read

Wafuasi Halisi wa Ahlul-Bayt A.S. na Sifa Zao

86. Al Imam Muhammad al Baqir a.s. alimwambia, Ja’bir, Al-Kafi, j. 2, Uk. 74:

“Je inatosheleza kwa mtu kujiita Shia na mfuasi wetu ati kwa kudhihirisha mapenzi yetu, Ahlul Bayt ? Kamwe sivyo hivyo !, Kwa kiapo cha Allah swt, huyo mtu kamwe hawezi kuwa mfuasi wetu isipokuwa yule ambaye amejawa khofu ya Allah swt na kumtii ipasavyo.

Ewe Ja’abir! Wafuasi wetu hawawezi kutambuliwa isipokuwa kwa sifa zifuatazo watakazo kuwanazo: unyenyekevu, kujitolea; uadilifu; kumsifu Allah kupita kiasi; kufunga saumu na kusali; kuwatii wazazi; kuwasaidia masikini, wenye shida, wenye madeni, na mayatima wanaoishi karibu naye; kusema ukweli; kusoma Qur’an; kuuzuia ulimi kusema chochote kuhusu watu isipokuwa kwa mapenzi; na kuwa mwaminifu kwa majama’a kwa maswala yote”

87. Amesema Sulayman Ibn Mahran kuwa Al-Amali, cha Saduq, Uk. 142:

Yeye alimtembelea Imam Ja’far as-Sadiq a.s. wakati ambapo baadhi ya wafuasi (Mashiah) walikuwa karibu naye na alimsikia Imam a.s. akiwaambia:

“(Mujiheshimu) muwe kama vito vya thamani kwa ajili yetu na wala kamwe musiwe wenye kutuaibisha sisi. Waambieni watu kuhusu mema, na muizuie ndimi zenu zisizungumze maneno maovu na mambo yasiyo na maana.”

88. Amesema Al-Imam Ja’far as-Sadiq a.s., Al-Kafi J. 2, Uk. 56:

“Kwa hakika, sisi huwapenda wale walio na busara, wenye kuelewa, wenye elimu, wenye kufanya subira, waaminifu na wenye imani. Kwa hakika Allah swt aliwajaaliwa Mitume a.s. kwa tabia njema. Kwa hivyo yeyote yule aliye na sifa hizo basi amshukuru Allah swt, lakini yule ambaye hana hayo basi amlilie Allah swt, Aliye Mkuu na Mwenye uwezo, na amwombe hayo. “Ja’abir kwa unyenyekevu alimwuliza Imam a.s. ndiyo yapi hayo”, na Imam a.s. alimjibu: “Nayo ni: Ucha-Allah swt, kutosheka, subira, kushukuru, kuvumilia, tabia njema, furaha, hima, bidii, shauku, ukarimu, ukweli na uwaminifu katika amana.”

89. Amesema Al-Imam Muhammad al-Baqir a.s., Al-Kafi, J. 2, uk.75:

“Yeyote yule anamtii Allah swt basi ni mpenzi wetu, na yeyote yule asiyemtii Allah swt basi ni adui wetu (sisi Ahlul-Bayt).”