read

6. Matumizi Ya Zaka

Amesema Allah (swt) katika Quran: Surah al – Tawbah, 9, Ayah 60:
“Wa kupewa Sadaqah ni mafakiri, na masikini, na wanaozitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Allah (swt), na wasafiri. Huu ni wajibu uliofaradhiwa na Allah (swt) . Na Allah (swt) ni Mwenye kujua Mwenye hikima.” (9:60)

Mali ya Zaka inaweza kugawiwa sehemu nane kama ilivyoelezwa katika ayah hii ya Qur'an Tukufu :
1. Fakiri

Ni mtu yule ambaye yeye hana uwezo wa kujilisha yeye pamoja na familia yake kwa muda wa mwaka mzima. Ambaye kwa hakika hana uwezo wa kurejesha sasa hivi au hata hapo mbeleni. Lakini yule mtu ambaye anamiliki majengo, milki au mali haitwi fakiri.
2. Masikini

Ni yule ambaye hali yake ni ngumu kuliko hata fakiri.
3. Wanaozitumikia

Ni mtu yule ambaye anakusanya Zaka kwa niaba ya Al-Imam Muhammad Mahdi, sahibuz-zamaan, (a.s) na kumfikishia Naibu wa Imam (a.s) au wanaostahiki.
4. Wa kutiwa nguvu nyoyo zao

Ni Waislamu wale ambao imani zao ni dhaifu hivyo kwa kuwasaidia na kuwapa nguvu kimaisha.
5. Kukomboa watumwa

Kutumia mapato ya Zaka kwa ajili ya kumfanya huru mtumwa ambaye yupo katika hali ya kuteswa mno au kumnunua na kumfanya awe huru
6. Wenye madeni

Kuwasaidia mapato ya Zaka wale wasiojiweza kulipa madeni wanayodaiwa.
7. Njia ya Allah (swt)

Mapato ya Zaka yanaweza kutumia katika kila shughuli zenye kuifaidisha Dini mfano ujenzi wa Misikiti au Madrassah ili Waislamu waweze kufaidika kwa kufanyia ‘ibada na vile vile kutolewe mafunzo ya Dini , au kutengeneza madaraja au kusuluhisha makundi mawili au watu wawili waliotafarukiana au kusaidia katika ‘ibada, n.k.

8. Wasafiri :

Kumsaidia msafiri ambaye amekumbwa na matatizo akiwa safarini ambaye hawezi kuchukua deni au kuuza kitu alichonacho kwa ajili ya kurudi nyumbani kwake hata kama yeye hatakuwa fakiri nyumbani kwake.