read

Mwenye Kuripoti Ahadith Aweje?

Kwa hakika somo hili ni kubwa na lenye kwenda kwa undani zaidi, lakini kwa ajili ya wasomaji, tunawaleteeni habari hizi kwa kifupi ili kuwafaidisha.

Katika lugha ya Kiarabu, mtu anayeripoti riwaya huitwa Rawi na sifa zake zimeelezwa na kubainishwa na Ma’ulamaa walio mabingwa wa elimu ya Ahadith:

1. Rawi lazima awe mtu mwenye akili na fahamu timamu. Riwaya zozote zitakazotolewa katika hali ya kuehuka au kurukwa na fahamu, basi hazitathaminika au kukubalika.

2. Ni lazima Rawi awe amebalehe na Mukallaf, yaani shariah za Dini ziwe zimeshakwisha kuwa faradhi juu yake. Hapa inawajumuisha vijana na watoto na wale wote ambao bado hawajabalehe lakini wanaweza kutofautisha baina ya wema na ubaya. Aina hii ya vijana hao huitwa Mumayyiz na hivyo riwaya zao zinapotimika masharti mengineyo, huweza kukubalika na kusadikika.

3. Ni lazima Rawi awe Mwislamu. Riwaya za mtu asiye Mwislamu haziwezi kuaminiwa au kusadikiwa.

4. Rawi lazima awe ni Mwislamu mfuasi wa Madhehebu ya Sh’iah Ithna-Asheria. Lakini iwapo kutakuwa na riwaya kutokea Mwislamu mfuasi wa Madhehebu mengine, basi kwa uzito wa dalili zinginezo na kufanya uchunguzi iwapo huyo Rawi ni mtu aaminiwaye katika historia.

5. Uadilifu wa Rawi pia ni sharti mojawapo, yaani asiwe akifanya madhambi makuu (ghunah-i-Kabira) na wala asiwe akirudiarudia madhambi madogo madogo (ghunah-i-saghirah).

Sheikh Tusi a.r. ametilia mkazo swala hili kwa kuelezea kuwa kuna tofauti katika uadilifu wa Rawi na mtoa ushahidi. Iwapo Rawi ni fasiki na iwapo itathibitika kuwa yeye katika riwaya yake na habari zake ni mkweli bila ya udanganyifu, basi riwaya yake inaweza kufuatwa.

6. Rawi asiwe msahaulivu, bali awe ni mtu mwenye kukumbuka vyema na udhibiti wake, (yaani haimaanishi kuwa Rawi asiwe akisahau kama mtu wa kawaida) yaani Rawi anapotaka kuelezea riwaya au Hadith, basi asiwe na mushkeli wa kuikumbuka.