read

Sadaka na Misaada

537. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Sadaka inalipia madeni na inaongezea katika barakah.”

538. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amenakili riwayah kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa:

“ Sadaka inamwepusha mtu na ajali mbaya.”

539. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. anasema kuwa:

“Mtu yeyote yule aliye mja wa Allah swt akiwa Mumin akatoa Sadaka, basi Allah swt baada ya kifo chake huyo mtu huwaweka vyema na kuwasaidia wananyumba yake katika hali njema.”

Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akaendelea kusema:

“Faida ya kutoa Sadaka ni kwamba inamsaidia kulipia madeni na vile vile kuongezea katika baraka.”

540. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Kusaidia na kutoa sadaka vyote hivyo vinaondoa umasikini na hurefusha umri wa mtu. Na yule anayetoa huweza kuepukana na aina sabini za ajali mbaya.

541. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. katika kuelezea tafsiri ya aya, ya Qur'an Tukufu, Sura Al-Layl, 92 , Ayah ya 5 na 6:

فَأَمَّا مَنْ أَعْطَىٰ وَاتَّقَىٰ

وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَىٰ

Hakika juhudi zenu bila ya shaka ni mbali mbali

Ama mwenye kutoa na akamcha Mungu.

Ndipo amesema kuwa;

Allah swt ndivyo anavyo walipa wale watendao mema, kwa mema yao mara kumi, au hata mara laki moja na hata zaidi ya hapo.

Na vile vile amesema kuwa: anayetoa katika njia ya Allah swt basi Allah swt humjaalia kila aina ya tawfiqi katika kazi hiyo ya khairi.”

542. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amemnakili Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa

“Mtu yeyote yule ambaye anamwamimi Allah swt kuwa atamlipa na atamwongezea zaidi ya kile anacho kitoa basi huyo mtu kwa moyo mkunjufu na bila aina ya ubakhili wowote atatoa sadaka na misaada kwa wingi kabisa.”

543. Amesema Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amemnakili Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa

“Siku ya Qiyama ardhi itakuwa imepata moto kupita kiasi na mumin watakuwa katika kivuli na kivuli hicho itakuwa ni kile alicho kuwa akitoa Sadaka.”

544. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amenakili riwayah moja kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akisema kuwa:

“Enyi watu! Toeni sadaka bila shaka sadaka inaongezea katika mali yenu, na hivyo mtoe sadaka na Allah swt atawarehemu.”

545. Al Imam Musa al-Kadhim a.s. amesema kuwa:

“ Toeni sadaka mjipatie riziki.”

546. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“ Toeni sadaka mjiongezee riziki yenu. Bila shaka anayeamini kuwa Allah swt hulipa mambo yote. Basi yeye huwapa sadaka masikini kwa kupita kiasi. Allah swt humjaalia riziki kwa njia mbalimbali kwa kile huyu mtu akitoacho katika mali yake.”

547. Al Imam ‘Ali ar-Ridha a.s. amenakili riwayah kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akisema kuwa:

“Kuwa na akida ya Tawhid ni nusu ya sehemu ya dini, enyi watu! Toeni Sadaka ili mpate riziki zaidi”.

548. Al Imam ‘Ali ar-Ridha a.s. ametoa riwayah kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa:

“Kuwa mali halisi ya mtu ni ile ambayo yeye ametolea sadaka.”

549. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema kuwa:

“Toeni Sadaka asubuhi na mapema ili balaa zisiwafikieni katika siku nzima.”

550. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amenakili riwayah kutoka Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kuwa:

“Sadaka ni kinga dhidi ya moto wa Jahannam .”

551. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alikuwa akisema:

“ Enyi watu muwatibu wagonjwa wenu kwa kutoa Sadaka.”

552. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. katika Nahjul Balagha amesema kuwa:

“Mnapoona riziki yenu inapungua na kuwa finyu basi muwe mkitoa sadaka ndivyo mtakuwa mkifanya biashara na Allah swt.”

553. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“ Imani ya muumini inakuwa na sifa nne za lazima,

Awe na tabia njema,

Awe mkarimu na mwepesi wa kutoa

Asizungumze zaidi ya yale yanayo takikana (hazungumzi mambo ovyo ovyo)

Hutumia kile kiasi kinacho takiwa, siyo mfujaji (anaotoa katika njia ya Allah swt).

554. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema kuwa:

“Iwapo mimi nitakwenda Hijja moja basi afadhali niwafanye huru watumwa kumi, lakini iwapo mimi nitajichukulia jukumu la kuwalisha familia ya Waislamu ambao wanashida ya chakula na ambao wanaishi kwa njaa nikawamalizia shida zao, nikawavalisha nguo wale ambao hawana nguo, na nikawarudishia heshima yao miongoni mwa watu, basi mimi ninaona jambo hili ni afadhali na bora zaidi kuliko hata kwenda kuhiji Hijja sabini.”

555. Al Imam Musa al-Kadhim a.s. aliijiwa na mtu mmoja na aliyeuliza,

“Ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w! Mimi ninazo pesa na utajiri je ni jambo gani afadhali nitoe sadaka au nimnunue mtumwa na kumfanya huru?”

556. Kwa hayo Al Imam Musa al-Kadhim a.s. alimjibu kuwa:

“Kuwa mimi ninaonelea kuwa kutoa Sadaka ni afadhali zaidi.”

557. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Siku moja Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwuliza Maimuna binti Harun, Je Kijakazi wako amekuwaje? Akasema Maimuna kwa hayo alimjibu Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., ‘Ewe Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.! Mimi nimemfanya huru.’

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwambia “Iwapo kama wewe ungelichukua jukumu la kumlisha, kumtunza, kumsaidia na kumwonea huruma basi ingekuwa afadhali zaidi.”

558. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Muwatibu wagonjwa wenu kwa Sadaka, na muzuie maafa kwa kuomba dua na kutoa sadaka muongezee riziki zenu zipanuke, na kwamba Sadaka inawaepusheni na mitego ya mashetani sabini.”

559. Siku moja walikuja wagonjwa wakilalamikia magonjwa yao mbele ya Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s., naye akawaambia;

“Nendeni mtoe Sadaka kwa ajili ya magonjwa yenu na mtapona, iwapo mtu atatoa Sadaka kwa kile akitumiacho kwa siku dharura wake, basi Allah swt huahirisha hata kifo chake na vile vile humwepusha na ajali mbaya.”

560. Al Imam ‘Ali ar-Ridha a.s. aliulizwa na Sahaba mmoja:

“Ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.! Mimi watoto wangu wawili wamefariki na amebakia mtoto wangu mdogo.”

Kwa hayo Al Imam ‘Ali ar-Ridha a.s. kamwambia:

“Basi toa Sadaka kwa niaba ya mtoto wako huyo.”

Na siku moja Al Imam ‘Ali ar-Ridha a.s. alipomtembelea huyo mtu akamwambia,

“Mwambie mtoto wako huyo atoe Sadaka kwa mkono wake walau kiasi kidogo chochote kile au hata kama kitakuwa ni kipande kidogo tu. Utambue wazi kuwa kiasi chochote kile hata kikiwa kiasi gani kama kitatolewa kwa roho safi basi mbele ya Allah huwa ni kipenzi, kwani Allah swt ameelezea kuwa:

Qur’an Tukufu, Surah Az-Zilzalah,99, Ayah7 - 8

فَمَنْ يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ

وَمَنْ يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ

Basi anaye tenda chembe ya wema, atauona !

Na anaye tenda chembe ya uovu atauona !

561. Vile viel Al Imam ‘Ali ar-Ridha a.s. alimwelezea kuwa:

“Allah swt amesema katika Qur’an Tukufu, Surah Al-Balad,90, Ayah11 – 16

فَلَا اقْتَحَمَ الْعَقَبَةَ {11}

وَمَا أَدْرَاكَ مَا الْعَقَبَةُ {12}

فَكُّ رَقَبَةٍ {13}

أَوْ إِطْعَامٌ فِي يَوْمٍ ذِي مَسْغَبَةٍ {14}

يَتِيمًا ذَا مَقْرَبَةٍ {15}

أَوْ مِسْكِينًا ذَا مَتْرَبَةٍ

Lakini hakujitoma kwenye njia ya vikwazo vya milimani.

Na nini kitakujuvya ni nini njia ya vikwazo vya milimani ?

Kumkomboa mtumwa;

Au kumlisha siku ya njaa

Yatima aliye jamaa,

Au masikini aliye vumbini

“Hivyo ewe Sahaba uelewe kuwa Allah swt anaelewa wazi wazi kuwa si watu wote wenye uwezo wa kuwanunua na wenye kufanya huru watumwa hivyo yeye ameweka thawabu hizo hizo kwa wale watakao toa Sadaka au watakao walisha yatima na masikini.”

562. Al Imam Musa al-Kadhim a.s. alijiwa mtu mmoja mbele yake na kuelezea habari za mtoto wake, na kwa hayo Al Imam akamjibu:

“Toa Sadaka kwa niaba yake.”

Na mtu huyo akajibu kuwa

“Sasa mtoto wake amekuwa na umri yaani amekuwa kijana.”

Basi Al Imam Musa al-Kadhim a.s. alimwambia kuwa

“Mtoto wako atoe Sadaka kwa mkono wake, hata kama itakuwa ni kipande cha mkate, na hapo ndipo Al Imam Musa al-Kadhim a.s. alisema riwayah ya Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. kuwa:

“Katika Israil alikuwa mtu mmoja aliyekuwa akimpenda mno mtoto wake, na akaona katika ndoto yake anaambiwa kuwa, mtoto wako huyo umpendaye mno atakufa usiku wa ndoa yake. Kulipowadia usiku wa arusi baba mzazi wa mtoto huyo, usiku kucha akawa katika wasiwasi na hakupata usingizi na kamwe hakupata raha usiku huo.

Na kulipo pambazuka asubuhi na mtoto alipotoka chumbani mwake akiwa hai basi baba yeke alimwuliza

‘Ewe mwanangu! Je katika usiku huu wako wa kuamukia leo umefanya mema yoyote?’

Kwa hayo mtoto akajibu

“Ewe baba yangu! hakuna jambo la maana sana lililotendeka, bali alitokezea masikini mmoja akaja mlangoni kuomba chakula, alikuwa na njaa na kile chakula walichokuwa wameniwekea, mimi nikampa chakula chote huyo mtu aliyekuja kuomba.’

Kwa hayo baba yake akasema

“Kwa sababu hii tu ndiyo Allah swt amekuondoshea balaa kubwa iliyokuwa ikupate wewe usiku huo.”

563. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. anasema kuwa:

“Kwa kutoa Sadaka kwa mkono wako mwenyewe basi unajiepusha na ajali mbaya, unajiepusha na balaa na maafa sabini na mitego ya mashetani sabini na ambamo kila shetani yuko anakwambia ‘ewe fulani! Usitoe Sadaka kamwe.”

564. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Mgonjwa atoe Sadaka kwa mkono wake mwenyewe na anayempa amwambie amwombee dua”.

565. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. katika hadith zake amesema kuwa:

“Mkono uliye juu yaani mtoaji ni afahali kuliko mkono ule ulio chini yake, yaani mpokeaji.”

566. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema kuwa:

“Kuna aina tatu ya mikono:

kwanza ni mkono ule wa Allah swt ambao uko juu kabisa na kwa hakika neema zote ni za Allah swt,

mkono wa pili ni ule mkono wa yule mtu anaye toa, ambaye anatoa katika njia ya Allah swt na

mkono wa tatu ni wa yule anaye pokea ambao mkono uliochini wa yule anayetoa. Kwa hivyo enyi watu chochote kile kinachobakia miongoni mwenu mtoe katika njia ya Allah swt na musikalifishe nafisi zenu”.

567. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alikuwa amemfanyia usia Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.; Ewe ‘Ali! Ninakufanyia usia wa mambo mema machache na uyakumbuke vyema.

Ewe Allah swt umsaidie Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Baada ya hapo wakati akifanya usia, Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alisema: Ama kuhusiana na sadaka tafadhali usiwe na mnunguniko wowote. Utoe kiasi kwamba mpaka uhisi kwamba wewe umefuja mali yako, lakini utambue wazi kuwa hiyo sio ufujaji bali hiyo umetoa katika njia ya Allah swt.”

568. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. anasema kuwa kuna riwayah kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa

“Toeni Sadaka, angalau hata kwa sa’ ya tende, na kama sa’ moja hiyo hamnayo basi mtoe tende kwa kiganja kimoja na hata kama hivyo haitawezekana basi mtoe tende kiasi chochote kile na kama hivyo haitawezekana basi mtoe angalau kokwa moja ya tende, na kama hivyo pia haitawezekana basi yule masikini aliyekuja kuwaomba mumwambie maneno mazuri na matamu na maneno matakatifu katika kumwelezea kuwa hakuna chochote, na hiyo pia ni sadaka.

Kwa sababu isitokee Siku ya Qiyama kwamba Allah swt atakapo kuuliza hesabu ya neema alizokujaalia akakuambia

‘Ewe mja! Mimi nilikupa mambo chungu nzima, sasa hebu angalia nafsini mwako je kwa kutumia neema hizo wewe umejiandalia nini?’

Na hapo wewe utaangalia sehemu zote nne za dunia na utajawa na masikitiko, na utakuta hakuna jambo lolote lile litakalo kuokoa dhidi ya adhabu za Allah swt.”

569. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema kuwa:

“Mtoe tende kiasi fulani kwani itawaokoa na moto wa Jahannam , mpanue riziki zenu na mteremshiwe riziki nyingi kwa kutoa Sadaka na kupitia dua mziondoe balaa na shida zenu.”

Mkumbuke kuwa kwa kutoa Sadaka hamtapungukiwa katika mali yenu. Na miongoni mwa jamaa zenu wanapokuwa na shida muwasaidiapo hiyo siyo Sadaka bali hiyo ni wajibu wenu.”

570. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema kuwa:

“Kulikuwa na mja mmoja aliyekuwa akifanya ibada ya Allah swt kwa umri wake wa miaka themanini.

Siku moja alimwona mwanamuke mmoja mzuri aliyekuwa akipendeza naye akawa ameingia katika mtego wake. Yeye alitimiza matamanio yake visivyo halali na mara akatokezea Malakul mauti (malaika anayetoa roho). Ulimi wake ulifunga kuongea na jasho lilianza kumtoka na kutokwa kwa roho na mara hapo alipita masikini akiomba.

Basi mtu huyu ambaye alikuwa katika hali ya kukata roho alimwambia yule masikini kwa ishara kuwa mahala fulani kuna mkate hivyo auchukue hivyo aweze kula huyo masikini, na masikini huyo alivyoelekezwa akauchukua mkate akaondoka zake.

Kwa hiyo ikatokea kwamba Allah swt aliibatilisha ibada zake za miaka themanini kwa sababu ya kuzini na ikatokea kwamba Allah swt akamsamehe madhambi yake yote kwa sababu ya kutoa Sadaka kwa moyo mkunjufu.”

571. Al Imam ‘Ali ar-Ridha a.s. amesema kuwa;

“ Katika zama za Bani Israil kuliwahi kutokea baa la njaa ambalo liliendelea kwa muda wa miaka mingi.

Katika wakati huo ikatokezea kwamba bibi kizee mmoja akiwa amekabwa na njaa kali, alikuwa ameketi akiwa na kipande kidogo cha mkate huku akitaka kukila kipande hicho, mara akasikia mlangoni sauti ikisema ya masikini aliyekuwa amekuja kuomba:

‘Ewe mja wa Allah swt! Mimi nakufa kwa njaa naomba unisaidie, bibi kizee huyo akajiambia kwa hakika Sadaka ndiyo wakati huu muafaka wa kutoa, na kile alichokuwa akila akakitoa haraka akampa huyo aliyekuwa akiomba.

Bibi kizee huyo alikuwa na mtoto mmoja aliyekuwa amekwenda porini na ghafla kule alishambuliwa na mnyama. Kwa kusikia sauti ya mtoto wake huyo bibi kizee ikimwita, alikimbia kumfukuza mnyama huyo na kwa muujiza Allah swt alimtuma Malaika Jibrail a.s kwenda kumwokoa mtoto huyo katika mdomo na mabano ya mnyama huyo muuwaji, na Malaika Jibraili a.s. akamwambia ‘Ewe bibi kizee ! Je umefurahi sasa? Kwa kile ulichokitoa sadaka basi Allah swt naye amekulipa mema yake.”

572. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema kuwa:

“ Mfanye mema katika hali ya shida na ufakiri, na wema huo ni Sadaka.

Toeni Sadaka kama itakuwa ni kiasi gani kwa udogo wake. Mnaweza kutoa kiasi cha tende mkajiokoa na Jahannam. Kwa hakika udogo huo siyo hoja na Allah swt ataulea udogo huo kama kwamba nyie mnavyo walea watoto wadogo wanaonyonya maziwa, na siku ya Qiyama wakati mema yenu hayo (mliyokuwa mkisema ni madogo) yatakapoletwa mbele yenu mtaona kuwa ni sawasawa na ukubwa wa milima mikubwa sana.”

573. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. ameseama kuwa Allah swt anasema kuwa:

“Hakuna kitu kingine mbali na Sadaka ambacho mtu anaweza kumpatia mtu mwingine kidhahiri, na kwa hakika mimi ndiye wakili wake musitahiki, na mimi ninayepokea kwa mikono Sadaka hiyo halafu hata ikiwa kama ni tende kidogo haidhuru mimi ndiye ninaitunza, kama vile mwanadamu anavyowatunza watoto wake.

Siku ya Qiyama huyo mtoa Sadaka atastaajabishwa mno kwa Sadaka zake ndogo alizokuwa akitoa zimekuwa kubwa kama milima ya Uhud, milima mikubwa sana.”

574. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amenakili riwayah kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa:

“Toeni Sadaka asubuhi na mapema kwa sababu kunaondoa balaa kwa siku nzima.”

575. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Kwa kutoa Sadaka asubuhi na mapema basi mtoa Sadaka huepukana na kila aina ya matatizo na mabaya yote kwa siku nzima.”

576. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Toeni Sadaka asubuhi, na kwa mapenzi kabisa, mwenyewe kutoa Sadaka amebahatika. Basi humwomba Allah swt amani kutokana na balaa zote zilizoko ardhini na mbinguni, na kwa hakika Allah swt humjaalia hivyo kwa sababu ya kutoa Sadaka.”

577. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. anaelezea kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwusia Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kuwa:

“Ewe Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.! Sadaka huondoa balaa ambazo lazima zitatokezea, na kwa kutenda mema pamoja na ndugu na majamaa kunarefusha umri.

Ya ‘Ali! Iwapo jamaa na ndugu ni watu wenye shida, basi kuwapa Sadaka hao haitakuwa ni Sadaka.

Ya Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.! Kusema maneno bila vitendo ni ya bure hayana maana, na Sadaka bila kuwa na nia nayo haiwi Sadaka.”

578. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. anasema kuwa: Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwuliza mtu mmoja

“Je leo umefunga Saumu?”

Mtu huyo alijibu

“La hapana! Ewe Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.”

Tena Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwuliza:

“Je leo umeshawahi kumtembelea aliye mgonjwa?”

Naye akajibu:

“Hapana! Ewe Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.”

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliendelea kumwuliza naye aliendelea kumjibu hapana hakufanya hivyo.

579. Mwishoni Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliendelea kumwuliza:

“Je umemlisha masikini yeyote?”

Naye akajibu: “Hapana Ewe Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.!”

Na hapo ndipo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alipomwambia huyo mtu:

“Nenda kwa wananyumba wako, nenda ukawatendee na uwe nao kwa mema na uwawie wema, basi hayo ndiyo yatakuwa Sadaka yako kwao.”

580. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. ameripoti riwayah kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ambaye ameseama:

“kwa baraka za Sadaka Allah swt humwondolea mwenye kutoa Sadaka balaa sabini, ambamo kuna magonjwa, madhara yatokanayo na moto, kuzama maji, kufunikwa na majumba mpaka kufa na atamwepusha ili asiwehuke au asiwe mwehu.”

581. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. ameripoti riwayah kutoka Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kuwa:

“Ili kutaka kuepukana na shari za madhalimu basi toeni Sadaka.”

582. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. anaelezea kuwa: Siku moja Myaudi mmoja likuwa akienda kukata miti porini na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwangalia na kuwaambia Masahaba wake:

“Myahudi huyu leo ataumwa na nyoka na kifo chake kitasababishwa na sumu ya nyoka. Myahudi huyo kama kawaida yake alikata kuni na alijitwisha kichwani mwake na akarud akiwa salama.

Na tena Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alipomwona Myahudi huyo akamwambia ateremshe mzigo wa kuni huo na auweke chini. Na Myahudi akafanya hivyo alivyoambiwa, na katika mzigo huo wa kuni wakaona kuna nyoka mweusi mwenye sumu kali sana huku akiuma kuni.

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwuliza Myahudi yule,’Je wewe leo umefanya jambo gani?’

Myaudi huyo akasema: Mimi nimekata kuni na kuzifunga tu, lakini wakati nilivyokuwa nikirudi nilibakiwa na vipande viwili vya mkate na kipande kimoja mimi nikala na kipande kimoja nikampa masikini Sadaka.

Hapo ndipo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akasema kwa kiapo cha Allah swt ni kwa sababu ya Sadaka ndiko balaa hii imekuondokea, kwa hakika Sadaka humwepusha mtu na ajali mbaya.”

583. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. siku moja alikuwa pamoja na Masahaba wake katika Masjid Nabawi, na upande mmoja wa ukuta ukaanguka chini. Kulikuwa na mtu mmoja hapo ambaye aliponea chupu chupu tu, kulianguka kizingiti kizito karibu na muguu wake. Lakini yeye bahati nzuri hakupata udhuru wowote.

Hapo Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. aliwaambia Masahaba wake, hebu mwulizeni huyu mtu leo amefanya matendo gani? Na wakati alipoulizwa huyo mtu akasema:

“Mimi nilipotoka nyumbani mwangu leo nilikuwa na kokwa chache za tende. Na kukatokezea na masikini mmoja akaniomba basi mimi nikampa kama Sadaka .

Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. akajibu

“Basi kwa sababu hiyo tu leo, Allah swt amekuepusha na balaa hii ambayo ingekumaliza.”

584. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. siku mmoja alimwambia Sahabi wake Mayassari kuwa:

“Ewe Mayassari je wajua kuwa wewe umeisha fikiwa na mauti mara nyingi, lakini Allah swt amekuongezea umri wako zaidi kwa sababu ya wewe kuwa mkarimu na kuwajali jamaa na ndugu zako umewawia wema ndio maanake umri wako umezidi.”

585. Al Imam Hasan al-'Askary a.s. anasema kuwa:

“ Wakati mmoja Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akiwa pamoja na wenzake walikuwa safari na wenzake hao walikuwa na mali nyingi sana. Na njiani wakapata habari kuwa wako majambazi wanaowapora matajiri mali zao. Kwa kusikia hayo hao matajiri walianza kutetemeka na wakaingiwa na hofu na wakaanza kumwuuliza Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. je tufanyeje sasa?

Na kwa hayo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akawajibu:

‘Mkabidhini mali yenu yule ambaye ataweza kuifadhi mali yenu, na kwa kweli ataitunza sana na baada la kupungua hata itazidi pia, sio hayo tu na pale mutakapo kuingiwa na shida ya mali yenu basi yeye kila siku atawarudishia pamoja na nyongeza yake. ‘

Kwa kusikia hayo hao wenzake aliokuwa nao katika safari wakamwuliza:

“Je ni nani huyo?”

Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akawajibu:

“Yeye ni miliki wa malimwengu zote Allah swt.”

Basi hao wenzake wakamwuliza je tunaweza kumkabidhi vipi mali zetu hizi? Hapo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akawaambia: Toeni Sadaka muwape wale wanaostahiki. Kwa kusikia hayo wakauliza ewe mjukuu wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.! Hapa tulipo tutawatoa wapi hawa masikini na mafakiri tutawatafuta wapi? Basi Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. aliwajibu: munuie kuwa sehemu moja ya mali yenu mtatoa Sadaka basi na msiwe na wasiwasi Allah swt atailinda mali yenu yote.

“Wale waliokuwa naye pamoja safarini walinuia hivyo kama vile Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alivyowaambi,a na Imam a.s. akawaambia sasa nyie mko katika amani ya Allah swt, na wakiwa wanaendelea na safari majambazi hao walikumbana nao na kwa kudura za Allah swt wao wakawapita salama usalimini bila ya kudhurika na kusumbuliwa, hadi wakafika mwisho wa safari yao.

Waliopofika tu mwisho wa safari yao wao wakatoa sehemu moja walizokuwa wamenuia kama Sadaka na sehemu iliyo bakia walifanyia biashara yao, na Allah swt akawajaalia baraka kiasi kwamba wakapata faida hata zaidi ya mara kumi.”

586. Siku moja Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alikuwa Mina pamoja na Masahaba wake wakila zabibu. Mara akatokezea mtu mmoja na akaomba. Basi Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. kwa mkono wake akachukua fungu moja la zabibu akampa basi huyo akakataa kupokea, akisema “mimi sitaki zabibu hizi bali ninataka pesa taselimu kama zipo ndio nichukue”.

Basi kwa kusikia hayo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akamwambia “Allah swt atakuzidishia” na Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. hakumpa chochote, baada ya muda si muda huyo mwombaji tena akarudi kwa Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. na akamwambia Imam a.s. “Nipe zile zabibu ulizokuwa ukitaka kunipa.” Na Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akamwambia Allah swt atakutafutia njia yake, pamoja na hayo Imam a.s. hakumpa chochote.

Wakati bado wakiwa wamekaa akatokezea mtu mwingine kuja kuomba, na Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alitoa mbegu tatu tu za zabibu akampa huyo mwombaji. Mwombaji huyo alianza kumshukuru Allah swt kwa kumjaalia riziki hiyo na akaonyesha shukurani kwa ujumla. Kwa kusikia hayo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alichota mikono ya zabibu miwili akampa na hapo tena huyo mwombaji akaendelea kumshukuru Allah swt zaidi na zaidi. Kwa kusikia hayo tena Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akamwambia mtumwa wake kama tuna pesa zozote zile tulizo nazo kwetu mpe huyo. Na huyo mfanyakazi wa Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. kwa amri yake alimpa Dirham Ishirini alizokuwa nazo. Mwombaji akiwa anachukua Dirham akasema: ‘Ewe Allah swt! Nakushukuru mno sana na hakuna mwingine wa kushirkishwa nawe. Kwa kusikia hayo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. nguo aliyokuwa amejifunika akampa huyo mwombaji na huyo mwombaji baada ya kuivaa na kujifunika na hiyo nguo akamshukuru Allah swt ambaye amemjaalia nguo ya kujifunika. ‘Ewe Aba ‘Abdillah! Allah swt akulipe kila la heri. Na baada ya kusema hayo akaondoka zake. Kwa kuona haya Masahaba wakamwambia Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. kuwa kila alivyoendelea yeye kumsifu Allah swt ndivyo wewe ulivyoendelea kumpa na kama asinge omba kwa kutaja jina la Al Imam a.s. lazima angeendelea kumpa chochote zaidi ya hayo.”

587. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“ Mimi nilinunua ardhi pamoja na mtu mmoja. Mtu huyo huyo alikuwa ni mnujumi, kwa hiyo yeye kila alipokuwa akipiga mahesabu yake na elimu ya nyota yake aliyokuwa nayo alikuwa akiangalia saa nzuri ndipo alipokuwa akienda shambani mwake, nami bila kujali kama saa mbaya nilikuwa nikienda shambani mwangu, na sisi tulipokuwa tayari basi ardhi au sehemu yangu ikawa na faida zaidi kuliko sehemu yake.

Kwa hivyo yeye bila kusita katika hali ya kustaajabisha aliniambia mimi sijawahi kuona kama hivi. Mimi kila saa zilizokuwa nzuri nilikuwa nikija shambani mwangu. Na wewe bila kujali saa nzuri au mbaya ulikuwa ukija kwenye shamba lako. Sasa itakuwaje mimi nipate hasara au kasoro?

Basi Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akamjibu ngoja nikwambie hadithi moja ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliyesema kuwa:

‘Mtu yeyote anayetaka Allah swt amwepushe na maovu na mabaya ya siku nzima basi yeye aianze siku yake kwa kutoa Sadaka, na yeyote anayetaka ajiepushe na balaa na maovu ya usiku basi yeye usiku unapoingia atoe Sadaka na ujue kwamba mimi daima ninapotoka nyumbani mwangu huwa ninatoa Sadaka. Kwa hivyo kufanya biashara na Allah swt hivi afadhali zaidi kuliko elimu yako ya nyota na kupiga ramli.”

588. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Mtoe Sadaka usiku kwa sababu huiondoa ghadhabu ya Allah swt, husamehe madhambi mazito, na hukusababishia hesabu zako siku ya Qiyamah zikaenda vizuri. Kutoa Sadaka katika siku kunaiongezea mali yako na kuilinda na kunaufanya umri wako uwe mrefu.”

589. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“ Kwa kutoa Sadaka yaani kunapokucha kunayeyusha madhambi kama vile chumvi inavyoyeyuka katika maji. Na kunapotolewa Sadaka usiku basi kunaondoa ghadhabu za Allah swt.”

590. Ibn ‘Abbas amesema kuwa: Allah swt amesema katika Qur'an Tukufu, Sura Al-Baqarah,2, Ayah 274

يَمْحَقُ اللَّهُ الرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ ۗ وَاللَّهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ كَفَّارٍ أَثِيمٍ

Wale wanao toa mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhaahiri, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi; wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika

“Aya hiyo imeteremshwa makhsusi kwa ajili ya Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kwa sababu yeye alikuwa anazo Dinar chache ambazo wakati wa usiku yaani baadhi ya Dinar hizo wakati wa usiku na baadhi wakati wa mchana na zinginezo katika hali ya siri na zinginezo zikiwa ni dhahiri alizokuwa akitoa Sadaka katika njia ya Allah swt.”

591. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alikuwa akisema kuwa:

“Kwa kutoa Sadaka kifichoficho ghadhabu za Allah swt hupoa.”

592. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Sadaka inayotolewa kidhahiri basi kuliko hiyo Sadaka inayotolewa kifichoficho ni afadhali zaidi.”

593. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. siku moja alisema kuwa:

“Mambo yanayomfikisha mtu moja kwa moja kwa Allah swt kama kipitio au (Wasila) ni imani. Na baada yake ni kuwatendea mema ndugu na majamaa zake mtu, ambaye inaongezea baraka katika mali yake na umri wake ukawa mrefu na Sadaka inayotolewa kifichoficho inamfanya huyo mtu asamehewe madhambi yake, na madhambi aliyokuwa yamemgadhabisha Allah swt kwa sababu ya kutomtii, yanabadilishwa kuwa mema na baadaye ni tabia njema na uwema, mambo ambayo yanaepusha ajali mbaya na inamfanya huru mtu katika makucha ya udhalilisho.”

594. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Kwa kutoa Sadaka kidhahiri kunaondoa aina sabini za balaa lakini kwa kutoa Sadaka kifichoficho kunamfanya mtu anusurike na ghadhabu za Allah swt.”

595. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema kuwa:

“Baba yake Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kila siku usiku alikuwa akitoka nyumbani pamoja na kifurushi cha fedha mgongoni mwake na mara nyingine alikuwa akichukua kufurushi cha vyakula na alikuwa akiwaendea wale wenye shida na dhiki.

Wakati akiwapelekea misaada hii majumbani mwao Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alikuwa akiufunika uso wake ili wasiweze kumtambua ni nani huyu anayewafikishia misaada mpaka majumbani mwao.

Wakati Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alipofariki ndipo hapo ikajulikana hawa wanaosaidiwa wenye shida hawapati misaada waliyokuwa wakipata, ndipo hapo wakajua kuwa aliyekuwa anawasaidia mpaka milangoni mwao alikuwa si mtu mwingine bali ni Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s . vile vile wakati Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alipolazwa wakati wa kuoshwa baada ya kufariki kulionekana mabegani mwake na mgongoni mwake alama zilikuwa zikionyesha kuwa alikuwa akibeba mizigo mizito kwa muda mrefu.

Na katika kipindi kimoja cha baridi kali sana yeye alikuwa amejifunika nguo ambayo ilikuwa inamsaidia asiisikie makali ya baridi wakati alikuwa ametoka nje ya nyumba anakwenda mahala fulani. Njiani alikutana na mtu ambaye alimwomba nguo hiyo ili naye aweze kujistiri na kujizuia dhidi ya makali ya baridi iliyokuwapo. Kwa maombi hayo Al Imam Zaynul 'Aabediin a.s. alimpa hiyo nguo naye akabaki bila nguo ya kujifunika au kujuzuia na baridi. Vile vile Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alikuwa kila mwaka akijifunika nguo ya kujizuia baridi na kipindi kilipokwisha alikuwa akiiuza na fedha zake zote zilizokuwa zikipatikana alikuwa akitumia katika kuwasaidia wenye kuhitaji misaada.”

596. Vile vile Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. alisema kuwa:

“Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alikuwa akiwasaidia na kuwalisha na kuwatunza familia zaidi ya mia moja katika mji wa Madina. Na alipokuwa akikaa kula mayatima, wazee, wagonjwa na masikini walikuwa wakikaa kula naye pamoja na Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s., na vile vile alikuwa akiwafungia vyakula kwa ajili ya kuwachukulia wale waliokuwa majumbani mwao au kama baba ni mzee alikuja kula huko basi alifungiwa chakula awapelekee mke na watoto zake nyumbani.

Vile vile yeye yasemekana kuwa alikuwa hakai kula pamoja na mama yake juu ya meza moja ya chakula na watu walipomwambia ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. wewe ni kigezo cha tabia njema na mfano bora katika Waislamu! Je kwanini hukai pamoja na mama yako katika kula chakula?.

Al Imam Zaynul 'Aabediin a.s. aliwajibu kuwa

“Mimi sikai na mama yangu kwa sababu yawezekana mama yangu akiangalia chakula moja labda akataka kuchukua na wakati huo mkono wangu ukawa mrefu kwenda kuchukua chakula hiki itakuwa kweli hiyo ni kitovu cha nidhamu na ndivyo maana yake ninajiepusha kukosa nidhamu mbele ya mama yangu.”

597. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema kuwa:

“Mtu anapotoa Sadaka ya chakula kwa ajili ya kuwapa masikini na mafakiri basi mujue kuwa aina hiyo ya Sadaka huondoa ufakiri na humwepusha mtu na kumuondolea ufakiri, na kuurefusha umri wake na humwepusha na aina sabini za vifo vya kutisha (ajali mbalimbali).”

598. Vile vile Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Siku ya Qiyamah wakati kutakuwa na jua kali lichomalo basi watu aina saba watakuwa wamepewa kivuli na Allah swt na mmoja wao ni yule anayetoa Sadaka ya vyakula kiasi kwamba mkono wa kushoto haupati habari kuwa mkono wa kulia umetoa Sadaka.”

599. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema kuwa:

“Enyi Waislamu! Je niwaambieni mambo matano ambayo kwa hakika ni mema, maneno hayo yanawapelekeni hadi Jannah.?

Masahabah wakajibu

“Naam lazima tuambie ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.! Naomba utuongoze.”

600. Kwa hayo Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. akasema:

“Mnapopatwa na misiba basi lazima ufanye subira na mujaribu kuficha, mutoe Sadaka kiasi kwamba mkono wa kulia unapotoa mkono wa kushoto usipate habari, muwatende mema wazazi wenu, na kwa hakika katika mambo hayo ndiyo kuna furaha ya Allah swt na kila mara mwezavyo kusema semeni La Haula wala Quwwata illa billahil ‘Aliyil ‘Adhiim kwa hakika hiyo ni hazina moja kubwa katika hazina za Jannah, na vile vile katika nyoyo zenu muwe na mapenzi ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. pamoja na Ahlul Bayt a.s.

601. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. daima ilikuwa akitoka usiku katika kiza huku amejitwisha mafurushi ya mapesa na vyakula kwa ajili ya kwenda kugawa kwa masikini katika mji wa Madina, alikuwa akiwafikishia misaada waitaji walipokuwa. Na siku ambayo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. aliaga dunia, watu wakaona misaada imesimama na watu hawakufikiwa na misaada hiyo ndipo walipokuja kujua kuwa misaada hiyo ilikuwa ikiletwa Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. ambaye daima alikuwa akificha uso wake ili watu wasijue kuwa ni yeye anayewafikishia misaada hiyo.

602. Mu’alla ibn Khuns anasema kuwa:

“Usiku mmoja kulikuwa kukinyesha manyunyu ya mvua, nikamwona Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akielekea katika makazi ya Banu Sai’d nami nikajaribu kumfuata nyuma kisirisiri na mara nikasikia katika giza kizito hicho kama kitu kimedondoka na nikamsikia Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akisema:

‘Ya Allah swt! Ninaomba vitu hivi nivipate tena.’

Na hapo mimi nikatokezea karibu ya Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s., nikatoa salamu. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. baada ya kuitikia salamu akaniambea je wewe ni Mua’alla ?

Nami nikamjibu:

‘Ndiyo ewe Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. ! Niwe fidia juu yako.

Hapo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akaniambia:

‘Naomba uniokotee vitu hapo chini unisaidie.”

Mu’alla anasema mimi katika giza kizito hicho nikaanza kupapasa aridhini na nikakuta kumbe ni vipande vya mikate na wakati ninamkabidhi Imam a.s mikate niliyo iokota katika giza kali nilihisi kifurushi alichokuwa nacho migongoni mwake kilikuwa kizito mno na hivyo nilimwomba Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. Lakini hakukubali nimsaidie kubeba kifurushi hicho.”

Lakini Imam a.s alikataa akaniambia

“Ninapendelea kuubeba uzito huu mimi mwenyewe kwa sababu huu ndiyo utakao kuwa ufanisi wangu katika siku ya Qiyamah na bora kwangu na hivyo unaweza kuja nami katika safari hii.”

Tulipokaribia katika makazi ya Banu Sa’id, Imam a.s. alikwenda kwa kila mmoja ambaye ni mwenye shida akamwekea mikate miwili na akarudi. Na wakati huo akaniambia kwa kutoa Sadaka usiku kunatuliza ghadhabu za Allah swt, na Allah swt usamehe madhambi makubwa, na kusahilisha hesabu katika siku ya Qiyamah.”

603. Zuhri anasema kuwa:

“Siku moja wakati wa baridi kali mno na ukungu ulikuwa umejaa mwingi mno mimi nilimwona Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. akiwa amejitwisha kifurushi kikubwa cha chakula na mzigo mkubwa wa kuni.

Nami sikusita nikamwambia ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.! Je nini haya?’

Imam a.s akanijibu nina nia mpango wa safari, na hivyo ndivyo ninavyojitayarisha kwa ajili ya mahitaji yangu.

Zuhri akasema:

‘Ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.! Mimi nakupa mfanyakazi wangu ambaye atakusaidia kukubebea mizigo yako hiyo mizito.”

Al Imam Zaynul 'Aabediin a.s. alimkatalia nami nikamwambia,

“Basi nipe mimi mwenyewe nikupunguzie kukusaidia huu mizigo. Kwa hayo Imam a.s. akajibu, lakini kwa kufanya hivyo mimi sitakuwa nimetoka katika wajibu wa kufika mwisho wa safari yangu vile inipasavyo kufika, kwa hiyo naomba uendelea na shughuli zako uniache peke yangu.”

Zuhri anasema:

“Baada ya kufika siku chache mimi nilipomwona Imam a.s nikamwambia,

“Ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.! Mimi sioni kama wewe ulikwenda safari yoyote ile.”

Imam a.s akamjibu:

“Naam ! Vile uchukuliavyo sivyo. Muradi wangu ulikuwa ni safari ya Aakhera. Mimi nilikuwa nikijitayarisha kwa ajili ya safari ya Mauti. Kumbuka kwamba kujikumbusha na kujitayarisha kwa mauti basi mambo mawili ni muhim, kwanza kujiepusha na yaliyo haramishwa na pili ni kutoa muhanga wa mali katika njia ya Allah swt.”

604. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. katika baadhi ya misemo yake

anasema.:

1. “Toeni Sadaka kwa basabu kunatuliza ghadhabu za Allah swt

2. Toeni Sadaka katika njia ya Allah swt kwa sababu ya riziki muliyojaaliwa na Allah swt kwa kufanya hivyo nyinyi mtahesabiwa katka wale wanaopigana katika njia ya Allah swt.

3. Yeyote yule ambaye ana imani kamili kuwa Allah swt hulipiza kile kinachopendwa na Mumin basi huyo mtu lazima ataitia nafsi yake katika shida na kwa kufanya mema.

4. Muwatibu wagonjwa wenu kwa Sadaka .

5. Muilinde na muihifadhi na kulinda mali yenu kwa kutao zaka1.

6. Urekebishe matumizi na mahitaji ya maisha yenu ili mweze kupima vyema.

7. Kuwaza na mawazo ni nusu ya uzee unaoletwa nawe.

8. Mwenye matumizi yenye mahesabu yaani anayebana matumizi kamwe hawezi kuwa mwenye shida na dhiki.

9. Kumsaidia yule mtu ambaye anaheshima na mkuu na kumsaidia yule ambaye ana madeni haya maneno mawili hayana kifani yoyote.

10. Kila jambo lina mazao yake, kwa hiyo mazao ya mema na kuwa na nia katika kutumia mali au chochote katika njia ya Allah na kwa ajili ya Allah swt basi mazao yake ni kwamba kufanya haraka kutekeleza azma hiyo na kamwe usifanye kucheleweshwa.

11. Muongezee na mupanue riziki yenu kwa kutoa Sadaka, kabla haitamjia na balaa, mwombe dua na kwa hakika mtaweza kujiepusha nayo na kujiokoa nayo.

605. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Kutoa Sadaka siku ya Ijumaa kuna thawabu na fadhila kubwa sana.”

606. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema:

“Msimkatalie masikini anayeomba siku ya ‘Arafah. Lazima mpeni chochote kile.”

607. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Mtu yeyote atakaye kuwa ametoa Sadaka katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, basi yeye atakuwa ameepukana na balaa za aina sabini.”

608. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alikuwa ameulizwa na mmoja

wa Masahaba wake,

“Ewe Mtume wa Allah swt! Ni Sadaka ipi iliyo bora kabisa kuliko zote!”

Kwa hayo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alijibu,

“Sadaka iliyo bora ni ile ya wakati ule ambapo mtoa Sadaka yuko salama u salimini, mwenye afya kamili na anayeishi maisha mema bila wasiwasi, na ambaye anauogopa umasikini.

Na wala msicheleweshe kiasi kwamba mpaka mwisho wa maisha yenu yameisha wafikia shingoni, na hapo ndiyo mnaanza kutoa usia kuwa kiasi fulani mpe masikini fulani na fulani mpe kiasi fulani na kadhalika. Kama tunaelewa kuwa mtu fulani kweli ni mstahiki wa msaada au Sadaka sasa kwa nini tusubiri mapaka sisi tunataka kufa ndiyo basi tuseme msaidieni wakati shida alikuwa nayo tangu hapo zamani?”

609. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. aliombwa na mtu mmoja kuwa ampatie nasiha, na hivyo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akamwambia:

“Tayarisha matayarisho yako ya safari, na matayarisho yako hayo yatume kabla wewe hujaenda safari. Jifanyie matendo yako mwenyewe yaani kama unataka kufanya mema uyatende mema kabisa katika uhai wako na mambo yoyote yale ambayo unayoona yanafaida kwako uyatende wewe mwenyewe na wala usiwatupie wengine kama unaweza kujitimizia wewe mwenyewe.2

610. Kwa kuzungumzia swala tulilozungumziwa hapo No. 2 hapo juu siku moja Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alikuwa amekwenda katika ghala la mtu mmoja ambaye alikuwa amefanya usia kuwa baada ya kifo chake maghala yake yote yaliyokuwa yamejaa kwa tende yagawiwe Sadaka kwa masikini. Na baada ya kifo chache ikatekelezwa usia wake na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alipokwenda kule baada ya kufagia akakuta kokwa moja ya tende imebakia mguuni mwake basi Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akainama akalichukua kokwa hilo la tende moja akasema:

“Kama mtu huyu katika uhai wake angelikuwa amegawa kokwa hii moja ya tende basi angepata thawabu zaidi kuliko hata mlima mkubwa kabisa wa Uhud.”

611. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amenakili riwayah kutoka kwa mababu zake a.s. kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alikuwa akisema:

“Pale anapokuja mtu yeyote usiku kugonga mlango kwa nia ya kuomba msaada, basi msimvunje moyo, msaidieni na hasa inapokuwa mwombaji aliyekuja ni mwanaume.”

612. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Allah swt kwa kila kazi amemweka mweka-hazina ambaye anaweka mahesabu yake isipokuwa Sadaka, ambaye mahesabu yake na utunzaji wake anaweka Allah swt mwenyewe. Baba yangu mzazi wakati alipokuwa akimpa chochote mwombaji alikuwa akikichukua tena na alikuwa akiubusu mkono wa huyo mwombaji, na alikuwa akiunusa kwa hamu sana, na ndipo baadaye alipokuwa akimrudishia na kumpa kitu hicho hicho.”

613. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. anasema:

“Allah swt amesema kuwa mimi nimewateua mawakili kwa kila jambo na ambao ndio wanaosimamia na kuweka ripoti zake isipokuwa Sadaka ambayo mimi mwenyewe ndiye ninayetunza habari zake.”

614. Mu’alla bin Khunais amesema kuwa Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alikwenda katika makazi ya Banu Sa’id na wale wote waliokuwa na shida aliwawekea mikate na kuondoka zake. Hapo mimi nilimwuliza Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s.:

“Ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.! Je hawa watu ni marafiki na wafuasi wenu?”

Kwa hayo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alimjibu:

“La! Hawa kama wangekuwa marafiki na wapenzi wetu na wafuasi wetu basi ningewaongezea kiasi cha punje ya chumvi”. 3

Hapo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. aliponielezea kwa uwazi zaidi kwamba siku moja Mtume ‘Isa bin Maryam a.s. alikuwa akipita ufuoni mwa bahari, na akatoa mkate kidogo kutoka kifurushi chake akatupa baharini. Baadhi ya wale aliokuwa nao wakamwuliza!

“Ewe Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.! Je umefanya nini bwana? Nini maana ya kutupa mikate baharini?

Mtume Isa a.s akawajibu:

“Katika bahari kuna viumbe vya Allah swt na iwapo kutatokezea na viumbe vyovyote vitakavyo kula humo kutokana na nilicho watupia basi kwa hakika katika ufalme wa Allah swt nitakuwa na thawabu nyingi mno.”

615. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema:

“Pozeni nyoyo zenu kwa sababu ya kiu kali kwani Allah swt hupendezewa sana na tendo hilo. Kwa hakika amebahatika yule mtu ambaye anawamalizia kiu wanyama kwani yeye siku ya Qiyamah atapata msaada mkubwa sana atakapokuwa katika hali ya kiu.”

616. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alikuwa akifunga safari baina ya Makkah na Madina, akaona kuwa kulikuwa na mtu mmoja aliyejitupa chini ya mti mmoja. Basi Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akamwamwambia mtu mmoja aliyekuwa naye, aende akamwulize hali yake, inawezekana labda alikuwa na kiu kali. Mtu huyo alipomwendea huyo mtu aliyekuwa amelala chini ya mti na kumwuliza hali yake basi ikajulikana kuwa mtu huyo alikuwa na kiu ya maji. Basi Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alimnywesha maji na akaondoka kuendelea na safari yao. Yule aliyekuwa naye safarini akasema,

“Ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ! Huyu mtu alikuwa ni Mnasara, watu kama hawa pia tunaweza kuwasaidia na kuwapa Sadaka?”

Basi Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akamjibu

“Naam ! Katika mazingira kama haya inawezekana.”

617. Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alikuwa pamoja na wafuasi wake nao katika safari, na waliketi kwa ajili ya kula chakula. Na akatokezea swala mmoja ambaye alikuwa akitafuta chakula, Imam a.s. akamwambia huyo

‘Swala njoo karibu, njoo ule nasi! Usiwe na wasiwasi utulie na ujue hapa kwetu hautakuwa na hofu yoyote, upo katika usalama.”

Kwa kusikia hayo Swala huyo alimsogelea Imam a.s. na alikula pamoja nao.

618. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema kuwa Siku moja baba yake alikuwa pamoja na wenzake katika bustani yake na walipoketi kula chakula na mara akatokezea Swala mmoja aliyekaribia.

Hapo Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. . ambaye ni baba yake na Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. akasema:

“Ewe Swala, jina langu mimi ni Al Imam Zaynul 'Aabediin bin Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. na mama yangu Bi Fatima az-Zahra a.s., njoo ushiriki nasi katika kula. Na Allah swt kiasi alichokuwa amemjaalia cha chakula huyo Swala alikula.”

619. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Hakuna mtu yeyote mwingine isipokuwa ni Mwislamu tu anayeweza kuchinja wanyama wenu wa dhabihu siku ya Iddi na Sadaka, na unapotoa Sadaka katika kutoa humo lazima wapewe Waislamu tu. Na unapotoa Sadaka katika mali zinginezo unaweza kuwapa Kafir Zimmi ambao wenye kuhitaji misaada hiyo.”

620. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. ameripoti riwayah moja kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa mtu mmoja alimwuliza Mutume s.a.w.w.:

“Ewe Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ! Je ni Sadaka ipi iliyo bora kabisa?”

Kwa hayo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alijibu:

“Sadaka ile ambayo watakayo pewa wale jamaa na ndugu ambao hata kama alikuwa amekorofishana nao au amegombana nao au hawana uhusiano nao kwa sababu ya magomvi.”

621. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Iwapo wewe unatoa kumi kwa ajili ya Sadaka , basi ili kuwasaidia Mumin toa kumi na nane na yule ambaye hawezi kabisa msaidie kwa ishiririni na kwa ajili ya kuwasaidia jamaaa na ndugu kwa wema utoe ishirini na nne.”

622. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema Riwayah kutokea kwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa amesema:

“Mtu yeyote atakaye wasaidia jamaa na ndugu zake katika kwenda Kuhijji au ‘Umra, basi Mtume Allah swt atamjaalia thawbu za Hijja mbili na ‘Umra mbili, na yoyote yule atakayemsaidia ndugu yake Mumin basi Allah swt atamlipa kusiko na kifani.”

623. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. ameseama kuwa:

“Iwapo mtu atawasaidia jamaa au ndugu zake ambao wana shida ni muhtaji basi hiyo siyo Sadaka.”

624. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amenakili riwayah moja ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akisema:

“Kwa mtu yeyote yule ambaye atakwenda mwenyewe kwenda kumsaidia jamaa au ndugu yake mwenye shida na kutoa kitu chochote kwenye mali yake na kumsaidia basi Allah swt atamjaalia ujira wa mashahidi mia moja na kwa kila hatua atakayotembea atamwandikia mema elfu arobaini, na kiasi hicho hicho cha maovu yake yatasamehewa. Na vile vile kiasi hicho hicho ataongezewa daraja lake mbele ya Allah swt na atamwandikwa miongoni mwa wale waja wake halisi waliofanya ibada yao kwa uhalisi kwa muda wa miaka mia moja.”

625. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s., aliulizwa na mtu mmoja:

“Ewe Mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ! Je yeyote yule anayekuja kuomba mlangoni anastahili kupewa Sadaka au badala yake tuwape jamaa na ndugu zetu Sadaka hiyo?”

Kwa hayo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. aliwajibu:

“Kwa hakika kuwapelekea msaada Sadaka jamaa na ndugu wa mtu zina thawabu nyingi zaidi.”

626. Al Imam Muhammad Sahibuz-Zamaan a.s. aliandikiwa barua na mtu mmoja akimwuliza,

“Iwapo mtu anaweza kunuia kuwa mimi katika mali yangu nitatoa sehemu fulani ya mali nitamsaidia mtu fulani na katika kipindi hicho iwapo atakuja kujua kuna mtu katika ndugu na jamaa zake ambaye ni kweli anashida na anahitaji msaada wake basi je huyo mtu anaweza kubadilisha nia yake ya kumsaidia jamaa yake badala ya kumpa mtu aliyekuwa amenuia hapo kabla?”

Al Imam Muhammad Sahibuz-Zamaan a.s. akamjibu kuwa:

“Utaangalia ukaribu wa watu hao na yule aliye karibu nawe katika madhehebu umpatie na lau kama wote wawili kama watakuwa wanatokana na dhehebu moja tu basi kwa mujibu wa kauli ya Al Imam Musa al-Kadhim a.s. kuwa kugawanywe kati kati yaani watu wote wawili wapewe nusu kwa nusu, kwa sababu iwapo kutakuwa na jamaa na ndugu ambao wana shida na taabu basi huwezi kutoa Sadaka na kuwapa wengine. Na kwa hakika kwa kufanya hivyo utakuwa umepata thawabu na fadhila za Sadaka.”

627. Al Imam Muhammad Sahibuz-Zamaan a.s. aliandikiwa barua na mtu mmoja akimwuliza kuwa:

“Je inawezekana mimi nikatoa Zaka au Sadaka kutoka mali yangu nikampa mtu ambaye si jamaa wala ndugu yangu?”

Na kwa hayo Imam a.s. alimjibu:

“Usimpe Zaka au Sadaka mtu yeyote mwingine isipokuwa wenzako na majamaa zako.”

628. Al Imam Muhammad Sahibuz-Zamaan a.s. aliulizwa:

“Je inawezekana kumpa Sadaka Nasibi (maadui wa Ahlul Bayt a.s.)?”

Imam a.s akamjibu kuwa:

“Musiwape Sadaka wala Zaka maadui wa Ahlul Bayt a.s. na ikiwezekana hata maji pia msiwape.”

629. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. aliulizwa kuwa:

“Je inaruhusiwa kumlisha mtu kama humwelewi kuwa ni Mwislamu au si Mwislamu?”

Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akajibu kuwa:

“Mtu ambaye humwelewi na kama huelewi chochote kuhusu urafiki au adui, basi yeye unaweza kumpa. Kwa sababu Allah swt anasema tuwatendee watu mema. Lakini yule aliye mpingamizi wa haki au ambaye anaelekea kuhusu upotofu na madhambi au anayewachukua watu kuelekea upotovu na madhambi, huyo msimpe.”

630. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. aliulizwa kuwa:

“Mara nyingi tunaona masikini wanaokuja kuaomba, lakini sisi tunakuwa hatuwafahamu, Je watu kama hawa tunaweza kuwapa?”

Kwa hayo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. aliwajibu

“Kama wewe moyoni mwako utaingiwa na huruma kwa ajili ya mtu huyo basi unaweza kumpa, ingawaje hata kama si kamili lakini hata kidogo itafaa.”

631. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Kidhahiri wapo waombaji wengi ambao (wengi wanatoka vijijini na maeneo karibu ya mji) hivyo nyie muwape Sadaka watoto, wanawake, wagonjwa, wadhaifu na wazee.”

632. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Mnapoijiwa na masikini kwa ajili ya kuomba ambao ni wazee kabisa na wanawake na watoto na wasichana wadogo basi muwasaidie Sadaka na vilevile muwasaidie Sadaka wale mnaoijiwa huruma mioyoni mwenu.”

633. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. aliulizwa kuwa:

“Mijini mwetu wanakuja waombaji wengi sana kutoka vijiji na vitongoji ambavyo viko karibu na mji ambamo humo wamechanganyikana Mayahudi, Manasara, Wakristo na hata Majusi (Wanaohabudu moto) sasa katika sura hii je tunaweza kuwasaidia Sadaka ?”

Kwa hayo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alijibu:

“Naam ! Mnaweza kuwapa.”

634. Al Imam ‘Ali an-Naqi a.s. aliandikiwa barua na humo akaulizwa:

“Je tunaweza kuwasaidia wale masikini waliopo mitaani ambao hatujui dini na wala Madhehebu zao?”

Kwa hayo Al Imam ‘Ali an-Naqi a.s. aliwajibu:

“Kama mtaweza kuwatambua wale maadui na wenye chuki na Ahlul Bayt a.s. na mukiwasaidia basi Allah swt hatakulipeni chochote ama wale ambao nyie hamuelewi Madhehebu yao basi hakuna matatizo yoyote katika kuwapa Sadaka. Na muwasaidie masikini wale wowote wanaoomba kama mtaingiwa na huruma mioyoni mwenu. Hata kama hamtaweza kuwaelewa dini na madhehebu zao… Insha-Allah hakuna tatizo lolote katika kutoa Sadaka katika sura kama hizi.”

635. Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alimwambia muhudumu wake:

“Yeyote yule anayekuja kuomba nyumbani kwake basi asimruhusu akaondoka hadi pale ahakikishe kuwa amemlisha chakula, hususan siku ya Ijumaa.”

Mwandishi anasema kuwa mimi nilimwambia Imam,

“Ewe mjukuu wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.! Kila mwombaji huwa si msitahiki.”

Kwa hayo Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alinijibu

“Ninaogopa kuwa inawezekana mwombaji akawa msitahiki lakini mimi nikamfukuza, isije tukapata matatizo na dhiki iliyo mpata Mtume Ya’aqub a.s na nyumba yake.”

636. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema:

“Msimvunje moyo mwombaji hata kama atakuwa amekuja kuomba katika usafiri wa farasi.”

637. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema:

“Iwapo mtoaji atakuwa anajua wema na fadhila za kutoa Sadaka basi kamwe hatamrudisha mtu yeyote bila ya kumpa kitu chochote.”

638. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Kamwe msiwarudishe mikono mitupu waombaji. Iwapo waombaji wengine wasingekuwa waongo na wadanganyifu basi kamwe wengine wasingerudipo.”

639. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kamwe hakumrudisha masikini yeyote aliye mwomba asaidiwe Sadaka. Na kama Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alikuwa hana chochote cha kumpa basi alikuwa akimwambia kwa lugha tamu Allah swt atakujaalia Insha-Allah.”

640. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Mtume Ibrahimu a.s. daima alikuwa akiwahudumia na kuwakarimu wageni, na pale alipokuwa hakuwapata wageni wowote wale, basi alikuwa akifunga mlango wake na akitoka kwenda kuwatafuta wageni.”

Na katika hadithi hiyo hiyo tunapata wakati mmoja Malaika Jibrail alimwijia Mtume Ibrahim a.s. na kumwambia:

“Allah swt amenituma safari hii kwa mja wake mmoja ambaye ameweka marafiki Wake kama ni Khalil Wake.”

Kwa hayo Mtume Ibrahim a.s. akaingiwa na shauku ya kutaka kumjua na akasema:

“Tafadhali sana naomba unitambulishe huyo umzungumzaye, nami nitapenda kwenda mbele yake.”

Jibrail a.s. akasema:

“Ewe Khalil (rafiki)! Ndiwe wewe tu !”

Basi Mtume Ibrahim a.s. akamwambia:

“Ewe Jibrail a.s.! Je kwanini umenifanyia hivyo ?”

Hapo Malaika Jibrail a.s. akamjibu:

“Kwa sababu wewe kamwe haujamnyooshea mkono yeyote, na wewe daima haujawahi kumkatalia yeyote aliyekuja kukuomba.”

641. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema sema kuwa Mtume Allah swt alikuwa akisema

“Kamwe msimrudishe mikono tupu mwombaji. Hata kama mtakuwa katika hali ya ugumu kiasi gani.

642. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema kuwa Mtume Musa a.s. wakati alipokuwa akimlilia Allah swt, Allah swt alimwambia:

“Ewe Musa hata kwa ukimpa kidogo mpe ili utunze heshima ya mwombaji, na kama hicho pia hauna basi kwa maneno matamu na kauli nzuri umwambie na kumwomba msamaha. Kwa sababu miongoni mwa waombaji mara nyingine si lazima atokane na binadamu au Majini bali anakuwa ni Malaika wa Rehema. Kwa hiyo Malaika huyo ndiye anaye wajaribu watu na kile nilicho kushauri ndiyo ujaribu kutegemea kupata jibu lake na huwa anawaombeamo kwa hivyo, ewe mwana wa Imran angalia vile tabia yako itakavyo kuwa”.

643. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. ameripotiwa riwaya kuwa siku moja mtu mmoja alikuja Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuomba kwa hapo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliwaangalia Masahaba wake na kuwaambia,

“Enyi Masahaba wangu ! Msaidieni.”

Na mmoja katika Masahaba wake akamsaidia kifaa cha dhahabu. Aliyekuja kuomba akasema

“Je leo ni -- yako?”

Yule Sahaba wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akajibu:

Naam ndiyo maana yake”.

Yule mwombaji akasema:

Mimi nimekubalia hivyo. Mimi si Jini wala si binadamu; bali mimi ni Malaika niliyetumwa na Allah swt nije nikujaribu na kwa hakika nimekuona wewe miongoni mwa watu wenye kushukuru neema za Allah swt. Mungu akujaalie kila la heri.”

644. Sa’ad bin Musayyab anasema kuwa Siku moja wakati wa swala ya asubuhi yeye alikuwa pamoja na Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s., akatokezea mwombaji mmoja na wakati huo Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. akasema:

“Mpeni huyo mwombaji---- kumbukeni kuwa---kamwe msimwondoe mwombaji katika hali ya kuhuzunika yaani msimwondoe mwombaji bila kumpa chochote”.

645. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. ananakili riwaya kutoka baba yake mzazi a.s. kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema kuwa:

“Mruhusu mwombaji aondoke hata kwa kidogo na kwa mapenzi na kwa huruma pia. Kwa sababu mara nyingi anayekuja kuomba huwa si kutoka binadamu au Majini bali huwa ni njia moja kwa kuwajaribia nyie kwa ajili ya kuwaongezea neema.”

646. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema katika Nahjul Balagha:

“Masikini anapokuja kwenu basi anakuwa ni mjumbe wa Allah swt na yeyote yule atakaye muudhi na atakayemhudhunisha basi atakuwa amemhudhunisha Allah swt na yeyote yule atakaye kuwa amempa chochote basi ajue kuwa amempa Allah swt”.

647. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. anaripoti kutoka kwa wazazi wake a.s ambao wamesema kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Wakati ‘Ummah wangu utakapogeuza uso au utakapo wageuzia uso wale wanao hitaji msaada wao na watakapoanza kutembea kwa maringo basi wakati huo Allah swt atasema: kwa kiapo cha utukufu na ukuu wangu hawa watu watakomeshana wao kwa wao na hivyo ndivyo nitakavyo waonjesha adhabu yao.”

648. Walid bin Sahib anasema kuwa:

“Siku moja mimi nilikuwa kwa Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. na hapo akatokezea mwombaji mmoja. Imam a.s alimpa chochote huyo mwombaji na akatokezea mwombaji wa pili naye akapewa chochote. Hivyo hivyo akatokezea mwombaji wa nne basi Al Imam a.s akamwambia Allah atakusaidia upate zaidi njia yako atakupanulia. Na baada ya hapo Imam a.s akasema iwapo mtu atakuwa na Dirham takriban elfu thelathini au arobaini, na akanuia akawa na mpango wa kuzitumia zote ambazo kimatokeo hatabakiwa na chochote basi mtu kama huyo atawekwa miongoni mwa wale watu ambao Allah swt huzitupilia mbali dua zao.”

Kwa hayo mimi nikasema

“Ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.! Je ni makundi gani ya watu hawa watatu?

Kwa hayo Imam a.s akajibu

“Mmoja wao ni yule ambaye ana mapesa na mali na baada ya kutumia vyote anaomba ‘ewe Mola wangu naomba unipe riziki’. Basi hapo Allah swt anamjibu ‘Je mimi sikukupanulia njia na kukuwekea sababu za wewe kujiwekea riziki yako?”

649. ‘Ali ibn Hamza anasema kuwa:

“Mimi nilimwuliza Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. swali kuwa yeye amesikika akisema mwalishe watatu---- na kama mnataka kuwapa chochote zaidi muwape ama sivyo nyie mmeshatimiza haki ya siku yenu hiyo”.

650. Walid bin Sabih daima alikuwa akisema kuwa:

“Mtu yeyote anayetoa Sadaka na iwapo Sadaka hiyo itakubaliwa au Sadaka hiyo itarudishwa basi yule mtoa Sadaka haruhusiwi kuila au kuitumia tena hiyo Sadaka kwa ajili yake. Na badala yake hana njia yoyote isipokuwa aigawe Sadaka kwa mtu mwingine. Hatakuwa na ruhusa kwa vyovyote vile vya kuitumia hiyo Sadaka isipokuwa Sadaka itatolewa tena Sadaka kwa mtu mwingine. Vile vile mfano wake inachukuliwa kuwa mtu anapomfanya huru mtumwa katika njia ya Allah swt na kwa ajili ya kutaka furaha ya Allah swt basi kamwe hawezi kumchukua tena yule mtuma(aliyefanywa huru) akamfanya mtumwa wake. Na baada ya kumfanya huru mtumwa na mtumwa atakapo rudi kwake basi hawezi kumweka vile alivyokuwa amemweka mwanzoni kabla ya kumfanya huru katika njia ya Allah swt. Na vivyo hivyo ndivyo swala hizi zinausiana na Sadaka pia.”

651. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Yeyote yule atakayekuwa ametoa Sadaka na iwapo Sadaka hiyo itamrejea yeye tena basi yeye mwenyewe hataweza kuitumia wala hataweza kuiuza, kwa sababu kitu hicho kilishatolewa katika njia ya Allah swt na kwa ajili ya ridhaa ya Allah swt na hivyo hakuna kitakachoweza kushirikishwa katika swala hilo, na mfano wake pia ni sawa na ule wa kumfanya huru mtumwa hivyo hataweza kurudishwa tena katika utumwa.”

652. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. anasema

“Iwapo mtu atanuia kutoa Sadaka kwa ajili ya mtu fulani anayeuhitaji msaada huo na wakati huo akapata kujua kuwa mtu huyo ameshaondoka, basi hawezi kuirudisha na kuichanganya hiyo mali katika mali yake na badala yake itambidi amgawie mtu mwingine.”

653. Amesema Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. kuwa: Kuna mtu alimwuliza iwapo mtu alimfanya huru mtumwa bado ambaye hajafikia umri wa kubalehe je sheria inasemaje?

Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alimjibu

“Hakuna tatizo lolote ndani yake lakini sheria itakayotumika hapo ni kama ile ya kutoa Sadaka (yaani baada ya kumfanya huru mara moja hauwezi kumrudisha katika utumwa tena).”

654. Al Imam ‘Ali ar-Ridha a.s. amesema:

“Dua ya mtu msiidharau au kusema kuwa haifai chochote. Mara nyingi dua muliyoombewa na Mayahudi au Manasara hukubaliwa. Ingawaje inawezekana kwa dua aliyo jiombea yeye mwenyewe haiwezi kukubalika.”

655. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Wakati mnapo wasaidia waombaji, muwaombe wawaombeeni dua hata kama dua zao wenyewe hazikubaliki kwa ajili yao wenyewe, mradi kuna uwezekano mkubwa kwa dua zao kwa ajili yenu zikakubalika.”

Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amenakiliwa na Abu Basir riwaya moja kuwa Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Wakati mtu anapomsaidia fakiri mwenye shida sana asiye na uwezo, na pale fakiri huyo anapomwombea dua, basi dua hiyo lazima inakubaliwa na Allah swt.”

656. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Wakati mnapowapa chochote waombaji; basi muwaombe wawaombeeni dua, kwa sababu inawezekana kwa sababu ya udanganyifu na ulaghai wake dua zake zenyewe kwa ajili yake zisikubaliwe lakini kwa ajili yenu dua zake zitakubaliwa.”

657. Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s.:

“Alikuwa akimwambia mfanyakazi wake, zuia kwa punde kidogo sadaka, ili mwombaji amalize kuomba dua.”

658. Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Na vile vile amesema:

“Dua ya fakiri na mwombaji kamwe hairudishwi au haitupiliwi mbali.”

659. Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amemwamrisha mfanyakazi wake kuwa:

“Wakati unapowapa chochote waombaji basi muwaambie wawe wakituombea heri.”

660. Al-Imam a.s. amesema:

“Wakati muwapapo chochote masikini na waombaji basi muwe mukiwaomba wawaombeeni dua kwa sababu wanapo waombeeni dua kwa ajili yenu dua zao hukubalika na inawezekana dua zao kwa ajili yao wenyewe hazikubaliki.”

661. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Iwapo mtu atapewa msaada ikapitia mikono themanini hadi ikamfikia aliye mustahiki basi kila mkono utapata haki sawa sawa ya malipo.”

662. Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Bora ya sadaka zote ni ile ambayo binaadamu baada ya kujitimizia mahitaji yake kwa moyo mkunjufu anatoa sadaka.”

663. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Yule atakaye fikisha msaada katika hali nzuri kwa mwenye kustahiki basi huyo mfikishaji wa sadaka atapata thawabu sawa kama za yule atakaye toa sadaka yake – hata kama katika kufikisha msaada huo kwa anayestahiki itachukua mikono elfu arobaini basi wote watapata malipo sawa kabisa kwani Allah swt hana upungufu wala kasoro ya aina yoyote ile, na wale watu wanaofanya Taqwa na kutenda mema basi laiti kama mungeweza kuelewa uhakika wa swala hili.”

664. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Watoaji ni wa aina tatu

1. kwanza ni Allah swt mwenyewe ambaye anatoa kwa ajili ya malimwengu zote.

2. Pili ni yule mwenye mali na

3. tatu ni yule msaada unaopitishwa katika mikono yake au ni mtu ambaye anafikisha misaada hiyo.”

665. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amenakiliwa riwaya na Abu Basir kuwa amesema:

“Watoaji ni wa aina tatu wa

    .1 kwanza kabisa ni Allah swt,

    .2 wa pili ni yule ambaye anatoa kutoka mali yake na

    .3 tatu ni yule anayefikisha kama msaidizi katika kufikisha msaada huo kwa mustahiki.”

666. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa:

“Allah swt amefaradhisha kwa waja wake kwa kusisitiza kuwa kama yafuatavyo,

    .1 kwanza uadilifu na mapenzi yake pamoja na muumini mwenzake kama vile ajipendeavyo yeye kwa ajili yake ndivyo ampendee muumini mwenzake.

    .2 pili awe ameweka hisa fulani au kiasi fulani katika mali yake kwa ajili ya kutaka kumsaidia muumin ndugu mwenzake. Na

    .3 tatu kumukumbuka Allah swt katika kila hali na hapa haimaanishi kuwa kwa kumsifu Allah swt peke yake au kwa kutoa uradi (tasbihi) bali hapa kuna maanisho ya kuwa kufanywe kwa kimatendo kabisa yale yaliyoelezwa katika dini yakiwa ni sehemu ya imani ya mtu.”

667. Aban ibn Taghlib anasema kuwa Siku moja yeye alimwomba Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amwelezee haki za muumini mmoja juu ya muumini mwingine. Kwa hayo Imam a.s. alimjibu:

“Ewe Aban! Achana nayo, usini shurutishe kukujibu ulicho uliza.

Nami nikamwambia:

“Ewe Mola wangu niwe fidia kwako.”

Na baada ya hapo niliendelea kumsisitiza Imam a.s. anielezee na ndipo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alipoanza kuniambia:

“Haki ya muumini mwenzako juu yako ni kwamba nusu ya mali yako iwe ni mali yake.”

Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akagundua kuwa rangi ya sura yangu imebadilika na akaniambia,

“Ewe Aban je huna habari kuwa Allah swt ameelezea habari za wale watu ambao wamezipenda nafsi za watu wengine kuliko hata nafsi zao?”

Nami nikamujibu

“Bila shaka, niwe fidia juu yako.”

Kwa hayo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akaendelea kujibu,

“Kwa hivyo nyie toeni nusu ya mali yenu muwape ndugu zenu muumini, na kwa hayo pia haitamaanisha kuwa nyie mmethibitisha mapenzi yenu kikamilifu, kwa sababu bado mko mnalingana. Kujitolea mhanga na kufikia kiwango hicho itathibitika pale ambapo hata katika nusu ya mali mliyobakia nayo mkatoa mkawagawia muumini ndugu zenu.”

668. Muhammad bin Ajlan anasema kuwa yeye alikuwa pamoja na Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. na mara akatokezea mtu mbele yao akatoa salamu, na Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akamwuliza

“Je ndugu uliowaacha huko nyuma hali zao ziko je?”

Basi huyo aliyekuja akawasifu na akatoa sifa zao na akaelezea kuhusu hali zao zilivyokuwa. Kwa hayo Imam a.s. akauliza:

“Je matajiri miongoni mwao wanawatunzaje wagonjwa wao?”

Basi huyo mtu akajibu:

“Ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ! Kidogo tu.”

Na Imam a.s. akamwuliza

“Je hao matajiri wanaonana mara ngapi na masikini?

Basi huyo mtu akajibu:

“Mara chache tu.”

Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akamwuliza

“Je hao matajiri wanawasaidia kwa mikono yao hao masikini?

Kwa hayo huyo mtu akasema

“Ewe Mawla ! Wewe unaniuliza mambo ambayo katika utamaduni wetu upo mchache sana.”

Kwa hayo Imam a.s. alimujibu

“Je wao watajidhaniaje kuwa wao ni Mashi’a wetu?”

669. Abu Ismail anasema kuwa:Yeye alimwambia Al Imam Muhammad al-Baqir a.s.,

“Ewe Maula niwe fidia juu yako! Kwa sasa hivi huko kuna Mashia wengi.”

Kwa hayo Imam a.s. akajibu:

“Je wanawasaidia na kuwahurumia mafakiri na wenye shida? Je wale wanao watendea mabaya sasa watu hao wema waliofanyiwa mabaya wanawasamehe hao wabaya walio watendea mabaya? Je wanasaidiana miongoni mwao katika kamari ? 4

Kwa hayo yote mimi nikajibu:

“Hapana sivyo hivyo.”

Hapo Imam a.s. akasema:

“Kwa hakika hao sio Mashia wetu. Basi mjue wazi kuwa Mashia wetu mienendo yao na desturi na utamaduni wao ni kama vile nilivyoelezea hapo.”

670. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. siku moja alimwuliza Sa’id bin Hassan,

“Je inawezekana miongoni mwenu kuwa muumini mmoja akatia mkono katika mfukoni mwa muumini wa pili na akajitolea kiasi cha fedha alizo na shida nazo bila ya kusita au kuogopa na muumini yule aliyetiliwa mkono mfukoni mwake asimzuie?”

Said bin Hassan akamjibu

“Ewe Mawla! Kwa hakika mimi sina habari na jambo kama hili.”

Kwa hayo Imam a.s. akamwambia

“Kwa hakika hakuna chochote.”

Hapo mimi nikamwambia Imam a.s.:

“Je hii inamaanisha kuwa sisi tumeisha teketea na kuangamia?”

Imam a.s. kwa hayo akamujibu:

“Sivyo hivyo, miongoni mwenu udugu na upendo bado haujaingia nafsini mwenu.”

Na katika maswala ya dua imesha zungumziwa hadithi moja ambamo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema zipo aina tatu za dua ambazo kwa kufika kwa Allah swt hakuna mtu anayeweza kuzizuia. Miongoni mwake moja ni

dua ya muumini anayemwombea muumini mwenzake na ambaye ametoa msaada kutoka mali yake kwa ajili ya ridhaa ya Allah swt na Ma’asumiin a.s. Na pili ni

dua kwa ajili ya muumini mwenzake ambaye pamoja na uwezo wake anaomba hivyo na ambaye baada ya kujua shida na dhiki kali ya muumini mwenzake hakuipuuzia bali amemsaidia.”

671. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. aliulizwa na mtu mmoja:

“Ewe Mawla! Je ni mtu gani mwenzi wako aliyebora kabisa?”

Kwa hayo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alijibu,

“Ni wale ambao wanawawia na kuwafanyia mema ndugu zao katika imani katika hali ya raha,starehe na shida.”

Na aliendelea kueleza kuwa

“Ewe Jamil, yeyote yule aliye nacho kingi basi kutenda kwake mema ni rahisi sana. Kwani Allah swt amewasifu wale walio nacho kidogo na huku wanafanya mema. Allah swt katika Qur’an Tukufu, Surah Hashri, 59, Ayah 9:

Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao, wanawapenda walio hamia kwao, wala hawaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyo pewa (Wahajiri), bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa.

672. Jamil bin Darraj anasema kuwa:

“Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alitukusanyisha na kutuambia

“Miongoni mwenu bora kabisa ni yule ambaye ni mkarimu na mtenda mema kwa wenzake na mwovu kabisa ni yule ambaye ni bahili na anawawia wengine kwa hali hiyo na bora ya matendo ni kule kutendeana mema pamoja na ndugu zenu na vile vile kuwatimizia haja na mahitaji yao na kwa hakika matendo haya yanamuudhi na kumvunja nguvu Shaitan na kunamwepusha mtu asiingie Jahannam na badala yake aingizwe Jannah. Ewe Jamil! Naomba uwafikishie habari hizi muumin halisi.”

673. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimfanyia usia Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kwa kumwambia:

“Ewe ‘Ali! Nina ku-usia mambo matatu ambayo kwa hakika yanathibitisha imani.

1. Moja ni kwamba wakati wa shida na dhiki kutoa mali au chochote na kuitumia katika njia ya Allah swt

2. pili kuwawia waadilifu watu

3. tatu ni kuwapa elimu wale wanao tafuta elimu kama wanataka kujifunza elimu.”

674. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amenakili riwaya moja kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ambaye amesema:

“Bora ya sadaka ni ile ambayo inatolewa bila ya kuwa na shida yoyote na inatolewa kwa furaha.”

Mwandishi anasema hadithi hii inawahusu wale ambao wana watoto, familia na ndugu na majamaa. Yeye anakuwa na majukumu ya kuwauliza na kuwatimizia haja hawa watu wanaomtegemea yeye na hivyo baada ya kumalizana nao anatoa sadaka kwa furaha.

675. Sama’a anasema kuwa:

“Siku moja alimwuliza Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s.,

“Iwapo mtu atakuwa na chakula cha kumtosha siku moja, je anaweza kumsaidia yule mtu mwingine ambaye hana chochote? Au tuseme kama mtu ana chakula cha kuweza kumsaidia mwezi mmoja anaweza kuwasaidia wengine ambao hawana kiasi hicho au yeye hana zaidi bali ana kiasi kile tu cha kumtosha yeye,na hivyo hawezi kumsaidia mwingine basi mtu kama huyo atakuwa amelaumiwa na kushutumiwa?”

Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akamjibu,

“Katika suala hili yapo mambo mawili, miongoni mwenu kuna watu ambao wao wanawasaidia na kuwapenda wengine zaidi kuliko nafsi zao na ambapo Allah swt amesema katika Qur’an Tukufu, Surah A-Hashr, 59, Ayah 9:

وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِنْ قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنْفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَنْ يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao, wanawapenda walio hamia kwao, wala wahaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyo pewa , bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa.

Na jambo la pili ni kwamba yule ambaye ana kiasi kile tu ambacho kinamtosha yeye tu, basi mtu kama huyo hayuko katika lawama.

Naam, mkono ulio juu uko afadhali kuliko mkono uliopo chini (yaani yule anayempa mtu mkono wa juu na yule anayepokea ni mkono wa chini)na daima wakati wa kutoa lazima aanzie na wale ambao kwa hakika wako chini ya utunzaji wake (anawajibika kuwatunza na kuwasaidia na kuwatimizia mahitaji yao).”

676. Al Imam Musa al-Kadhim a.s. aliambiwa na ‘Ali bin Sued Assinani:

“Ewe Mawla! Naomba unifanyie usia”.

Kwa hayo Imam a.s. alimwambia

“Fanya Taqwa. Na umwogope Allah swt”.

Na hapo Imam a.s. alinyamaza kimya, basi yeye akasema:

“Ewe Imam a.s.! Nina shida kubwa sana. Mimi nimeshindwa kabisa sina uwezo wowote, yaani fikiria kwamba sina nguo yoyote juu ya mwili wangu iwapo fulani ibn fulani asingenivulia nguo zake akanipa na kunivalisha mimi.”

Katika kumjibu Al Imam Musa al-Kadhim a.s. alimujibu,

“Funga saumu na utoe sadaka.”

Naye kwa kunyenyekea alisema:

“Je nitoe katika yale ambayo mimi ninasaidiwa na watu? Na nitoe kiasi gani kutoka humo?”

Al Imam Musa al-Kadhim a.s. alimjibu

“Chochote kile Allah swt anachokufikishia katika riziki yako toa humo sadaka, kwa kufanya hivyo acha nafsi yako ivumilie kidogo kwa ajili ya kuwatolea wengine walio na shida pia.”

677. Abu Basir ananakili riwaya moja ama kutoka kwa Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. au Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. kuwa:

“Yeye aliuliza, bora ya sadaka zote ni ipi?”

Imam a.s. akamujibu,

“Sadaka bora ni kutoka ile mali ambayo mtu hana nyingi (kitu ambacho unacho kidogo au cha kukutosheleza tu wewe, unatoa humo sadaka), je wewe huna habari

Allah swt amesema katika Qur’an Tukufu, Surah A-Hashr, 59, Ayah 9:

Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao, wanawapenda walio hamia kwao, wala wahaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyo pewa , bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa.

678. Hakika hadithi moja ndefu Masufi walileta dalili moja mbele ya Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. kuwa:

“Allah swt amesema katika Qur’an Tukufu, Surah A-Hashr, 59, Ayah 9:

Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao, wanawapenda walio hamia kwao, wala wahaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyo pewa , bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa.

Je hii ayah inamaanisha kuwa mtu atoe yote yale na afilisike kabisa?”

Imam a.s. aliwajibu

“Kwa ayah hiyo ni ufafanuzi ambavyo watendaji walikuwa wakitenda kama Allah swt alikuwa ameruhusu. Hakuna aliye wazuia hao, na ujira wao pia upo kwa Allah swt, lakini hiyo ni amri ya Allah swt ambayo ni kinyume na matendo yao.

Na sababu ya kufanya hivyo ni kwamba Allah swt anamwonea huruma muumin ili huyo muumin asiweze kuwaletea shida na kuwadhuru nafsi za wananyumba katika familia yao watoto – dhaifu na watoto wadogo, wote walio dhaifu, na ambao hawawezi kustahimili njaa, wazee waume kwa wanawake.

Iwapo mimi nitakuwa na kipande kimoja cha mkate na nikagawa sadaka, basi wale wote wanaonitegemea mie wataangamia na kuteketea.

Ndyio maana Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema, iwapo mtu atakuwa na kokwa tano za tende au mikate mitano au Dinar tano au Dirham tano na yeye anataka kuzitumia zote, basi itakuwa ni vyema kabisa iwapo yeye azitumie kwa ajili ya wazazi wake, na baadaye kwa ajili yake mwenyewe na watoto wake na tabaka la tatu kwa ajili ya ndugu na jamaa zake ambao wana shida na wanahitaji msaada wake, na baada ya hapo awasaidie majirani ambao ni mafakiri, na mwishoni kabisa atumie kwa ajili ya kuwasaidia wengineo katika njia ya Allah swt.

Na baadaye akaendelea kusema kuwa siku moja ilitokea mtu mmoja kutokea Ansaar alifariki. Kwa mujibu wa usia wake yeye alikuwa na watumwa watano au sita ambao wote walifanywa (kwa mujibu wa usia huo) huru na wakaondoka zao na huko nyuma familia yake hakuwaachia chochote watoto wadogo wadogo na wana nyumba yake wote wakawa ni muhtaji, wakawa wao sasa wanategemea misaada kutoka wengine ilhali huyu bwana alikuwa na watumwa watano au sita.

Na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alipojulishwa habari hizo alisikitika mno na akasema,

“Laiti kama nyie mngelikuwa mmenijulisheni kabla kuwa mtu huyo amewafanya watoto na wenye nyumba yake kuwa muhtaji (ni watu wenye kuhitaji misaada na sadaka) basi mimi kamwe nisingelikubali mtu huyu azikwe katika makaburi ya Waislam.’

Halafu anaedelea kusema kuwa wazee wetu wamenakili riwaya kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa mtoaji sadaka inambidi kwanza awatimizie mahitaji ya wale wanao mtegemea yeye; na wale ndugu na jamaa walio wakaribu zaidi ndio awape kwanza (yaani wazazi, mke, watoto na ndugu zake na majamaa wanaofuatia wa karibu zaidi) na baada ya hapo majamaa na ndugu wenye uhusiano wenye ujamaa nao wa mbali ndio wapewe”.

679. Al Imam ‘Ali bin Abi Talib a.s. Amenakiliwa hadithi yake moja isemayo kuwa:

“Wakati muwapapo sadaka masikini muwaombe wawaombeeni dua, na akaendelea kusema, baadaye kuubusu mkono wa yule uliyemsaidia (uliyempa sadaka) kwa sababu sadaka unayoitoa kwanza inakwenda katika mikono ya Allah swt ndipo inapoingia katika mikono ya mwombaji.

Kama vile Allah swt anavyosema katika Qur’an Tukufu, Surah Tawba, 9, Ayah 104:

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنْ كُنْتُمْ فِي شَكٍّ مِنْ دِينِي فَلَا أَعْبُدُ الَّذِينَ تَعْبُدُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ وَلَٰكِنْ أَعْبُدُ اللَّهَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُمْ ۖ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ

Je! Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anapokea toba ya waja wake, na anazikubali Sadaka, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba na Mwenye kurehemu?

680. Ahmad bin Fahad anaandika katika kitabu chake kuwa:

“ Al Imam Zaynul 'Abediin bin Hussein bin ‘Ali bin Abi Talib a.s. wakati wa kutoa sadaka alikuwa akiubusu mkono wake mwenyewe, na mtu mmoja alimwuuliza sababu ya kufanya hivyo na Al Imam Zaynul 'Abediin bin Hussein bin ‘Ali bin Abi Talib a.s. alimjibu,

“Kwa sababu kufanya hivyo ni kwamba sadaka kwanza inakwenda katika mkono wa Allah swt ndipo baadaye huishia katika mkono wa mwombaji.”

681. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Sadaka inayotolewa na muumin kwa hakika inafika mikononi mwa Allah swt na baadaye ndio anapewa aliye mwombaji. Na akaendelea kuelezea ayah ya Qur’an Tukufu, Surah Tawba, 9, Ayah 104:

أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ هُوَ يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَأْخُذُ الصَّدَقَاتِ وَأَنَّ اللَّهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ

Je! Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anapokea toba ya waja wake, na anazikubali Sadaka, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba na Mwenye kurehemu?

682. Jabir Al J’ufi amenakili riwaya kutoka Al Imam Muhammad

al-Baqir a.s. kuwa Al Imam Amir al-Muuminiin ‘Ali bin Abi Talib a.s. amesema kuwa:

“Siku moja nilitoa sadaka ya Dinar moja, hapo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akaniambia,

“Je unajua sadaka inapotolewa na mkono wa muumin kabla yake yeye anakuwa amejitoa nje ya mitego ya masheitani sabini? Na kabla ya yule mwombaji hajapokea hiyo sadaka inakwenda katika mikono ya Allah swt?

Allah swt anatuambia katika Qur’an Tukufu, Surah Tawba, 9, Ayah 104:

Je! Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anapokea toba ya waja wake, na anazikubali Sadaka, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba na Mwenye kurehemu?

683. Mu’alla bin Hunais ananakili riwaya moja kutoka Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. kuwa amesema:

“Kila kitu Allah swt amekiwekea mtunza hesabu wake, isipokuwa sadaka tu, kwamba yeye ndyeo mwenyewe anayeishughulikia. Na baba yangu a.s. alipokuwa akimpa masikini au mwombaji sadaka yoyote, alikuwa akiichukua tena akawa akiinusa na kuibusu na tena alikuwa akimrudishia mwombaji mikononi mwake kwa heshima na adabu.

Kwa sababu sadaka anayopewa mwombaji kwanza inakuwa imepitia katika mikono ya Allah swt ndipo inapoishia katika mikono ya yule anayeomba. Kwa hiyo mimi pia nimependelea kukibusu kitu kile ambacho kimeshaingia katika mikono ya Allah swt ndipo kikaenda katika mkono wa mwombaji!”

684. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Kwa kila kitu isipokuwa sadaka tu Allah swt amemweka Malaika kutunza habari zake – na sadaka ameiweka katika usimamizi wake mwenyewe.”

685. Muhammad bin Muslim ameripoti riwaya moja ama kutokea Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. au Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. kuwa:

“Al Imam Zaynul 'Abediin bin Hussein bin ‘Ali bin Abi Talib a.s. kila alipokuwa akimpatia sadaka mwombaji basi alikuwa akiibusu mikono ya mwombaji huyo. Na alitokezea mtu akauliza sababu ya kufanya hivyo naye akajibu kwa sababu inatoka kwenye mikono ya Allah swt na inaingia katika mikono ya mwanadamu huyo mwombaji.”

686. Al Imam ‘Ali bin Abi Talib a.s. amesema:

“Ujue kuwa uso wako unaong’ara kwa heshima na adabu, na wewe wakati unapokwenda kuomba na ukarefusha mikono yako kwa ajili ya kuomba basi heshima na adabu hiyo inayeyuka na kuanza kudondoka kutoka usoni mwako. Sasa ni kuangalia uyeyukaji huo unamdondokea nani ndio wewe unatakiwa ujue uangalie na ujue.”

687. Ibn Fahad ameripoti riwaya kutoka Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. kuwa:

“Shi’a wetu hata kama watakuwa wakifa kwa njaa basi kamwe wakati wowote ule hawatainyoosha mikono yao kwa mbele ya watu kwa ajili ya kuomba.”

688. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Mtu yeyote anayenyoosha mkono wake na kufungua kiganja chake kwa ajili ya kuomba, basi ushahidi wake utupiliwe mbali.”

689. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Iwapo mwombaji angelikuwa akijua yale majukumu na wajibu walio nao katika kufanya hivyo, basi kamwe asingeomba chochote kwa mtu yeyote. Na vile vile na kutokumpa mwombaji pia kuna majukumu na wajibu mkubwa sana iwapo watu wangelijua basi kamwe wasingeli wakatalia kuwasaidia watu.”

690. Siku moja Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliwaambia Masahaba wake:

“Ni kwa nini hamfanyi bay’a yangu (utiifu wangu)?”

Basi Masahaba wakamjibu:

“Ewe Mtume wa Allah swt! Sisi tumeshakwisha kufanya bay’a yako tangu mwanzoni.”

Kwa hayo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akasema, “Mfanye bay’a katika swala ambalo mle kiapo kuwa nyinyi kamwe hamtanyoosha mikono yenu kwa wengine kwa ajili ya kuomba.”

Na baada ya kula viapo hivyo ikaonekana mandhari tofauti kabisa miongoni mwa Masahaba kiasi kwamba hata mtu alipokuwa akidondosha mkongojo wake basi alikuwa akiteremka kutoka usafiri wake wa mnyama kama ngamia n.k. kuteremka chini na kujiokotea mkonojo wake, na kamwe alikuwa hamwambii mtu mwingine amwokotee na kumpa hiyo bakora yake iliyoanguka”

691. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema:

“Iwapo mtu atakwenda mbio mbio msituni akakata kuni na mzigo huo akauchukua kuja nao kwa hiyo atakuwa ametunza heshima na hadhi yake, basi jambo hilo ni afadhali kuliko udhalilisho wa kuomba.”

692. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Yeyote yule aliyetuomba sisi tunampa na yeyote yule aliyetoa na yeyote yule aliye shukuru basi Allah swt atamfanya awe tajiri.”

693. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema:

“Kwa kuwaomba watu mahitajio yako ni kuteketeza na kuangamiza heshima yako, na vile vile ustahi wako pia unamalizika. Na kwa hakika kile walichonacho wao utajiri wao inambidi mtu akate tamaa asitegemee chochote yaani asiwe na tamaa ya aina yoyote na hakika hii ndio inayo hesabika kuwa ni heshima kubwa ya muumin. Kumbukeni kuwa tamaa ni ufakiri wa aina mojawapo.”

694. Ja’bir amenakili riwaya kutoka Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. kuwa amesema:

“Allah swt ameweka karaha kwa wale wanao omba kwa kung’angania na kwa kufuatilia.”

695. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. amesema kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Enyi watu! Msiombe wakati watu wanapokuwa katika makundi, isitokee kwamba kwa sababu ya ubahili wao ikawawia nyie machungu.”

696. Mufadhdhal bin Kais bin Rumman anasema kuwa:

“Yeye siku moja alikuwa katika huduma ya Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s., na mimi nikamdokezea kidogo kuhusu matatizo niliyokuwa nayo. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akamwambia kijakazi wake:

Naomba ule mfuko. Na akaniambia Abu Ja’far (Manthur) amenitumia hizi Dinar mia nne kwa ajili ya msaada, hivyo chukua wewe. Na uende ukamalize shida na dhiki uliyo nayo.”

Nami nikamwambia:

“Hapana! Kwa kiapo cha Allah swt mimi niwe fidia juu yako – mimi sina nia hiyo – mimi nilikuwa natarajia kuwa wewe uniombee dua kwa Allah swt ili shida na dhiki niliyonayo isiniwie ngumu bali iwe nyepesi.”

Kwa hayo Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akasema,

“Pamoja na mimi kukuombea dua, kamwe usiwaambie mbele ya umati wa watu shida zako kwani kwa kufanya hivyo wewe utapoteza heshima na hadhi yako.”

697. Harith Hamdani anasema kuwa yeye amesikia hadithi ya

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kutokea kwa Al Imam ‘Ali bin Abi Talib a.s. kuwa:

“Maombi ni amana za Allah swt katika vifua vya watu na yeyote yule atakayeficha siri hiyo basi atapata thawabu za ibada.”

698. Kulayni anasema kuwa Bwana Luqman alimpa mafunzo mwanake kwa kumwambia:

“Ewe mwanangu, mimi nimeisha kunywa dawa na magamba yaliyo chungu kabisa, lakini mbele ya shida na dhiki hakuna kitu kinachozidi uchungu wake. Iwapo wewe utapitia katika hali kama hiyo, basi kamwe usiseme maombi yako mbele ya watu, kwa sababu wewe katika macho yao utaanguka heshima na taadhima yako, na watu hao hawawezi kukufaidisha chochote na badala yake nakuomba umwombe yule ambaye anakujaribu kwa mitihani ya aina hiyo, na bila shaka ni yeye tu anayeweza kukuondolea matatizo na dhiki iliyokukabili, hivyo umwombe yeye tu (Allah swt). Yeye ni nani duniani ambaye amemwomba Allah swt na akarudi mikono mitupu, na yupo ambaye aliweka matarajio na matumaini yake kwa Allah swt na akajikuta ametoka mtupu?”

699. Imeripotiwa kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa amesema:

“Ewe ‘Ali! Allah swt ameweka ni amana miongoni mwa waja wake katika hali ya shida na ufukara, na yeyote yule atakayeweza kuificha hiyo amana basi ajue kuwa yeye ni mtu ambaye amedumisha ‘ibada na anapata fadhila za wale walio dumisha ‘ibada na wanao funga saumu, lakini yeyote yule ambaye anaitoboa na kuitangaza hiyo amana ya Allah swt kwa kudhihirisha na kufanya bayana siri ya shida na ufukara wake kwa wengine, na hao watu baada ya kumsikiliza hawamsaidii basi mjue kuwa huyo mtu kwa hakika wamemuua. Mauaji haya sio kwa upanga au kwa mkuki bali ameuawa kimoyo.”

700. Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. ameripoti riwaya kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa amesema:

“Enyi wenye shida na masikini! Tunzeni heshima zenu na mpeni Allah swt furaha ya mioyo zenu ili kwamba Allah swt awalipe mema kwa ufukara na shida zinazo wakabili na kama nyie hamtafanya (isije mkakufuru na kuvuka mipaka kwa sababu ya kukosa subira na hikima) hivyo basi mtambue kuwa mtapata adhabu na gadhabu za Allah swt.”

  • 1. Ndugu msomaji kitabu hiki kinazungumzia mambo ya sadaqah na kuna kitabu kimoja nimekitarjumu katika lugha ya kiswahili kinachozungumzia dhambi kuu, kutokulipa zaka na sadaqah. Kwa hiyo ili kutaka kusema habari zaidi kuhusu zaka naomba usome kitabu hicho hutapata kulipa mambo marefu na mapana juu ya zaka.
  • 2. Mara nyingi sisi hatufanyi mambo mema hatutoi Sadaka, hatusali hatufungi saumu na tunafanya usia wakati wa kufa tunategemea tuache usia kwamba kazi fulani nilikuwa nataka kuifanya mtoto wangu aifanye, Sadaka fulani nilikuwa nataka kuitoa mtoto wangu aitoe, siku fulani sikusali mtoto wangu anisalie, saumu sikufunga mtoto wangu anifungie saumu zangu nk. Kwa hakika mambo kama hayo hayana dhamana kuwa yatatimizwa hivyo unaweza kukosa wewe vyote na ukawa umestahiki wa ghadhabu na adhabu za Allah swt siku ya Qiyamah.
  • 3. Yaani Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. alikuwa anamaanisha hapa kuwa angewaongezeapo kidogo.
  • 4. Nimekitarjumu kitabu juu ya kamari: Katika Islam Uharamisho wa Kamari. Na kimechapwa na Bilal Muslim Mission of Tanzania, DSM, Box 200333