read

Marafiki na Urafiki

506. Mtume Muhammad s.a.w.w. Amesema, Bihar al-Anwaar, J. 74, Uk. 192:

“Mtu anaathirika kwa imani ya marafiki zake. Kwa hivyo, muwe waangalifu kabisa katika urafiki wenu pamoja nao.1

507. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s., Amesema: Bihar al-Anwaar, J. 76, Uk. 267:

“Uwe rafiki wa yule ambaye atakuwa ndio heshima yako, si wewe uwe heshima yake. (Ufanye urafiki na wale walio juu yako ili wewe uweze kupata maendeleo kutokana na urafiki huo).

508. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. Amesema, Bihar al-Anwaar, J. 74 Uk. 282:

“Ndugu yangu mpenzi ni yule (anayenitambulisha) makosa na kasoro zangu.

509. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Amesema, Khisal-i-Sadduq, J. 1, Uk. 88.:

“Kwa hakika kuna marafiki wa aina tatu kwa ajili ya Muislam:

1. Rafiki anayesema mimi niko pamoja nawe iwapo upo hai au umekufa: Na haya ndio matendo yake.

2. Rafiki anayesema mimi rafiki yako hadi ukingoni mwa kaburi na nitakuacha: hawa ni watoto wake.

3. Rafiki anayesema mimi nitakuwa nawe hadi pale utakapo kufa: hii ni mali ambayo ataiacha humu duniani kwa warithi wake baada ya kifo chake.

Tanbih

Kutokana na riwaya hii, tunaelewa kuwa kitu ambacho kitakuwa pamoja na huyo mtu aliye kufa na kuaga dunia hii katika siku ya Qiyamah ni imani na matendo yake mema. Na suala hili limezungumziwa katika ahadithi nyingi sana za Kiislam na vile vile katika ayah za Qur’an tukufu, kwa mfano:

510. Allah swt anatuambia katika Qur’an Sura Ar-Raa’d, 13, ayah ya 29.

الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ طُوبَىٰ لَهُمْ وَحُسْنُ مَآبٍ

Wale walio amini na wakatenda mema watakuwa na raha na marejeo mazuri.

511. Allah swt anatuambia katika Qur’an Sura Al-Kahf,18, ayah 30.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ إِنَّا لَا نُضِيعُ أَجْرَ مَنْ أَحْسَنَ عَمَلًا

Hakika wale walio amini na wakatenda mema – hakika Sisi hatupotezi ujira wa anaye tenda mema.

512. Allah swt anatuambia katika Qur’an tukufu Sura Al-Kahf, 18, ayah ya 107.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَانَتْ لَهُمْ جَنَّاتُ الْفِرْدَوْسِ نُزُلًا

Hakika wale walio amini na wakatenda mema mashukio yao yatakuwa kwenye Pepo za Firdausi.

513. Allah swt anatuambia katika Qur’an tukufu Sura Maryam,19, ayah ya 96.”

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَيَجْعَلُ لَهُمُ الرَّحْمَٰنُ وُدًّا

Hakika walio amini na wakatenda mema Arrahmani Mwingi wa Rehema atawajaalia mapenzi.

514. Amesema Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. , Bihar al-Anwaar, J. 74 Uk. 187:

“Muwe waangalifu katika kutafuta marafiki wa kweli na mujaribu kuwafanyia majaribio, kwa sababu wao watakuwa ndio msaada wenu pale mnapokuwa katika hali nzuri na watetezi wenu pale mtapokuwa katika shida na matatizo.”

515. Amesema Al Imam Zaynul 'Abediin a.s. , Bihar al-Anwaar, J. 78, Uk. 141:

“Kukutana pamoja na wacha Mungut kunawaleteeni mema.”

516. Al Imam Zaynul 'Abediin a.s. Amesema, Bihar al-Anwaar, J. 78, Uk. 151:

“Jitahadharisheni na urafiki wa watendao madhambi, na kuwasaidia madhalimu.”

  • 1. Kwa hakika tunaona leo vijana hata wazee wameathirika sana katika jamii kwa sababu ya marafiki kijana anakuwa na marafiki wabaya walevi atakuwa mlevi wavuta bangi atakuwa anavuta bangi wenye kutumia madawa ya kulevya naye atatumia madawa ya kulevya wakiwa wanaenda kwenye mambo ya uasherati na watoto watakuwa waasherati n.k. vivyo hivyo utaona hawa vijana wanajitenga na utamaduni wa nyumbani kwao kwa sababu ya kuathirika shauri ya urafiki wa wenzao wengine hata wanathubutu kutoroka nyumbani n.k. Ndio kwa sababu hiyo utaona Uislam unatia umuhimu sana katika suala hili la kuwachukua marafiki ambao wana tabia nzuri ili maingiliano yetu nao yasitutoe katika dini na utamaduni wetu utaona wengine wakati wa kusali ndio wanapenda kwenda kupiga masoga mabarazani kwa hiyo nasi pia tunaacha kusali tunakalia kupiga soga na wana mbinu nyingi sana za kutupotosha sisi ili maadili yetu yavuje yamomonyoke tuwe na majina ya Waislam lakini tusiwe na tabia na desturi za Kiislam.