read

3. Historia ya Uandishi wa Hadith Katika Sunni:

Kazi zote zilizopo hadi leo zinazohusu Hadith zilikuwa zimekusanywa katika kipindi cha karne 2 A.H./8 A.D. au katika karne ya 3 A.H./9 A.D. Historia inatuonyesha kuwa katika kukaribia karne ya 2 A.H. kulitokezea idadi ndogo ya Muhaddithun ambao walianza kuziandika Hadith, ingawaje hazikuwa na mpangilio. Baadaye mkusanyiko huu mdogo ulikuwa kiini cha kazi zote kubwa. Hata hivyo wingi wa Hadith zilizopo sasa kwa kukusanywa, zilienezwa kwa desturi ya kutamkwa (kusemwa), na wakati zilipokuja kuandikwa vitabuni, zilikuwa hazikuwahi kuandikwa popote kabla yake.

Ucheleweshwaji katika kuandikwa kwa Hadith ni swala mojawapo muhimu katika historia ya Hadith. Umuhimu wake ni wa ukweli kwamba kucheleweshwa huu kuliathiri hasa kuhusu utunzi na idadi ya Hadith pamoja na uwepesi wao wa kuzushwa (zikaongezwa na kupunguzwa na hatimaye zikawa ni zile zilizo na uongo) na matatizo mengi mengineyo yanayohusiana.

Jambo la umuhimu katika swala hili linawahusu wale ambao ndio waliokuwa wamesababisha ucheleweshwaji huo wa kuandikwa kwa Hadith. Mwelekeo wao ulikuja kama ni mfano kwa ajili ya wengine katika kutoziandika Hadith. Katika sehemu yetu hii, tutaweza kuchambua makusudio yao na athari za mwenendo wao wa aina hiyo juu ya Hadith.

Kila kinachoweza kukusanywa kwa shida katika Historia ni kwamba baadhi ya Makhalifa walizuia uandikaji wa Hadith kwa sababu fulani fulani. Baada yao kikundi cha Sahaba na Tabiun waliwafuata katika swala hili. Kwa mujibu wa msemo "Watu hufuata dini ya wafalme wao," wao walijiepusha na uandikaji wa Hadith kwa kukubali na kuridhia kwa kuharamishwa hivyo.

Wao walizihifadhi Hadith za Mtume s.a.w.w. kwa kuzikariri tu (kwa kuzihifadhi akilini mwao tu). Kama vile tutakavyoona hapo mbeleni, wao nyakati zinginezo walijaribu kurejea katika kuziandika, ili kuyateketeza maandishi yao katika kipindi cha mwisho wa maisha yao, kama kwamba maandishi hayo yaliwasaidia wao tu katika kuhifadhi kwao. Kumbukumbu hizo za Hadith zilizokuwa zimeandikwa hazikutumiwa kwa kutaka kuzihifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo. Ni jambo la kuvutia sana kuona kuwa kupigwa marufuku wa uandikaji wa Hadith katika Sunni ulitolewa na watawala wao; na vile vile ile amri ya kuziandika Hadith pia zilitolewa na watawala wao.

Al-Zuhri anasema:

"Sisi tulikuwa tukichukia mno uandishi wa elimu, hadi hapo wakuu wetu walipotulazimisha kuyaandika hayo. Hapo baadaye tulikuja kugundua kuwa hapakuwapo na yeyote miongoni mwa Waislam waliopinga."

Al-Zuhri anaendelea kusema:

"Wafalme waliniambia kuandika elimu ('ilm, yaani Hadith) kwa ajili yao. Baada ya kuwaandikia kwa muda fulani, mimi nilishikwa na aibu mbele ya Allah swt; (mimi nilijiuliza): Je, kwa nini nimejitayarisha kwa ajili ya kuwaandikia wafalme na wala si kwa ajili ya watu wengineo!?" 1

Ni dhahiri, kama vile itakavyokuja kuonekana kwamba Hadith hazikuwa ni kweli kwa ajili ya Sahaba na Tabiun wote. Wengi wao na akiwemo ‘Ali ibn Abi Talib a.s. waliziandika Hadith na vile vile waliwaambia wengine kufanya hivyo. Wengine walianza kuziandika Hadith wakati sheria zilizowekwa na Makhalifa juu ya kutoziandika Hadith zilipobadilishwa na amri ya Kikhalifa kutoka kuziandika Hadith.2

'Umar ibn Abd al-Aziz (101 A.H./719 A.D.) ndiye aliyekuwa Khalifa wa kwanza kuamrisha wanazuoni wa miji mbalimbali kuziandika Hadith na kumpelekea huyo Khalifa maandishi yote. 3 Imeripotiwa kuwa Khalifa alimwandikia Muraah ibn Kathir akimwomba amwandikie Hadith za Mtume s.a.w.w. 4 Vile vile yeye alimwandikia Abu Bakr ibn Muhammad Hazm: "Andika Hadith yoyote ile ya mtume s.a.w.w. uliyonayo na kunitumia na chochote kile kilichonakiliwa kutoka kwa Umar, kwa sababu ninayo hofu kuwa utafika wakati ambapo Hadith zitakuwa zimetoweka." 5 Yeye pia aliwaandikia watu wa Madinah akiwataka wamwandikie chochote kile kilichobakia cha Hadith za Mtume s.a.w.w. 6

Ripoti hizi zinaonyesha wazi wazi kuwa uandikaji wa Hadith haukuwa jambo lenye umuhimu hadi wakati huo, hata hivyo, haimaanishi kuwa hapakuwepo na Hadith zilizokuwa zimeandikwa hadi wakati huo.

Pamoja na kifo cha Umar ibn Abd al-Aziz kazi hii haikufuatiliwa na Makhalifa waliofuata, na kwa mara nyingine tena uandikaji wa Hadith uliangukia katika kusahauliwa. Kukariri (kuhifadhi katika akili) ndiyo iliyokuwa njia iliyobakia.

Hadith za kusemwa mdomoni tu (bila ya maandiko) ndiyo iliyokuwa njia ya uenezaji wakati ambao Sunni walirithi kutoka vizazi vyao vilivyowatangulia, ilisababisha upinzani mkubwa mno katika kuziandika Hadith. Sisi twaweza kuelewa vyema hali hii wakati tutakapokuja kujua kuwa baadhi ya Muhaddithun walichukizwa mno na uandishi wa Hadith hadi kufikia mwishoni mwa karne ya 2 A.H./8 A.D. Kauli za wanahistoria kuhusiana na ukusanyaji wa Hadith hapo mwanzoni zinaelezea hayo hayo.

Abd al- Razzaq anaelezea kuwa mtu wa kwanza kuzikusanya Hadith alikuwa Abd al-Malik ibn Jurayj, aliyejulikana kama Ibn Jurayj (150 A.H./767 A.D.) Vile vile Abd al-Rahman Al-Awzai (88-157 A.H./707-773 A.D.) alikuwa ni miongoni mwa wale walioanza kuzikusanya Hadith.7

Al-Dhahabi anaandika kuwa, katika kipindi hiki ndipo Wanazuoni wa Kiislamu walianza kuandika Hadith, Fiqh na tafsiri katika mwaka 143 A.H./760 A.D. Wafuatao ndio waliokuwa wakiongoza katika kazi hizo nao ni Ibn Jurayj katika mji wa Makkah, Malik (179 A.H./795 A.D.) huko Madinah, al-Anzai katika Syria, Said ibn Abi Urwah (156 A.H./783 A.D.) huko Basrah, Muammar huko Yemen, Sufyan al-Thawri (156 A.H./783 A.D.) huko Kufah. Kabla ya kipindi hicho, hata hivyo, Muhaddithun waliongoza wakiripoti Hadith kutokea kukariri au kutokea kwa waliotegemewa lakini zilikuwa ni mikusanyo isiyokuwa na mipangilio.8

Mahali pengine yeye ni mbainifu zaidi wakati asemapo: "Ibn Jurayj na Ibn Abi Urwah walikuwa ni miongoni mwa watu wa kwanza katika ukusanyaji wa Hadith na Muammar ibn Rashid alikuwa ni wa kwanza miongoni mwao huko Yemen." 9 Ipo habari iliyoripotiwa na Abd al-Aziz ibn Muhammad al-Darwardi kuwa mtu wa kwanza kukusanya elimu alikuwa Ibn Shihab al-Zuhri. 10 Ibn Shihab al-Zuhr (124 A.H./742 A.D.) mwenyewe anaripotiwa akiwa amesema: "Umar ibn Abd al-Aziz alituamrisha kuzikusanya Hadith za Mtume s.a.w.w. Kufuatiwa hayo sisi tuliandika katika sura ya kitabu, na kupeleka nakala ya kitabu hicho katika sehemu zote za utawala wake." 11

Ni dhahiri, ingawaje Hadith zilikuwa zikikusanywa kwa kiasi fulani katika siku hizo, kazi ya ukusanyaji ilianza kuzorota kwa sababu ya upingamizi uliofuatia kifo cha Umar ibn Abd al-Aziz, na vile anavyosema al-Dhahabi, kazi hiyo ya ukusanyaji wa Hadith uliahirishwa au kuachwa kwa kipindi cha nusu karne.

Ibn Hajar anasema:

“Kazi ya ukusanyaji na upangaji (tabwib) wa Hadith ulianza katika miaka ya mwishoni mwa kipindi cha tabi'un, yaani ni kwamba, wakati ambapo Wanazuoni wa Kiislam walipokuwa wameenea katika miji. Wa kwanza katika ukusanyaji wa Hadith walikuwa ni Rabi ibn Subayh na Sa'id ibn Abi Urwah... hadi wakuu miongoni mwa Wanazuoni wa tabaka la tatu walipokusanya ahkam. 12

Al-Dhahabi pia anaelezea kitu kama hicho. 13 Kutokana na taarifa hizo inaweza kudadisiwa kuwa ukusanyaji wa Hadith uliotokezea katika sehemu mbili: Sehemu ya kwanza ni mkusanyiko usio kamilifu mwanzoni mwa karne ya 2 A.H./8 A.D. na sehemu ya pili ni ukusanyaji uangalifu katika sehemu yake ya pili. Hajji Khalifah anakubaliana na haya pale asemapo:

“Wakati Islam ilipoenea katika sehemu mbalimbali, na miji ya Islam ilipopanuka, tabi'un walisambaa mote humo. Baada ya muda, mkuu wao alipofariki dunia na hivyo ndivyo ilivyokuwa imekuja kuathiri ukusanyaji wa Hadith. Wanazuoni walianza kuhisi haja ya kuziandika Hadith na kuzihifadhi kwa njia ya kuziandika. Katika maisha yangu, lilikuwa ni jambo la maana la kuziandika Hadith, kwa sababu kukariri tu kuna uwezekano mkubwa wa kuweza kuja kupoteza fahamu au kuzipotoa. Baada yao, kulitokezea kipindi cha wataalamu wa Hadith kama Ibn Jurayj na Malik ibn Anas. Inasemekana kuwa mtu wa kwanza katika kukusanya Hadith alikuwa Rabi ibn Subay wa Basrah. Baada ya huyo, zoezi kama hili lilikuwa ni la kawaida. 14

Kutokana na taarifa hizo, tunaweza kumalizia kuwa, kulikuwapo na vipindi vitatu katika mpitilio wa Hadith za kutamkwa. Kipindi cha kwanza kilidumu mwanzoni hadi mwishoni mwa karne ya 1 A.H. /7 A.D., katika kipindi hiki uandishi wa Hadith haukuwapo wala haukujaribiwa isipokuwa tu katika hali chache ambapo Sahaba walijaribu kuziandika kwa kwenda kinyume na amri ya Makhalifa.

Katika kipindi cha pili, kuanzia mwanzoni mwa karne ya 2 A.H./8 A.D. hadi kwa kufikia katikati, kulitokezea uandishi na ukusanyaji wa Hadith katika hali isiyokuwa kamilifu na pia mambo yaliyoandikwa yaliweza kukusanywa.

Katika kipindi cha tatu, kilichoanzia katikati ya karne ya 2 A.H./8 A.D., uangalifu mkubwa ulielekezwa katika ukusanyaji na uandikaji wa Hadith ikiwa ni shughuli muhimu kimsingi. Vitabu vichache mno vilivyoandikwa katika kipindi hiki vinaweza kupatikana na baadhi ya mikusanyiko ya zamani sana pia vinaweza kupatikana - kama vile musannaf Ibn Abi Shaybah, musannaf ya Abd al-Razzaq na Muwatta ya Malik ibn Anas yalikuwa yameanzishwa katika sehemu ya pili ya karne ya 2 A.H./8 A.D.

Kwa mujibu wa ripoti ya al-Dhahab, musnad ya kwanza ilikusanywa na Nu'aym ibn Hammad. 15 Yahya al-Hamani 16 huko Kufah na al-Musd 17 huko Basrah nao ndio waliokuwa wa kwanza miongoni mwa Wanazuoni wa miji hii katika kukusanya musnad.

Sababu za Uchelewesho Katika Uandishi wa Hadith:

Inafahamika vyema kabisa kuwa Mtume s.a.w.w., kuanzia mwanzoni kabisa mwa Utume wake, aliupatia umuhimu zaidi kuhusu uandishi wa Qurani. Kimatokeo Qurani ikawa ipo mbali na makosa au mabadiliko (tahrif). Hata hivyo, katika hali ya Hadith kwa mujibu wa imani yetu mbali na ruhusa au amri ya Mtume s.a.w.w. kwa kuhusiana na uandishi wa Hadith na mbali na ukweli kwamba Hadith zilikuwa zimeandikwa katika zama za uhai wa Mtume s.a.w.w., sio kwamba tu kuwa haukupewa umuhimu kwa kazi, pia iliweza hata kupingwa. Upingamizi huo ulisababisha matatizo mengi kuhusiana na Hadith, ambayo tutayaona hapo mbeleni.

Uchelewesho huo wa kuziandika Hadith na matokeo yenye hatari yalifanya kikundi kimoja kumtupia lawama na a’udhubillah Mtume s.a.w.w. Wao walitambua wazi kuwa upingamizi wa uandishi wa Hadith iwapo itatokea kwa Mtume s.a.w.w., basi haitaweza kulaumiwa, kwani Mtume s.a.w.w. hawezi kulaumiwa; hata hivyo, iwapo wataielezea kwa wengine basi itatoboa udhaifu wao. Kwa hivyo, walimwelekezea Mtume s.a.w.w. kuwa ndiye aliyekataza kuandikwa kwa Hadith.

 • 1. Al-Tabaqat all-kubra, vol 2. uk. 389; al-Musnaf ya Abd al-Razzaq, vol. 1, uk. 285; Taqyid al-Ilm. uk
  107.
 • 2. Jami’bayan al-Ilm, vol.1, uk.92.
 • 3. Al-Musannaf ya Abd-Razzaq, vol.7, uk.337.
 • 4. Al-Tabaqat al-Kubra, vol.7, uk 447.
 • 5. Sunan al-Darimi, vol.1,uk.126; Taqyid al-Ilm uk. 105,106.
 • 6. Sunan al Darimi, vol.1. uk. 126; Akbhar Isbahan, vol 1, uk. 312; Tadhrib al-rawi, uk. 90 ya al-
  Siyuti..
 • 7. Al-Jarh wa al-ta’dil, vol. 1, uk.184.
 • 8. Tarik al-Khulafaa, uk. 261 ya al-Suyuti.
 • 9. Tadhkirat al-Huffadh, vol. 1, uk. 169,170,191,203.
 • 10. Jami’bayan al-Ilm, vol. 1, uk.88,91.
 • 11. Jami’bayan al-Ilm, vol. 1, uk.92.
 • 12. Muqaddamata Fath al-Bari, uk.4,5.
 • 13. Tadhkirat al-Huffadh, vol.1, uk.160.
 • 14. Kashf al -zunun, vol. uk. 237.
 • 15. Tadhkirat al-huffadh, vol. 1, uk.419.
 • 16. Ibid., vol.uk. 423 (kama hapo 44)
 • 17. Tadhkirat al-huffadh, vol.1, uk.423; Tadrib al-rawi uk. 88,89.