read

Madhambi na Athari Zake

90. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w, Biharal- Anwar, J. 77, Uk. 79 na Mustadrak Al-Wasail, J.11, Uk. 330:

“Msitazame udogo wa dhambi, lakini muangalie mliyemuasi (Allah swt).”

91. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Bihar al- Anwar, J. 70, Uk.18:

“Iwapo mtu anapenda kujiona vile alivyo mbele ya Allah swt, basi ajitathmini kwa madhambi na maasi yake mbele ya Allah swt; basi kwa kipimo hicho ndivyo alivyo huyo mtu mbele ya Allah swt.”

92. Al-Imam Ja’far as-Sadiq a.s. aliwauliza watu ni kwa nini wanamwudhi Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Basi mmoja wa watu alimwuliza Imam a.s. vipi, naye Imam a.s. aliwaambia, Usul-i-Kafi , J.1, Uk. 219:

“Je hamujui kuwa matendo yenu yanajulishwa kwa Mtume Mtukufu s.a.w.w na pale aanapoona madhambi dhidi ya Allah swt miongoni mwao, basi husikitishwa mno. Kwa hivyo msimuudhi Mtume wa Allah swt na badala yake mnatakiwa kumfurahisha (kwa kutenda mema).”

93. Amesema Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Ghurur al-Hikam, Uk. 235:

“Kukosa kusamehe ni kasoro moja kubwa kabisa na kuwa mwepesi katika kulipiza kisasi ni miongoni mwa madhambi makubwa kabisa.”

94. Kutokea Asbaghi bin Nabatah kutokea kwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Amesema, Al-Khisal,cha as-Sadduq, J. 2, Uk. 360:

“Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa Allah swt anapoikasirikia Ummah na kama hakuiadhibu basi bei za vitu vitapanda juu sana yaani maisha yatakuwa ghali, maisha yao yatakuwa mafupi, biashara zao hazitaingiza faida, mazao yao hayatukuwa mengi, mito yao haitakuwa imejaa maji, watanyimwa mvua (itapungua), na watatawaliwa na waovu miongoni mwao.”

(Yaani Hadith hiyo juu inatubainishia kuwa iwapo kutakuwa na jumuiya ambayo imejitumbukiza katika madhambi basi wanabashiriwa kupatwa na mambo saba hayo yaliyotajwa.)

95. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. Amesema kuwa amekuta katika kitabu cha Al-Amir al-Muminiin Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. akisema kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.Amesema, Safinat –ul-Bihar, J. 2, Uk.630:

“Wakati zinaa itakapokithiri katika jumuiya basi idadi za mauti za ghafla zitakithiri; na patakapokuwa na uovu basi Allah swt atawatumbukiza katika maisha ya ghali na hasara. Wakati watu watakapoacha kulipa zaka , basi ardhi itazinyakua baraka zake kutokea mazao, matunda, madini na vitu vyote kama hivyo.

Wakati watakapotenda bila haki kwa mujibu wa Shariah, basi itakuwa sawa na kumsaidia dhalimu na ugaidi. Na watakapozikiuka ahadi zao, basi Allah swt atawafanya maadui wao kuwasaliti na kuwakandamiza. Wakati watakapoacha uhusiano pamoja na ndugu na Jama’a zao, basi yote yale wayamilikiayo yatakwenda mikononi mwa waovu.

Na wakati watakapojiepusha na kutoa nasiha ya mambo mema na kuyakataza maovu na kama hawatawafuata waliochaguliwa Ahl-ul-Bayt a.s., basi Allah swt atawasalitisha kwa walio wenye shari miongoni mwao na katika hali hii, wataomba duaa lakini hazitakubalika.”

96. Amesema Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s., Bihar al- Anwar , J .70, Uk. 55:

“Machozi hayaishi illa kwa nyoyo kuwa ngumu, na nyoyo haziwi ngumu illa kukithiri kwa madhambi.”

97. Allah swt alimwambia Mtume Dawud a.s.: Ithna-Ashariyyah, Uk. 59:

“Ewe Dawud ! Wabashirie habari njema wale watendao madhambi kuhusu msamaha wangu, ambayo inajumuisha kila kitu kilichopo humu duniani, ili wasikate tamaa ya msamaha wangu; na waonye wale watendao mema kwa adhabu zangu ili wasije wakajifanyia ufakhari kwa utii wao, kwani ufakhari ni dhambi mbaya kabisa.”