read

Mwandishi

Ayatullah Murtaza Mutahhari, alizaliwa mwaka wa 1920, na alikuwa ni miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu hodari sana na waandishi mashuhuri wa zama hizi. Alikuwa amezama sana katika kujifunza kimapokeo (traditional learning) na alivutiwa na watetezi wa masomo haya ya kimapokeo. Alikuwa ni mwanafalsafa na alikuwa amesoma falsafa kwa undani sana. Kazi yake ina sifa ya uwazi wa kifalsafa ambao ulimfanya awe na sifa ya kushughulikia tatizo la msingi la fikra ya kidini ambalo ndio kiini cha kitabu hiki.

Ayatullah Mutahhari alipata elimu yake ya msingi ya theolojia kutoka kwa baba yake, Sheikh Muhammad Husain, huko kwao, katika mji wa Fariman, Ayatulah alipofikisha umri wa miaka kumi na mbili alijunga na kituo cha elimu cha Mashhad, na hapo alisoma kwa miaka mitano. Kisha alienda Qum kituo kikuu cha elimu ya Kiislamu. Alikaa na kusoma hapo kwa miaka kumi na tano. Alihitimu masomo yake katika Imani za Kiislamu na Maarifa ya Sheria chini ya usimamizi wa mwanafalsafa mashuhuri Allamah Muhammad Husain Tabatabai, Imam Khomeini na wanazuoni wengine wakubwa. Kisha akahamia Tehran.

Katika kipindi cha elimu yake Ayatulah alihisi kuwa wakomunisti walitaka kuibadilisha dini takatifu ya Uislamu na kuharibu roho yake kwa kuchanganya mitazamo yao ya kumkana Mwenyezi Mungu na Falsafa ya Uislamu na kwa njia ya kuzitafsiri Aya za Qur’ani kiyakinifu. Kwa kusema kweli, sio ukomunisti tu uliomshughulisha Ayatullah. Pia aliandika tafsiri ya Qur’ani, na falsafa, maadili, sosholojia, historia na masomo mengine mengi. Katika kazi zake zote, lengo lake lilikuwa ni kujibu hoja potofu zilizotolewa na watu mbali mbali dhidi ya Uislamu, kuonyesha udhaifu wa itikadi nyingine na kuonyesha utukufu wa Uislamu. Aliamini kuwa ili kuonyesha uongo wa Ukomunisti na itikadi nyinginezo ilikuwa muhimu sana kutoa maana juu ya ukomunisti na kuielezea taswira halisi ya Uislamu.

Ayatullah Mutahhari aliandika kwa uangalifu na bila kuacha wala kuchoka toka enzi za uwanafunzi hadi mwaka 1979, mwaka aliouawa shahidi. Kazi zake nyingi zimechapishwa ndani na nje ya Iran. Ameandika vitabu vingi na si juu ya mada anazozipendelea bali juu ya mada zinazohitajika. Kila ilipotokea kuwa kitabu fulani juu ya mada muhimu za Kiislamu kinahitajika na hakipo basi alikiandika.

Kazi za Mutahhari hazikuvumiliwa na wale wanaomkana Mwenyezi Mungu na hivyo waliamua kumuondoa mnamo tarehe 1 Mei mwaka 1979. Kifo chake cha kishahidi kilikuwa ni msiba mzito. Habari za msiba huu zilipomfikia Imam Khomeini hakuweza kuyazuia machozi yake. Katika salamu zake za rambirambi alisema; “Nimenyang’anywa mwanangu kipenzi. Ninaomboleza kifo cha yule ambaye alikuwa ni matunda ya uhai wangu”.

Maelfu wa Waislamu walihudhuira mazishi yake. Alizikwa Qum jirani na kaburi la Bibi Fatima Ma’sumah.

Ayatullah Mutahhari alikuwa ni mtu mashuhuri katika nyanja za kidini na kielimu nchini Iran. Alifanya kazi katika Chuo Kikuu cha Tehran kama Mkuu wa Idara ya Theolojia na Mafunzo ya Kiislamu.

Wakati alipouawa shahidi alikuwa ni Rais wa Baraza la Kikatiba la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na alikuwa akitekeleza majukumu yake kwa namna inayofaa kabisa.

Kazi zake zimetafsiriwa na kuchapishwa katika lugha za Kifaransa, Kiarabu, Kituruki, Kikurdi na Kiingereza.

‘The Islamic Seminary’ ilipata heshima ya kuchapisha baadhi ya vitabu hivi.