read

Akili

155. Mtukufu Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema

“Hakika heri yote hupatikana kwa akili”.

156. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Akili ni jahazi ya elimu.”

157. Mtukufu Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“ Hakugawa Allah swt kwa waja wake kitu kilicho bora kuliko akili, usingizi wa mwenye akili ni bora kuliko kukesha kwa mtu mjinga, kufuturu (kutofunga) kwa mtu mwenye akili ni bora kuliko Saumu ya mtu mjinga, na kutosafiri kwa mtu mwenye akili ni bora kuliko safari ya mtu mjinga”.

158. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema

“Ubinadamu wa mtu hutokana na akili yake.”

159. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.: Kumwambia mtoto wake Al Imam Hassan ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s.:

“Ewe Mwanangu! Hakika ya utajiri ni utajiri wa akili na ufakiri mkubwa ni kuwa mtu mpumbavu.”

160. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Akili ndio mjumbe wa haki.”

161. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Rafiki wa kila mtu ni akili yake, na adui ni ujinga wake”.

162. Mtukufu Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Mwenye kutekeleza (vitendo) kutokana na kile anachojua, Allah swt humrithisha (humjalia) elimu ambayo haijui.”

163. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Akili ni kitu cha maumbile, huzidi kwa elimu na majaribio.”

164. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Asiejaribu mambo hudanganyika.”

165. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Na majaribio ya muda mrefu ni nyongeza ya akili.”

166. Al Imam Musa al-Kadhim a.s. amesema:

“Ewe Hisham! Hakika kwa Allah swt juu ya watu kuna dalili (burhani) mbili: Dalili ya wazi, na dalili ya ndani. Na ama ile ya wazi ni Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Manabii na Maimamu a.s. na ama ya ndani ni akili.”

167. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema

“Mwenye kuwa nayo akili, amekuwa na dini.”

168. Mtukufu Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Mwenye kuijua nafsi yake, hakika amemjua Allah swt.”

169. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Huzijua mtu aibu za nafsi yake, ni maarifa yenye kunufaisha zaidi.”

170. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Na akili ni ngao (ngome) ya majaribu.”

171. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema

“Na kila ujuzi unahitaji majaribio.”

172. Mtukufu Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Kutafuta elimu ni bora kuliko kufanya ibada. Amesema Allah swt:

Hakika wanaomwogopa Allah swt miongoni mwa waja wake ni wanachuoni.

173. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema

“Hakuna zaka iliyo bora katika elimu kuliko kuifanyia kazi.”

174. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Mwenye kuwa na yakini (uhakika wa jambo) hufanya amali (kazi) hali ya kuwa yeye ni mwenye kupigania Jihadi.”

175. Mtukufu Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Lau (mtihani wa Allah swt) husubiri, na asiyefahamu hakanushi.”

176. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Hasubiri mtu yeyote katika uchungu wa haki ila yule anae kuwa na yakini (uhakika) wa matokeo yake.”

177. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Hakuna kitu chochote kile ila kina upeo wake,”

akaulizwa” Ni nini upeo wa Yaqini (kuwa na uhakika)?. Akasema “Usiogope kitu chochote.”

178. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Kutoa majabali kutoka mahali pake ni rahisi kuliko kuutoa moyo kutoka katika chochote.”

179. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Haisafiki kazi mpaka isihi (iwe sahihi) elimu.”

180. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Mwanachuoni katika zama zake, hayamhujumu matatizo.”

181. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Aliye kamilika kiakili hayawi mazito kwake matatizo.”

182. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Akili iliyokamilika, ndiyo yenye kuvunja mabaya.”

183. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Lengo la elimu ni kufanya kazi vizuri”.

Maelezo 1

Katika nadharia za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na Mawasii wake, elimu ni kitu bora kuliko kitu kingine chochote kile, kiasi kwamba jambo hili limeweza kuwastajaabisha watu wengi kutokana na hadithi nyingi zilizo pokewa zinazo sifa ubora wa elimu, hadithi kadhaa zimesikiwa toka kwenye ulimi wake Mtukufu Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na Maimamu a.s. Lakini je! Mshangao huo utabaki mpaka lini? Mshangao mbele ya uhakika wa mambo yalivyo hausaidii kitu. Je hatuamini kwamba maendeleo ya Dunia na Akhera hupatikana kwa elimu?. Jibu liko wazi kwamba kwa elimu hupatikana na maendeleo. Kwa hiyo tunajionea wazi kuwa thamani ya elimu iko juu sana.

Maelezo 2

Mwanadamu hutokea akajifunza elimu, lakini elimu yake ikawa ni upuuzi mtupu na balaa kwa watu, kutokana na kule kuvuka mpaka kwake na kuitumia elimu yake isivyo ndivyo na kinyume cha mtu mwenye akili, matokeo ya mtu wa ina hii ni kugundua mambo ambayo hayana faida yoyote kwa wengine, elimu kama hii humpoteza yeye mwenyewe na ummah pia katika dunia na akhera, hatimaye mtu huyu hugunduwa utengenezaji wa pombe na mabomu.

184. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Inamtosha mtu kuwa mjinga kwa kutokuzijua aibu zake.”

185. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Enyi watu! Hakuna heri katika dini isiyo na mafunzo ndani yake.”

186. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Mfanya ibada bila ya mafunzo Ni Kama punda mwenye kuzunguka, anazunguka na wala hachoki.’’

187. Mtukufu Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Mwenye kueneza elimu basi anao ujira mfano wa mwenye kutekeleza kwa hiyo (kutokana na elimu hiyo).”

188. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Upingeni ujinga kwa elimu.”

189. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Katika kuwasifu waja wa Allah swt: Na wakasimamisha masikio yao (kwakusikiliza) elimu yenye manufaa kwao.”

190. . Al Imam Musa al-Kadhim a.s. amesema:

“Nimekuta elimu ya watu iko katika mambo manne:

Kwanza kati ya hayo manne ni kumjua Mola wako,

Pili kujua alicho kiumba,

Tatu kujua anacho taka kwako,

Nne kujua chenye kukutoa katika dini yako.”

191. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Lau ningeijiwa na kijana miongoni mwa vijana wa ki-Shi’a hajifunzi (elimu ya dini) ninge mtia adabu.”

192. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Rafiki wa kila mtu ni akili yake na adui wake ni ule ujinga wake.”

193. . Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Mwenye akili ni kufikiri ataona (kuona muongozo)

194. Al Imam Musa al-Kadhim a.s. amesema:

“Kila kitu kina dalili, dalili ya mwenye akili ni kufikiri na dalili ya kufikiri ni kunyamaza.”

195. Mtume Mtukufu Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Kufikiri kwa muda wa saa moja ni bora kuliko ibada ya mwaka.”

196. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Kufikiri ni kioo kilicho safi.”

197. Al Imam Hassan al-'Askari a.s. amesema:

“Haikuwa ibada kwa uwingi wa kufunga na kusali, hakika ya ibada ni kufikiri (na kuzingatia) kuhusu Allah swt.”

198. Mtukufu Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Elimu ndio kichwa cha kila heri na ujinga ndio kichwa cha kila shari.”

199. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Ujinga ni mauti.”