read

Taqwa na Umuhimu Wake Kwa Waislamu

46. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. , Bihar al- Anwar, J. 71, Uk. 373:

“Miongoni mwa kitu kilicho muhimu kabisa kwa kuwafikisha watu hadi kufikia Peponi ni taqwa na tabia njema.”

47. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. , Bihar al- Anwar , J.77, Uk. 130:

“Wakati wa kutoa uamuzi wa kitu, fikiria matokeo yake. Iwapo ni nzuri kwako wewe kuendelea na maendeleo, fuata hivyo, lakini iwapo inakupotosha, uiachilie mbali ...”.

48. Aliulizwa Al-Imam As - Sadiq a.s. kuhusu maana ya Taqwa, na alijibu , Safinat ul-Bihar, J.2, Uk.678:

“Allah swt asikukose mahala pale alipokuamrisha wewe uwepo, na asikuone pale ambapo amekuharamishia wewe kuwepo

49. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Mustadrak Al-Wasa’il-ush-Shi’h, J.8, Uk.466 no. 10027:

“Onyesha heshima zako kwa ajili ya Allah swt kama vile utakavyoonyesha heshima zako mbele ya mtu mwema miongoni mwa ukoo wako.”

40. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. , Ghura-ul-Hikam, Uk. 321:

“Kwa mtu kuinamisha macho yake kutamwia kama kizuizi dhidi ya matamanio (shahwa) yake.”

50. Amir-ul-Muminiin Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amewaambia wana wake Al Imam Hassan ibn Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. na Al Imam Hussein ibn Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. wakati ‘Abdur Rahman ibn Muljim (Allah amla’ani) alipokuwa amempiga dharuba ya upanga kichwani mwake, katka Nahjul Balagha, Barua no. 47:

“Ninawasihini nyote mumwogope Allah swt na nyinyi wala musiwe na uchu wa starehe za dunia hii hata kama itawakimbilia nyinyi. Wala musikisikitikie kitu chochote cha dunia hii ambacho mumekikosa. Semeni ukweli na mutende (kwa kutumai) malipo. Muwe adui wa mdhalimu na msaidizi wa mdhulumiwa.”

51. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. , Nahjul Balagha, Barua no. 31:

“Ninawauusieni kumwogopa Allah swt, Ewe mwana wangu, kubakia katika Amri Zake, kuujaza moyo wako kwa ukumbusho Wake na kubakia katika kumtegemea Yeye tu. Hakuna Hakuna ushikamano unaotegemewa kuwa madhubuti baina yako na Allah isipokuwa wewe iwapo utaishikilia menyewe.

52. Abi Osama Amesema kuwa alimsikia Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. akisema, Al-Kafi, J.2, Uk. 77

“Muwe nakhofu za Allah, taqwa, ijtihadi, kusema ukweli, uaminifu katika amana, tabia njema na ujirani mwema. Muwaite wengine kwenu (kwa tabia zenu njema), wala si kwa maneno tu. Muwe watu wenye kupendeza na kamwe musiwe watu wa kutuaibisha. Ninawausieni murefushe rukuu’ na sujuda zenu. Kwani kila mmoja wenu anaporefusha rukuu’ na sujuda basi Shaytani hulia nyuma yenu kwa kusea ‘ Ole wangu ! yeye ametii; amesujudu na mimi nilikataa.”

53. Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein bin Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Amesema, Bihar al- Anwar , J.69, Uk. 277:

“Kwa hakika marafiki wa Allah hawatakuwa na khofu yoyote juu yao wala hawata kuwa watu wenye kuhuzunika) iwapo watadumisha yaliyofaradhishwa na Allah swt, wakafuata Sunnah za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.wakajiepusha na yale yaliyoharamishwa na Allah swt, wakawa wacha Allah swt wema katika kile walichonacho katika utajiri na wadhifa wa humu duniani, wakajitahidi kujitafutia kile kilicho halali, wakaamua kutojifakharisha wala kutojilimbikia katika mali na utajiri isipokuwa katika kutoa misaada na kutoa malipo ya kulipa yaliyofaradhishwa kwake. Basi kwa hakika hao ndio waliobarikiwa katika mapato yao na watalipwa mema kwa yale waliyoyatanguliza huko Aakhera.”

54. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. , Mustadrak al-Wasa’il, J. 12, Uk. 89:

“Kwa hakika Wana wa Adam wapo sawa na meno ya kitana kuanzia zama za Mtume Adam a.s. hadi leo, na wala hakuna utukufu wa Mwarabu juu ya asiye Mwarabu, wala Mwekundu juu ya Mweusi isipokuwa kwa Taqwa.”

55. Amesema Al-Imam Ja’far as-Sadiq a.s., Al-Kafi, J. 2, Uk. 76:

“Kwa hakika, tendo dogo kabisa lifanywalo pamoja na Taqwa ni bora kabisa kuliko tendo kubwa (au matendo mengi) lifanywalo bila Taqwa.”