read

Utukufu na Umuhimu wa Wanazuoni

208. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. katika Bihar al- Anwar , J. 2, Uk. 49:

“Yapo makundi mawili ya Ummah wangu kwamba wanapokuwa wacha iAllah swt, Ummah wangu utakuwa sahihi na wakati watakapokuwa wameingiliwa na ufisadi, basi Ummah wangu utageuka kuwa waovu.”

Kwa hayo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliulizwa kuhusu waliokuwa wakimaanishwa. Alijibu: “Wanazuoni wa Din na watawala.”

209. Amesema Imam Muhammad al-Baqir a.s. katika Bihar al- Anwar , J. 1, Uk. 222:

“Utakapokuwa umekutana na Mwanazuoni basi uwe mwenye kutaka kujua mengi kuliko kujifanya msemaji zaidi, na ujifunze namna ya kusikiliza na namna ya kuzungumza vyema, na wala usimkatize kauli yake yoyote atakayokuwa akizungumza.”

210. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. katika Ithna-Ashariyyah, Uk. 245:

“Ewe ‘Ali ibn Abi Talib ! Malaika Jibraili alitamani kuwa mwanadamu kwa sababu saba zifuatazo:

1. Sala za Jama’a

2. Uhusiano pamoja na wanazuoni

3. Kudumisha amani miongoni mwa watu wawili

4. Kuwahurumia na kuwahishimu mayatima

5. Kuwatembelea na kuwajua hali wagonjwa,

6. Kuhudhuria na kushiriki katika mazishi

7. Kuwagawia maji mahujjaji

Kwa hivyo nyinyi pia muwe watu wa kuzipenda na kuvitekeleza vitu hivyo.”

211. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Amesema katika Nahjul Balagha, Semi No. 265:

“Iwapo matamshi ya watu wenye busara yatakuwa katika malengo yao, basi huwa kama matibabu, lakini yanapokuwa siyo sahihi basi ni sawa na ugonjwa.”

212. Amesema al-Imam Hassan al ‘Askari a.s. katika Al-Ihtijaj, J. 2, Uk. 155:

“Maulamaa wa Kishia’h ni walinzi wa mishikamano ya Islam. Kwa hivyo, yeyote yule katika wafuasi wetu anayechukua jukumu hili basi ni bora kuliko kupigana vita dhidi ya Waroma (kwa sababu huyu analinda mishikamano ya imani zetu).

213. Amesema al-Imam ‘Ali ar-Ridha a.s. katika Bihar al-Anwar , J. 2, Uk. 5:

“Jihadharini kuwa hakimu wa kidini wa kweli ambaye anapatia watu mema na huruma, na kuwahifadhi dhidi ya maadui wao, kuwazidishia neema za Peponi na kuwapatia ridhaa za Allah swt kwa ajili yao (kwa kupitia hidaya).”

214. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Amesema katika Bihar al-Anwar , J.2, Uk. 43:

“ ….Malipo kwa Mwanazuoni ni zaidi kuliko malipo ya mtu afungaye saumu nyakati za mchana na kusali nyakati za usiku na akipigana vita vya jihadi kwa ajili ya Allah swt. Na, wakati mwanazuoni anapokufa, basi kutatokezea pengo katika Islam ambalo haliwezi kuzibwa illa kwa aina yake tu.”

215. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Amesema katika Nahjul Balagha,semi No. 147:

“Ewe Kumayil ! Wale wanaojilimbikizia utajiri na mali ni watu waliokwisha kufa hata kama watakuwa bado hai, wakati maulamaa (wanazuoni) wenye elimu watabakia hadi hapo dunia itakapo bakia. Hata kama watakufa lakini mafunzo na mifano yao itabakia mioyoni mwa watu.”

216. Amesema al-Imam Husayn a.s. katika Tuhaful ‘Uqul, Uk. 172:

“ ….. Kwa hakika, njia ya masuala ya Waislamu na hukumu za Shariah zipo katika mikono ya Wanazuoni ambao ndio wenye amana za Allah swt katika mambo ayatakayo na yale asiyoyataka …”