read

Elimu na Thamani Yake

98. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Bihar al- Anwar , J. 2, Uk. 25:

“Waalimu pamoja na wanafunzi wanashirikiana katika kulipwa mema wakati watu wengine hawabahatiki.”

99. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Bihar al- Anwar , J. 2, Uk. 121:

“Yeyote yule aienezaye Dini kwa watu bila ya yeye mwenyewe kuwa na elimu ya kutosha, basi anaidhuru Dini zaidi kuliko vile anavyoitumikia.”

100. Amesema Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. , Nahjul Balagha, semi No. 482:

“Thamani ya kila kitu ni katika ubora wake.”

Yaani thamani ya mtu ni katika elimu yake. Cheo na utukuzo wake utakuwa katika kiwango cha elimu aliyonayo. Macho yetu hayaangali sura, urefu, ukubwa wa mwili wa mtu bali humthamini kwa kufuatana na kiwango cha elimu aliyonayo. Hivyo inatubidi sisi sote tujitahidi katika kutafuta na kuipata elimu kwa kiasi tuwezacho.

101. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. katika Bihar al- Anwar, J. 2, Uk.36:

“Elimu ni amana ya Allah swt juu ya ardhi hii na wanazuoni ndio wenye amana hii. Hivyo yeyote yule atendaye kwa mujibu wa elimu yake, basi kwa hakika ameiwakilisha amana vile ipasavyo”

102. Al-Imam Muhammad Baqir a.s. amesema:, Bihar al- Anwar ,J. 78, uk. 189:

“Jitafutieni elimu kwa sababu kujifunza ni matendo mema na kusoma kwenyewe ni ‘ibada.”

103. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.Amesema:, Bihar al- Anwar , J. 1, Uk. 179:

“Mtu ambaye anatafuta elimu, ni sawa na mpiganaji vita katika njia ya Allah swt.”

104. Amesema Al-Imam Ja’far as-Sadiq a.s. katika Bihar al- Anwar , J. 2, Uk. 92:

“Uichunge sana elimu yako na utazame ni kwa nani unaitoa.”

105. Amesema Al-Imam Ja’far as-Sadiq a.s. katika Al-Kafi, J.1, Uk.36:

“Muitafute elimu na kuipamba kwa subira na ukuu; na uwe mnyenyekevu kwa yule ambaye anaitafuta elimu kutoka kwako”

106. . Amesema Al-Imam Ja’far as-Sadiq a.s. katika Al-Kafi, J. 1, Uk. 35:

“Yeyote yule ajifunzae elimu na kutenda vilivyo, na kuifundisha kwa ajili ya Allah swt, basi Malaika watamtukuza mbinguni .”

107. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. katika Bihar al- Anwar , J.1, Uk. 204:

“Wema wa duniani humu pamoja na Aakhera ni pamoja na elimu.”