read

Sifa na Tabia Zinazokubalika

78. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Al-Kafi, J.2, Uk.235:

“Je, niwatambulisheni Mu’miin ni nani? Muumin ni yule ambaye waumini wengine wanamwamini kwa nyoyo zao na mali pia. Je niwatambulisheni Mwislamu ni nani ? Mwislamu ni yule ambaye Waislamu wengine wanakuwa wamehifadhika kwa ulimi na mikono yake….. Ni haramu kwa Mumiin kumfanyia ubaya mumin mwenzake, au kumwacha katika hali ya shida, au kumsengenya au kumkataa kwa ghafla.”

79. Amesema Al-Imam Ja’far as-Sadiq a.s. Usul-i-Kafi, J.2, Uk. 374:

“Haimpasi Mwislamu kuhudhuria au kushiriki katika mikutano au mikusanyiko ambapo Sharia za Allah swt zinavunjwa na kwamba yeye (huyo Mwislamu) hana uwezo wa kuyazuia hayo.”

80. Amesema Al-Imam Ja’far as-Sadiq a.s. Khisal cha Sadduq, J. 1, Uk. 88:

“Yeyote yule kwa tabia yake husema ukweli, basi matendo yake yametakasika; Na Allah swt humwongezea riziki yule aliye na nia njema; na yeyote yule awatendeaye mema familia yake, Allah swt humwongezea umri mrefu.”

81. Amesema Amir-ul-Muminiin ‘Ali ibn Abi Talib a.s., Safinat ul-Bihaar, J.1, Uk.599:

“Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.. alijiwa na mtu mmoja aliyeomba kufundishwa tendo kwayo ataweza kupendwa na Allah swt pamoja na watu, utajiri wake utaongezeka, mwili wake utakuwa na siha nzuri, umri wake utaongezeka na atainuliwa Siku ya Qiyama pamoja na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w..

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimjibu: ‘Hizi ndizo njia sita zinazohitaji sifa sita:

Iwapo wataka Allah swt akupende, lazima umwogope na ujiepushe na madhambi, Iwapo wataka watu wakupende, lazima uwe mkarimu kwao na ukatae walichonacho mikononi mwao, Iwapo wataka Allah swt akuongezee utajiri wako, hunabudi kutoa malipo yaliyofaradhishwa kwako i.e. Zaka, Khums, na zinginezo.

Iwapo wataka Allah swt aupatie mwili wako afya njema, basi uwe ukitoa sadaqa kila mara iwezekanavyo, Iwapo wataka Allah swt aurefushe umri wako, basi uwe ukiwajali majama’a zako,

Iwapo wataka Allah swt akuinue pamoja nami Siku ya Qiyama, basi ni lazima urefushe sujuda zako mbele ya Allah swt, aliye Pekee na Mmiliki.”

82. Amesema Al-Imam Ar-Ridhaa a.s. Imam wa Nane, ‘Uyun-ul-Akhbaar ur-Ridhaa, J.1, Uk.256:

“Mumin hawezi kuwa mumin kamili hadi hapo atakapokuwa na mambo matatu: Sunna za Allah swt, Sunna za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na Sunna za Imam a.s. wake. Ama Sunna za Allah swt ni kuzificha siri zake; kama vile Allah swt anavyosema katika Sura Al-Jinn, 72, Ayah 26 & 27.

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا {26}

إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِنْ رَسُولٍ فَإِنَّهُ يَسْلُكُ مِنْ بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ رَصَدًا

Yeye ndiye mwenye kujua ya siri, wala hamdhihirishii yeyote siri yake, Isipo kuwa Mtume wake aliye mridhia. Naye huyo humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake.

Na ama Sunnah za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.ni kule kupatana na kuelewana na watu, wakati ambapo Allah swt alimtuma Mtume wake kuwapenda watu na Amesema: ‘Uzoee usamehevu na uwafundishe mema na ujiondoe kutoka majaheli

Ama kuhusu Sunnah za Imam a.s. (kuwa imara na) mwenye subira katika siku nzuri na siku mbaya na nzito, ambavyo Allah swt anatuambia katika Sura Al-Baqara, 2, Ayah 177.

لَيْسَ الْبِرَّ أَنْ تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ وَآتَى الْمَالَ عَلَىٰ حُبِّهِ ذَوِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَالسَّائِلِينَ وَفِي الرِّقَابِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَالْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَاهَدُوا ۖ وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ وَحِينَ الْبَأْسِ ۗ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ

Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Allah swt na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake, Jama’a na mayatima na masikini na wasafiri, na akawa anashika Sala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.

83. Amesema Al Imam Muhammad al-Taqi a.s. (al-Jawad Imam wa Tisa), Muntah al-‘Amal, Uk.229:

“Mumin anahitaji mambo matatu: mafanikio yatokayo kwa Allah swt, mwenye kujipa mawaidha, kukubaliwa na yule ampaye nasiha.”

84. Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Imam wa Nne, aliulizwa:

“Ewe mwana wa Mtume ! Huanzaje siku yako ?” Na Imam a.s. alijibu, Bihar al- Anwar, J.76, Uk. 15:

“Mimi huanza siku yangu huku nikitakiwa kutimiza mambo manane (8):

Allah swt ananitaka nitimize yaliyafaradhiwa juu yangu;

Na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.. ananitaka nitimize yale yaliyo Sunna yake;

Familia yangu inanitaka mimi niwatimizie mahitaji yao kama chakula n.k.;

Nafsi yangu inanitaka niitimizie matamanio yangu;

Shaytani aninitaka mimi nitende madhambi;

Malaika wawili wanaonihifadhi wananitaka mimi nitende matendo kwa moyo halisi,

Malaika wa Mauti anataka roho yangu na

Kaburi inautaka mwili wangu.

Basi mimi ndivyo nilivyo baina ya mzunguko wa matakwa hayo.”

85. Amesema Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. , Bihar al- Anwar , J. 67 Uk.305:

“Kwa hakika kila kitu kinashawishiwa na Mumin kwa sababu Dini ya Allah swt inamfanya yeye awe ni mtu mwenye nguvu, na wala yeye kamwe hashawishiwi na kitu chochote kile, na kwa hakika hii ndiyo dalili ya kila Mumin.”