read

Umuhimu wa Maarifa

144. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alielekea Msikitini na huko akakuta makundi mawili ya Waislamu. Kikundi cha kwanza kilikuwa kikijifunza elimu ya Dini, na kikundi cha pili kilikuwa kinafanya ‘ibada.

Kwa kuona hayo amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.:

“Vikundi vyote viko katika kheri, ama hawa wanamwomba Allah swt na hawa wanajifundisha na kuwafundisha wengine wasio na elimu, kwa hakika hawa ndio bora, nimetumwa kwa watu ili kuwafundisha.”

Kisha akakaa pamoja nao.

145. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“Ewe Kumail ! Hakuna harakati zozote utakazozifanya, ila unahitaji kuwa na maarifa.”

146. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“ Kukosa macho ni jambo jepesi kuliko kukosa mwanga (maarifa)”.

147. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

”Usizungumzie usilolifahamu”.

148. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:

“ Elimu ni msingi wa kila heri”.

149. Amesema Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s.:

“ Katika hadith inayotokana na mababa zake, toka kwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. ambae ameipokea toka kwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.

“Watu wengine walio na thamani (qimmah) kwa watu ni wale walio na elimu nyingi kati yao, na wale wenye thamani duni kati yao ni wale wachache wao wa elimu”.