read

Shiah na Hadith

Kwa hakika Mashiah wana mchango mkubwa sana katika uandishi wa Hadith na katika hali ambayo ni sahihi. Na wa kwanza kabisa ni mchango Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. ambao hauna kifani, je litakuwa ni kosa gani iwapo wafuasi wake watamfuata yeye katika kuzidumisha na kuzihifadhi sirat na sunnah za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.?

Katika historia vile vile tunapata mambo yaliyowazi kabisa kuwa kulikuwa na baadhi ya Masahaba wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ambao walikuwa wakikataa kabisa kusiandikwe Hadith kwa sababu ya visingizio kuwa vilikuwa vikigongana na ayah za Qur'an Tukufu. Na wapo Masahaba wengine pia wameadhibiwa vifungo na adhabu mbalimbali kwa ajili ya kunakili na kusambaza Hadith za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.

Kwa hakika Ibn Hajar anaandika katika Futuh al-Bari utangulizi wake jambo moja la kustaajabisha, kuwa yeye anasema,

“Mwanzoni mwa Waislam kulikuwa na utata katika uandishi wa Hadith, kwa sababu baadhi yao walikuwa wanasema kuwa ni karaha kuziandika. Na katika wale waliokuwa wakisema kuwa ni makuruh alikuwepo ‘Umar bin Al Khattab, Ibn Masoud na Abu Sai’d Al Khudhri. Na katika upande wa pili ambao walikuwa wakieneza Hadith kwa usahihi walikuwa ni Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s., mtoto wake Al Imam Hassan ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. na vile vile Anas alikuwapo. Na kwa hakika Mashi’ah wamekuwa mbele katika kueneza Hadith zilizokuwa sahihi na miongoni mwao nawaletea majina yao:

1. Mtumwa wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliyekuwa akiitwa Abu Rafi’, na ambaye alikuwa miongoni mwa wale Waislam wa mwanzoni kabisa.

Bwana ‘Abbas mjomba wake Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ndiye aliyekuwa amempa zawadi huyo, na wakati huyo mtumwa alipompa habari Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa mjomba wake huyo Bwana ‘Abbas ameukubalia Uislam, basi Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kwa kusikia hiyo habari njema alimfanya huru huyo mtumwa kwa sababu ya kuleta habari hizo njema. Katika fadhila zake tunaona kuwa yeye alifanya Hijra mara mbili, na amesali katika Qibla zote mbili na amefanya Bay’a ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. mara mbili.

Na vile vile ameshiriki katika vita vya Jihad vingi sana pamoja na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., na baada ya kifo cha Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. yeye hakumwacha Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. na daima alikuwa naye pamoja. Alikwenda na Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. hadi Kufa, Nchini Iraq na alishiriki naye katika vita vitukufu vyote vilivyotokea na alikuwa ni mtu mmoja aliyekuwa akiaminiwa sana na Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kiasi kwamba yeye alikuwa akitunza Baitul Maal pia.

Yeye alifariki akiwa na umri wa miaka themanini na tano. Na yeye ni miongoni mwa Rawi wa Kishi’ah 1 wanaoaminiwa na kusadikiwa, naye ameandika kitabu kimoja ambamo ameandika riwaya za Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kinachoitwa Kitabu Sunan Wal-ahkam Wal-Qadhaya. Katika vitabu vya ‘ilmul Rijal kitabu hiki ni muhimu sana na chenye faida kubwa sana.

2. Bwana Salman Muhammad (Al Farsi) ambaye baada ya kifo cha Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliandika habari za Jasliq kwa niaba ya Mfalme wa Roma

3. Asbagh bin Nabata, aliandika usia wa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alioumfanyia Bwana Malik Ashtar, vile vile aliandika Nasiha alizomfanyia mtoto wake Muhammad. Asbagh bin Nabata alikuwa ni mmoja wa Masahaba wa karibu sana wa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.

4. Suleim bin Kais Al Hilali yeye ameandika kitabu chenye Ahadith ambacho kinatumika mpaka sasa hivi na kwa mara ya mwisho kilikuwa kimechapwa huko Najaf Al Ashraf, nchini Iraq. Hadith zake zimetokana na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. mwenyewe na vile vile Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.; Miqdad, Salman, Abudhar na wapenzi wa Ahlul Bayt a.s.

5. Mitham al-Tammaar yeye alikuwa mmoja wa Masahaba mashuhuri na mshupavu wa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. yeye naye ameandika kitabu ambacho Sheikh Sadduq amekitumia katika ‘Aamali na vile vile Tabari ametumia katika Basharatul Mustafa.

6. Zaid bin Wahab Aljahni ambaye ametunga kitabu kimoja ambamo ameandika hotuba zote za Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alizokuwa akizitoa siku za Ijumaa na Idi, kwa hakika ameufanyia ‘umma huu ihsani kubwa sana. Ibn Hajar na Ma’ulamaa wengine wanasema kuwa huyu bwana Zaid bin Wahab Thiqqah na wanampa Ukuu. Yeye amefariki katika mwaka takribani 96 Hijriyyah.

7. Mkusanyiko mkubwa kabisa wa semi na Dua za Ma’sumin a.s. yanayojulikana kama Sahifa al-Kamila na vile vile inajulikana kama Zaburi Al Muhammad. Kitabu hicho kimekuwa tangia uhai wa Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. na humo kumeandikwa semi zao n.k. ambayo yalikuwa yamesimamiwa kikamilifu na Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. ndiye aliyefanya mpango huo.

8. Jabir bin Yazid bin Al Harith Al Jaufi, yeye ameziandika yaani yeye katika nuru ya ahadith za Masumin a.s. ameandika Tafsiri, vita vya Jamal, Siffin, na Naherwaan, na vile vile ameandika kuuawa kwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. na Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Yeye amefariki katika mwaka 128 Hijriyyah.

9. Bwana Abu Hamza Thumali (aliyefariki mwaka 150 Hijriyyah) alikuwa mmoja Sahabi mashuhuri mwaminifu kabisa wa Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. na Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. na ameweza kutunga kitabu kiitwacho Annawadir Wa-Dhuhud. Vile vile amefanya tafsiri ya Qur'an Tukufu pia.

10. Vile vile miongoni ma Masahaba wa Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. na Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. alikuwa akiitwa Muhammad bin Keis Al Bijalli ambaye ameandika kitabu kiitwacho Qadhaya Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.

11. Aban bin Taghlib (aliyefariki mwaka 141 Hijriyyah) ni kwamba wote wanaafikiana kuwa yeye ameishi katika zama za Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s., Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. na Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s., na Hadith zao alizozileta huyu Aban bin Taghlib zinasemwa kuwa ni Asili. Yaani inamaanisha kuwa Hadith zake hizo yeye alizoziandika zimetoka moja kwa moja kutoka kwa Maimamu a.s. na si kwa kupitia watu wengine walizozisikia inamaanisha kuwa ni yeye mwenye amezisikia hizo.

12. Takriban waliosomea elimu ya Hadith ilifikia elfu nne au na zaidi kuanzia katika zama za Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. na Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. Siku moja Hassan bin ‘Ali Alwashakhi yeye alikutana na wale watu waliokuwa wakizoea kuzisema Hadith si chini ya mia tisa katika Masji Al-Kufa, na wengi wa wale waliokuwa wakizisema hizo Hadith walikuwa wakisema tumeambiwa Hadith hii na Ja’far bin Muhammad yaani zilikuwa ni Hadith asili ambazo huyo mtu amezisikia moja kwa moja kutoka kwa Maimamu a.s.

13. Ibn Nadhir katika kitabu chake Fahrist amemwandikia yule Yunus bin ‘Abdul Rahman na habari zake kuwa ni mtu mmoja mwaminifu na mwenye kutegemewa kabisa ambaye miongoni mwa Masahaba wa Al Imam Musa al-Kadhim a.s. na Al Imam ‘Ali ar-Ridha a.s. Kwa hakika kitabu hiki ni chenye manufaa sana kiitwacho Jawamiul Aasar.

14. Ibn Nadhir katika kitabu chake Fahrist amewaandika watoto wawili wa Sa’id bin Himad ambao ni Hussein na Hassan na vile vile ameandika habari zao pia, kuwa hawa watu walikuwa ni hodari kabisa katika ‘elimu ya Hadith,Fiq-h na Manaqib. Hao wote walikuwa wana kitabu walichokitunga juu ya Hadith na walikuwa ni miongoni mwa Masahaba wa Al Imam Muhammad Taqi Al Jawad a.s. na Al Imam ‘Ali ar-Ridha a.s.

15. Fadhl Bin Shaazan Nishapouri (aliyefariki 260 Hijriyyah) yeye amewahi kuwa Sahaba wa Maimam watatu a.s. ambao ni, Al Imam Muhammad at-Taqi a.s., Al Imam ‘Ali an-Naqi a.s. na Al Imam Hassan al-'Askari a.s. Naye ameandika vitabu vitatu:

• Cha kwanza Kitabul Faraidh Al Akbar,

• cha pili Kitabu Faraidh Al Awsat,

• cha tatu Kitabu Faraidh Al-Asghar ambacho ni mashuhuri.

16. Na baada ya hapo hii kazi ya ukusanyaji na uandishi wa Hadith ulikuwa umeendelezwa na Masahaba na wazee na wameweza kuleta kazi nne zilizo kubwa kabisa. Kazi hizo nne ambazo mpaka leo zinajulikana kwa jina la mashuhuri Kutub Al-‘Arbi’a yaani inajulikana kwa jina la vitabu vinne.

1. Kitabu Cha kwanza kabisa ni Al Kafi, ambacho kimetayarishwa na kuandikwa na Thiqqatul Islam Al Quleyni a.r. (amefariki mwaka 329 Hijriyyah) katika kitabu hiki zipo Hadith takribani elfu kumi na sita.

3. Cha Pili ni kitabu kingine kinachoitwa Man la haydharul faqih ambacho kimeandikwa na Bwana Abu Ja’far As-Sadduq humo takribani Hadith elfu sita zinapatikana. Vile vile kulikuwa na kitabu chake kingine kijulikanacho kwa jina Madinatul ‘Ilm ambacho Shahid a.r. amekizungumzia. Na kwa kutokana na fitina za zama hizi kitabu hiki hakipo yaani hakipatikani Na Sheikh Sadduq a.r. katika mwaka 381 Hijriyyah

5. & 4. Tunapata vitabu viwili mashuhuri na vyenye faida sana ambavyo vinavyoitwa Tahdhibul Ahkam na kingine Al-Istibsaar vyote vikiwa vya Sheikh Taifah Bwana Ja’far Muhammad bin Hassan Tusi (aliyefariki mwaka 460 Hijriyyah). Kwa kuunganisha vitabu vyote viwili zipo Ahadith elfu kumi na nane zilizo andikwa.

Kwa hakika katika zama zote hizi elimu hii ya Hadith na katika nuru ya Ayah za Qur'an Tukufu na Sunnah ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ‘ummah umeweza kuwatambua na kuwafuata Ahlul Bayt a.s. na kuweza kujipatia ma’arifa yao na Masahaba.

Katika kila zama kazi zilikuwa zikifanyika kwa kiwango fulani katika kuendeleza jitihada hizi za Hadith lakini katika mwaka wa 11 Hijriyyah kulifanywa kazi moja kwa kiasi kikubwa sana cha kutungwa kwa kitabu kiitwacho Bihar Al Anwar ambacho kilitungwa na Muhaqqiq ‘Allama Majlisi a.r. (aliyefariki 1111 Hijriyyah), kitabu hicho ambacho kilikusanya Hadith kwa wingi. Kwa hakika kitabu hiki kimoja yaani Bihar Al Anwar sisi hatujakipa heshima kiasi inavyotakiwa na wala sisi hatujafaidika nacho kiasi tunachotakiwa kufaidika nacho.

Bihar Al Anwar ni kitabu ambacho Hadith ambazo hazikuandikwa katika Kutub Al-‘Arbi’a basi hizo Hadith zinapatikana katika kitabu hiki cha Bihar Al Anwar. Kwa hakika kitabu hiki kina Juzuu ishirini na sita lakini katika Jamhuri ya Kiislam ya Iran na Beirut wamejaribu kukipanga katika vitabu vidogo zaidi ambavyo vimefikia Juzuu mia moja na kumi, ambavyo hata mimi ninavyo. Katika zama hizi vitabu hivyo na vingine vingi vinapatikana kwa urahisi katika CD za compyuta ambavyo mtu hana haja ya kujitwisha vitabu hivyo na inakuwa rahisi kutafuta masuala atakayo.

Kwa hakika Maulamaa wamefaidika sana na Hadith zilizo andikwa katika Bihar Al Anwar na vile vile inadhihirisha vile wanavyoonyesha kuisifu na kuiheshimu kazi hiyo na hapa nimejaribu kuwaletea baadhi ya majina yao ambao wamekuwa katika zama zake hizo na mmoja miongoni mwao kama Marhum ‘Allamah Majilisi alipewa ruhusa ya kunakili yaani ‘ijaza ya riwaya.

1. Muhammad bin Hassan Hurri ‘Aamili aliyefariki mwaka 1104 na mwandishi wa kitabu kinachoitwa Wasa’il as-Shi’ah, nacho kimechapwa si chini ya Juzuu ishirini.

2. Mullah Muhsin Faiz Khashani aliyefariki 1091 na ambaye ni mwandishi wa Al-wafi Kitabu hiki kina Juzuu kumi na nne kinazungumzia juu ya Usul, Furu’, Sunan, na Ahkam.

3. Mulam ‘Abdullah bin Nurullah Bahrani mwandishi wa kitibu kiitwacho Al Awalim kitabu hiki kiko katika Juzuu mia moja.

4. Sheikh Muhammad Ridha bin Abdul Latif Tabrizi, aliyefariki mwaka 1158 na ni mwandishi wa kitabu kiitwacho As-Shifa’.

Sote kwa pamoja tunaomba kwa Allah swt nguvu zetu na jitihada zetu hizi azikubalie. Iwapo kumetokezea au kumebakia kasoro zozote katika kutarjumu basi tunamwomba Allah swt atusamehe na ninawaomba Wanazuoni na wenye Elimu wajaribu kusaidia turekebishe kwa sababu katika kukitarjumu kitabu hiki hapakuwapo na matayarisho kamili kuanzia awali.

Na kazi hii imefanywa kwa nia njema kwa matarajio kuwa itatumika kwa nia njema na itafaa kutukupeleka mahala pema. Inshallah.

Naomba kazi yangu hii niiweke mbele kwa idhini ya Allah swt.

Na kuiweka mbele ya Al Imam Muhammad Sahibuz-Zamaan a.s. iwe ni kama zawadi kwake.

  • 1. Nimetarjumu orodha ya Waandishi 100 wa Kishi’ah wanaojuikana na walio ma’arufu katika vitabu vya Ahl as-Sunnah. Kwani wengi wa Masunni wanadai kuwa Mashi’ah ni Rafidhi (walio asi) na wengine majahili kuthubutu kusema kuwa Mashi’ah ni Makafiri. Hivyo itakuwa vyema iwapo utapata makala hiyo ukaisoma.