gani kilichokusibu kiasi cha kukufanya uanze kulia hivi?"

Yule mtu akamjibu: "Mimi ni mgeni mjini humu. Nilifika ili nikae siku chache. Mimi nilikuwa na fedha na vitu vya thamani ambavyo kwa khofu ya waizi niliviwekesha kama amana kwa mwuza mafuta ya manukato ambaye nilipomwendea baadaye anirejeshee, alisema ati mimi ni mwehu na hivyo akafanikiwa katika kunigeuka.

Bahlul aliwambia: "Usihuzunike! Mimi nitahakikisha kuwa huyo Atar (mwuza mafuta ya manukato) atakurudishia amana yako kwa wepesi kabisa."

Akamwuliza ni Atar yupi, na baada ya kumfahamu, alisema: "Kesho saa fulani nitakusubiri dukani mwake na usinisemeshe kama kwamba haunijui. Na utawaambia kuwa nirudishie amana yangu!" Mtu huyo akakubali.

Hapo moja kwa moja, Bahlul alimwendea yule Atar na kumwambia: "Mimi nimepata safari ya ghafla ya kwenda khurasan na ninavyo vito na dhahabu vya thamani ya Ashrafi elfu thelathini ambazo ninataka kukuwekesha amana. Iwapo nitarudi salama basi nitachukua mali yangu na iwapo nitakuwa sikurudi hadi siku fulani fulani basi wewe utakuwa msimamizi wa mali hiyo na utaiuza na kujenga msikiti mmoja kwa fedha zake."

Atar alifurahishwa mno kwa hayo na akasema: "Usiwe na shaka! Je hiyo amana utaileta lini?"

Bahlul alimjibu: "Kesho saa fulani. "Na akaondoka zake. Na alishona mfuko mmoja wa ngozi na humo akaweka lakiri yake. Ulipofika wakati waliopeana Bahlul akatokezea na mfuko wake huo, wakati wanazungumza na Bahlul, akatokezea yule mgeni akamwambia mwenye duka "Ewe Bwana! Naomba amana yangu niliyokuachia."

Kwa kuwa mwenye duka, alikuwa na tamaa kubwa ya kifurushi cha Bahlul na ili kuonyesha uaminifu wake, alimwamuru mfanyakazi wake akamletee mfuko wa mgeni huyo.

Mgeni huyo alipoona kuwa amerudishiwa mfuko wake bila ya hata neno moja, alimshukuru Bahlul na kumwombea dua njema.
Akaondoka mjini.

(30). Harun Rashid Na Tapeli

Mtu mmoja alitokezea mbele ya Harun Rashid akidai mgeni, hivyo Harun Rashid alianza kumwuliza habari mbali mbali kuhusu mazao, madini na viwanda hadi kuulizia vile vile habari za Bara Hindi. Kwa hakika Tapeli huyo aliweza kumjibu Khalifa kwa ustadi hadi kumfanya Khalifa avutiwe naye.

Tapeli alimwambia Khalifa: "Huko Bara Hindi kunapatikana dawa fulani ambayo inamrudishia mtu nguvu za ujana wake. Iwapo mzee wa umri wa miaka sitini akiitumia dawa hiyo, atarudiwa na nguvu za kijana wa miaka ishirini."

Khalifa alivutiwa mno kwa bayana zake za madini na dawa za Bara Hindi na akasema: "Je utahitaji kiasi gani cha fedha ili kukugharamia wewe ukaniletee ile dawa na madini?"

Mtapeli huyo, akampigia hesabu ya Dinar elfu hamsini kugharamia safari hiyo.

Khalifa Harun Rashid alimwamuru mweka hazina ya Umma wa Kiislam, ampatie huyo mtapeli hizo Dinar elfu hamsini. Baada ya kupatiwa, mtapeli aliondoka zake.

Khalifa alikuwa akivumilia kurudi kwa mtapeli huyo kwa muda mrefu mno, lakini hakurejea wala kusikika habari zake. Khalifa kwa haya, alikuwa akisikitika na kuhuzunika mno hadi kutaka kulia alipokuwa akikumbuka.

Siku moja alipozungumzia habari za tapeli, Jaafer Barki na baadhi ya watu walikuwapo. Akiwa katika hali ya hasira, Harun alisema:

"Iwapo nitamnasa huyu mtapeli, basi nitamtoza Dinar zaidi na vile vile atakatwa kichwa chake na kukitundika katika mlango wa Mji ili iwe ni fundisho kwa wengine."

Bahlul akicheka alisema: "Ewe Harun! Kisa chako hiki ni sawa na kisa cha kuku, bibi kizee na fisi."
Harun akauliza "Je kisa hicho kikoje, hebu nielezee!"

Bahlul alianza: "Siku moja paka mwitu alimnasa kuku wa bibi kizee mmoja na alianza kufukuzwa na bibi huyo, huku akisema "Tafadhalini nishikieni, paka huyu ameniibia kuku wangu mzito wa kuku wawili!" Basi paka huyo alipoyasikia hayo akaanza kuwaza kuwa anasingiziwa bure kwani kuku aliyemuiba yu mwepesi tu.
Mara akatokezea fisi, naye kamwuliza kuku kilichomkera. Kuku akamwelezea anavyosingiziwa, hapo fisi akamwambia muweke yule kuku juu ya ardhi ili aweze kumpima uzito wake.

Alipoachwa tu kuku juu ya ardhi, yule fisi akamchukua na kukimbia naye huku akisema "Mwambie bibi kizee kuwa uzito wa kuku huyu ni mara tatu.!"
Harun Rashid alifurahishwa mno kwa kisa hicho na limpongeza Bahlul.

(31). Harun Rashid Na Mvuvi.

Siku moja ya Idi,Harun Rashid alikuwa akicheza mchezo wa shatranji (michezo ya kamari) pamoja na mke wake Zubeidah, ambapo Bahlul alitokezea na akiwaangalia wakicheza. Mara hapo akatokezea mvuvi mmoja akiwa na samaki mnono kwa ajili ya Khalifa.

Wakati huo huyo Khalifa (wa Umma wa Waisilamu) alikuwa amelewa chakali chakali! Na hapo aliamrisha kuwa huyo mvuvi alipwe Dirham elfu nne kama zawadi yake. Mke wake, Zubeidah, hapo alimbishia kwa kusema: "Kiasi hiki ni kikubwa mno kwa ajili ya mvuvi huyu mmoja kwani wewe unatakiwa kuwalisha majeshi na shughuli zako za kila siku na utakapowapa malipo kidogo basi watasema kuwa wao ni bora ya mvuvi. (huku wakilipwa chini ya mvuvi) na iwapo utawapa zaidi basi hazina ya Umma itakwisha mara moja."

Harun Rashid alipendezewa na maneno ya Zubeidah,na aksema: "Je nifanyeje sasa

Zubeidah akamwambia: "Mwite huyo mvuvi na umuulize iwapo samaki huyo ni jike au dume. Iwapo atakwambia ni jike basi mwambie hatumtaki na iwapo atakwambia ni dume, vile vile mwambia hatumtaki.

Hivyo ndivyo utakavyoweza kuondokana naye na kukwepa kumlipa Dirhan zozote,kwani atarudi na samaki wake."

Bahlul, kwa kuwa alikuwa hapo hapo, alimwambia Harun, "Ewe Khalifa! Jiepushe na farebi (ulaghai) wa wanawake, na usimuuzi mvuvi ila tu mridhishe."

Harun hakukubaliana na Bahlul na alimuita mvuvi akamwuliza: "Je samaki huyo ni jike au ni dume?"

Mvuvi aliibusu ardhi na akasema: "Samaki huyu si jike wala dume bali ni mukhnnaht (tabia ya kike)!"

Harun alifuraheshwa kwa majibu hayo ya mvuvi. Na papo hapo akatoa amri ya kulipwa Dirham elfu nne. Wakati mvuvi alipokuwa akitoka nje ya jumba la Khalifa, ikadondoka Dinar moja, hivyo akainama na kuiokota.

Zubeidah, akamwambia Harun, "Huyu mtu hana hata shukrani. Kwani Dinar moja tu inadondoka, hakuiacha bali akainama na kuichukua. "Kwa hayo Harun hakupendezewa na harakati hizi za mvuvi, hivyo alimwita tena.

Bahlul alisema: "Ewe Khalifa, mwachie aende zake usimzuie wala usimwite tena!"

Lakini Harun hakumsikiliza, bali alimwita na kumwambia: "Loh! Wewe una roho ndogo sana kwani hata Dinar moja haukuiacha ili watumea wangu wakaiokote."

Mvuvi akatoa heshima zake tena na akasema: "Ewe Khalifa! Mimi si hivyo unavyonidhania bali huwa ninajua kutoa taadhima kwa neema niipatayo. Nimeiokota hiyo Dirham kwani upande mmoja umeandikwa aya za Quran Tukufu na upande wa pili kuna muhuri wa Khalifa mtukufu. Sasa itawezekanaje mimi kuiachia chini ije ikakanyagwe na mtu hivyo kuvunjiwa heshima na ikawa ni utovu wa adabu zetu."

Khalifa alifurahishwa kwa majibu ya mvuvi huyo na hakusita kutoa amri ya kulipwa Dirham elfu nne zingine.

Bahlul hapo akamwambia: "Je sikukukataza usimzuie wala usimwite tena? Kwani nilijua kuwa yu mtu hodari."

Hapo Harun alisema kwa hasira: Mimi ni mwehu hata kuliko wewe kwani wewe umenikataza mara tatu lakini mimi sikukusikia wewe na badala yake nilimfuata mwanamke huyo ambaye amenitia hasarani!"

(32). Swali Juu Ya Amin Na Ma'amun.

Siku moja bahlul alikuwa akienda kwa Harun na wakakutana njiani. Harun akamwambi: "Je wakwenda wapi?"

Bahlul akamjibu: "Kwako wewe!"
Harun akamwambia: "Mimi nakwenda shuleni kujua hali ya Amin na Ma'amun na maendeleo yao. Hivyo iwapo utapenda kuandamana nami, basi tufuatane pamoja."

Bahlul alikubali na hivyo walifika shuleni lakini wakakuta watoto hao wawili wametoka nje kidogo.

Harun alimwuliza mwalimu hali na tabia za watoto wawili hao.
Mwalimu alimjibu: "Amin ni mtoto wa kiongozi wa akina mama na Kiarabu, lakini ni mpumbavu na mwenye akili na fahamu ndogo, na kinyume chake ni Ma'amun ambaye ni hodari mwenye akili na mwerevu!

Harun alitamka: "Mimi si yaamini hayo!"
Mwalimu akachukua karatasi akaiweka chini ya zulia alipokuwa akikalia Ma'amun na akaliweka tufali chini ya zulia alilokuwa akilikalia amin. Baada ya muda mdogo tu, wote wawili walirejea darasani. Walipomwona tu baba yao, wote wawili walitoa heshima zao, na wakaketi nafasini kwao.

Ma'amun alipoketi, hakutulia, aliitazama dari na alitazama kushoto na kulia. Hapo mwalimu alimwuliza: "Ewe Ma'amun mbona unakodoa macho huku na huko? Je umekuwaje?"

Ma'amun alimjibu: "Baada ya kutoka darasani na kurejea nahisi kuwa hii ardhi imeinuka kiasi cha unene wa karatasi moja au dari la darasa limeteremka chini kiasi hicho. Yaani kwa kifupi, Zulia langu limeinuka kwa kiasi cha karatasi moja."

Papo hapo mwalimu alimwuliza Amin: "Je na wewe wahisi hivyo?"
Amin alimjibu: "La! Mimi sihisi chochote kile, nipo sawasawa."
Kwa kuyasikia hayo mwalimu alicheka na akawaambia watoke nje ya darasa na akamwambia Harun alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa maneno yake kuthibitika kweli mbele yake.

Hapo Khalifa alimwuliza: "Je nini sababu ya tofauti hizo?"
Bahlul akasema: "Ewe Khalifa! Iwapo utanipa ahadi ya amani na kusalimika kwangu kutokana na wewe mimi nitaweza kukujibu sababu zenyewe."

"Unayo amani na utasalimika, haya elezea yale uyajuayo kuhusu swala hili." Allimjibu Harun.

Hapo ndipo Bahlul alipoanza kuelezea kwa kinaganaga: "Uhodari na uwerevu wa watoto unatokana na sababu mbili - kwanza, wakati mwanamme na mwanamke wanapokutana kimwili pamoja na taratibu njema basi watoto wazaliwao huwa werevu, hodari na wakakamavu. Sababu ya pili, mwanamme na mwanamke wanapotokana na damu na ukoo tofauti basi watoto wao huwa wenye akili, werevu na wenye nguvu. Na vivyo hivyo ndivyo ilivyo katika mimea na wanyama, na hayo yameshakwisha kuthibitishwa, kwa mfano, iwapo kutapandikizwa tawi la tunda aina moja katika aina ya tunda lingine la jinsi hiyo hiyo, basi tunda jipya litakuwa tamu na lenye ladha nzuri kuliko tunda la mti wenyewe. Na iwapo kutakutanishwa kimwili kwa farasi na punda, basi kutazaliwa nyumbu ambaye atakuwa hodari na mwenye nguvu, mwepesi kuliko hao wazazi wake.

Kwa kifupi, kasoro aliyo nayo Amin katika kufikiri na fahamu ni kwa sababu ya Khalifa na Zubeidah wanatokana na damu na ukoo mmoja ambapo Ma'amun anaonekana mwerevu, hodari na mwenye akili ni kwa sababu mama yake mzazi ametokana na ukoo na damu tofauti na ile ya Khalifa, na tofauti yake ni kubwa!"

Khalifa kwa majibu hayo alicheka na kusema: "Mwehu atasema hayo hayo na wala hawezi kutegemewa kusema kingine cha akili." Lakini mwalimu aliyasadikisha maneno ya Bahlul moyoni mwake.

(33). Bahlul Amjibu Khalifa.

Harun Rashid alikuwa akirudi kutoka Hijja na njiani alikuwapo Bahlul aliyekuwa akimsubiri. Alipomuona Harun Rashid, alipaaza sauti yake na akasema mara tatu: "Harun! Harun! Harun!"

Khalifa aliuliza "Je ni nani yule aniitaye hivi?"
Watu walimwambia: "Si mwingine ila ni Bahlul."
Hapo Bahlul aliitwa, na alipokaribia, aliulizwa "Je mimi ni nani?"

Bahlul alimjibu, "Wewe ni yule mtu ambaye atatkiwa kutoa majibu ya dhuluma iwapo itafanyika mashariki au magharibi" (Kwani Harun alikuwa Khalifa wa dola nzima hivyo aliwajibika).

Harun alipoyasikia hayo aliangua kilio na kusema: "kwa hakika umesema ukweli, sasa niombe ombi lako ili nikutimizie."

Bahlul hakuchelewa kusema: "Naomba unisamehee madhambi yangu yote na kuniingiza Peponi."

Harun alimjibu: "Deni haliwezi kulipa deni! Kwani wewe mwenyewe unadaiwa na Umma mzima, hivyo warejeshee mali zao Umma wote. Haipendezi wala kusihi kwangu mimi kupokea mali ya watu wengine waliodhulumiwa."

Khalifa akasema: "Mimi ninatoa amri ya wewe kupatiwa milki na utajiri kiasi cha kukulisha wewe umri mzima ili uishi kwa raha na mustarehe bila ya kusumbuka."

Bahlul alimjibu, "Sisi sote ni viumbe vya Allah s.w.t. na huwa ametupatia sote riziki, sasa itawezekanaje yeye akupe wewe riziki na kunisahau mimi?"

(34). Bahlul Na Sheikh Junaid

Siku moja Sheikh Junaid Baghdadi alitoka nje ya mji wa Baghdad ili kutembea na kutazama mandhari nzuri. Kwa kuwa alikuwa ni Sheikh hodari na maarufu, alifuatwa na wafuasi wake. Sheikh aliwauliza hali ya Bahlul, wao wakamjibu." Yeye ni mtu mwenda wazimu, je unayo kazi gani naye?"

Sheikh aliwajibu: "Niitieni kwani ninayo kazi naye."
Basi watu walitoka kumtafuta Bahlul, walimkuta upweke. Sheikh alifika mbele ya Bahlul.

Sheikh alipomwendea na kumkaribia Bahlul, alikuta ameweka tufali chini ya kichwa akiwa katika hali ya kuwaza. Sheikh alimtolea salaam naye akajibu na akauliza: "Je wewe ni nani?"

Sheikh alimjibu: "Mimi ni Junaid Baghdad."
Bahlul alimwuliza: "Si wewe ndiye Abul Qasini?"
"Naam!" akajibiwa.
Bahlul akamwambia: "Je ni wewe mwenyewe Sheikh Baghdad ambaye unawafunza watu ilimu ya kiroho?"

Sheikh akajibu: "Naam!"
Bahlul akamwuliza: Je wewe wajua namna ya kula chakula chako?"

Sheikh alimjibu: "Mimi husema Bismillah, na hula kile kilicho mbele yangu, huchukua matonge madogo madogo na huweka upande wa mdomo wangu, hutafuna pole pole, huwa sitazami matonge ya wengine. Wakati wa kula huwa ninamkumbuka Mwenyezi Mungu na kila tonge nilalo husema Alhamdulillah na hunawa mikono kabla na baada ya kula."

Kwa kusikia hayo, Bahlul aliinuka aksimama na kwa kukasirika alisema: "Loh! Wewe wataka kuwaongoza viumbe ambapo hadi sasa hata haujui vile ule chakula chako" akasema hayo na akajiondokea.

Wafuasi wa Sheikh wakasema: "Ewe Sheikh! Huyu mtu ni mwehu!"

Sheikh akawajibu: "huyu ni mwendawazimu lakini yupo hofari katika kazi zake. Inatubidi tumsikilize kwa makini kwani huwa anasema maneno sahihi." Naye akaondoka kumfuata Bahlul, akisema "Ninayo kazi naye."

Bahlul alipotokezea katika upweke, aliketi. Sheikh alimwendea. Bahlul aliuliza: "Je wewe ni nani?"

Sheikh alijibu:
"Sheikh Baghdad ambaye hajui hata kula chakula."

Bahlul alimwambia:
"Iwapo wewe hujui kula chakula,basi je unajua namna ya kuzungumza?"

Sheikh alimjibu: "Naam!"
Bahlul alimwuliza: "Je unazungumzaje?"
Yeye alimjibu:"Huwa ninazungumza kwa sauti ya chini, wala sizungumzi pasipo hitajika na wala sizungumzi kupita kiasi. Huzungumza kiasi cha uwezo wa wasikilizaji kunielewa."

Huwalingania watu dini ya allah s.w.t. na Mtume s.a.w.w. Huwa sizungumzi kiasi cha kuchukiwa na wasikilizaji. Huwa mwangalifu ya yale yaliyo dhahiri na bitini." Kwa kifupi, alielezea taratibu zote zihusianazo na mazungumzo.

Bahlul alisema: "Loh! Acha kula usivyojua, hata kuzungumza pia haujui?" Na mara hii tena akaondoka zake baada ya kuyasema hayo.

Wafuasi wa Sheikh walisema: "Ewe Sheikh, je umeona kuwa huyu ni mwenda wazimu tu, sasa waweza kutegemea nini kutoka kwa mwendawazimu huyu?"

Sheikh Junaid akawaambia "Nina kazi naye. Nyinyi hamuwezi kujua."

Tena alimfuata Bahlul, naye akamwuliza: "Mbona unapenda kunifuata niendako, je unanitakia nini? Wewe hujui namna ya kula chakula na wala namna ya kuzungumza, sasa jee wajua namna ya kulala?

Naye akamjibu: "Naam"
Bahlul akamwuliza: "Je ualalaje?"
Sheikh alimjibu: "Baada ya sala ya Isha' na kumaliza shghuli zangu, huanza kuvaa mavazi yaliyotoharika." Alielezea taratibu na desturi zote azijuazo za kulala.

Hapo Bahlul akamwambia: "Mimi nimeshaelewa kuwa wewe hata desturi ya kulala pia haujui."

Na Bahlul alipotaka kuondoka tu, Junaid alimshika na kumwambia: "Ewe Bahlul! Mimi hayo masuala matatu siyajui, naomba kwa jina la Mwenyezi Mungu unifundishe!"

Bahlul alimwambia: "Mimi nimekuwa nikijitenga nawe kwa sababu wewe ulidai kuwa unajua vyote. Lakini kwa kuwa umekiri mwenyewe kuwa haujui, basi sikiliza "haya yote uliyoyazungumza wewe ni maswala ya matawi tu kwani misingi ni kuwa kila tonge lako liwe tonge halali kwani iwapo utatekeleza desturi zote za kula ambapo tonge lenyewe ni haramu basi hakutakufaidia chochote bali kutaongezea kiza moyoni mwako."

Junaid akasema: "Mwenyezi Mungu akujalie malipo mema!" Akaendelea Bahlul: "Katika kuzungumza, kwanza kabisa moyo na nia zinatakiwa ziwe safi na mazungumzo yenyewe yanatakiwa yawe ka ajili ya furaha za Allah s.w.t. Iwapo utazungumza ufidhuli au upuuzi basi kutakuletea madhara tu kwa hivyo, ukimya utakuwa wenye manufaa. Vile vile ulivyozungumzia desturi za kulala pia ni matawi tu."

"Misingi yake ni kuwa unapojitarisha kulala, ni lazima moyo wako usiwe na bughudha, kisasi na husuda dhidi ya Waislamu. Usiwe na tamaa ya mali ya dunia, na unapotaka kulala umkumbuke Allah s.w.t."

Junaid aliubusu mkono wa Bahlul na akamwombea dua njema. Wafuasi walikuwepo hapo wakidhani Bahlul yu mwenda wazimu, walishangaa kuona busara zake.

Kwa hivyo, imetufundisha kuwa iwapo usipojua kitu usiwe na aibu ya kuulizia vile Sheikh Junaid alivyojifunza kwa Bahlul.

(35). Bahlul Na Qadhi

Mtu mmoja alinuia kwenda Hijja msimu huo. Kwa kuwa alikuwa na watoto wadogo wadogo, hivyo alichukua Ashrafi elfu moja akaziweka kwa Qadhi kama amana katika ofisi ya serikali, na akasema: "Iwapo nitakufa huko huko, basi fedha hizi utazisimamia wewe na utakuwa na uwezo wa kuwapatia kiasi chochote utakacho familia yangu amana yangu!

Baada ya kutoka Ofisini mwa Qadhi, aliondoka kwenda Hijja. Alifariki bado akiwa safarini. Watoto wake walipokua na kupata fahamu, walimwendea Qadhi kudai amana ya baba yao. Naye Qadhi akawajibu: "Kwa mujibu wa wasiya wa baba yao aliyoitoa mbele ya watu, mimi ninao uwezo wa kuwapa kiasi nikitakacho mimi. Kwa hivyo nitawapa Ashrafi mia moja tu!"

Watoto hao walianza kuleta vurugu. Hivyo Qadhi aliwaita wale wote waliokuwako wakati akipokea Ashrafi na kuwauliza: "Je mlikuwapo siku ile ambapo baba watoto hawa aliponiachia amana ya Ashrafi elfu moja na kuniambia kuwa niwape tu kiasi nitakacho mimi."

Wale wote waliitikia kuwa hayo ndivyo yalivyokuwa.
Kwa hivyo Qadhi alisema: "Basi mimi sintawapeni zaidi ya Dinar mia moja."

Wale watoto walijuta mno na walianza kuwaambia watu lakini hakuna mtu aliyeweza kupata ufumbuzi kwani lilikuwa swala la sharia. Pole pole na Bahlul akaja akapata habari. Akawachukua wale watoto hadi kwa Qadhi, na kumwambia: "Je kwanini hauwapatii haki yao mayatima hawa?"

Qadhi akamjibu: "Ulikuwa ni wasia wa baba yao kuwa niwape kiasi nitakacho mimi, hivyo sitawapa zaidi ya dinar mia moja."

Hapo Bahlul alimnasa Qadhi na akamwambia: "Ewe Qadhi! Wewe unataka Dinar mia tisa na kwa mujibu wa kauli yako, marehemu alikwambia uwape watoto wake kile kiasi utakacho wewe, na hivyo ni Dinar mia tisa ndizo uwape hawa!"

Qadhi alishindwa mbinu za kuwababaisha wale watoto na hivyo alilazimika kuwapa wale mayatima Dinar mia tisa.

(36.). Swali Kuhusu Mtume Lut A.S.

Watu walimwuliza Bahlul: "Je mtume Lut a.s. alitokana na ukoo gani?"
Alijibu: "Ni dhahiri kwa jina lake kuwa alikuwa ni Mtume wa walawiti na waovu."
Watu wakamwambia: "Kwanini wamwaibisha Mtume wa Allah s.w.t. kwa jibu kama hilo?"
Akawajibu Bahlul: "Mimi sikumsema vibaya mtume, bali nimewaambia kuhusu ukoo wake na hayo ni sahihi."

(37). Swali Kuhusu Sheitan

Mtu mmoja mwovu kabisa alimwuliza Bahlul:
"Mimi nimetamani mno kumwona Sheitan."
Bahlul alimjibu: "Iwapo nyumbani kwako hamna kioo cha kujitazama basi tazama kweye maji safi na yaliyotulia, basi utamwona sheitani."

(38). Bahlul Na Mhudumu

Mhudumu mmoja wa Harun Rashid alikula jibini na ikabakia kidogo katika ndevu zake.
Bahlul alimwuliza: "Je unakula nini?"
Mhudumu alijibu: "Nimemla njiwa>"
Bahlul lalimwambia: "Mimi nilikwishaelewa kabla hata ya wewe kuniambia."

Hapo mhudumu alimwuliza: "Je ulitambuaje?"
Bahlul alimjibu: Ndevuni mwako kuna mabaki ndiyo yaliyonijulisha. "Mimi nilikwishaelewa kabla hata ya wewe kuniambia"

Hapo mhudumu alimwuliza: "Je ulitambuaje?"
Bahlul alimjibu: Ndevuni mwako kuna mabaki ndiyo yaliyonijulisha. "(alimaanisha kuwa alichokula na akisemacho ni vitu tofauti na hivyo amesema uongo!)"

(39). Bahlul Na Harun Wawinda

Siku moja Harun Rashid pamoja na kikundi cha watu wake walikwenda kuwinda. Bahlul pia alikuwamo. Katika tafuta tafuta yao, akaonekana swala mmoja, hapo Khalifa alimlenga mshale, lakini haukumpata yule swala.

Bahlul akasema: "Vyema kabisa!"
Khalifa alinyamaa, na akasema: "Je wanitania? Kwa mzaha huo?"

Bahlul alimjibu: "La hasha! Mimi nimemsifu swala huyo vile alivyoukwepa mshale wako!"

(40). Bahlul Na Mwenye Nyumba

Siku moja Bahlul alikwenda Basara, na kwa kuwa kule hakuwa na mwenyeji hivyo aliweza kukodi chumba kimoja kwa siku kadhaa. Chumba hicho kilikuwa kikuu mno na kulipokuwa kukivuma upepo basi kulikuwapo na sauti.

Bahlul alimwendea mwenye nyumba, akamwambia: "Ewe bwana! Wewe umenipa chumba ambacho kinapovumiwa na upepo basi kuta na dari zake zinaanza kupiga sauti ambazo zinatishia maisha yangu kwani yapo hatarini."

Bwana nyumba alikuwa mcheshi alianza kusema katika kumjibu: "Hapana jambo lolote lililo baya. Wewe watambua vyema kabisa kuwa vitu vyote vinamtukuza Mola na Kumsifu na hivyo ndivyo chumba chako kinavyofanya."

Bahlul alimwambia: "Hayo ni kweli kabisa kwani kila kitu kinamtukuza Mola na hatimaye huangukia kusujudu pi, hivyo mimi nahofu kule kusujudu kwa chumba chako, hivyo itanibidi nihame haraka iwezekanavyo!" (Kusujudu akimaanishi kubomoka).

(41). Khalifa Na Ulevi

Siku moja Bahlul alikwenda kwa Harun na akamkuta Khalifa akiwa katika hali ya kuleva vileo, kwa kuona hayo, Khalifa alitaka kuficha aibu yake isije ikatobolewa nje. Kwa hivyo, alianza kumwuliza Bahlul maswali: "Je kula zabibu ni haraam?"

Bahlul alimjibu: La, si haram."
Khalifa akauliza: "Baada ya kula zabibu, je mtu akinywa maji hukumu yake inakuwa vipi?"

Bahlul alimjibu: "Hakuna kitu!"
Khalifa aliuliza tena: "Iwapo baada ya kula zabibu na kunywa maji, mtu akakaa juani kwa kitambo, je hukumu yake nini?"

Bahlul akamjibu: "Hapo pia hapana kitu."
Hapo Khalifa akanena: "Iwapo Zabibu na maji yakiwekwa juani kwa kitambo, basi itakuwaje haramu?

Basi Bahlul naye pia alimjibu vivyo hivyo: "Iwapo utamwekea udongo kidogo juu ya kichwa cha mtu, jee itamdhuru?

Khalifa alimjibu: "La! Haitamdhuru."
Bahlul aliuliza tena: Iwapo udongo huo huo ukachanganywa na maji, likatengenezwa tofali na hilo tofali akapigwa nalo, je litamdhuru?"

Hapo Khalifa akajibu: "Bila shaka tofali litavunja kichwa chake."

Bahlul alimjibu: "Iwapo udongo ukichanganywa na maji unaweza kuvunja kichwa cha mtu na kuweza kumdhuru ndivyo vivyo hivyo zabibu na maji ikichanganywa itatengeneza kitu tofauti ambacho kimeharamishwa na sheria za Islam na kusema kuwa si toharifu. Kwa kunywa kinywaji hicho kinamletea mnywaji madhara mengi mno na hustahiki adhabu kali mno katika Islam."

Khalifa alistajabishwa mno kwa ufasaha wa Bahlul katika majina yake na papo hapo aliamrisha pombe zote ziondolewe pale.

(42). Bahlul Na Mnajimu

Alikuja mtu mmoja kwa Harun Rashid na akadai kuwa na ilimu ya unajimu. Ikatokea Bahlul kuwapo hapo, na yule Mnajibu akaketi karibu na Bahlul.
Bahlul alimwuliza: "Je waweza kuniambia mtu aliyeketi karibu nawe?"

Mnajibu akasema: "La! simjui,
Bahlul alimwambia: "Si maajabu hayo! Wewe huwezi kumjua mtu aliye karibu nawe, sasa itawezekanaje ukatuambia ukweli kuhusu habari za nyota zilizo mbinguni?"

Mnajimu huyo akanyamaa kwa maneno ya Bahlul na akaondoka kutoka baraza lile.

(43). Bahlul Na Kitabu Cha Falsafia

Ilikuwa ni siku ya Idd, Bahlul alikwenda msikitini alikuta watu wengi mno wameshajazana na hivyo hapakuwa na nafasi na viatu vya kila aina vilikuwa vimezagaa kila mahala. Kwa kuwa alikwisha ibiwa viatu vyake hapo awali, hivyo alihofu kuibiwa safari hii pia, ndivyo maana akatoa leso yake akaviviringishia na alipoingia Msikitini aliketi katika kona moja akiuangalia mno ule mzigo alionao. Ubavuni mwake alikuwapo mtu mmoja ambaye alimwuliza: "Mimi ninadhani kuwa wewe umekichukua kitabu muhimu mno, je kinahusu somo lipi?"

Bahlul alimjibu: "Kitabu cha Falsafia!"
Yule aliuliza: "Je umenunua kutoka duka lipi?"
Bahlul alimjibu: "Nimenunua kutoka duka la mshona viatu!"

(44). Kumwelimisha Punda?

Mtawala wa Kufa aliletewa Punda mmoja mzuri sana kama zawadi. Watu waliokuwapo katika Baraza walianza kumsifu huyo punda, mara mmoja miongoni mwa waliokuwepo, alisema: "Ehee! Mimi nitamuelimisha Punda huyu, hivyo nipo tayari kuwa mwalimu wake."

Mtawala alipoyasikia hayo, alisema kwa furaha: "Maneno hayo aliyoyasema lazima uyatimize na hivyo ukifanikiwa nitakuzawadia utajiri mkubwa na lau utashindwa, basi nitatoa amri ya kuuawa."

Huyo mtu alijutia mzaha wake . Pasi na lingine la kusema au kufanya, aliomba apatiwe kipindi fulani ili aweze kutekeleza hayo. Mtawala alimpa siku kumi tu.

Mtu huyo alimchukua yule Punda akamleta nyumbani mwake. Kwa kweli alikuwa amezongwa na mawazo na kutaabika mno kwani alikuwa haelewi ni lipi la kufanya. Hatimaye alimwacha Punda nyumbani na yeye akaondoka kwenda sokoni. Hapo njiani alikutana na Bahlul na kwa kuwa alikuwa akimjua Bahlul busara zake, hivyo hakusita kumuomba msaada wake katika swala mushkeli kama hilo.

Bahlul alimwambia: "Ndiyo, naam! Mimi ninayo mbinu humo. Utafanikiwa iwapo utatekeleza vile nikuambiavyo."

Bahlul alimwambia: "Usimpe chakula chochote kwa siku nzima. Chukua kitabu kimoja uweke ndani mwake uwele kidogo, na hivyo ndivyo umlishe huyo Punda, kwani atakuwa akila kutoka kitabuni. Na hivyo utekeleze kwa siku zote. Na ikifika siku ya kumi, usimpe chochote, abakie na njaa kali. Hapo ndipo umlete mbele ya mtawala na mbele ya watu wote ukiweke kitabu hicho mbele ya punda bila chalula chochote ndani yake."

Huyo mtu alifanya hivyo hivyo kama alivyoelekezwa na Bahlul. Ilipowadia siku ya kumi, alimwendea Mtawala pamoja na kitabu na Punda na mbele ya wote akamuachia mbele yake Punda kile kitabu. Kwa kuwa punda alikuwa na njaa kali mno, hivyo alianza kufunua kila ukurasa wa kitabu hicho katika kutafuta chakula kama vile alivyokuwa amezoea. Huyo punda alipofikia ukurasa wa mwisho, akaelewa kuwa chakula chake hakikuwapo, na hivyo alianza kulia kwa sauti kubwa akitaka kuwaelezea wote kuwa alichokuwa akitaka ni chakula kwani alikuwa na njaa kali mno, lakini waliokuwapo hapo walidhani kuwa punda analilia kitabu kingine kwani amekimaliza hicho. Kwa kuyaona hayo, Mtawala huyo alijua kuwa kwa kwel i punda amesomeshwa na hivyo anajua kusoma kitabu.

Mtawala alitimiza ahadi yake kwa kumpatia zawadi nono yule mtu hivyo Bahlul alimsaidia asiadhibiwe kwa kuuawa.

(45). Bahlul Na Tapeli

Siku moja Bahlul alikuwa na sarafu ya dhahabu mkononi mwake. Mtu mmoja alipoina, kwa kuwa alijua kuwa yu mwenda wazimu, alimwambia "Nipe, hiyo moja, nami nitakupa sarafu kumi za rangi hiyo."

Bahlul alipoziona sarafu zake, alitambua kuwa zilikuwa ni za shaba ambazo hazikuwa na thamani yoyote ile. Hapo Bahlul alimwambia: "Nitakukubalia iwapo wewe utalia mlio wa punda mara tatu."

Huyo Tapeli alikubali na akatoa mlio kama punda. Hapo ndipo Bahlul alipomwambia: "Nawe ni punda wa ajabu sana, pamoja na kuwa na upunda huu umetambua kuwa sarafu yangu ni ya dhahabu na zile ulizonazo nawe ni za shaba zisizo na thamani yoyote.

Kwa kuyasikia hayo, Tapeli akaondoka zake moja kwa moja.

(46). Ujanja Wa Bahlul

Siku moja mjini Baghdad, mtu mmoja alikuwa akidai kuwa yeye hadi leo hajawahi kudanganyika. Na katika kikundi hicho, Bahlul pia alikuwepo.

Bahlul alimwambia huyo mtu: "Ni kazi ndogo sana lakini kwa wakati huu ninayo shughuli maalum ambapo sina fursa."

Huyo mtu alisema: "Kwa kuwa unajua kuwa wewe hautaweza, hivyo unasingizia shughuli maalum. Hata hivyo, nenda ukimalize shughuli zako na uwahi haraka kwani mimi ninakusubiri papa hapa."

Bahlul alimwambia:
"Ndiyo, nisubiri hapa hapa kwani mimi nitafika sasa hivi."

Kwa hiyo, Bahlul akaondoka zake, na wala hakurudi tena. Hapo nyuma yule mtu alisubiri kwa masaa mawili bila ya dalili zozote za Bahlul kurudi. Alisema akiwa amekasirika:
"Kwa hakika Bahlul ni mtu wa kwanza kuniweka sawa kwani amenikalisha masaa yote bila sababu yoyote."

(47). Uamuzi Wa Bahlul

Mwarabu mmoja masikini alifika Baghdad. Alipokuwa akipita mitaani alikuta duka la kuuza vyakula vya kila aina na alinusa harufu nzuri nzuri za vyakula hivyo, lakini hakuwa na fedha za kununua kwa hiyo aliutoa mkate mkavu aliokuwa nao na akaanza kuupasha moto kwa mvuke wa vyakula vilivyokuwemo ndani ya sufuria.

Mwenye duka akaangalia kwa punde, na mkate ulipokwisha, masikini alitaka kuondoka zake. Hapo mwenye duka alimzuia na kudai malipo, hapo ndipo palipoanza zogo baina yao wakati wakiendelea na zogo hilo, Bahlul alipita hapo, Mwarabu yule alitaka asaidiwe usuluhisho.

Bahlul alimwambia mwenye duka: "Je huyu mtu amekula chakula chako au hakula?
Mwenye duka alijibu: "Chakula hakijaliwa bali bila shaka amefaidika kwa mvuke wake."

Bahlul alimwambia mwenye duka: "Ama hayo ni kweli kabisa, sikiliza!" Huku akitoa sarafu kutoka mfukoni mwake, alizihesabu moja baada ya nyingine na vile vile alikuwa akizidondosha chini zikitoa sauti. Hapo akamwambia mwenye duka: "Chukua sauti hizi za sarafu."

Mwenye duka kwa ajabu alimwambia: "Je huu ni utaratibu gani wa kulipa fedha?"
Bahlul alimwambia: "Kwa mujibu wa uadilifu na uamuzi wangu, mtu ambaye anauza harufu na mvuke bnasi malipo yake ni zile sauti za sarufu."

(48). Bahlul Azuru Makaburi

Bahlul alikuwa akipendelea zaidi kukaa makaburini. Siku moja alipokuwa makaburini, Harun Rashid alifika hapo akienda mawindoni. Alipomfikia Bahlul alimwuliza: "Je Bahlul, wafanya kitu gani hapa?"

Bahlul alimjibu: "Mimi nimekuja kuwaona wale watu ambao hawawasengenyi watu na wasiotarajia chochote na ambao hawawezi kunidhuru chochote."

Harun alisema: "Je wewe waweza kuniambia kuhusu Qiyama, Sirati na maswali yatakayoulizwa kuhusu hii Dunia?"

Bahlul alimwambia: "Waambie wahudumu wako wawashe moto na kuweka kikaangio cha mkate juu ili ipate moto."

Ilipopata moto, Bahlul alisema: "Ewe Harun! Mimi nitasimama juu ya kikaangio hiki nitajitayarisha na nitakutajia kile nilichokula na kile nilichovaa."

Harun alikubali hayo.
Bahlul alisimama juu ya kikaangio kilichopata moto na kwa upesi upesi akaanza kusema: "Bahlul, kilalio, mkate wa mtama na siki!" na alipomaliza, aliteremka chini huku miguu yake haikuungua hata kidogo.

Ilipofika zamu ya Harun Rashid, alianza kujitaarufisha kwa mujibu wa matakwa yake, na kabla haja maliza kujitaarufisha, miguu yake ikaaungua na kumfanya aanguke chini. Alikuwa akijitaarufisha tu na wala hakuanza kuongelea yale aliyokula au kuvaa.

Hapo ndipo Bahlul aliposema: "Ewe Harun! Maswali ya Qiyama yatakuwa hivi hivi. Wale wote watakaokuwa waja wema wa Mwenyezi Mungu, wenye kukinai na wasio na tamaa ya dunia ndio watu watakao pata raha kwa kupita haraka maswali na majibu ama wale wenye kupenda dunia na starehe zake, basi wao watabakia juu ya mtihani huo kwa muda mrefu pamoja na udhia wote."

(49). Bahlul Na Mgeni

Mgeni mmoja alifika Baghdad na alipofika katika Baraza la Harun Rashid, aliuliza maswali mengi mno ambayo mawaziri pamoja na wenye ilimu walishindwa kuyajibu ipasavyo. Kwa kuona hali hiyo, Khalifa alighadhabika mno (kwa kuwa alikuwa ni Khalifa wa Umma, ilimbidi ayajibu maswali yote, badala yake) akatishia kumpa mali ya wote hao, yule mgeni. Lakini wote walimwomba muda wa masaa ishirini na manne(24) , na Khalifa aliwapa muhula huo.

Mmoja wao akasema, "Mimi nadhani tumtafute Bahlul ambaye ndiye pekee atakayeweza kutoa majibu sahihi ya mgeni huyo."

Hivyo walimtafuta Bahlul na kumwelezea yote yaliyotokea. Bahlul alikubali kumjibu mgeni, naye atafika hapo. Alimwelekea mgeni akisema: "Maswali unayoyapenda, unaweza kuyauliza, mimi nipo tayari kukujibu."

Mgeni huyo aliinua fimbo yake na akachora duara moja, kisha akamtazama Bahlul. Na Bahlul bila ya kusita akachora mstari katikati ikigawa katika sehemu mbili sawa.

Mgeni akachora duara nyingine, na Bahlul akaigawa katika sehemu nne, na alimwambia mgeni kuwa: "Sehemu moja ni kavu wakati sehemu tatu zilizobakia ni maji."

Mgeni alitambua kuwa Bahlul alkwishamjibu ilivyo sahihi kabisa, hivyo alimsifu Bahlul mbele ya wote.

Baada ya hapo, mgeni huyo akakiweka kiganja cha mkono wake kwa kugeuza juu ya ardhi huku akiinua vidole vyake kuelekea mbinguni.

Bahlul alifanya kinyume na vile alivyofanya yaani vidole vikaelekea chini ardhini na mkono wake chini. Kwa hayo Mgeni alimsifu mno Bahlul mbele ya Khalifa, akisema: "Lazima uwe na fakhari kwa kuwa na mwenye ilimu kama Bahlul."

Khalifa kauliza: "Mimi sikuelea maswali hayo wala majibu yake."

Hapo mgeni alianza kumjibu: "Kuchora kwangu duara na Bahlul kugawa ni kuelezea kuwa dunia imegawanyika katika sehemu mbili- Kaskazini na kusini. Na mduara wa pili, ulielezea kuwa dunia ina sehemu nne ambayo Bahlul alimchorea mistari miwili. Sehemu moja ardhi kavu wakati sehemu tatu ni maji. Na niligeuza viganja vyangu na vidole juu kulimaanisha kuota mimea na majani.

Na Bahlul alifanya kinyume na vile nilivyofanya mimi akimaanisha kuwa miti na mimea huhitaji mvua na miale ya jua. Kwa hakika kunatakiwa kufanya ufakhari kwa kuwa na mtu hodari kama Bahlul!"

Watu wote walimshukuru Bahlul kwa kuwasaidia na kubakiza heshima yao na kuponea chupuchupu adhabu za Harun Rashid.

(50). Bahlul Aenda Bafuni

Siku moja Bahlul alikwenda bafuni (bafu za kulipia fedha ) na huko wahudumu hawakumjali ipasavyo bali walimdharau tu. Lakini yeye alioga na alipotoka nje akaenda moja kwa moja kwa mwenye mali, akampa Dinar kumi.

Wahudumu walipoona hayo, walijuta mno kwani wangalipatapo chochote kama bakhshishi yao.

Juma lililofuatia, tena alikwenda bafuni kuoga. Safari hii wahudumu walimkaribisha vyema na kumpa kila aina ya huduma ipasavyo. Alipomaliza kuoga, aliwapa wahudumu Dinar moja tu. Hao walimwuliza kwa hasira: "Loh! Juma lililopita bila ya huduma zozote ulilipa Dinar kumi na leo vipi baada ya huduma zote hizo unatoa Dinar moja tu.?"

Bahlul aliwajibu: "Malipo ya leo nilikuwa nimeshalipa wiki iliyopita, hivyo ninatoa Dinar moja tu ili mjue, muwe daima mukikwahudumia wateja wenu vile iwapasavyo bila ya kuweka tamaa mbele."

(51). Bahlul Na Mzozo Wa Kuku

Siku moja mfanyabiashara mmoja kutoka Bara Hindi alileta mali huko Baghdad na alipofika wakati wa njiani alibakia pamoja na msafara, na aliagiza chakula kwa mpishi mmoja, aliletewa kuku na mayai machache yaliyochemshwa. Baada ya kulala alipoamka alikuta msafara umeishaondoka na hivyo hakuweza kumlipa mpishi fedha za kuku na mayai.

Baada ya mwaka mmoja kupita ikatokea kuwapo papo hapo, aliagiza chakula cha jioni. Mpishi alimletea vile vile yaani kuku na mayai machache yaliyochemshwa. Kulipokucha alimwita mpishi, na kumwambia: "Mimi unanidai deni la mwaka jana la kuku na mayai machache. Naomba unipatie hisabu hiyo na ya leo ili niweze kukulipa kwa pamoja."

Mpishi, baada ya kupiga mahesabu yake kwa makini, alimwambia mfanyabiashara amlipe Dinar elf moja. Mfanyabiashara huyo aliposikia chakula cha jioni kugharimu Dinar elfu moja, alichukia na kusema: "Mimi nadhani kuwa wewe umewehuka kwa kudai Dinar elfu moja za kuku mawili na mayai machache."

Mpishi alimjibu: "Loh! Unathubutu kuniambia mwehu huku mimi nimepiga mahesabu yangu kwa uangalifu ili nisije kukudai zaidi hata chembe kidogo?"

Mfanyabiashara akasema: "Mimi nashukuru mno lakini umefikiaje kiasi hiki cha madai?"

Mpishi akamjibu: "Tafadhali zingatia kwa makini kabisa nikuambiayo. Gharama hiyo ninayokudai imetokana na wewe kula kuku na mayai sita hapo mwaka jana.

Iwapo kuku huyo angalikuwa hai basi mayai hayo angalilalia na hivyo angaliangua vifaranga. Na kila kifaranga angalitaga mayai kama hayo na vifaranga. Kwa hivyo, mimi ningalimiliki maelfu ya mayai na vifaranga, lakini yote hayo, nimekuachia wewe waniambia kuwa mimi ni mwendawazimu!"

Wasafiri wote katika msafara walivutiwa na ugomvi huo, nao walifanya kila jitihada katika kuwanyamazisha na kuwasuluhisha lakini ilishindikana. Hatimaye ilifikiwa kuchukua hatua za kwenda mbele ili kupatia ufumbuzi wa maswala hayo.

Mshauri alipoelezwa habari kwa ukamilifu, alitoa uamzi: "Ewe mfanyabiashara! Unatakiwa kumlipa mpishi huyu Dinar elfu moja."

Kwa hayo, mfanyabiashara alihangaika na kubabaika kwani hakuelewa lipi la kufanya. Mmoja wa wasafiri, alikuwa ni rafiki yake Bahlul na alitambua kuwa ufumbuzi wa haki unaweza tu kutolewa na Bahlul. Basi aliwaambia: "Enyi wenzangu! Kutoka hapa hadi Baghdad si mbali na hivyo nitawaletea Qadhi wa Baghdad ili tupate hukumu yake katika swala hili. "Aliondoka mbio akimtafuta Bahlul, na alimkuta katika msikiti mmoja ambapo alimwelezea habari zote.

Alirudi pamoja na Bahlul hadi msafara huo. Walipoukaribia ule msafara, Bahlul alimwambia yule mtu "Wewe tangulia, nami ninakufuata kwa miguu na vile vile uwaambia kuwa mimi nitafika baada ya nusu saa hivyo wanisubiri. Qadhi ameahidi, atafika tu!"

Huyo mtu aliwaambia hivyo hivyo,na watu wote walianza kupima kila dakika. Ilipofika nusu saa wakaona bado Qadhi hajafika, alifika baada ya saa moja na nusu na kila mmoja alisimama kutoa heshima zake. Aliketi na kuwaambia kuwa amekwisha pata habari za mgogoro wa mfanyabiashara na mpishi. Alisema: "Mimi naomba msamaha kwa kuchelewa kwani nilikuwa nikikoboa ngano, kwani ngano iliyokobolewa inaota vizuri zaidi na hivyo nilishughulishwa na hayo."

Wote waliokuwapo walianza kusema: "Huyu Qadhi ni mtu wa ajabu kwani anakoboa ngano kabla ya kupanda shambani."

Bahlul aliwajibu: "Kwani nini mumestaajaabishwa kwani kwenu hapa kuku aliyepikwa pia huweza kutaga mayai."

Mshauri alisema: "Qadhi huyu amesema yaliyo sahihi kwani kuku aliyepikwa hatoi vifaranga!"
Hatimaye, watu waliafikiana neno kwa kumpa fedha za kumridhisha yule mpishi. Nao wote wawili walikumbatiana kwa kufurahi.

(52). Harun Ajenga Jumba La Kifalme

Harun alijijengea jumba la kifalme, na ilipokuwa tayari, siku moja alikuwa darini akiangalia mandhari yaliyomzunguka. Mara alimuona Bahlul akiangalia jengo hilo jipya.

Harun alimwita kwa kusema: "Ewe Bahlul! Ninalo ombi, je unaweza kuniambia maneno mazuri mno kwa ajili ya Jumba hili langu la kifalme?"

Bahlul alitafuta mkaa na aliandika kwa haraka juu ya ukuta wa Jumba hilo maneno yafuatayo: "Umeinua ardhi ambapo umeipotosha Din. Iwapo umeijenga kwa fedha za Umma, basi kwa hakika umedhulumu na kwa hakika Mwenyezi Mungu hawapendi madhalimu."

(53). Ulipaji Wa Deni.

Mtu mmoja alinuia kumchokoza Bahlul katika imani yake kuhusu Imam al-Mahdi (a.f.) na kudhihiri kwake ili kueneza utawala wa haqi na uadilifu duniani kote.

Katika kikao kimoja ambapo na Bahlul pia alikuwapo, alisema: "Ewe Bahlul! Je si wewe unaitakidi kuwa Imam wako wa 12 al-Mahdi (a.f.) atadhihiri katika zama za mwisho wa dunia na ataleta utawala wa haki na uadilifu? Iwapo wewe u-thabiti juu ya itikadi hii basi nikopeshe dinar mia tano ambazo nitakupa wakati Imam wako atakapodhihiri."

Bahlul alimjibu: "Bila shaka hiyo ndiyo itikadi na Imani yangu na niko tayari kukukopesha hivyo lakini ni lazima unihakikishie kuwa wewe hautakuwa umegeuzwa kuwa mbwa au nguruwe! Iwapo utageuzwa, basi nani atakayelipa?"

Kwa kusikia hayo wote waliokuwapo wakaangua kicheko na yule mchokozaji akabung'aa asiwe na la kusema. Bahlul alijiondokea.

(54). Bahlul Na Mafuvu Ya Kale

Siku moja Bahlul alikuwa amekaa makaburini akiwa na fimbo ndefu, huku akichunguza mafuvu mengi ya vichwa vya zamani yaliyokuwa yametawanyika hapa na pale. Harun Rashid alipita hapo na kumwona Bahlul akichunguza mafuvu hayo, Alisema: "Ewe Bahlul! Wafanya nini?"

Bahlul alimjibu: "Najaribu kutambua kama mafuvu haya ya vichwa ni ya wafalme au ni ya mafukara, kwani yote nayaona sawa!"
"Na hiyo fimbo ni ya nini?" aliuliza Harun.
"Naipimia ardhi." alijibu Bahlul.
Alianza Harun kwa kudhihaki: "Je unapima ardhi, hoja gani?"
Bahlul alimjibu: "Ewe Harun! Urefu wa mikono mitatu kwangu mimi ijapokuwa mimi ni masikini ni sawa na mikono mitatu kwangu kwako wewe ijapokuwa una fahari na mali!" (Yaani wote wanaingia katika kaburi la vipimo sawa hakuna ubaguzi wa tajiri kupewa pana au masikini kupewa finyo!)

55. Bahlul Kufikisha Salaam

Bahlul alipokuwa katika hali ya ufukara, basi hakuna mtu aliyekuwa akimsalimia. Lakini baada ya kipindi kupita, alijipatia mali na hivyo akawa ni miongoni mwa matajiri. Hapo kila mtu akimwona anmtolea salaam: “Bwana Bahlul Salaam ……” Basi hapo Bahlul alikuwa akiwajibu: “Ndiyo bwana, salaam zako nitazifikisha ….” Na hivyo alikuwa akijiondokea.

Siku moja, mtu mmoja alijikaza na kumwuliza Bahlul tafsiri ya majibu atoayo wakati anaposalimiwa. Bahlul alimwelezea : “Mimi nilipokuwa fukara, hakuna aliyekuwa akinisalimia…. Na sasa kwa kuwa nimepata mali, basi nyote mwanijia mbio kunitolea salaam…… mimi ni yule yule Bahlul, kamwe sijabadilika vyovyote vile. Hivyo ninaamini kuwa ni mali yangu ndiyo itolewayo salaam… na ndiyo maana mimi ninaporudi nyumbani mwangu huenda katika hazina ya mali yangu na kuzifikisha salaam zenu mulizonitolea.”

Kwa kuyasikia hayo, bwana huyo alijiondokea kimya huku akikiri aliyoyatambua Bahlul.