read

9. Khums

Baada ya Zaka iliyofaradhishwa inakuja Khums iliyofaradhishwa ambayo Allah (swt) amewawekea kwa ajili ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w). pamoja na Ahlul Bayt (a.s), ambapo Zaka kwao ni haramu. Na iwapo mtu yeyote hatalipa Khums hata kwa Dirham moja au chini yake, basi huyo atakuwa ni mdhulumaji wa haki ya watajwa hapo juu. Na iwapo atajihalalishia kwa ajili yake mwenyewe na kukataa kutoa khums, basi naye pia atakuwa miongoni mwa Makafiri kwani hali kama hizo zimekwishaelezwa kwa undani katika kurasa zilizopita lakini katika Qur'an Tukufu imeelezwa kuwa ni shuruti la imani juu ya Allah (swt) kama vile Allah (swt) anavyotuelezea katika Sura al-Anfaal, 8, Ayah 41:

“NA JUENI ya kwamba ngawira mnayoipata, basi khums (sehemu moja katika tano) ni kwa ajili ya Allah (swt) na Mtume, na jamaa, na mayatima, na masikini, na wasafiri, ikiwa nyinyi mmemuamini Allah (swt) na tuliyoteremsha kwa mja wetu(Muhammad) siku ya kipambanuo (katika Vita vya Badr), siku ( Waislamu na Makafiri ) yalipokutana majeshi mawili. Na Allah (swt) ni Muweza wa kila kitu.” (8:41)

Al Imam Ja'afer as-Sadiq (a.s) amesema, katika Man la yahdhurul Faqihi, J.2, uk.41:
“Kwa kuwa Allah (swt) ametuharamishia Zaka sisi Ahlul-Bayt (a.s)hivyo ametuwekea Khums kwa ajili yetu na hivyo Sadaqah pia ni haram kwetu na zawadi imeruhusiwa kwa ajili yetu.”

Al Imam Muhammad al-Baqir (a.s) amesema, katika Usuli Kafi, J. 1, Uk.545:
“Hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kununulia chochote kutoka kifungu ambacho Khums haijalipwa na hadi pale wasipoifikisha kwa wanaostahiki kwetu.”

Vile vile Al Imam Muhammad al-Baqir (a.s) amesema, katika Al-Kafi, J.1, Uk. 546:
“Siku ya Qiyamah wakati ule utakuwa mgumu kabisa pale wanaostahiki Khums watakapotokezea kudai haki zao kutoka wale wasioilipa.”

1. Kuongezeka Kwa Neema Na Kutoharisha Mali

Miongoni mwa marafiki tajiri mmoja kutokea Uajemi alimwandikia barua Al-Imam ‘Ali ar-Ridha (a.s) na alimwomba Imam (a.s) ruhusa ya kuitumia mali ile ambayo khums haijatolewa. Basi Imam (a.s) alimwandikia majibu kama ifuatavyo :
Imenakiliwa kutoka Al-Wafi, Al-Kafi na Tahdhib
“Bila shaka Allah (swt) ni Wasi’ na Mkarimu na amechukua dhamana ya kumlipa thawabu na malipo mema yule mtu ambaye atatekeleza hukumu zake na ameweka adhabu kwa yeyote atakayekwenda kinyume ya hayo. Bila shaka mali iliyo halali kwa ajili ya mtu ni ile ambayo Allah (swt) ameihalalisha na kwa hakika Khums ni dharura yetu na ni hukumu ya Dini yetu na ni njia ya kujipatia kipato kwa jili ya riziki sisi na wenzetu na imewekwa kwa ajili ya kulinda hishima zetu dhidi ya wapinzani wetu. Hivyo kamwe musiache kutoa na kulipa Khums. Na kila inapowezekana kusijikoseshe Du’a zetu na kwa hakika kwa kutoa Khums kunazidisha riziki yenu na kutoharisha na ni hazina kubwa kwa ajili ya Siku ile ambayo kutakuwa na taabu tupu na mateso (Siku ya Qiyamah. Na kwa hakika Mwislamu sahihi ni yule ambaye amemwahidi Allah (swt) kwa ahadi na ‘ibada, basi atimize kwa ukamilifu. Na iwapo atakubali kwa mdomo tu ilhali moyoni anakataa na kupinga basi atambue kuwa yeye si mwislamu.”

Al-Imam Muhammad Mahdi, sahibuz-zamaan, (a.s) kwa kupitia Naibu wake makhsusi Muhammad bin ‘Uthman , alimwandikia barua Abul Hasan Asadi, kama ifuatavyo, katika Akmalud-Diin Saduq, Mlango Tawqi’at, Uk. 563 :
“Bismillahir Rahmanir Rahiim.
Allah (swt) , Malaika na watu wote wanamlaani mtu yule ambaye anajihalalishia hata kwa Dirhamu moja kutoka haki yetu.”

Kwa kusoma barua hiyo Abul Hasan Asadi anasema :
“Mimi nilifikiri kuwa mtu yeyote anayjihalalishia kwa kuila mali ya Imam (a.s) (na wala si yule mtu ambaye anaila bila kujua kuwa kujihalalishia na katika maharamisho yote ya hukumu za Allah (swt) ni kwamba kuhalalisha kile alichokiharamisha Allah (swt) , basi mtu huyo atakuwa mustahiki wa laana hizo zote, na hivyo kwa misingi hiyo hiyo hakuna tofauti baina ya hukumu zingine na ile ya kula mali ya Imam (a.s))

Lakini kwa kiapo cha Allah (swt) ambaye amembashiria Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w). ! Mie nimeona katika yale yaliyokuwa yameandikwa katika barua hiyo ya Imam (a.s) na nikashtuka mara moja na kwa hakika madhumuni ya barua hiyo ilikuwa ni yenye maana kuwa Allah (swt) pamoja na Malaika na watu wote wanamlaani yule mtu ambaye anaila hata Dirhamu moja kutoka mali yetu (haki yetu sisi Saadat). Hata kama hatakuwa akidhani kuwa ni halali kwa ajili yake.”

Pamoja na hayo zipo hukumu za Khums zipo riwaya nyingi mno.

2. Khums Iliyofaradhishwa, Aina Na Matumizi Yake

Khums imefardhishwa katika vitu saba :
1. Ngawira (mali inayopatikana vitani kwa kushinda)

2. Hazina inayopatikana kwa kutumbukia majini

3. Hazina

4. Faida itokanayo na biashara

5. Mali halali iliyochanganyikana na mali haramu na kiasi chake kisijulikane.

6. Ardhi ile ambayo Kafiri Dhimmi anainunua kutoka Mwislamu.

7. Madini kama dhahabu, fedha, chuma, shaba, mafuta, Firozah, ‘Aqiiq, chumvi n.k.

Kila kifungu kina hukumu zilizoelezwa kwa marefu na mapana katika vitabu vya Fiq-hi.

Khums inatakiwa kugawiwa sehemu mbili:
1. Sehemu ya kwanza ni haki ya Saadat ambao ni masikini, mafukara au ambaye ameishiwa katika safari

2. Sehemu ya pili ni ya Al-Imam Muhammad Mahdi, sahibuz-zamaan, (a.s) ambaye kwa sasa yupo ghaib na hivyo kumfikishia Naibu wake ambaye ni Mujtahid Jame’ Sharait au kutumiwa katika kazi ambazo Mujtahid Jame’ Sharait ameruhusu.

Katika kitabu cha Kalimat Tayyibah kumeandikwa hekaya zaidi ya arobaini ambazo zinaonyesha namna ya kufanya uwema pamoja na Saadat na faida zilizopatikana kwa kufanya mapenzi na meam pamoja nao. Sisi tunawaleteeni hekaya moja ambayo imenakiliwa kwa kupitia mifululizo mingi ya walioyoifikisha katika Muntakhab Ad-diin, Kitabu fadhail Shaadhaan na Tohfatul Azhar na wasilatul al-Mal kuwa:
‘Ibrahim bin Mahran kwamba katika mji wa Kufah kulikuwa na jirani yangu aliyekuwa akiitwa Abu Ja’afar, mtu mwenye heshima kubwa sana. Kila Sayyed aliyekwenda kwake kumwomba chochote, yeye aliwapa na alipolipwa alipokea na pale ambapo alikuwa halipwi, alikuwa akimwambia karani wake aandike kuwa Al Imam 'Ali ibn Abi Talib (a.s) amekopa kiasi hicho. Hivi ndivyo ilivyokuwa ikiendelea kwa muda mrefu, na kwa bahati mbaya ulimwijia wakati mbaya ambapo yeye alifilisika na kuwa fakiri.

Siku moja alipokuwa amekaa nyumbani kwake huku akiangalia daftari lake la madeni aliyokuwa akiwadai watu. Kwa kila jina la mtu aliyekuwa hai, alimtuma karani wake kwenda kufanya madai na kwa yule aliyefariki, iwapo ameacha mali, basi aliwaomba jamaa wamlipe. Na kwa yule ambaye hana arithi wala hakuacha chochote cha kuweza kufanya madai yake, yeye alikuwa akichora mstari.

Katika siku hizo hizo, siku moja alipokua ameketi nje mlangoni mwake huku akiliangalia daftari lake la madeni, kulipita mpinzani wake mmoja ambaye alimdhihaki kwa kumwambia,”Je Al Imam 'Ali ibn Abi Talib (a.s) amekufanyiaje, je amekulipa madeni yako?”

Kwa kuyasikia hayo, alihuzunika mno na akaondoka zake. Basi usiku huo alimwota Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w). akiwa pamoja na Al-Imam hasan (a.s) na Al-imam Hussayn (a.s) katika ndoto yake. Mtume (s.a.w.w). aliuliza ‘Je baba yenu yuko wapi? Al Imam 'Ali ibn Abi Talib (a.s) ambaye alikuwa yupo nyuma ya Mtume (s.a.w.w). alijibu. ‘Naam, nipo hapa.Ewe Mtume wa Allah (swt)!’

Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w). alimwuliza Al Imam 'Ali ibn Abi Talib (a.s), “Je ni kwanini haumlipi huyu mtu haki yake?”

Al Imam 'Ali ibn Abi Talib (a.s) alijibu’ “Ewe Mtume wa Allah (swt)! Mimi nimemletea haki yake yote.”

Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w). akamwambia, “Basi mpe achukue.”

Al Imam 'Ali ibn Abi Talib (a.s) alitoa mfukoa mmoja mweupe na kumpa huyo mtu na kumwambia, “Hii ndiyo haki yako.”

Hapo Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w). akasema, “Pokea haki yako na siku yoyote utakapoijiwa na watoto wake kwako kwa kukuomba chochote, na unacho basi uwape na kamwe usiwanyime. Nenda kamwe hautakuwa na shida wala dhiki ya aina yoyote ile.”

Mtu huyo analezea kuwa alipofumbua macho yake kutoka usingizini, aliukuta mfuko ule ule ukiwa mkononi mwake na alimwamsha mke wake na kumwambia awashe taa. Anasema, “Nilipofungua mfuko huo, kulikuwa na Ashrafii elfu moja kamili.” Mke wangu aliniambia kuwa inawezekana mimi nimekopa mali hiyo kutoka kwa matajiri, nikamwambia kuwa sivyo na hapo nilimsimulia kisa kizima. Baadaye nilikichukua kidaftari changu na kuanza kupiga hisabu ya deni la Al Imam 'Ali ibn Abi Talib (a.s) ambalo nilikuwa nikiwapa Saadat na nikakuta kuwa jumla yake imekuwa ni Ashrafii elfu moja kamili kama alivyonilipa Al Imam 'Ali ibn Abi Talib (a.s) Hakukuzidi wala kupungua!