read

Hadith Zilizotolewa

Kwa mujibu wa kanuni hizi nne, mmefahamu kuwa Hadith inapoangukia kuwa dhaifu haimaanishi kuwa ni Hadith ya uongo, yenye mfululizo dhaifu, na kwa dalili zinginezo na kwa nyenzo zinginezo inaweza kuthibitika kuwa Hadith hiyo inaweza kukubalika, Lakini inapokuwa imekosewa kabisa basi huitwa Kidhb (uongo) au Iftira’ (tuhuma). Yaani utaratibu uliotumiwa wa kuwanasibisha Ma’sumiin a.s. haupo wenye ukweli, bali tunaweza kusema kuwa ni tuhuma. Hadith hizo ni uzushi mtupu. Katika historia ya elimu ya Hadith, utaratibu huu mmoja ni tatizo kubwa mno kuling’amua iwapo Hadith hii ni uzushi au la.

Sayyid Murtadha ‘Alamal Hudaa a.r. anasema:

“Zipo baadhi ya sehemu za Hadith katika Mashia na Waislamu wote kwa ujumla ambazo zimejazwa makosa na uzushi ambazo zinatufanya kuzichukulia kuwa ni Hadith za uongo. Katika Hadith hizo kuna mambo fulani fulani ambazo kwa hakika si rahisi kukubalika kiakili na ni pingamizi mtupu. Kwa mfano imani juu ya jabr (ushurutisho) yaani mwanadamu ameshurutishwa na Allah swt katika matendo ya madhambi na uasi, au siku ya Qiyamah Allah swt ataonekana n.k. na hivyo inamaanisha kuwa kunahitajika uchuguzi na utafiti mkubwa katika kuthibitisha ukweli wa usahihi wa Hadith kama hizo.”

Imam ‘Ali a.s. amesema: “Mtume Muhammad s.a.w.w. alisema

“Enyi watu, kutakithiri mno kuninasibishia mambo ya uzushi, hivyo mutambue kuwa mtu yeyote kwa makusudi ataninasabisha na uongo au uzushi wowote, basi hakuna mahala pale pengine isipokuwa ni Jahannam tu.”

Katika zama hizi ni lazima kufahamu ‘Ilmul Hadith na Rijal yaani kujua habari za wale wenye kuleta riwaya. Kazi hii ni ya wale mabingwa katika fani hii na wala si ya wale wenye elimu kidogo ambao wamejua Kiajemi na Kiarabu kidogo hivyo wakaanza kuwapotosha watu.

Sasa tuangalie ni kwa sababu gani kumetokezea haja ya kutaka kuzichuja Ahadith na tuwaangalie watu mbalimbali ambao wamefanya juhudi za kuingiza uongo na uzushi na tuhuma katika Ahadith.

1. Baada ya kifo cha Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kulizuka mgogoro kuhusu ukhalifa ambapo kulitokezea makundi mawili. Kundi moja likidai kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alikuwa amekwisha elezea ni nani atakaye kuwa Khalifa baada yake na kundi la pili likaanza kuzua Hadith kuwa swala hilo liachiwe ‘ummah wa Kiislamu kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alisema kuwa ukhalifa baada yake hautatokana na Bani Hashim (uzushi mtupu).

3. Wakati Uthman alipouawa, basi Ma’uwiya bin abi Sufiyan kwa hila zake alitupa tuhuma za mauaji yalilengwa kwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Hapo kuliibuka Hadith za kuzuliwa katika kuwatukuza Bani Umayyah, umadhulumu wa Uthman na hukumu juu ya Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. katika mauaji ya Uthman. Si hayo tu, bali Hadith zile zilizokuwa zikielezea fadhila za Imam ‘Ali a.s. pia zilianza kubadilishwa na kupotoshwa. Mfano, ipo ayah ya Qur’an tukufu: ‘wa minanaasi manyashrii nafsahubtighaa mardhatillah’ Aya hii inatoa shuhuda ya tukio lililotokea katika usiku wa Hijrah ambapo Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alijitolea nafsi yake kwa ajili ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Kwa amri za Mu’awiyah, Hadith hii ikageuzwa kuwa imeteremka kwa ajili ya Ibn Muljim kwa sababu yeye alikuwa ameiweka nafsi yake hatarini katika kumwua Imam ‘Ali a.s.

5. Makhariji walizua Hadith chungumzima kuhusu akida zao na Waislamu kwa ujumla pia walizizua Hadith nyingi mno katika upinzani wao

7. Ma’ulamaa wa Kiislamu walianza kuzua na kutumia hizo Ahadith katika kuzieleza na kuziendeleza fikra, nadhiri na akida zao. Mu’tazila, Tasawwuf, Gulat na Ash-Ari na wengineo wote wakaanza kuzua Hadith katika kueneza imani zao. Iwapo utabahatika kukisoma kitabu kiitwacho Ihyaul Ulumiddiin basi ndipo utakapokuja kujua hali halisi ya uovu huu wa kuzua Ahadith za kiuongo dhidi ya Ma’sumiin a.s. ambazo kwa hakika hazikubaliki kuwa zimesemwa nao. Kwa kutoa mfano, tunawaleteeni chache ili muweze kuziangalia:

    a) Ahmad bin Mansur anasema kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Baina mikono miwili ya Allah swt kuna maandiko fulani ambamo kuna majina ya wale watu ambao wanaitikadi kuhusu kuwapo kwa uso na kuonekana kwa Allah swt siku ya Qiyama. Na Malaika wanaona fakhari kwa majina hayo!

    c) Mamun bin Ahmad Harwi anamnakili Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akisema:

“Kuna mtu mmoja katika ‘Ummah wangu ambaye ni hatari hata kuliko Shaytani, na jina lake ni Muhammad bin Idris (yaani Imam Shafi’i) na vile vile kuna mtu mwingine ambaye yuko sawa na nuru kwa ‘Ummah wangu, na jina lake ni Abu Hanifa.”

Tanbii: Mwandishi wa Lisanul Mizaan anaandika kuwa sababu kubwa ya kuizua Hadith hii ni kwamba huko Khurasan, wafuasi wa Imam Shafi’I walikuwa wengi.

    e) Ahmad bin Nasr anasema kuwa siku moja alimwota Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. katika ndoto akimwambia;

“Itakuwa wema kwako kumtii Shafi’i kwani anatokana nami na Allah swt yu radhi naye”

    g) Kwa hakika jambo lakusikitisha mno ni kwamba hawa wataalamu wa kuzua (wazushi) ni watu ambao wameilimika vyema katika masomo ya Qur’an na Hadith. Mafunzo ya Qur’an hayakuwa yenye maana kwao bali wametilia mkazo masilahi na ulafi wa dunia hii.

Ayatullah al-Khui r.a. anaandika katika kitabu chake Al-Bayan fi Tafsiril Qur’an, Uk. 28 kuwa kuna rundo kubwa kabisa la riwaya za uongo na zilizozuliwa, ambamo hawa wazushi wamechukua tahadhari kuwa kusije kukapunguzwa fadhila za Qur’an, basi wamezua Hadith zao binafsi; na wamezirembesha kwa fadhila mbalimbali kiasi kwamba zinapopimwa kwa kauli za Allah swt zinajulikana kuwa ni za uongo mtupu. Mfano Abu Ismah Faraj bin Abi Maryam al-Maruzi, Muhammad bin Akasha al-Kirmani, Ahmad bin Abdillah Juibarri na wengineo wengi.

Wakati mtu mmoja alipomwuliza Abu Ismah kuwa amezitoa wapi Hadith chungu mzima kutokea kwa Ikramah na Ibn ‘Abbas kuhusu fadhila za Sura moja moja za Qur’an tukufu ? Alianza kusema: “Mimi niliona kuwa watu wameanza kuipa mgongo hiyo Qur’an na badala yake wanajishughulisha mno na fiqhi ya Abu Hanifa, watu wamejishughulisha kuisoma Maghazi ya Muhammad bin Is-Haq, basi mimi nimezusha Hadith hizo juu ya Qur’an kwa kutaka furaha ya Allah swt …!

    i) Wakati kulikuwapo utawala wa Bani ‘Abbas, basi Ma’ulamaa wenye tamaa ya dunia walizizusha Ahadith nyingi mno katika kuelezea fadhila za watawala hao. Katika Tarikhul Khulafa anaandika as-Sayyuti:

“Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema kuwa yeye alipoona kuwa Bani Marwan wanachezea Mimbar yangu, basi hapo mimi nilisikitishwa mno. Na hapo baadaye nikaona Bani ‘Abbas pia wanachezea, na kwa hayo mimi nilifurahishwa mno.”

Abu Hurairah ananakiliwa riwaya moja kuwa siku moja Mtume Muhammad s.a.w.w. alitoka nje, na hapo alikutana na Baba mkubwa ‘Abbas, na alimwambia: “Ewe Abul Fadhl ! Je nikupe habari njema ?

‘Abbas alisema: “Naam, Ewe Mtume wa Allah swt !” Ndipo Mtume Muhammad s.a.w.w. aliposema: “Allah swt ameitengeneza swala hili (yaani Dini hii ya Islam) kwangu na kuishia kwa ‘Ummah wangu.” Na akaendelea kusema: “Wakati kizazi chako kitakapoishi Iraq, watakuwa na usukani huu wa Islam kwa muda mpaka atakapodhihiri Mtume Isa a.s. na kumkabidhi.”

Tanbihi: Ni jambo la kushangaza mno kuwa huyu huyu as-Suyuti ameandika kitabu kimoja juu ya masuala ya uzushi kiitwacho Al-Lulil Mansukh (Lulu bandia) na amewatahadharisha Waislamu kujitahadharisha na Hadith kama hizo za uzushi, pamoja na hayo yeye mwenyewe amenakili riwaya nyingi mno zilizo bandia na Ahadith zilizo zuliwa na hivyo ameshiriki kikamilifu katika kuifikishia Islam jeraha kubwa.

    k) Baadhi ya makafiri na maadui wa Islamu wamekuwa wakiishi miongoni mwa Waislamu na kujihusisha katka harakati za kueneza sumu hii miongoni mwa Waislamu kwa hila na njama mbalimbali. Wao ili kutaka kutimiza mikakati yao hiyo ya kueneza upotofu, wamekuwa wakijishughulisha na uzushi wa Ahadith za Mtume Muhammad s.a.w.w. na Ma’sumiin a.s. na walikuwa wakizileta mbele ya watu. Ibn Abil Awjah amekiri mwenyewe kuwa yeye ameingiza kiasi cha Ahadith zipatazo elfu nne zilizozuliwa miongoni mwa Ahadith zilizo za kweli.

    m) Katika kipindi cha mwanzo cha Islam, watu walikuwa na shauku kubwa ya kusikiliza visa na masimulizi mbalimbali na katika hali hii kuliibuka wasimulizi wengi wa masimulizi kama hayo na hivyo wao walikuwa wakifanya kila jitihada za kukusanya habari na porojo za kila aina na walikuwa wakiongezea chumvi na pilipili ili kwamba mazungumzo yao yalete ladha nzuri na kuwavutia watu.

Matokeo yakawa ni kwamba Mayahudi walikuwa wamezusha visa na hadithi nyingi kuhusu mitume yao, hivyo mazushi hayo yakapata soko kubwa miongoni mwa Waislamu, na rundo kubwa hili linajulikana kwa jina la Israiliyyaat 1 Hadith zilizozushwa juu ya Mitume a.s. inapatikana katika Tarikhul Ambiya’ na hususan katika tafisiri za Ayah ambazo zinazungumzia habari za Mitume a.s.

Ibn Jawzi anaandika kuwa Imam Ahmad bin Hambal na Yahya bin Mu’in walikuwa wakisali Msikitini na wasimuliaji wakaja wakatandika mikeka yao tayari kuanza masimulizi yao mbele ya halaiki kubwa ya mashabiki wao.

Wasimulizi wakiendelea na masimulizi yao, wakasema: “Mimi binafsi nimemsikia Ahmad bin Hambal na Yahya bin Mu’in kuwa wao wamewasikia Rawi fulani fulani kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema: “Mtu yeyote atakaye sema La ilaha Illallaah basi Allah swt atamwumba ndege mmoja ambaye mdomo wake utakuwa wa dhahabu na macho ya marjaan…” Hivyo wao walizielezea habari za ndege huyo, na kama tukianza kuziandika tutaandika kurasa ishirini zinginezo.

Kwa hakika watu walipoyasikia haya walianza kuyumba na kwa kutoa shukurani zao walianza kuwatupia mapesa hao wasimulizi, nao walibakia kimya kwa muda zaidi kidogo ili waendelee kupata zawadi zaidi, na hapo ndipo Yahya bin Mu’in alipojitokeza na kumwita aje mbele yake. Msimulizi alikuja mbio mbio hapo mbele kwa kutarajia kupata zawadi nono, ndipo Yahya alipomwuliza: “Je habari zote hizi zisizo na miguu umeyatoa wapi?” Akajibu: “Nimemsikia Yahya bin Mu’in na Ahmad bin Hambal.”

Yahya na Ahmad bin Hambal walishikwa na bumbuwazi na walibakia wakitazamana, na hapo ndipo Yahya kwa hasira alimgeukia msimulizi na kumwambia: “Je hauoni aibu? Wewe umethubutuje kuzusha uongo dhidi yetu ilhali tukiwa mbele yako ? Jina langu ni Yahya bin Mu’in na huyu ndiye Ahmad bin Hambal.”

Yule msimulizi alianza kusema: “Mimi daima nimekuwa nikisikia kuwa Yahya bin Mu’in ni mtu mpumbavu na mjinga kabisa, na kwa hakika nimepata uthibitisho huo leo hii, kwa hakika ni ajabu kubwa ! Je dunia hii nzima ina Yahya bin Mu’in na Ahmad bin Hambal nyie wawili tu na wala haina wengine? Kwa kusema ukweli mimi nimewanakili riwaya mbalimbali Yahya bin Mu’in sabini na Ahmad bin Hanbal sabini.” Kwa kusema hayo msimulizi alijiondokea zake.

    o) Kulizuliwa Ahadith nyingi mno katika kutukuza makabila na Miji ya Kiislamu. Tazameni mfano mmoja. Imeripotiwa kuwa al-Imam ar-Ridha a.s. amesema kuwa Mji mtukufu wa Qum umeitwa hivyo kwa sababu hapo ndipo Safina ya Mtume Nuh a.s. iliposimama baada ya kuisha kwa tufani. (Katika lugha ya Kiarabu neno Qum linamaanisha kusimama).

    q) Katika zama za Makhalifa watu walikuwa wakijishughulisha mno katika kuzusha Hadith za uongo au kuzigeuza maana ili waweze kupata zawadi, hongo au kutukuzwa miongoni mwa watu. Katika zama za Mahdi ‘Abbasi ambaye alikuwa khalifa wa Bani ‘Abbas, aliijiwa na mtu mmoja aitwaye Ghiyas Bin Ibrahim ambaye aliwakuta njiwa wengi mno katika kasri ya khalifa, na kwa hayo alisema: “Ipo riwaya kutokea Mtume Muhammad s.a.w.w. kuwa imeruhusiwa mashindano matatu tu yaani ngamia, farasi na njiwa.”

Kwa hayo, khalifa alimpa zawadi na wakati alipokuwa akiondoka, khalifa alimwambia:

“Mimi nashuhudia kuwa huyu aliyetupa mgongo amemnasibishia Mtume Muhammad s.a.w.w. uongo.”

  • 1. Msomaji anaombwa kujaribu kusoma kitabu nilichokitarjumu katika lugha ya Kiswahili kwa jina la Tadhwin al-Hadith (Uchunguzi juu ya ukusanyaji na uandishi wa Hadith) ambamo swala hili limezungumzwa kwa marefu na mapana.