read

Hadith ni Nini ?

Mawaidha na Nasiha maneno aliyoyazungumza Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ni Hadith kwa kifupi, maneno yoyote yaliyotoka mdomoni kwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. mbali na ayah za Qur'an Tukufu, ama yale aliyoyatenda kuonyesha, hayo yote ni Hadith. Vile vile maneno na matendo yote ya Ma’asumin a.s. pia ni Hadith yaani yataingizwa katika Hadith. Kutokana na Hadith sisi tunaweza tukajua na kufuatilia na kutekeleza mambo ambayo ni usuliFuru’, Sunnah na Faradhi.

Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kwa maisha yake yote alikuwa pamoja na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Hivyo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. popote pale alipokuwa akiwapa watu nasiha na mawaidha katika mambo mbalimbali na kuwaongoza katika masuala mbalimbali basi Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. daima alikuwa akinufaika na hayo yaliyokuwa yakisemwa na kutendwa na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.

Na ndivyo alivyosema “Sisi ndio dalili za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na vile vile ndio Sahaba wake halisi, na sisi ndio ufunguo wa hazina yake ya elimu na mlango wa mji wake wa elimu1 alioutangaza Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na mtu yeyote hawezi kuingia katika nyumba au mji isipokuwa kwa kupitia mlango wake.”

“Kwa kiapo cha Allah swt ! Mimi nina elimu na ma’arifa ya Utume na maneno ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Sisi Ahlul Bayt a.s. ni milango ya hekima na kwa hakika sisi ndio tunayo nuru ya hukumu za Allah swt. (Nahjul Balagha).

Katika historia tunapata habari kuwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. ndio aliyekuwa mtu ambaye amekusanya na kuwa na hazina kubwa ya Hadith za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Tumepata kuona kuwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. yeye daima alikuwa akiziandika Hadith za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na kuzielewa na kuzikariri vyema kabisa.

Kwa amri ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ndipo Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alitayarisha kitabu kimoja ambamo kumeandikwa Hadith za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na Sunnah zake, na kitabu hicho kinaitwa Sahifat Jami’a na kitabu kingine kinaitwa Kitabul Faraidh, ambamo katika vitabu hivyo vyote viwili kumeandikwa Ahkam za Sharia.

Vitabu hivyo vimenakiliwa katika vitabu vingine mfano Sahih Buhari amenakili kwenye kitabu chake ambao ni upande wa Masunni. Na upande wa Mashi’ah Ma’ulamaa wa Kishi’ah Sheikh Sadduq a.r. amenakili katika kitabu kinachoitwa Manla yahdharulfaqih na Sheikh Tusi a.r. kinachoitwa Tahdhib na Thiqqatul Islam Quleyni r.a amenakili katika Al Kafi.

  • 1. Ipo Hadith ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa “Mimi ni mji wa elimu na Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. ni mlango wake” na vile vile amesema “Mimi ni hazina ya elimu na Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. ni ufnguo wake.” Na zipo Hadith nyingi kama hizo.