read

Ndoa Ya Muda – I

Moja ya sheria tukufu za Uislamu kwa mtazamo wa sheria ya Ja’fari (Shia) ni kuwa kuna aina mbili za ndoa, ndoa ya kudumu na ndoa ya muda maalumu.

Baadhi ya athari zinazotokana na aina hizi mbili za ndoa ni sawa (zinafanana) na nyingine ni tofauti. Kuna tofauti mbili za msingi tu kati ya ndoa hizi mbili. Moja ni kuwa katika ndoa ya muda, mwanaume na mwanamke huingia katika mkataba wa ndoa ya muda maalum. Muda ukiisha wanaweza kuongeza au kuachana.

Tofauti nyingine ni kuwa kuna uhuru mkubwa zaidi wa kuchagua katika ndoa ya muda. Wanaooana wanaweza kuwekeana masharti yoyote wanayopenda. Kwa mfano, katika ndoa ya kudumu mume anawajibika kumtunza mke wake na kumtimizia mahitaji yake ya kila siku. Pia anapaswa kumpatia mavazi, malazi na mahitaji mengine ya lazima kama vile matibabu. Lakini katika ndoa ya muda, kila kitu hutegemea masharti ya mkataba. Inawezekana kuwa mume anaweza kuwa hana uwezo au hayuko tayari kubeba gharana za mke wake, au mke anaweza asipende kutumia fedha za mume wake.

Katika ndoa ya kudumu mke anapaswa kumtambua mume wake kuwa ni mkuu wa familia na kumtii katika mambo ambayo yamo ndani ya mipaka ya familia, lakini katika ndoa ya muda hili linategemea masharti ya mkataba wa ndoa waliyowekeana. Katika ndoa ya kudumu, mke na mume wanarithiana, lakini katika ndoa ya muda hawarithiani.

Hata hivyo, katika ndoa ya muda, baada ya nikaha kusomwa, wanandoa hutambuliwa kuwa ni mume na mke halali na wanaweza kuingiliana lakini kabla ya hapo hawaruhusiwi kabisa kufanya hivyo (tendo la ndoa).

Tofauti kuu kati ya ndoa ya muda na ndoa ya kudumu ni kuwa ndoa ya muda huweka masharti (majukumu) machache zaidi kwa wanandoa. Masharti yake hutegemea hiari, matakwa na makubaliano yao wao wenyewe. Kwa asili aina hii ya ndoa huwapa wanandoa uhuru fulani, na huwapa wao uhuru wa kuamua ni muda gani ndoa itadumu.

Katika ndoa ya kudumu si mume wala mke anayeweza kutumia njia za kuzuia mimba bila idhini ya mwenzake, lakini katika ndoa ya muda idhini sio jambo la lazima. Hii ni aina nyingine ya uhuru waliopewa mume na mke.

Mtoto anayezaliwa katika ndoa ya muda ana hadhi sawa kisheria na mtoto aliyezaliwa ndani ya ndoa ya kudumu.

Mahari: Mahari lazima ipangwe wakati wa ndoa, lakini malipo yake halisi yanaweza kutegemea makubaliano ya wanandoa wote wawili.

Mahari ni ya lazima katika ndoa zote mbili ya muda na ya kudumu ingawa kuna tofauti kuwa kutopangwa kwa mahari katika ndoa ya muda huibatilisha ndoa hiyo, lakini kutopangwa kwa mahari katika ndoa ya kudumu hakubatilishi ndoa. Ikiwa mahari haikupangwa wakati wa kufunga ndoa, mke hustahili mahari ambayo imezoeleka eneo hilo.

Katika ndoa ya kudumu, mume amekatazwa kabisa kumuoa mama au binti wa mke wake na mke amekatazwa kuolewa na baba au mtoto wa mume wake. Hali iko hivi pia katika ndoa ya muda.

Kama ilivyokuwa hairuhusiwi kutoa pendekezo la kumuoa mke aliyeolewa ndoa ya kudumu, halikadhalika hairuhusiwi kutoa pendekezo la kumuoa mwanamke aliye ndani ya ndoa ya muda. Mtu akizini na mwanamke aliyeolewa ndoa ya kudumu hiki huwa ni kizuizi cha kudumu cha yeye kutokumuoa mwanamke huyo na halikadhalika mtu akizini na mke wa mtu aliye katika ndoa ya muda huwa amejiwekea kizuizi cha kudumu cha yeye kutokumuoa mwanamke huyo.

Baada ya kupewa talaka, katika ndoa ya kudumu mke hupaswa kukaa eda, kipindi ambacho haruhusiwi kuolewa na mwanaume mwingine, halikadhalika katika ndoa ya muda baada ya ule muda waliokubaliana kuisha, mke anapaswa kukaa eda pia. Tofauti pekee ni kuwa kwa mke wa kudumu, eda ni miezi mitatu, ambapo kwa ndoa ya muda eda ni vipindi viwili vya hedhi, au siku 45. Kuwaoa madada wawili kwa wakati mmoja hairuhusiwi katika ndoa zote mbili, ya muda na ya kudumu. Hii ndio maana ya ndoa ya muda kwa mujibu wa sheria ya Shia.

Ni wazi kuwa tunaiunga mkono sheria hii kama itazingatia masharti yake. Ikiwa baadhi ya watu waliitumia vibaya huko nyuma au bado wanaitumia vibaya, hilo ni jambo ambalo liko nje ya sheria. Kufutwa kwa sheria hii, kama inavyopendekezwa na watu wa kisasa (modernist) hakuwezi kuwa na manufaa yoyote kwani kwa kuifuta maovu hayatakoma, isipokuwa tu yatachukua sura mpya. Vile vile, kufutwa kwa sheria hii kutasababisha kuzuka kwa maovu mengine mengi. Kinachotakiwa ni kuwa badala ya kutafuta dosari za sheria hii, watu wanapaswa kusaidiwa wajirekebishe na kuelimishwa.

Sasa hebu tuangalie kwanini ni muhimu kuwa na taasisi ya ndoa ya muda sambamba na ndoa ya kudumu. Ikiwa ndoa ya muda ni muhimu je inakubaliana na hali za sasa na mawazo ya kisasa ya maadili? Tunataka kulijadili swali hili chini ya vichwa viwili.

Maisha ya sasa na ndoa ya muda. Dosari na uovu wa ndoa ya muda.

Maisha Ya Sasa Na Ndoa Ya Muda.

Kama tulivyojifunza huko nyuma, ndoa ya kudumu huwapa majukumu mazito wanandoa wote wawili, mume na mke.

Hata hivyo, hakuna mvulana au msichana ambaye wakati wa kupevuka, ambapo huwa katika shinikizo kubwa la hamu ya ngono, huwa amejiandaa kwa ndoa ya kudumu. Mahitaji ya zama hizi yameongeza urefu wa kitambo kati ya kupevuka kwa asili na kupevuka kijamii, ambapo mtu huwa na uwezo wa kujenga familia. Katika zama za kale, ambapo maisha yalikuwa rahisi, mvulana alikuwa anaweza kuanza kufanya kazi fulani toka kipindi cha awali kabisa cha kupevuka kwake na akaendelea nayo hadi mwisho wa uhai wake. Lakini sasa hivi hili haliwezekani tena.

Mvulana humaliza hatua mbali mbali za elimu akiwa na umri wa miaka 25, ikiwa hakufeli katika hatua yoyote. Hapo ndipo anapoweza kutarajiwa kuwa na kipato chake mwenyewe. Huchukua miaka mingine mitatu au minne ya kujiandaa na kuweza kuoa. Mambo yanakuwa hivi pia kwa msichana anayependa kupata elimu bora maishani.

Mabarobaro Na Mihemko Ya Ngono.

Leo hii ukimuambia mvulana wa miaka 17, ambaye ndio anakuwa katika kilele cha hamu ya ngono, aoe, watu watakucheka. Hali itakuwa hivyo hivyo kwa msichana mwanafunzi wa miaka 16. Katika umri huu wote, wavulana na wasichana hawawezi kubeba majukumu ya ndoa ya kudumu, sio tu kwao kama mume na mke bali na kwa watoto wao pia watakaozaliwa.

Kipi Ni Bora: Utawa Wa Muda, Ukomonisti Wa Ngono, Au Ndoa Ya Muda?

Tunajua maumbile yalivyo, lakini hali hiyo ya maisha katika ulimwengu wa sasa haituruhusu kuoa tukiwa na umri wa miaka 16 au 17. Maumbile hayako tayari kuchelewesha upevukaji au hamu ya ngono hadi tutakapomaliza elimu yetu. Je vijana wetu wapo tayari kuishi maisha ya ubikra kwa muda hadi hapo watakapokuwa na uwezo wa kuoa ndoa ya kudumu? Hata kama kijana mwenyewe yuko radhi kustahamili, je, maumbile yapo tayari kumsamehe asipatwe na shinikizo na hitilafu za neva ambazo kwa kawaida matokeo yake ni kumfanya ajiepusha kutokana na tendo la kawaida la ngono, kama ilivyobainishwa na wataalamu wa kisasa wa sayansi ya akili?

Sasa tumebakiwa na njia mbili tu. Ya kwanza ni kumruhusu mvulana kushirikiana ngono na mamia ya wasichana, na msichana kushiriki katika uhusiano haramu na wavulana wengi, na kisha kutoa mimba nyingi. Hii inamaanisha kuwa kivitendo tunaruhusu Ukomonisti wa ngono. Kwa hakika, tukitoa uhuru usio na mipaka kwa wavulana na wasichana, tutakuwa tunakidhi matakwa ya Azimio la Haki za Binaadamu, kwa sababu kwa maoni ya watu wengi wenye akili finyu, Azimio linataka kuwa, ikiwa wanaume na wanawake wataenda motoni, basi waende pamoja mkono kwa mkono.

Lakini swali ni iwapo itawezekana kwa wavulana na wasichana hawa ambao watakuwa wamefanya ngono zisizo na idadi wakati wa kipindi chao cha masomo, kuishi maisha ya kawaida ya familia.

Njia ya pili ni ndoa huru ya muda. Kwa kuanzia ndoa ya muda humpa kila mume mke mmoja kwa wakati mmoja. Ikiwa kila mwanamke ana mwanaume mmoja, ni wazi kila mwanaume atakuwa na mwanamke mmoja, isipokuwa pale ambapo jinsia moja itakuwa kubwa sana kuliko nyingine. Hivyo wavulana na wasichana wanaweza kupita katika kipindi chao cha masomo bila kupata madhara ya kuishi maisha ya utawa wa muda, au kuangukia katika lindi la Ukomonisti wa ngono.

Ndoa Ya Majaribio.

Kimsingi inawezekana kwa mwanaume na mwanamke wanaokusudia kuona ndoa ya kudumu wakawa kila mmoja hana imani ya kutosha juu ya mwenzake, hivyo wakaoana kwa majaribio kwa muda fulani. Wakiwa wameaminiana vya kutosha, huendelea kuishi maisha ya ndoa, vinginevyo wanatengana. (kwa hiyo, tofauti kati ya mtindo wa Kimagharibi wa uhusiano pamoja na mwanamke na Uislamu ni kuwa kwa Wamagharibi hakuna dhana ya mfumo wa ndoa kati ya mwanamke na mwanaume ambapo katika Uislamu wenzi huhesabiwa kuwa mke na mume hata kama ni kwa muda).

Nadharia Ya Russell Ya Ndoa Ya Muda.

Katika kitabu chake ‘Matrimony and Morals’ mwanafalsafa maarufu sana wa Kiingereza, Bertrand Russell, anasema kuwa malaya wanauhifadhi usafi wa kimaadili (kutozini) wa wake zetu na binti zetu. Mtazamo huu ulipotolewa kwa mara ya kwanza na Luckey katikati ya kipindi cha utawala wa Victoria watetea maadili walikereka sana, ingawa hata wao hawakujua kwanini. Hata hivyo hawakuweza kuzivunja hoja za Luckey. Mantiki ya watetezi wa maadili ilikuwa, kama watu wangefuata maadili yao, malaya wasingekuwepo. Lakini walielewa fika kuwa hakuna aliyezingatia walichosema.

Hii ndio kanuni ya kizungu ya kukabiliana na hatari inayoletwa na wanaume na wanawake wasioweza kufunga ndoa ya kudumu, na iliyotajwa hapo juu ni kanuni iliyopendekezwa na Uislamu. Ikiwa kanuni hii ya kizungu itazingatiwa na jukumu hili likakabidhiwa kwa kundi fulani la wanawake wenye bahati mbaya, je hii itakuwa inaafikiana na heshima ya utu wa mwanadamu na staha ya mwanamke na kiini cha Azimio la haki za Binadamu?

Bertrand Rusell, katika kitabu chake, ameingiza sura ya ndoa ya majaribio pia. Anasema kuwa Lindsay, ambaye kwa miaka mingi alikuwa jaji wa Denver, na kwa nafasi yake hiyo alikuwa na nafasi ya kutosha ya kuchunguza ukweli wa mwenendo wa maisha, alipendekeza kuwa iwepo ‘ndoa ya wenzi’ (companionship marriage). Lakini kwa bahati mbaya jaji huyu alilazimika kupoteza kazi yake kwa kuwa alikuwa anajali maslahi ya vijana mno kuliko kuwajengea ndani yao hisia ya dhambi. Ili kuhakikisha anafukuzwa, mengi yalisemwa na kanisa Katoliki na Ku Klux Klan, (chama cha siri cha watu ambao hawataki watu weusi kushirikiana na watu weupe – wabaguzi wa rangi nchini Marikani).

Ndoa ya wenzi ilipendekezwa na msomi anayependelea kuhifadhi mila za kale kwa nia ya kuweka jambo litakaloleta uimara katika mahusiano ya ngono. Lindsay alibaini kuwa tatizo kubwa la ndoa lilikuwa ni ukosefu wa fedha. Fedha haihitajiki kwa ajili ya watoto watakaozaliwa tu, lakini pia kwa sababu haimuwajibikii mwanamke kubeba gharama za matunzo ya familia. Anafikia hitimisho kuwa vijana wanapasa kufunga ndoa za wenzi (muda) ambazo ni tofauti na ndoa za kawaida katika njia tatu. Kwanza nia ya ndoa hii sio kuzaa watoto.

Pili kwa vile mwanamke huwa hajazaa mtoto, kuachana muda unapokwisha huwa jambo rahisi. Tatu, katika suala la talaka, mwanamke hustahili kulipwa masurufu baada ya kuwa ameachwa. Hapana shaka kwamba mapendekezo ya Lindsay yanafaa na yanatekelezeka, kama yangekuwa yamekubaliwa kuwa sheria, yengetarajiwa kuwa na matokeo mazuri kwa maadili.

Ambacho Lindsay na Russell wanakiita ndoa ya wenzi ni tofauti kidogo tu na ndoa ya muda katika Uislamu, lakini pendekezo hili linaonyesha kuwa wanafalsafa wa fani hii wamebaini kuwa ndoa ya kawaida ya kudumu haikidhi mahitaji yote ya jamii.