read

Neno La Mchapishaji

Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza, kwa jina la: “Woman and her rights.” Sisi tumekiita: “Haki za Wanawake Katika Uislamu .”

Kitabu hiki, Haki za Wanawake Katika Uislamuni matokea ya utafiti wa kielimu uliofanywa na Mwanachuoni wa Kiislamu, Allamah Murtaza Mutahhari.

Allamah Murtaza Mutahhari, mwandishi wa kitabu hiki ameichambua historia ya maisha ya mwanamke katika nchi za Magharibi na Mashariki (Asia) na mifumo yao ya ndoa. Mwandishi amerejea vyanzo vya wanasaikolojia na wanasosholojia wa Magharibi ili kuthibitisha hoja zake. Madhumuni yake ni kutaka kuthibitisha kwamba Uislamu una mfumo mzuri wa ndoa na haki za wanawake, kinyume na wanavyoamini watu wa Magharibi na wengine waliokuwa na kasumba ya umagharibi.

Inakubaliwa na kila rafiki na adui kuwa Qur’ani Tukufu ilifufua haki za wanawake. Hata maadui wanakiri angalau kwamba Qur’ani wakati wa kuteremshwa kwake ilichukuwa hatua kubwa katika kuboresha hali ya mwanamke na kurejesha haki zake za binadamu. Qur’ani ilifufua haki za mwanamke kama mwanadamu na kama mwenzi wa mwanaume katika utu na haki za binadamu lakini haikupuuza jinsia yake wala jinsia ya mwanaume.

Kwa maneno mengine Qur’ani haikupuuza maumbile ya mwanamke. Ndio maana kuna kuwafikiana kikamilifu kati ya kanuni za maumbile na kanuni za Qur’ani. Mwanamke katika Qur’ani ni sawa na mwanaume katika maumbile. Vitabu hivi viwili vikubwa vya kimungu (Qur’ani na maumbile), kimoja kikiwa kimeumbwa na kingine kikiwa kimekusanywa, vinakubaliana na kuafikiana kabisa. Nia ya kitabu hiki ni kuangazia na kuelezea kuafikiana huku.

Kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote. Kutokana na ukweli huu, Taasisi yetu ya ‘AlItrah Foundation’ imeona ikitoe kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili, kwa madhumuni yake yale yale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili, ili kuongeza ujuzi wao katika masuala ya dini na ya kijamii.

Tunamshukuru ndugu yetu, Aziz Njozi kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.

Mchapishaji:
AlItrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar es Salaam, Tanzania.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa
Fatima Zahra
Binti anayeheshimika wa Mtukufu Mtume wa Uislamu,
na kiigizo cha wanawake wa Ulimwengu.