read

Utambulisho wa Ma’sumiin A.S. Katika Ahadith: Kuniyyat na Alqaab

Mara nyingi tunaposoma vitabu vya riwaya tunapata majina mengine yaliyotofauti na majina ya asili. Hivyo tunaona katika Ahadith kuwa Ma’asumiin a.s. wanatambulishwa kwa majina yanayoitwa Kuniyyat au Ilqab, kwa mfano: Qala Abul Hasan ( yaani amesema Abul Hasan ) au Qala Abu ‘Abdillah (yaani amesema Abu ‘Abdillah) n.k. na hapo ndipo tunakuwa hatuelewi ni Ma’sum a.s. yupi ambaye amesema hayo.

Waarabu wanayo desturi ya kuwaita wazee wao si kwa majina yao bali kwa majina mengineyo yaan Kuniyyat au Alqaab. Hivyo inatubidi tupate ufafanuzi zaidi kuhusu majina hayo yanayotumiwa kwa ajili ya Ma’sumiin a.s zaidi ya mara moja. Na hivyo Maulamaa wetu wametuelewesha ilivyo sahihi kabisa.

Wakati wa kujaribu kufafanua juu ya Laqab au Kuniyyat kunatiliwa maanani kuhusu maneno na maana ya Hadith, zama za kusemwa na habari za wale wanaoziripoti, ndipo hapo panapoweza kutambuliwa kwa Alqaab au Kuniyyat katika Hadith hiyo kunatambulishwa Ma’sumiin a.s. yupi.

Hivyo kuelezea hayo na mengineyo, maelezo yafuatayo yatasaidia kutoa mwanga katika swala hili kwa ujumla:

1. Abul Qasim

Kuniyyat hii inatumika kwa ajili ya Mtume Muhammad s.a.w.w. na Imam al-Mahdi a.s. Iwapo kutaripotiwa riwaya kuwa Abul Qasim tu, basi ijulikane kuwa ni Imam al-Mahdi a.f

2. Abu Muhammad

Kuniyyat hii inatumika kwa ajili ya Imam Hasan a.s., Imam Zaynul Aabediin a.s na Imam Hasan al-‘Askari a.s. lakini iwapo kutaandikwa riwaya kwa Abu Muhammad tu tutatambua kuwa riwaya hiyo ni kutoka Imam Hasan al-‘Askari kwa sababu riwaya za Imam Zaynul Aabediin a.s. zinatajwa kwa jina lake tu, bali zipo riwaya chache mno tu kwa Kuniyyat yake.

3. Abu ‘Abdillah

Kuniyyat hii inatumika kwa ajili ya Imam Hussein a.s na vile vile inatumika kwa ajili ya Imam Ja’far as-Sadiq a.s.

4. Abul Hasan

Kuniyyat hii inatumika kwa ajili ya Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. , Imam Musa ibn Ja’far a.s., Imam ‘Ali ibn Musa al-Ridha a.s. na Imam ‘Ali an-Naqi a.s. Iwapo kutakuwapo na Abul Hasan tu katika riwaya, basi kutatambuliwa Imam Musa ibn Ja’far a.s. Na iwapo kutaandikwa Abul Hasan Thani (Abul Hasn wa pili) basi kutakuwa kumefanywa ishara kwa Imam ‘Ali ar-Ridha a.s. na pale panapoandikwa Abul Hasan Thalith (Abul Hasan wa tatu) basi tujue kuwa kunamaanishwa Imam ‘Ali an-Naqi a.s.

5. Abu Ibrahim

Katika Hadith Kuniyyat hii inatumika hasa kwa ajili ya Imam Musa ibn Ja’far a.s.

6. Abu Is-Haq

Kuniyyat hii inatumika kwa kumtambulisha Imam Ja’far as-Sadiq a.s.

7. Abu Ja’far

Kuniyyat hii inatumika kwa ajili ya Imam Muhammad al-Baqir a.s. na Imam Muhammad Taqi a.s. Lakini iwapo kutakuwapo na Abu Ja’far tu au Abu Ja’far Awwal, (Abu Ja’far wa kwanza) basi ijulikane kunamaanishwa kwa Imam Muhhammad al-Baqir a.s.

Na iwapo kutaandikwa Abu Ja’far Thani (Abu Ja’far wa pili) basi kutambuliwe kuwa ni Imam Jawad a.s. Kwa mara chache mno Abul Hasan inatumika kwa ajili ya Imam Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. lakini mahala pengi mno kunatumika Kuniyyat yake mahsusi ya Abul Hassanain.

Alqaab

Wakati pale utakapoona riwaya zinanakiliwa kutoka kwa ‘Aalim, Sheikh Faqih au ‘Abdi Salih, basi mutambue kuwa kunamaanishwa kwa Al Imam Musa al-Kadhim a.s.

Vile Al Imam Ja’far as-Sadiq a.s. anajulikana kwa alqaab zifuatazo: Abu ‘Abdillah, Faqih na ‘Aalim.

‘Allamah Majlisi a.r. anasema kuwa mahala pengi mno katika riwaya kunapotajwa Faqih basi kunamaanishwa kwa Imam ‘Ali an-Naqi a.s. na kwa mara chache mno kunatumika kwa ajili ya Imam Hasan al-‘Askari a.s na Imam al-Mahdi a.s.

Naqi, Mazii, Sahibul ‘Askar na Hajjul kunamaanisha Imam Hasna al-‘Askari a.s.

Sahib na Sahibuddaar zinatukika makhsusi kwa ajili ya Imam al-Mahdi a.s. Lakini Sahibun Nahiyah inapokuja, basi kwa mara nyingine hutumika kwa ajili ya Imam ‘Ali an-Naqi a.s. au Imam Hasan al-‘Askari a.s.

‘Allamah Majlisi anasema kuwa mara nyingine katika Ahadith hutumika maneno Ghaib, ‘Alil au Gharim basi inatubidi kuelewa Imam al-Mahdi a.s.

Iwapo kutakuwapo bi ahadihima (kwa mojawapo) basi itatubidi tuelewe kuwa ni ishara kwa Imam Muammad al-Baqir a.s. au Imam Ja’far as-Sadiq a.s.

Na iwapo tutakuwa bi ‘Askariyyen, tuelewe kuwa ni Imam Alian-Naqi a.s. na Imam Hasan al-‘Askari a.s.

Vile vile iwapo tutaona bi Kadhimain basi kunamaanishwa Imam Musa al-Kadhim a.s. na Imam Mahammad at-Taqi a.s.

Kwa mukhtasari, zipo alqaab nyingi ambazo zinajulikana kimakhsusi kwa ajili ya Ma’sumiin a.s. kama vile Amir al-Muuminiin, Mujtaba Shahid, Zaynul Aabediin, Baqir, Sadiq, Kadhim, Ridha, Jawad, Hadi, ‘Askari, na Sahibuz Zamaan (salaam ziwe juu yao wote).