read

Sababu Za Kihistoria Za Mitala II

Tamaa ya mwanaume katika ngono na utawala wake wa kibabe peke yake sio sababu tosha za kuibuka kwa mitala. Lazima ziwepo sababu nyingine zilizochangia katika mwanaume muasherati kukidhi hamu yake ya kuwa na wanawake wa aina mbalimbali. Ni rahisi zaidi kujiingiza katika ngono holela kuliko kuwa na mwanamke wa chaguo lake kama mke wake wa halali na kujitwisha jukuma la kutunza watoto wake wa baadaye. Mitala huwa mashuhuri katika jamii zile tu ambazo zinajali maadili na zinazuia ngono holela na mwenye kiu ya uasherati hulazimika kulipa gharama ya kutaka aina mbalimbali za wanawake kwa kumkubali mwanamke anayehusika kuwa mke wake wa halali na kubeba jukumu la kuwa baba wa watoto wa mwanamke huyo.

Sasa hebu tuangalie kama kuna sababu zozote za kijografia, kiuchumi au kijamii zilizochangia kuibuka na kuwepo kwa ndoa za mitala.

Sababu Za Kijiografia

Montesquieu na Gustav Leobeon wanasisitiza kuwa hali ya hewa na tabia za nchi ndio sababu kuu za maendeleo ya mitala. Wasomi hawa wanaamini kuwa tabia ya nchi na hali ya hewa ya nchi za Mashariki zinaifanya mila hii isiepukike huko. Katika nchi za Mashariki, wanawake hupevuka na kuzeeka haraka zaidi, hivyo mwanaume huoa mke wa pili na wa tatu. Pia wanafikiri kuwa mwanamke mmoja hawezi kukidhi kiu ya ngono ya mwanaume aliyekulia katika tabia ya nchi za Mashariki.

Gustav Leobeon katika kitabu chake “History of Islamic and Arab Culture” (Historia ya utamaduni wa Kiislamu na kiarabu) anasema: “Mila ya ndoa za mitala haikuanzishwa na dini. Ni matokeo ya tabia za nchi, tabia ya watu wa huko na sababu nyingine zinazohusiana na maisha ya Mashariki. Haihitajiki kusisitiza sana kuwa hizi ni sababu zenye nguvu sana. Pia tabia zao za kimwili na kimhemko, unyoyeshaji wao wa watoto na magonjwa yao mara nyingi huwalazimisha wanawake wa Mashariki kujitenga na waume zao. Kwa kuzingatia tabia za nchi za Mashariki (Hali ya Hewa) pamoja na tabia za kitaifa za wanaume wa Mashariki, huwa haiwezekani kwa wanaume kustahamili kutengana na wake zao japo kwa muda mfupi, hivyo ndoa za mitala zimekuwa ni mila.”

Montesquieu katika kitabu chake, “The Spirit of Law” anasema: “Katika nchi za kitropiki wanawake hupevuka wakiwa na umri wa miaka nane, tisa au kumi na baada ya kuolewa punde huwa wajawazito. Tunaweza tukasema kuwa katika nchi za kitropiki, mimba hushika mara moja tu baada ya ndoa.”

Predo, alipokuwa anayaelezea maisha ya Mtume wa Uislamu, anasema kuwa alimuoa Khadija akiwa na umri wa miaka mitano na alianza kumwingilia akiwa na umri wa miaka nane. Kwa sababu ya ndoa za mapema, wanawake katika nchi za kitropiki huzeeka wakiwa na umri wa miaka ishirini. Anasema kuwa huanza kuzeeka hata kabla ya kupevuka.

Katika nchi zenye tabia ya vuguvugu, wanawake hubaki na ujana na uzuri wao kwa muda mrefu zaidi. Huchelewa kupevuka na huwa wamekomaa zaidi na wanakuwa na uzoefu zaidi wakati wanapoolewa. Hupata watoto katika umri mkubwa zaidi, na mume na mke huzeeka takribani kwa wakati mmoja. Hivyo ndivyo usawa kati ya mwanamke na mwanaume unavyopatikana na wanaume huwa hawahitaji kuwa na mke zaidi ya mmoja.

Hivyo ni kwa sababu ya tabia ya nchi ndio maana sheria imekataza mitala huko Ulaya lakini ikairuhusu huko Asia.

Maelezo haya sio sahihi. Mila ya mitala haiko katika nchi za kitropiki tu huko Asia. Katika kipindi cha kabla ya Uislamu mila hii ilikuwa mashuhuri sana nchini Iran, ambapo tabia ya nchi ni ya vuguvugu. Ni uzushi kabisa kusema kuwa katika nchi za Mashariki wanawake huzeeka wakiwa na umri wa miaka ishirini, kama ilivyodaiwa na Montesquieu. Inashangaza pia kusikia kuwa Mtume wa Uislamu, alimuoa Khadija akiwa na umri wa miaka mitano na kwamba alianza kumwingilia akiwa na umri wa miaka nane. Kila mtu anaelewa kuwa Mtume alimuoa Khadija, wakati yeye Mtume, alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano na Bibi Khadija alikuwa na umri wa miaka ishirini na nane, ingawa baadhi ya vyanzo vya kihistoria vyenye makosa vinasema kuwa Khadija wakati huo alikuwa na umri wa miaka arobaini.

Pili, ikikubaliwa kuwa kuwahi kwa umri wa uzee kwa wanawake na nguvu nyingi za urijali kwa wanaume ndizo sababu ya mila hii, kwa nini watu wa Mashariki hawakujiingiza katika ngono holela na ufuska kama wenzao wa Magharibi ambao walifanya ngono holela na ufuska katika zama za kati na za sasa. Kama alivyoonyesha Gustav Leabeon, suala la mume kuwa na mke mmoja limebakia katika vitabu vya sheria lakini halionekani katika maisha halisi ya kila siku.

Tena, katika nchi za Mashariki, mitala ipo katika muundo wake wa Kisheria. Mwanamume humkubali mwanamke mhusika kama mke wake wa kisheria na halali na anapaswa kubeba jukumu la kuwa baba wa watoto wa mwanamke huyo. Mitala iliyopo Ulaya ni ile haramu na isiyokuwa ya kisheria pamoja na ndoa za siri. Mwanaume wa Magharibi hujiingiza katika ngono holela na hukwepa majukumu yanayohusiana na ndoa.

Mitala Huko Magharibi

Tunaona kuwa ni muhimu kutoa maelezo mafupi ya mitala huko Ulaya katika zama za kati kama yalivyoelezewa na mwana historia mashuhuri wa kimagharibi. Maelezo haya yanapasa kuwafunua shuka jeusi wale wanaozikosoa nchi za mashariki kwa mitala kwamba licha ya dosari zinazodaiwa, mitala zilikuwa ni ndoa zenye heshima zaidi kuliko kile kilichokuwepo Ulaya.

Will Durant katika kitabu chake, History of Civilization, Juz.17, anatoa maelezo ya kuvutia juu ya hali ya maadili nchini Italia katika kipindi cha uamsho. Hapa chini tunatoa muhtasari wa yale aliyosema chini ya kichwa “Morals in Sexual Relations”.

Katika utangulizi wake mfupi anasema kuwa kabla ya kuelezea maadili ya Italia, tunaweza kusema kuwa kwa asili mwanamume ni mwenye asili ya kuoa wake wengi. Ni vikwazo vikali vya kimaadili, kazi nyingi ngumu na umaskini na uwajibikaji wa hali ya juu wa mke, kwa pamoja ndio vinaweza kumlazimisha kubaki na mke mmoja.

Kisha anasema kuwa uzinifu haukuwa jambo geni katika zama za kati kabla ya zama za uamsho. Kama ilivyokuwa kwamba katika zama za kati dhambi ya zinaa ilishutumiwa na watu walihimizwa kuishi maisha ya usafi, halikadhalika katika kipindi cha uamsho (Renaissance), vijana, wasomi walifundishwa kuwa na tabia njema na kutunza ubikra kwa wanawake.

Wasichana waliokuwa wanatoka katika familia zinazoheshimika walikuwa kwa kiasi fulani wakitengwa na wanaume wasiokuwa na familia yao na walifundishwa faida za kutunza ubikra wao hadi watakapoolewa. Wakati fulani mafundisho haya yalikuwa yanawaingia kichwani na kusaidia. Inaripotiwa kuwa ilikuwa kwamba ikitokea msichana akinajisiwa alikuwa akijizamisha majini na kufa. Haya lazima yatakuwa ni matukio haba sana, kwa sababu askofu alikuwa akichukua taabu ya kujenga mnara baada ya kifo chake ili kukumbuka usafi wake wa kimaadili.

Idadi ya waliokuwa wakifanya mapenzi kabla ya ndoa lazima itakuwa ilikuwa kubwa, kwa sababu kulikuwa na idadi kubwa ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa katika kila mji wa Italia. Lilikuwa ni jambo la fahari kwamba mtu alikuwa hana mtoto wa nje ya ndoa, lakini kuwa naye mmoja halikuwa ni jambo la aibu. Kwa kawaida mume alimshawishi mke wake wakati wa ndoa kuja kwa mumewe pamoja na mtoto wake (wa huyo mwanamke) aliyemzaa nje ya ndoa. Ili alelewa pamoja na watoto wa ndani ya ndoa. Kuzaliwa nje ya ndoa halikuwa ni doa katika utukufu wa yeyote. Isitoshe cheti cha uthibitisho kuwa mtoto husika ni wa ndani ya ndoa kilikuwa kinaweza kupatikana kirahisi kwa kumpa rushwa kiongozi wa kanisa.

Iwapo watoto wa ndani ya ndoa wenye haki ya kurithi walikuwa hawapo, basi watoto wa nje ya ndoa walikuwa wakirithi mali na hata kiti cha ufalme kama ilivyokuwa kwa Frante I ambaye, alimrithi Alfonso I, Mfalme wa Naples. Pius – II alipokuja Bavaria mwaka 1459, alipokelewa na wana wa mfalme saba, ambapo wote walikuwa ni watoto wa nje ya ndoa. Uhasama na uadui kati ya watoto wa nje ya ndoa na wale wa ndani ya ndoa ndio ilikuwa sababu muhimu ya migogoro katika zama za uamsho. Liwati nayo ilikuwa ni kufufuliwa tu kwa desturi ya kale ya kigiriki.

San Bernardino aliikuta aina hii ya upotofu na uchafu ikiwa imeenea sana huko Naples akahisi kuwa hali hiyo inahatarisha kutokea kwa adhabu waliyopewa watu wa Sodoma. Artino aliikuta hali hii chafu huko Roma pia. Umalaya pia ulikuwa katika kiwango cha juu. Mwaka 1490, kati ya wtu wote 90,000 wa Roma, wanawake 6,800 walikuwa wamesajiliwa kama malaya. Idadi hii haihusishi mahawara na malaya ambao hawajasajiliwa. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 1509, kati ya watu laki tatu wa mji huo, kulikuwa malaya 11,654. Katika karne ya 15, msichana ambaye alikuwa amefikisha umri wa miaka 15 hali ya kuwa hana mume alionekana kama doa katika jina zuri la familia.

Katika karne ya 16 “umri wa mkosi” ulisogezwa mbele hadi miaka 17, ili kumuwezesha msichana kupata elimu ya juu. Wanaume, ambao walikuwa wanafurahia huduma za malaya waliokuwa wameenea kila sehemu, walikuwa wanavutiwa kuoa ikiwa tu mwanamke mhusika aliahidi kumpatia mahari ya kuvutia. Kwa mujibu wa mfumo wa zama za kati, mke na mume walitarajiwa kupendana na kushirikiana katika huzuni na furaha. Inavyoonekana matarajio haya kwa kiasi fulani yalifikiwa, lakini bado uzinifu ulikuwa umejikita mizizi. Ndoa nyingi za watu wa tabaka la juu zilikuwa ni za kidiplomasia zilizofungwa kwa maslahi ya kisiasa na kiuchumi. Waume wengi waliona kuwa ni haki yao kuwa na bibi pembeni. Mke alikuwa anakasirika sana lakini alikuwa analazimika kuizoea hali hiyo.

Miongoni mwa watu wa tabaka la kati uzinifu ulionekana kuwa ni mila halali. Machiavelli, na rafiki zake inaonekana hawakujisikia vibaya juu ya hadithi za kutokuwa kwao waaminifu ambapo walikuwa wakibadilishana wake. Ilikuwa mke naye akifuata nyendo za mumewe za kutokuwa mwaminifu, kwa kawaida alikuwa anaipuuzia tabia yake wala hakuona wivu wala kukereka.

Hii ndio hali ya maisha ya watu ambao wanaona kuwa mitala ni uhalifu usiosameheka wa watu wa Mashariki na wakati mwingine wamekuwa wakiilaumu hali ya hewa (tabia ya nchi) kwa kusababisha mila hii isiyokuwa ya kibinadamu. Lakini hali ya hewa ya huko kwao haiwaruhusu kutokuwa waaminifu kwa wake zao na kuvuka mipaka ya mke mmoja!

Pia inafaa ieleweke kuwa kutokuwepo kwa mitala ya halali miongoni mwa wazungu, iwe mizuri au mibaya, hakutokani na dini ya Kristo, ambaye kamwe hakuikataza. Kinyume chake, dini ya Kristo inazithibitisha kanuni za Agano la kale ambalo waziwazi linazitambua ndoa za mitala. Hivyo tunaweza kusema kuwa dini ya Kristo inaruhusu mitala na Wakristo wa kale walikuwa wakioa na kuolewa mitala. Hivyo kujiepusha kwa wazungu kisheria na mitala lazima kutakuwa kumetokana na sababu nyinginezo, sio dini.

Hedhi

Baadhi wanasema kuwa ndoa za mitala zimetokana na hedhi za mwanamke na mchoko anaoupata baada ya kuzaa na kutopenda kwake kufanya ngono wakati wa kunyonyesha.

Will Durant anasema kuwa katika jamii za kijima wanawake huzeeka haraka. Hiyo ndiyo sababu kwamba ili wawanyonyeshe watoto wao kwa muda mrefu na ili warefushe tofauti ya umri kati ya mtoto mmoja na mwingine bila kuziziba kiu za wanaume zao za kupata watoto, na ili kuwawezesha waume zao kukidhi hamu yao ya ngono huwahimiza waume zao kuoa mke mpya. Mara nyingi imeonekana kuwa mke wa kwanza, kwa nia ya kupunguza uzito wa majukumu yake, humshawishi mume wake kuoa mke wa pili ili apate watoto zaidi na mali zaidi.

Hapana shaka kwamba hedhi ya mwanamke na uchovu wake baada ya kuzaa, kijimai, huwaweka mwanaume na mwanamke katika nafasi tofauti.

Sababu hizi humfanya mwanaume amgeukie mwanamke mwingine, lakini hizi peke yake haziwezi kuwa sababu ya mitala isipokuwa tu kama kuna vikwazo vya kijamii na kimaadili vinavyozuia ngono holela, sababu hizo zinaweza kuwa na nguvu tu ikiwa mwanaume hayuko huru kufanya ngono holela.

Kikomo Cha Kipindi Cha Kuzaa Kwa Wanawake

Baadhi wanaamini kuwa kikomo cha kipindi cha kuzaa kwa wanawake ni moja ya sababu zilizoibua ndoa za mitala kwani inaweza kutokea kwamba mwanamke anafikia umri huu kabla hajazaa watoto wa kutosha. Inawezekana pia kwamba watoto wameshakufa.

Katika hali hizo, kama mume hataki kumtaliki mke wake wa kwanza na wakati huo huo anataka watoto zaidi, basi anakuwa hana namna isipokuwa kuongeza mke wa pili, au wakati fulani hata mke wa tatu. Halikadhalika utasa wa mke wa kwanza unaweza kuwa ni sababu ya mume kuoa mke wa pili.

Sababu Za Kiuchumi

Sababu za kiuchumi zimetajwa pia kuwa ni sababu ya mitala. Inasemekana kuwa katika zama za kale wake wengi na idadi kubwa ya watoto vilikuwa vinachukuliwa kuwa ni rasilimali ya kiuchumi. Alikuwa akiwatumikisha wake na watoto wake na wakati mwingine alikuwa akiwatendea kama watumwa. Wakati mwingine aliamua hata kuwauza. Wengi wa watumwa hawakutekwa vitani bali waliuzwa na baba zao.

Hii inaweza kuwa sababu ya mitala. Kwa sababu mwanaume anaweza kupata watoto tu kwa kumkubali mwanamke kuwa ni mke wake wa halali. Ngono holela haiwezi kufanikisha jambo hili. Hata hivyo hii sio sababu ya ndoa zote za mitala.

Baadhi ya jamii za kijima zilikuwa zikioa wake wengi zikiwa na wazo hili kichwani. Lakini si watu wote walioa wake wengi kwa lengo hili. Katika zama za kale, mitala ilikuwa ni mila iliyozoeleka katika matabaka mbalimbali. Wafalme, wana wa wafalme, machifu, mitume na wafanya biashara walikuwa na wake wengi.

Kama tunavyojua, matabaka haya, kamwe hayakuwanyonya kiuchumi wake zao wala watoto wao.

Idadi Ya Wanafamilia

Kupenda idadi kubwa ya watoto na kupanuka kwa familia, kumekuwa ni moja ya sababu za mitala. Mitazamo ya mwanamke na mwanaume juu ya idadi ya watoto wanayoihitaji inaweza kutofautiana. Idadi ya watoto ambayo mwanamke anaweza kuzaa ni ndogo sana, awe na mume mmoja au waume wengi.

Lakini idadi ya watoto ambayo mwanaume anaweza kuzaa inategemeana na idadi ya wanawake alionao. Kinadharia inawezekana mwanaume akawa na maelfu ya watoto kwa kupitia mamia ya wanawake alionao. Tofauti na ulimwengu wa sasa, katika ulimwengu wa kale idadi ya wanafamilia iilikuwa inahesabika kuwa ni sifa muhimu ya kijamii. Makabila na koo zilifanya kila linalowezekana kuongeza idadi yao, ilikuwa ni fahari ya ukoo kuwa na kabila kubwa. Ni wazi kuwa ndoa za mitala ndio ilikuwa ni njia pekee ya kufikia lengo hili.

Uwingi Wa Wanawake

Sababu ya mwisho na muhimu zaidi ambayo ilichangia kuibuka kwa ndoa za mitala ni kuwa mara zote wanawake huwa ni wengi kuliko wanaume. Sio kwamba idadi ya wanawake wanaozaliwa ni kubwa kuliko ya wanaume. Ikitokea katika sehemu fulani wanawake zaidi wamezaliwa katika sehemu nyingine wanaume zaidi watazaliwa. Lakini bado idadi ya wanawake wanaofaa kuolewa ni kubwa kuliko idadi ya wanaume wanaofaa kuoa. Sababu ni kuwa idadi ya vifo vya wanaume mara zote imekuwa kubwa kuliko wanawake. Inawezekana kwamba ikiwa ndoa ya mke mmoja mume mmoja itazingatiwa kikamilifu, idadi kubwa ya wanawake itabaki bila waume wa halali, watoto wa ndani ya ndoa na maisha ya familia.

Hakuna shaka kwamba kwa uchache hii ndio ilikuwa hali ya mambo katika jamii za kijima. Tayari tumeshanukuu maoni ya Will Durant anayesema kuwa katika jamii za kijima, uhai wa mwanaume mara zote ulikuwa hatarini kwa sababu mara zote alikuwa akishughulika katika kuwinda na kupigana na hii ndio sababu kwamba idadi ya vifo vya wanaume ilikuwa kubwa kuliko wanawake. Kwa kadri idadi ya wanawake ilivyozidi kuongezeka, kulikuwa na mambo mawili tu ya kuchagua ama kuruhusu mitala au kuilazimisha idadi kubwa ya wanawake kuishi maisha yao yote bila kuolewa.