read

Umma wa Waislam Katika Zama za Mwisho.

984. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., amesema Waqayi-ul-Ayyam, Uk. 439:

“Kutakuja zama miongoni mwa watu kuwa:
1. Wao hawatawaheshimu Wanazuoni wao (yaani Maulamaa) ila kwa mavazi yao mazuri;

2. wao hawatasikiliza Qur'an Tukufu ila kwa sauti ya kuvutia;

3. Na wao hawatamwabudu Allah swt isipokuwa katika mwezi wa Ramadhani tu;

4. wanawake wao hawatakuwa na aibu,

5. maskini miongoni mwao hawatakuwa na subira,

6. na matajiri wao hawatakuwa wakarimu, kwani wao hawataridhirika kwa kidogo na wala hawatakinai kwa wingi.

7. Wao hawatashiba kwa kingi, wao watafanya kila jitihada kwa ajili ya matumbo yao;

8. dini yao itakuwa ni mapesa (mali na utajiri);

9. na wake zao ndio watakuwa Qiblah zao (tunapoelekea kusali huko Al-Ka’abah tukufu);

10. na majumba yao ndio itakuwa Misikiti yao;

11. wao watakimbia kutoka Maulamaa wao kama vile kondoo anavyo kimbia kutoka kwa mbwa mwitu.

Hapo watapokuwa kama hivyo (basi Allah swt atawatumbukiza katika mambo matatu).
1. Atawaondolea baraka katika mali zao.

2. Watakufa (kutoka humu duniani) wakiwa hawana imani iliyo halisi.”

3. Watatawaliwa na mtawala dhalimu.

985. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema, Bihar al-Anwaar, J. 23, Uk. 22:

“Utafika wakati katika umma wangu kwamba :
1. watawala wao watakuwa wakatili na wadhalimu,

2. Maulamaa na Wanazuoni wao watakuwa waroho wa mali na utajiri na watakuwa na imani kidogo,

3. waumini wao watakuwa ni wanafiki,

4. wafanya biashara wao watakuwa wakijishughulisha kwa kutoa na kupokea riba na kuficha maovu na kasoro ya vitu wanavyonunua na kuuza na

5. wanawake wao watakuwa wamejihusisha mno na mambo ya kujirembesha ya dunia.

6. Hivyo, wakati huo, mwovu kuliko wote miongoni mwao ndio watakaokuwa wakiwaongoza wao, na

7. wema miongoni mwao watakuwa wakiwaita watu lakini hakuna mtu atakaye wajibu.”

986. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., amesema Al-Ithna-'Asheriyyah, Uk. 202:

“Utafika wakati katika Umma wangu ambapo wao watakuwa wakipenda vitu vitano na kuvisahau vitu vitano:
1. Wao watakuwa wakiipenda dunia na kuipuuzia Akhera.

2. Wao watapenda mali na kusahau hesabu ya siku ya Qiyamah

3. Waume zao watawapenda wanawake waovu na kuwasahau Hur al-‘Ayn

4. Wao watapenda majumba na watayasahau makaburi yao.

5. Wao watajipenda wenyewe kupita kiasi na kumsahau muumba wao.

Kwa hakika watu kama hawa hawanipendi mimi na mimi pia siwapendi wao.”