Utangulizi

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Namshukuru Mwenyeezi Mungu ambaye nyoyo zamtambua kwa utukufu Wake, maozi hayamuoni na mawazo hayashibishi sifa Zake.

Namshukuru kwa neema Zake pindi alipotuletea Mtume Wake wa mwisho kwetu, Muhammad (s.a.w.w) aliyetusomea dalili Zake na kututakasa na itikadi chafu chafu na pia akatufunza Qur'ani na Hikima.

Mwanadamu mara humkosea Mwenyeezi Mungu na kuidhulumu nafsi yake hadi kwamba moyo ukafunga kiza akili ikakosa mizani na nafsi kwa inda amba dhambi si makosa! Kwa msingi huu mwanadamu huhitaji wasila kumfikishia kilio chake na maombi yake kwa Mwenyeezi Mungu. Dua ndiyo wasila wakutuunganisha na radhi za Mwenyeezi Mungu (s.w.t.).

Dua ni ulingano ambapo mja hudhihirisha ufukara, unyonge na udhaifu wake kwa Mola Mkwasi, Mwenye kumiliki kila kitu. Mja huinyosha mikono yake mitupu kwa unyenyekevu na unyonge, na kutaka msaada kutoka kwa Mkamilifu Muumba Mwenye uweza juu ya kila kitu, Mwingi wa huruma na ukarimu, Mwenye busara Mjuzi kwa kila jambo, Mwenye kusikia maombi ya kila anaemuomba. Dua ni lugha ya mapenzi na ni chimbuko la mahaba ya mja kwa Mola wake na ndiyo taa ya waliyokizani na ni tulizo la wanaohangaika.

Twasoma katika Qur'ani tukufu:-

"Asema Mola wenu: niombani nitawajibu, hakika wale wajivunao kufanya ibada yangu, bila shaka wataingia Jahannamu, wadhalilike” (Al-Mu'minuun 60).

"Sema: Mola wangu asingewajali lau sikule kumuomba kwenu" (Al-Furqaan 77)

"Na pindi waja wangu wakuulizapo hakika yangu, Mimi nipo karibu, najibu maombi kila anaeniomba nao waitikie mwito wangu na waniamini mimi huenda wakaongoka”. (Al baqara 186)

Namshukuru Mwenyeezi Mungu aliyenipa uweza wa kuifasiri dua hii maarufu kwa jina la Kumayl. Dua hii ilisikika mara ya kwanza, ikisomwa kwa sauti nzuri ya kusisimua na kuhuzunisha kutoka kwa Amirul Mu'minin Imam Ali Ibni Abi Twalib (a.s.).

Kumayl Ibni Ziyaad (r. a.) amesema "Nilikuwa nimekaa na Amiril Mu'miniin katika msikiti wa Basra pamoja na jamaa katika swahaba zake, akizungumzia juu ya tarehe 15 ya mwezi wa Sha'bani, akasema 'Hawi mja yeyote atakae kuukesha usiku huu na akaomba kwa dua ya Khidhri, maombi yake yatajibiwa'".

Katika kuifasiri kwangu niliipanga kwa vifungu ili kukidhi haja za wasomaji wa makamo mbalimbali ya kiroho, na kwa wengine kuwapa fursa ya rakizi kwa utulivu wanayo ya tamka.

Na nawashukuru ndugu walionipa moyo kuifanya kazi hii na kwa fikra walizochangia za kilugha au za uwandishi. Ewe Mola mrehemu Muhammad na aali zake utupe usuhuba wake mzuri na utulinde tusitengane naye hapa duniani na kesho Akhera.

Na kwa wazazi na wazee pamoja na ndugu waliyoniongoza na kunitakia mema nawaombea maghofira kutoka Kwako Ewe Mola.

Mwenyeezi Mngu atutakabiliye amali zetu sote pia.

Sayyid Ahmad Aqyl.