read

Kuwa Makini Kuhusu Akhera

217. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. katika Bihar al- Anwar, J. 1, Uk. 203,

“Wafuasi wa Mtume Isa a.s. walimwuliza ni watu gani wawafanye marafiki wao, naye a.s. aliwajibu: “Pamoja na wale ambao wanapokuwa nanyi humkumbusha Allah swt, mazungumzo yao hukuzidishieni elimu na matendo yao huwavutieni ninyi kutenda matendo mema kwa ajili ya Aakhera.”

218. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.Amesema katika Qurar-ul-Hikam, Uk. 335:

“Kusiwepo na shughuli ya aina yoyote ile ambayo itakuzuia kutenda matendo kwa ajili ya Aakhira, kwa hivyo, muda wa kufanya hivyo upo mdogo sana.”

219. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.Amesema katika Qurar-ul-Hikam, Uk. 274:

“Yeyote yule atakayeiuza Aakhera yake kwa maisha ya humu duniani, basi kwa hakika amepoteza yote kwa pamoja.”

220. Al-Imam ‘Ali ibn Muhammad al-Hadi a.s. Amesema katika Bihar al- Anwar, J. 78, Uk. 370:

“Kumbuka pale utakapokuwa kitandani ambapo mauti imekukalia kichwani na huku umezungukwa na ndugu na majama’a zako, na hapo hakuna mganga anayeweza kukuepusha na kifo hicho wala hakuna rafiki anayeweza kukusaidia.”

Jannah

221. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema,

“Kila mtu katika Jannah atahudumiwa kwa vitu vizuri vya Jannah kiasi kwamba hata atakapopata wageni kwa malaki na malaki lakini hakutapungua chochote… neema nyingi tele…”

222. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alijibu:

“Allah swt ni mwadilifu. Iwapo matendo mema ya mwanamme yatakuwa zaidi ya mwanamke, basi mwanamme atapewa fursa kwanza kufanya chaguo na uamuzi iwapo anapendelea kuishi na mke wake au hapana. Na vivyo hivyo iwapo matendo mema ya mwanamke yatakuwa zaidi basi naye atapewa chaguo kama hili yaani iwapo atapenda kuishi na mume wake au hapana. Iwapo mwanamke huyo hatamchagua bwanake awe mume wake hapo Jannah, basi huyo mwanamme aliyekuwa mume wake humu duniani hatakuwa mume wake huko Jannah .”

223. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alisema kuwa Allah swt amesema katika Qur’an Tukufu Sura-i-Yasin,36, Ayah ya 78

وَضَرَبَ لَنَا مَثَلًا وَنَسِيَ خَلْقَهُ ۖ قَالَ مَنْ يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ

‘Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake – akasema: “Nani atakaihuisha mifupa na hali imesagika ?”

224. Katika Milango yote 8 ya Jannah kumeandikwa:

Hakuna mungu mwingine isipokuwa Allah swt tu; Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ni Mtume Wake; Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. ni mja (Walii) Wake halisi,

225. Mlango wa kwanza

Katika mlango wa kwanza wa Jannah kumeandikwa:

    • Zipo njia mbalimbali za kujipatia kila kitu, na njia za kujipatia riziki ni nnne:

    • kutosheka,

    • kutumia katika njia sahihi,

    • kukana kisasi na

    • kufanya uhusiano pamoja na watu waliookoka yaani katika njia nyoofu.

226. Mlango wa pili

Zipo njia mbalimbali za kujipatia kila kitu, na njia za kujipatia furaha katika maisha ya Aakhera ni nne:

• Kuonyesha huruma kwa mayatima,

• kuwawia wema wajane,

• kuwasaidia wacha-mungu katika kufanikisha malengo yao na

• kuwaangalia na na kuwasaidia masikini na wasiojiweza.

227. Mlango wa tatu

Zipo njia mbalimbali za kujipatia kila kitu, na na njia za kujipatia siha njema katika maisha haya mafupi ni nne:

• Kuongea kwa uchache,

• kulala kidogo,

• kutembea kidogo na

• kula kidogo.

228. Mlango wa nne

• Yeyote yule amwaminiaye Allah swt na siku ya Qiyamah basi lazime awe mkarimu kwa wageni wake;

• Yeyote yule amwaminiaye Allah swt na siku ya Qiyamah basi lazime awe mkarimu kwa jirani zake;

• Yeyote yule amwaminiaye Allah swt na siku ya Qiyamah basi lazime awe mkarimu kwa wazazi wake;

• Yeyote yule amwaminiaye Allah swt na siku ya Qiyamah basi lazime awe ni mwenye kusema mema au anyamaze kimya.

229. Mlango wa tano

• Yeyote yule ambaye hataki kunyanyaswa siku ya Qiyamah, basi naye asimnyanyase mtu yeyote;

• Yeyote yule ambaye hataki kusengenywa siku ya Qiyamah, basi naye asimsengenye mtu yeyote;

• Yeyote yule ambaye hataki kudhalilishwa siku ya Qiyamah, basi naye asimdhalilishe mtu yeyote;

• Mtu yeyote yule ambaye anataka kujishikiza kwa umadhubuti katika maisha haya mafupi na yale ya Aakhera, basi lazima atoe shahada kuwa: Hakuna mungu mwingine isipokuwa Allah swt tu; Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ni Mtume Wake; Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. ni mja (Walii) Wake halisi.

230. Mlango wa sita

• Yeyote yule anayetaka kaburi lake liwe pana na lenye nafasi ya kutosha (kutombana) basi ajenge Misikiti;

• Yeyote yule anayetaka asiliwe na wadudu au minyoo ya ardhini, aifanye Misikiti iwe nyumba yake ( yaani awe akiizuru kwa mara nyingi kama kwamba anaishi humo );

• Yeyote yule anayetaka kubakia salama, (yaani asipate shida na taabu za kiu katika maisha haya na yale ya Aakhera ambapo kila mtu atakuwa akitafuta hata tone moja la maji ) basi awe akifagia Misikiti;

• Na yeyote yule ambaye anataka kuiona nafasi yake hapo Jannah basi atengeneze sakafu na kuweka mazulia au mikeka katika Misikiti.

231. Mlango wa saba

• Moyo halisi unapatikana kwa mema manne:

• Kuwatembelea wagonjwa,

• kutembea nyuma ya jeneza,

• kununua sanda kwa ajili ya maiti na

• kulipa madeni.

232. Mlango wa nane

• Yeyote yule anayetaka kuingia katika milango hii basi lazima awe na sifa nne zifuatazo:

• Ukarimu,

• adabu njema,

• moyo wa kujitolea na

• kujiepusha katika kuwadhuru waja wa mungu.

233. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. ananakiliwa riwaya na Muhammad ibn Qays katika ukurasa wa 115 wa kitabu Al-Mahasin:

“Siku moja Shaitani alimwona Mtume Nuh a.s. akisali, basi Shaitani alimwonea wivu Mtume Nuh a.s. na hakuweza kujizuia, akasema. “Ewe Nuh ! Allah swt aliyetukuka, Mkuu, amejenga mwenyewe Bustani ya Eden , akapanda miti na kutiririsha mito ndani mwake. Na kisha akaangalia mandhari hayo na kusema, “Kwa hakika waumini na waongofu ndio washindi ! La, Kwa Utukufu wangu ! Mtu mwenye utovu wa adabu (mwenye madhambi) kamwe hataingia kuishi humu.’”

234. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alisema,

“Mitume wote wamekatazwa kuingia Jannah kabla yangu, na mataifa yote yamekatazwa kuingia humo kabla ya waumini watufuatao sisi, sisi Ahlul Bayt a.s., kuingia ndani mwake.”

235. Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amenakiliwa akisema, uk.139, J.8 ya Bihar al-Anwar, akisema,

“Jannah inayo milango sabini na moja ya kuingilia: Ahlul Bayt a.s. yangu na wafuasi wao wataingilia milango sabini, wakati ambapo watu wengine wataingilia mlango uliobakia.”

Taqwa

236. Qur’ani Tukufu , Sura al-Maryam 19, Ayah 63:

تِلْكَ الْجَنَّةُ الَّتِي نُورِثُ مِنْ عِبَادِنَا مَنْ كَانَ تَقِيًّا

Hiyo ndiyo Jannah tutayowarithisha katika waja wetu walio kuwa wachamungu.

237. Vile vile twaambiwa katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Hujurat , 49, Ayah 13:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُمْ مِنْ ذَكَرٍ وَأُنْثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِنْدَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ

Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumewajaalia kuwa mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allah swt ni huyo aliye mchamungu zaidi katika nyinyi….

238. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Maidah, 5, Ayah 85:

فَأَثَابَهُمُ اللَّهُ بِمَا قَالُوا جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ جَزَاءُ الْمُحْسِنِينَ

Basi Allah swt atawalipa, kwa yale waliyoyasema, Bustani zipitazo mito kati yake; humo watadumu. Na haya ndiyo malipo ya wafanyao wema.

239. Allah swt anasema katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Tawbah, 9, Ayah 111:

إِنَّ اللَّهَ اشْتَرَىٰ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنْفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُمْ بِأَنَّ لَهُمُ الْجَنَّةَ ۚ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَيَقْتُلُونَ وَيُقْتَلُونَ ۖ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنْجِيلِ وَالْقُرْآنِ ۚ وَمَنْ أَوْفَىٰ بِعَهْدِهِ مِنَ اللَّهِ ۚ فَاسْتَبْشِرُوا بِبَيْعِكُمُ الَّذِي بَايَعْتُمْ بِهِ ۚ وَذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

Hakika Allah swt amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwa kuwa wao watapata Jannah. Wanapigana katika Njia ya Allah swt – wanauwa na wanauawa. Hii ni ahadi aliyojilazimisha kwa Haki katika Taurati na Injili na Qur'an. Na nani atimizae ahadi kuliko Allah swt ? Basi furahini kwa biashara yenu mliyo fanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.

240. Allah swt anasema katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Naziat,79,Ayah 40 – 41:

وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَىٰ

فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَىٰ

Na ama yule anayeogopa kusimamishwa mbele ya Allah swt Mlezi, na akijizuilia nafsi yake na matamanio, Basi huyo, Jannah itakuwa ndiyo makaazi yake !

241. Allah swt atuambia katika Qur’ani Tukufu, Surah al-Waqia,56,Ayah 10–12:

وَالسَّابِقُونَ السَّابِقُون

أُولَٰئِكَ الْمُقَرَّبُونَ

فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ

Na wa mbele watakuwa mbele.

Hao ndio watakao karibishwa

Katika Bustani zenye neema.

242. Qur’ani Tukufu , Sura al-Dahar, 76, Ayah 12:

وَجَزَاهُمْ بِمَا صَبَرُوا جَنَّةً وَحَرِيرًا

Na atawajaza Bustani za Jannah na maguo ya hariri kwa vile walivyo subiri.

243. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Ra’d, 13, Ayah 24:

سَلَامٌ عَلَيْكُمْ بِمَا صَبَرْتُمْ ۚ فَنِعْمَ عُقْبَى الدَّارِ

Hao ndio watu wa Jannah, watadumu humo, kuwa ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda.(Wakiwaambia) Assalamu ‘Alaikum ! amani iwe juu yenu, kwa sababu ya mlivyo subiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera.

244. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Nisaa, 4, Ayah 13:

تِلْكَ حُدُودُ اللَّهِ ۚ وَمَنْ يُطِعِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

Na anayemtii Allah swt na Mtume wake, Yeye atamtia katika Jannah zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.

245. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Safaat, 37, Ayah 39 – 43:

وَمَا تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ

إِلَّا عِبَادَ اللَّهِ الْمُخْلَصِينَ

أُولَٰئِكَ لَهُمْ رِزْقٌ مَعْلُومٌ

فَوَاكِهُ ۖ وَهُمْ مُكْرَمُونَ

Wala hamlipwi ila hayo hayo mliyokuwa mkiyafanya.

Isipokuwa waja wa Allah swt walio khitariwa.

Hao ndio watakaopata riziki maalumu,

Matunda, nao watahishimiwa.

246. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Maidah, 5, Ayah 119:

قَالَ اللَّهُ هَٰذَا يَوْمُ يَنْفَعُ الصَّادِقِينَ صِدْقُهُمْ ۚ لَهُمْ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

Allah swt atasema: Hii ndiyo Siku ambayo wasemao kweli utawafaa ukweli wao. Wao watapata Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu milele. Allah swt amewawia radhi, nao wawe radhi naye. Huku ndiko kufuzu kukubwa.

247. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura Ta-Ha, 20, Ayah 75– 76:

وَمَنْ يَأْتِهِ مُؤْمِنًا قَدْ عَمِلَ الصَّالِحَاتِ فَأُولَٰئِكَ لَهُمُ الدَّرَجَاتُ الْعُلَىٰ

جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ جَزَاءُ مَنْ تَزَكَّىٰ

Na atakayemjia naye ni Muumini aliye tenda mema, basi hao ndio wenye vyeo vya juu.

Bustani za milele zipitazo mito kati yake,wadumu humo. Na hayo ni malipo ya mwenye kujitakasa.

248. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura ‘Ali Imran, 3, Ayah 133-136:

وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِنْ رَبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ {133}

الَّذِينَ يُنْفِقُونَ فِي السَّرَّاءِ وَالضَّرَّاءِ وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ ۗ وَاللَّهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ {134}

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَنْ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ {135}

أُولَٰئِكَ جَزَاؤُهُمْ مَغْفِرَةٌ مِنْ رَبِّهِمْ وَجَنَّاتٌ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ {136}

Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Jannah ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyowekwa tayari kwa wachamungu,

Ambao hutoa wanapokuwa na wasaa na wanapokuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Allah swt huwapenda wafanyao wema;

Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakijidhulumu nafsi zao humkumbuka Allah swt na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao – na nani anayefuta dhambi isipokuwa Allah swt ? – na wala hawapendelei na waliyo yafanya na hali wanajua.

Hao malipo yao ni msamaha kwa Mola wao Mlezi, na Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu, na mwema mno ujira wa watendao.

249. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Rahman, 55, Ayah 46:

وَلِمَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ جَنَّتَانِ

Na mwenye kuogopa kusimamishwa mbele ya Allah swt atapata Jannah (Bustani) mbili

250. Al-Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema katika Majma’ul Bayan:

“Mtu yeyote ambaye anajua na kutambua wazi kuwa mimi nifanyapo jema au baya, basi Allah swt yupo anashuhudia matendo yangu haya, basi mtu kama huyu daima atakachokuwa akikifanya basi atakuwa mwangalifu mno katika matendo yake na atajiambia kuwa lau nitafanya kazi hii njema basi Allah swt atalipa mema kadha na kadha na lau nitafanya maasi na madhambi, basi Allah swt ataniandikia adhabu kadha wa kadha. Kwa hivyo watu kama hawa wamewekewa Bustani mbili katika Jannah.”

251. Qur’ani Tukufu , Sura al-Mujadilah, 58, Ayah 21:

كَتَبَ اللَّهُ لَأَغْلِبَنَّ أَنَا وَرُسُلِي ۚ إِنَّ اللَّهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ

Allah swt ameandika: Hapana shaka Mimi na Mtume wangu tutashinda. Hakika Allah swt ni Mwenye nguvu, mwenye kushinda.

Tawallah maana yake ni kuwa rafiki wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na Ahl al-Bayt a.s. na

Tabarrah inamaana ya kujiepusha na kujiweka mbali na kutokuwa na uhusiano wowote pamoja na wale maadui wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. pamoja Ahl al-Bayt a.s.

252. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Ma’arij, 70, Ayah 22 -34:

وَالَّذِينَ فِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ مَعْلُومٌ {24}

لِلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ {25}

وَالَّذِينَ يُصَدِّقُونَ بِيَوْمِ الدِّينِ {26}

وَالَّذِينَ هُمْ مِنْ عَذَابِ رَبِّهِمْ مُشْفِقُونَ {27}

إِنَّ عَذَابَ رَبِّهِمْ غَيْرُ مَأْمُونٍ {28}

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ {29}

إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ {30}

فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ {31}

وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ {32}

وَالَّذِينَ هُمْ بِشَهَادَاتِهِمْ قَائِمُونَ {33}

وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ {34}

أُولَٰئِكَ فِي جَنَّاتٍ مُكْرَمُونَ

Isipokuwa wanaosali,

Ambao wanadumisha Sala zao,

Na ambao katika mali yao iko haki maalumu

Kwa mwenye kuomba na anayejizuilia kuomba;

Na ambao wanaisadiki Siku ya Malipo,

Na ambao wanaiogopa adhabu itokayo kwa Mola wao Mlezi.

Hakika adhabu ya Mola wao Mlezi si ya kuaminika nayo

Na ambao wanahifadhi tupu zao.

Isipokuwa kwa wake zao, au iliyowamiliki mikono yao ya kuume, basi hao hawalaumiwi –

Lakini wanaotaka kinyume ya haya, basi hao ndio wanaoruka mipaka.

Na ambao wanazichunga amana zao na ahadi zao,

Na ambao wanasimama imara katika ushahidi wao,

Na ambao wanazihifadhi sala zao.

Hao ndio watakao hishimiwa Jannah.

253. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema, katika Al-Kafi:

“Katika mlango wa Jannah kumeandikwa ‘Yapo mema kumi kwa mtoa Sadaka na mema kumi na nane kwa mkopeshaji madeni.”

Sifa Nne za Watu wa Jannah

254. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.:

“Yeyote yule atakayekuwa na sifa nne basi Allah swt ataliandika jina lake miongoni mwa watu wa Jannah:

Mtu ambaye mwepesi kwa kutoa shahada kuwa hakuna mungu mwingine isipokuwa Allah swt tu na Mimi Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ni Mtume wa Allah swt.

Mtu ambaye anasema: Alhamdu lillaah pale apatapo neema

Mtu yule asemaye Astaghfirullah pale atendapo dhambi

Na yule asemaye Inna lillaahi wa inna ilayhi rajiun pale apatapo msiba.

255. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Mumin masikini na mafukara ndio watakaokuwa wa kwanza kuingia Jannah kwa miaka arobaini kabla ya Mumin matajiri kuingia Jannah.

(Nitawapeni mfano. Ni sawa na meli mbili zinazopita katika vituo vya ukaguzi wa maofisa wa forodha. Naye baada ya ukaguzi anaona kuwa meli moja haina chochote, ipo tupu, hivyo ataiachilia ipite na kuendelea na safari yake. Na pale anapoikagua meli ya pili, anakuta kuwa imejaa shehena na hivyo huisimamisha na kuanza uchambuzi na ukaguzi.)

256. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliulizwa kuhusu Ayah ya Qur'an Tukufu: Surah al-Waqiah, 56, Ayah ya 10 , 11 , 12

وَالسَّابِقُونَ السَّابِقُونَ {10}

أُولَٰئِكَ الْمُقَرَّبُونَ {11}

فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ

Na wa mbele watakuwa mbele

Hao ndio watakao karibishwa

Katika Bustani zenye neema

257. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akasema:

“Jibrail a.s. kaniambia: ‘Inamaanisha Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. na Mashi’ah. Wao ndio watakao kuwa wa kwanza kabisa kukaribia Jannah, wakiwa wamemkurubia Allah swt, Aliye Mkuu, kwa heshima mahususi waliyojaaliwa.’”

258. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Alimwambia Imam ‘Ali bin Abi Tali as:

“Je itakuwaje pale ambapo wewe utakuwa umesimama mbele ya Jahannam, na Daraja (Siraat) litakapowekwa, na watu watakapoambiwa: ‘Vukeni Daraja (Siraat) hili.’

Na wewe utauambia moto wa Jahannam ‘Huyu ni kwa ajili yangu, na huyu ni ka ajili yako!’

Hapo Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alijibu:

“Ewe Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., je ni nani hao watakaokuwa pamoja nami?”

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akamjibu:

“Hao ni Mashi’ah wako, watakuwa pamoja nawe popote pale uwapo.”

Amepokewa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akisema:

“Haki ipo pamoja na Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. na Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. yupo pamoja na haki.”

Jahannam

259. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. kuhusu adhabu katika daraja la tatu la Jahannam (iitwayo Saqar) ni kama ifuatavyo:

“Humo yako Mateso makali mno, inapopumua wakazi wake huungua kuwa majivu kwa kutokana na joto lake, lakini hawatakufa. Nyama yao itaunganikana tena … Humo pia kuna kisima kiitwacho Saqar ambayo ni kwa ajili ya wale wajivunao, wakandamizaji na wadhalimu, na walioasi na ambapo mateso yatakuwa makubwa zaidi.

Iwapo hii ndiyo itakuwa hali ya daraja la nne la Jahannam sasa hebu fikiria hali itakayokuwa katika daraja la tano, sita na saba.

Tumwombe Allah swt atuepushe na Jahannam! Amin.

260. Al Imam Musa al-Kadhim a.s. amesema:

“Muelewe waziwazi kuwa hakuna atakayeishi katika Jahannam kwa milele isipokuwa kafiri, Munafiki na watendao madhambi na uasi. Ama kwa watu wataomaliza kutimiza kipindi cha adhabu zao, watatolewa huru kutoka Jahannam.”

261. Qur’an Tukufu Surah ya Al-Balad, 90, Ayah ya 19-20 zisemazo:

وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِنَا هُمْ أَصْحَابُ الْمَشْأَمَةِ {19}

عَلَيْهِمْ نَارٌ مُؤْصَدَةٌ

Lakini waliokanusha Aya Zetu, hao ndio watu wa upande wa shari.

Moto uliofungiwa (kila upande) utakuwa juu yao.

Qur’ani Tukufu Surah al-Humazah, 104, Ayah 5 – 9:

وَمَا أَدْرَاكَ مَا الْحُطَمَةُ {5}

نَارُ اللَّهِ الْمُوقَدَةُ {6}

الَّتِي تَطَّلِعُ عَلَى الْأَفْئِدَةِ {7}

إِنَّهَا عَلَيْهِمْ مُؤْصَدَةٌ {8}

فِي عَمَدٍ مُمَدَّدَةٍ {9}

Hasha! Bila shaka atavurumizwa katika (Moto unaoitwa) Hutama.

Na ni jambo gani litakalokujulisha (hata ukajua) ni nini (Huo Moto unaoitwa) Hutama? Ni Moto wa Allah swt uliowashwa (kwa ukali barabara).

Ambao unapanda nyoyoni.

Hakika huo (Moto) watafungiwa (wewemo ndani yake ).

Kwa magogo marefu marefu

262. Qur’ani Tukufu Surah al-Mursalat, 77: Ayah ya 32:

إِنَّهَا تَرْمِي بِشَرَرٍ كَالْقَصْرِ

"Hakika (Moto huo) hutoa macheche yaliyo kama majumba."

Milango ya Jahannam

263. Mlango wa kwanza

• Yeyote yule atakayekuwa na matumaini katika Allah swt basi daima atakuwa mtu mwenye furaha na mafanikio;

• Yeyote anayekuwa na khofu ya Allah swt basi anajaaliwa usalama;

• mtu mwovu na aliyepotoka na mstahiki wa adhabu za Allah swt ni yule ambaye hana matumaini yoyote kwa Allah swt na wala hana khofu ya aina yoyote ile ya Allah swt.

264. Mlango wa pili

• Yeyote yule asiyetaka kufanywa uchi Siku ya Qiyama, basi awavalishe nguo wale walio uchi humu duniani,

• Yeyote yule asiyetaka kupatwa na kiu Siku ya Qiyamah, basi awanywishe wale wenye kiu humu duniani,

• Yeyote yule asiyetaka kupatwa na njaa Siku ya Qiyamah, basi awalishe wale wenye njaa humu duniani.

265. Mlango wa tatu

• Allah swt huwalaani wale wasemao uongo,

• Allah swt huwalaani wale walio mabakhili,

• Allah swt huwalaani wale wanaowanyanyasa na kuwakandamiza wanyonge.

266. Mlango wa nne

• Allah swt humdhalilisha yule ambaye anaidharau Dini ya Islam,

• Allah swt humdhalilisha yule anayewakashifu Ahl ul-Bayt a.s. ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.

• Allah swt humdhalilisha yule ambaye anawasaidia wadhalimu katika kuwadhulumu watu.

267. Mlango wa tano

• Msiendekeze matamanio yenu, kwani matamanio yanapingana na tendo la kusadikisha;

• Musiyaongelee zaidi yale yasiyowahusu kwani mtaondoka katika Baraka za Allah swt;

• Na kamwe msiwe wasaidizi wa madhalimu.

268. Mlango wa sita

• Mimi nimeharamishiwa kukubalia Mujtahid (hawa ni wanavyuoni ambao wamefikia upeo wa juu wa Ijtihad, yaani uwezo wa kutoa fatwa).

• Mimi nimeharamishiwa kukubalia wale wanaofunga saumu.

269. Mlango wa saba

• Ujihisabie mwenyewe matendo yako kabla hujafanyiwa hesabu ya matendo yako;

• Uikaripie nafsi yako kabla wewe hujakaripiwa;

• Na mwabudu, Allah swt aliye Mkuu na aliyetukuka, kabla ya wewe hujafika mbele yake na ambapo hautaweza tena kumwabudu na kumtukuza.

270. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amenakiliwa katika uk.145, J.1 ya al-Zamakhshari’s Rabee’ al-Abrar akiwa amemwuliza Malaika Jibrail a.s.:

“Je ni kwa nini mimi kamwe sijamwona Malaika Mikaili a.s. akicheka au kutabasamu?”

Malaika Jibraili a.s. alimjibu:

“Mikaili kamwe hajacheka wala kutabasamu kuanzia pale Jahannam ilipoumbwa. ”

271. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema,

“Katika safari yangu ya usiku wa (‘Israa), mimi nilisikia sauti kubwa mno, hivyo nilimwuliza Malaika Jibrail a.s., ‘Je sauti hii kubwa ni ya nini, Ewe Jibraili ?’

Naye alinijibu,

‘Ni jiwe lililotupwa kutokea juu kuangukia ndani mwa Jahannam , na imekuwa ikianguka kwa muda wa vipindi sabini vya baridi, na sasa ndipo ilipofika chini.”

272. Abu ‘Asim ‘Ubayd ibn ‘Umayr ibn Qatadah al-Laythi, Hakimu wa Makkah (aliyefariki 68 A.H.), amesema,

“Jahannam hupumua mara moja kwa sababu yake Malaika na Mitume a.s. wote hutetemeka, kiasi kwamba hata Mtume Ibrahim a.s. alipiga magoti na kusema, “Ewe Mola wangu ! Nakuomba uniokoe!”

273. Abu Sa’eed al-Khudri amenakiliwa akisema,

“Iwapo milima itapigwa kwa rungu mara moja inayotumiwa na Malaika wa Jahannam , basi itavunjika vipande vipande na kuwa vumbi.”

274. Tawoos ibn Keesan al-Khawlani amenakiliwa akisema,

“Wakati Jahannam ilipoumbwa, Malaika walishtushwa mno, na wakati nyie wanaadamu mulipoumbwa, basi walitulia.” (kwa mantiki kuwa haikuubwa kwa ajili yao bali ajili ya wanadamu)

275. Al-Hasan ibn Yasar al-Basir amesema,

“Kwa kiapo cha Allah swt! Hakuna hata mja mmoja wa Allah swt anayeweza kustahimili joto la Jahannam ! Tumeambiwa iwapo mtu atasimama Mashariki na Jahannam ikawa upande wa magharibi na ikafunuliwa kidogo tu, basi bongo ya mtu huyo aliye Mashariki itachemka. Iwapo kama kiasi cha ndoo moja ya usaha wa Jahannam ukimwagwa juu ya ardhi hii ya dunia, basi hakuna hata kiumbe kimoja kitabakia hai.”

276. Abu Zar al-Ghaffari, Allah swt amwie radhi, alikuwa akisema,

“Waambieni wale ambao hupenda kulimbikiza utajiri wao kuwa watachomwa nayo juu ya paji la uso wao, pembeni mwao, na migongoni mwao hadi watakapokuwa wamejaa kwa mioto.”

277. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema, kama vile tuambiwavyo katika uk.243, J.8, ya Bihar al-Anwar,

“Hakuna Mja wa Allah swt mwenye utajiri au mali na hataki kulipa Zaka isipokuwa kwamba atachomwa kwa vipande hivyo vya mapesa vitakavyokuwa vimepashwa moto katika moto wa Jahannam na kwamba watatumbukizwa katika adhabu hizo kuanzia juu ya vipaji vyao vya nyuso zao na migongo yao hadi pale Allah swt atakapokuwa amemaliza kupokea mahisabu na adhabu za waja wake Siku ya Qiyamah, muda ambao ni wa maelfu ya miaka kwa mujibu wa mahisabu yetu. Hapo ndipo watakapotumwa ama kuingia Jannah au Jahannam.”

278. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Italetwa mbele yake, naye atachukizwa nayo; na itakapoletwa karibu yake, itauchoma uso wake na kifuvu kitadondoka. Iwapo ataweza kunywa hata kidogo kutokamo, basi matumbo yake yatakatika vipande vipande na kutokezea sehemu za nyuma ya kutokezea haja kubwa.”

279. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ameripotiwa akisema,

“Sala za mtu anayekunywa pombe hazikubaliwi kwa siku arobaini; na iwapo atakufa huku pombe ikiwamo tumboni mwake, basi Allah swt atamlazimisha anywe sadiid, maji yatokayo kwenye sehemu za uchi wa malaya ambayo yatakusanywa katika birika huko Jahannam na kupewa watu hawa, na kwayo matumbo na ngozi zao zitachomwa.”

280. Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. anavyotupatia picha ya Jahannam, tumwombe Allah swt asitutumbukize humo:

‘Janga kubwa kwa mtu ni kule kutumbukia katika Jahannam; yeye atajihisi kuwa anachemshwa mzima mzima, na ataona mateso yake yasiyoona mwisho, na kiumbe fulani kinakoroma na kupumua, viumbe vyote vilivyo humo hukosa raha na kamwe hawapati fursa ya kupumzika, na kamwe hawatapata kupumzika kutokana na adhabu zake au mauti ya uhakika. Yeye hasinzii hata kidogo wala hakutakuwa na mapumziko katiko mateso yake: Kutakuwa na maumivu ya kudumu kiasi ambacho tunamwomba Allah swt atunusuru na kutusaidia.’ (Hotuba 83).

281. Kwa hakika ni mahala pabaya kabisa kuliko sehemu yoyote ile, mahala ambapo mikono ya wakazi wake yanakuwa yamefungwa shingoni mwao, na vichwa vyao vimefungwa na miguu yao kwa minyororo na mavazi yao yametengenezwa kwa lami. Mashati yao yametengenezwa kwa moto wakati ambapo adhabu zao za moto usiozimika kamwe hazitakwisha kamwe mahala ambapo mlango wake utakuwa umejazwa watu, katika moto mkali kabisa kiasi kwamba sauti zao zinasikitisha na kutisha, na miale ya moto ikipaa na kufikia kila sehemu na wala hakuna kujitoa kutoka humo na wala hakuna muda utakaokwisha,na wala haina mwisho wake kwa wale wanaoteketezwa na kuchomwa humo.’ ( Hotuba 109 ).

282. ‘Joto lake ni kali mno, kufikia chini kwake ni mbali mno, sakafu yake ni chuma, vinywaji vyake ni usaha.’ (Hotuba 120).

283. Siku ya Qiyamah, madhalimu wote wataletwa bila ya kuwapo na mtu yoyote wa kuwasaidia au kuwatetea, na hivyo watatumbukizwa katika moto wa Jahannam na humo watasagwasagwa kama vile machine za kusaga zifanyavyo, hadi hapo watakapogonga vichwa katika sakafu ya chini kabisa.’ (Hotuba 164)

284. ‘Iwapo Malik (msimamizi wa Jahannam) atakuwa mkali, husababisha sehemu yake moja kuminyana na sehemu zingine, anapogombeza, milango yake huruka juu na chini (hutema kama volkeno). (Hotuba 183)

285. Ayah 23 ya Surah al-Fajr, 89 na katika Ayah zinginezo pia:

وَجِيءَ يَوْمَئِذٍ بِجَهَنَّمَ ۚ يَوْمَئِذٍ يَتَذَكَّرُ الْإِنْسَانُ وَأَنَّىٰ لَهُ الذِّكْرَىٰ

Basi Siku hiyo italetwa Jahannam. Siku hiyo mwanadamu atakumbuka, lakini kukumbuka huko kutamfaa nini ?

286. Qur’ani Tukufu , Sura al-Nisaa, 4, Ayah 140:

وَقَدْ نَزَّلَ عَلَيْكُمْ فِي الْكِتَابِ أَنْ إِذَا سَمِعْتُمْ آيَاتِ اللَّهِ يُكْفَرُ بِهَا وَيُسْتَهْزَأُ بِهَا فَلَا تَقْعُدُوا مَعَهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ ۚ إِنَّكُمْ إِذًا مِثْلُهُمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ جَامِعُ الْمُنَافِقِينَ وَالْكَافِرِينَ فِي جَهَنَّمَ جَمِيعًا

Naye amekwisha kuteremshieni katika Kitabu hiki ya kwamba mnaposikia Aya za Allah swt zinakanushwa na zinafanyiwa kejeli, basi msikae pamoja nao, mpaka waingie katika mazungumzo mengine. Hivyo mtakuwa nanyi mfano wao hao. Hakika Allah swt atawakusanya wanafiki na makafiri wote pamoja katika Jahannam.

287. Vile vile Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Surah al-Nisaa 4, Ayah 145:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ وَلَنْ تَجِدَ لَهُمْ نَصِي

Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka ya chini kabisa Jahannam, wala hutompata yeyote wa kuwanusuru.

288. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Nisaa, 4, Ayah 55:

فَمِنْهُمْ مَنْ آمَنَ بِهِ وَمِنْهُمْ مَنْ صَدَّ عَنْهُ ۚ وَكَفَىٰ بِجَهَنَّمَ سَعِيرًا

Basi wapo miongoni mwao walioamini, na wapo walioyakataa. Na Jahannam yatosha kuwa ni moto wa kuwateketeza.

289. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Jinn, 72, Ayah 23:

إِلَّا بَلَاغًا مِنَ اللَّهِ وَرِسَالَاتِهِ ۚ وَمَنْ يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا

... Na wenye kumuasi Allah swt na Mtume wake, basi hakika hao watapata Moto wa Jahannam wadumu humo milele.

290. Allah swt antuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Nisaa, 4 , Ayah 115:

وَمَنْ يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِنْ بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

Na anayempinga Mtume baada ya kudhihirikia uwongofu, na akafuata njia isiyokuwa ya Waumini, tutamuelekeza aliko elekea, na tutamwingiza katika Jahannam. Na hayo ni marejeo maovu.

291. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Kahaf, 18, Ayah 106:

ذَٰلِكَ جَزَاؤُهُمْ جَهَنَّمُ بِمَا كَفَرُوا وَاتَّخَذُوا آيَاتِي وَرُسُلِي هُزُوًا

Hiyo Jahannam ni malipo yao kwa walivyokufuru na wakafanyia kejeli Ishara zangu na Mitume wangu.

292. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu,Sura al-‘A’raf, 7, Ayah 179:

وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنْسِ ۖ لَهُمْ قُلُوبٌ لَا يَفْقَهُونَ بِهَا وَلَهُمْ أَعْيُنٌ لَا يُبْصِرُونَ بِهَا وَلَهُمْ آذَانٌ لَا يَسْمَعُونَ بِهَا ۚ أُولَٰئِكَ كَالْأَنْعَامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ ۚ أُولَٰئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ

Na tumeiumbia Jahannam majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni nyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walio ghafilika.

293. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-‘A’raf, 7, Ayah 18, Akasema:

قَالَ اخْرُجْ مِنْهَا مَذْءُومًا مَدْحُورًا ۖ لَمَنْ تَبِعَكَ مِنْهُمْ لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنْكُمْ أَجْمَعِينَ

Toka humo, nawe umekwisha fedheheka, umekwisha fukuzwa. Hapana shaka atakaye kufuata miongoni mwao, basi nitaijaza Jahannam kwa nyinyi nyote.

294. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura az-Zumar, 39, Ayah 32:

فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنْ كَذَبَ عَلَى اللَّهِ وَكَذَّبَ بِالصِّدْقِ إِذْ جَاءَهُ ۚ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِلْكَافِرِينَ

BASI NI NANI dhalimu mkubwa kuliko yule aliyemsingizia uwongo Allah swt na kuikanusha kweli imfikiapo ? Je! Siyo katika Jahannam makazi ya hao makafiri?

295. Na vile vile Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-A’raf, 7, Ayah 36:

وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَاسْتَكْبَرُوا عَنْهَا أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

Na wale watakaokanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi, hao ni watu wa Motoni; humo watadumu.

296. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Hud, 11, Ayah 113:

وَلَا تَرْكَنُوا إِلَى الَّذِينَ ظَلَمُوا فَتَمَسَّكُمُ النَّارُ وَمَا لَكُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ مِنْ أَوْلِيَاءَ ثُمَّ لَا تُنْصَرُونَ

Wala msiwategemee wanao dhulumu, usije ukakuguseni Moto. Wala nyinyi hamna walinzi badala ya Allah swt, wala tena hamtasaidiwa.

297. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Surah al-Maidah,5, Ayah 2:

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۖ إِنَّ اللَّهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ

…. Na saidianeni katika wema na ucha Mungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui….

298. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Jathiyah, 45, Ayah 24:

وَقَالُوا مَا هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا يُهْلِكُنَا إِلَّا الدَّهْرُ ۚ وَمَا لَهُمْ بِذَٰلِكَ مِنْ عِلْمٍ ۖ إِنْ هُمْ إِلَّا يَظُنُّونَ

Na walisema: Hapana ila huu uhai wetu a duniani – twafa na twaishi, na hapana kinacho tuhiliki isipokuwa dahar. Lakini wao hawana elimu ya hayo, ila wao wanadahani tu.

299. Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. anasema

Safari ndefu lakini matayarisho ya safari ni madogo. Tukiwa watumwa wa dunia basi tutatumbukia Jahannam .

300. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema katika Mizanul Hikmah kuwa:

“Mapenzi ya dunia ndiyo chanzo chote cha kila aina ya madhambi.”

301. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al- ‘Asra’, 17, Ayah 18:

مَنْ كَانَ يُرِيدُ الْعَاجِلَةَ عَجَّلْنَا لَهُ فِيهَا مَا نَشَاءُ لِمَنْ نُرِيدُ ثُمَّ جَعَلْنَا لَهُ جَهَنَّمَ يَصْلَاهَا مَذْمُومًا مَدْحُورًا

Anayetaka yapitayo upesiupesi, tutafanya haraka kumletea hapa hapa tunayoyataka kwa tumtakaye. Kisha tumemwekea Jahannam; ataingia humo hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa na kufurushwa.

302. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Tawbah, 9, Ayah 34 – 35:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ كَثِيرًا مِنَ الْأَحْبَارِ وَالرُّهْبَانِ لَيَأْكُلُونَ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ وَيَصُدُّونَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ ۗ وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنْفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَبَشِّرْهُمْ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ

يَوْمَ يُحْمَىٰ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ ۖ هَٰذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنْفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنْتُمْ تَكْنِزُونَ

Enyi mlioamini! Hakika wengi katika makuhani na wamonaki wanakula mali za watu kwa batili na wanazuilia Njia za Allah swt. Na wanaokusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia ya Allah swt. Wabashirie khabari ya adhabu iliyochungu.

Siku (mali yao) yatakapotiwa moto katika moto wa Jahannam , na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, “Haya ndiyo (yale mali) mliojilimbikia nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkikusanya.”

(Imeelezwa katika riwaya kuwa neno lililotumika katika Ayah hii kanz inamaanisha mali yoyote ile ambamo zaka haijatolewa).

303. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Anfal, 8, Ayah 15 – 16:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا زَحْفًا فَلَا تُوَلُّوهُمُ الْأَدْبَارَ

وَمَنْ يُوَلِّهِمْ يَوْمَئِذٍ دُبُرَهُ إِلَّا مُتَحَرِّفًا لِقِتَالٍ أَوْ مُتَحَيِّزًا إِلَىٰ فِئَةٍ فَقَدْ بَاءَ بِغَضَبٍ مِنَ اللَّهِ وَمَأْوَاهُ جَهَنَّمُ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ

Enyi Mlioamini! Mkikutana na waliokufuru vitani msiwageuzie mgongo.

Na atakayewageuzia mgongo wake siku hiyo – isipokuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi – basi atakuwa amestahiki ghadhabu ya Allah swt . Na pahala pake ni Jahannam, na huo ni mwisho muovu.

304. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Maida, 5, Ayah 32:

مِنْ أَجْلِ ذَٰلِكَ كَتَبْنَا عَلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ أَنَّهُ مَنْ قَتَلَ نَفْسًا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الْأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا ۚ وَلَقَدْ جَاءَتْهُمْ رُسُلُنَا بِالْبَيِّنَاتِ ثُمَّ إِنَّ كَثِيرًا مِنْهُمْ بَعْدَ ذَٰلِكَ فِي الْأَرْضِ لَمُسْرِفُونَ

Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika wakiwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi.

305. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Nisaa, 4, Ayah 93:

وَمَنْ يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا

Na mwenye kumuuwa Mumiin kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannam humo atadumu, na Allah swt amemkasirikia, na amemlaani, na amemuandalia adhabu kubwa.

306. Qur’ani Tukufu , Sura al-’Ali Imran, 3, Ayah 21:

وَمَنْ يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا

Hakika wanaozikataa Ishara za Allah swt , na wakawauwa Manabii pasipo haki, na wakawauwa watu waamrishao Haki wabashirie adhabu kali.

307. Watu wa Jannah watawauliza watu wa Jahannam kile kilichowaingiza Jahannam. Nao watawajibu kuwa wao hawakuwa miongoni mwa waliokuwa wakisali. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Muddathir, 74, Ayah 39 – 46:

إِلَّا أَصْحَابَ الْيَمِينِ {39}

فِي جَنَّاتٍ يَتَسَاءَلُونَ {40}

عَنِ الْمُجْرِمِينَ {41}

مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ {42}

قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ {43}

وَلَمْ نَكُ نُطْعِمُ الْمِسْكِينَ {44}

وَكُنَّا نَخُوضُ مَعَ الْخَائِضِينَ {45}

وَكُنَّا نُكَذِّبُ بِيَوْمِ الدِّينِ {46}

Isipokuwa watu wa kuliani.

Hao watakuwa katika mabustani, wawe wanaulizana

Khabari za wakosefu:

Ni nini kilichokupelekeni Motoni (Saqar) ?

Waseme: Hatukuwa miongoni waliokuwa wakisali.

Wala hatukuwa tukiwalisha masikini.

Na tulikuwa tukizama pamoja na waliozama katika maovu.

Na tulikuwa tukiikanusha Siku ya malipo.

308. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Surah al-Fussilat, 41, Ayah 7:

الَّذِينَ لَا يُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُمْ بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ

Ambao hawatoi Zaka na wanaikataa akhera.

309. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Nisaa, 4, Ayah 10:

إِنَّ الَّذِينَ يَأْكُلُونَ أَمْوَالَ الْيَتَامَىٰ ظُلْمًا إِنَّمَا يَأْكُلُونَ فِي بُطُونِهِمْ نَارًا ۖ وَسَيَصْلَوْنَ سَعِيرًا

Hakika wanaokula mali ya mayatima kwa dhuluma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni.

310. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al- Baqarah, 2, Ayah 275:

الَّذِينَ يَأْكُلُونَ الرِّبَا لَا يَقُومُونَ إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا إِنَّمَا الْبَيْعُ مِثْلُ الرِّبَا ۗ وَأَحَلَّ اللَّهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا ۚ فَمَنْ جَاءَهُ مَوْعِظَةٌ مِنْ رَبِّهِ فَانْتَهَىٰ فَلَهُ مَا سَلَفَ وَأَمْرُهُ إِلَى اللَّهِ ۖ وَمَنْ عَادَ فَأُولَٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {275}

Wale walao riba hawasimami ila kama anavyosimama aliyezugwa na Shaitani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba. Lakini Allah swt ameihalalisha biashara na ameiharamisha riba. Basi aliyefikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi,, kisha akajizuia, basi yake ni yaliyokwisha pita, na mambo yake yako kwa Allah swt. Na wenye kurudia basi hao ndio watu wa Motoni, humo watadumu.

Allah swt huiondolea baraka riba, na huzibariki sadaka…

311. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Ibrahim, 14, Ayah 28 – 29:

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ بَدَّلُوا نِعْمَتَ اللَّهِ كُفْرًا وَأَحَلُّوا قَوْمَهُمْ دَارَ الْبَوَارِ {28}

جَهَنَّمَ يَصْلَوْنَهَا ۖ وَبِئْسَ الْقَرَارُ

Hebu hukuwaona wale waliobadilisha neema ya Allah swt kwa kukufuru, na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamizo ?

Nayo ni Jahannam ! Wataingia. Maovu yaliyoje makazi hayo !

312. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Surah al-Mutaffifiin, 83, Ayah 1 – 10:

وَيْلٌ لِلْمُطَفِّفِينَ {1}

الَّذِينَ إِذَا اكْتَالُوا عَلَى النَّاسِ يَسْتَوْفُونَ {2}

وَإِذَا كَالُوهُمْ أَوْ وَزَنُوهُمْ يُخْسِرُونَ {3}

أَلَا يَظُنُّ أُولَٰئِكَ أَنَّهُمْ مَبْعُوثُونَ {4}

لِيَوْمٍ عَظِيمٍ {5}

يَوْمَ يَقُومُ النَّاسُ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ {6}

كَلَّا إِنَّ كِتَابَ الْفُجَّارِ لَفِي سِجِّينٍ {7}

وَمَا أَدْرَاكَ مَا سِجِّينٌ {8}

كِتَابٌ مَرْقُومٌ {9}

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِلْمُكَذِّبِينَ

Ole wao hao wapunjao!

Ambao wanapojipimia kwa watu hudai watimiziwe.

Na wao wanapowapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza.

Kwani hawadhani hao kwamba watafufuliwa

Katika Siku iliyo kuu,

Siku watapomsimamia watu Mola Mlezi wa walimwengu wote ?

Hasha! Hakika maandiko ya wakosefu bila ya shaka yamo katika Sijjin.

Unajua nini Sijjin ?

Kitabu kilichoandikwa.

313. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Humaza, 104, Ayah 1 – 9.

وَيْلٌ لِكُلِّ هُمَزَةٍ لُمَزَةٍ {1}

الَّذِي جَمَعَ مَالًا وَعَدَّدَهُ {2}

يَحْسَبُ أَنَّ مَالَهُ أَخْلَدَهُ {3}

كَلَّا ۖ لَيُنْبَذَنَّ فِي الْحُطَمَةِ {4}

وَمَا أَدْرَاكَ مَا الْحُطَمَةُ {5}

نَارُ اللَّهِ الْمُوقَدَةُ {6}

الَّتِي تَطَّلِعُ عَلَى الْأَفْئِدَةِ {7}

إِنَّهَا عَلَيْهِمْ مُؤْصَدَةٌ {8}

فِي عَمَدٍ مُمَدَّدَةٍ {9}

Ole wake kila safihi, msengenyaji !

Aliyekusanya mali na kuyahisabu.

Anadhani kuwa mali yake yatambakisha milele !

Hasha! Atavurumishwa katika Hutama

Na nani atakujuvya ni nini Hutama ?

Moto wa Allah swt uliowashwa.

Ambao unapanda nyoyoni.

Hakika huo utafungiwa nao

Kwenye nguzo zilionyooshwa.

314. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Surah al-Mumin, 23, Ayah 43:

مَا تَسْبِقُ مِنْ أُمَّةٍ أَجَلَهَا وَمَا يَسْتَأْخِرُونَ

Hapana umma uwezao kutanguliza ajali yake wala kuikawiza.

315. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Asra’, 17, Ayah 27:

إِنَّ الْمُبَذِّرِينَ كَانُوا إِخْوَانَ الشَّيَاطِينِ ۖ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِرَبِّهِ كَفُورًا

Kwa hakika wabadhirifu ni ndugu wa Masheitani. Na Shaitani ni mwenye kumkufuru Mola wake Mlezi.

316. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Zukhruf, 43, Ayah 74:

إِنَّ الْمُجْرِمِينَ فِي عَذَابِ جَهَنَّمَ خَالِدُونَ

Kwa hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya Jahannam

Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa.

317. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Nisaa, 4, Ayah 14:

وَلَنُسْكِنَنَّكُمُ الْأَرْضَ مِنْ بَعْدِهِمْ ۚ ذَٰلِكَ لِمَنْ خَافَ مَقَامِي وَخَافَ وَعِيدِ

Na anayemuasi Allah swt na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake, (Allah swt ) atamtia Motoni adumu humo, na atapata adhabu ya kudhalilisha.

318. Allah swt amewaamrisha Malaika kuwa:

Mtu anaponuia kutenda jambo jema wamwamdikie thawabu. Na anapoanza kutembea katika kulifanya tendo jema basi hapo pia anaongezewa thawabu nyingi na pale anapolianza kutenda tendo jema basi huongezewa zaidi ya hayo na anapomaliza kulitenda tendo jema basi hapo analipwa thawabu nyingi mno zisizo na hisabu.

319. Lakini mtu anaponuia kutenda dhambi basi hapo haandikiwi adhabu, na anajitoa kwenda kutenda dhambi napo pia haandikiwi kwa sababu inawezekana akarudia njiani na anapolianza tendo ovu pia kuna uwezekano wa kutolikamilisha na kwa masikitiko makubwa, anapolikamilisha basi kwa huruma zake Allah swt, huandikiwa dhambi moja tu.