read

Uislamu Na Maisha Ya Kisasa II

Mwanadamu sio kiumbe pekee anayeishi maisha ya kijamii. Wanyama wengi, na hususan wadudu hupenda kuishi pamoja na kushirikiana. Wanafuata kanuni za mgawanyo wa kazi, uzalishaji na ugavi na kutoa na kupokea amri.

Nyuki, na baadhi ya wadudu jamii ya mchwa wana mfumo huu bora wa maisha, mfumo ambao utamchukua mwanadamu, anayejiona kuwa ni mfalme wa viumbe vyote, miaka au hata karne ili kufikia kiwango hicho cha ufanisi.

Ustaarabu wao (wadudu hawa) haujapitia vipindi kama vile zama za mwituni, zama za mawe na zama za nyuklia. Toka mwanzo wamekuwa na ustaarabu na mfumo wa namna moja kama tu walivyo leo. Ni mwanadamu aliyeanzia sifuri. Tazama :

وَخُلِقَ الْإِنْسَانُ ضَعِيفًا

“Mwanadamu aliumbwa dhaifu .”Suratul Nisaa 4:28

Kwa upande wa wanyama, mahitaji yao ya maisha hayabadiliki. Kwao usasa na fasheni mpya havina maana. Ulimwengu wa kale na ulimwengu wa sasa kwao hauna tofauti yoyote. Kwao sayansi haifanyi ugunduzi wowote ule. Bidhaa mpya kabisa nyepesi na nzito za viwanda hazikuingia katika soko lao; kwa nini? Kwa sababu wanaishi kwa silika na sio kwa akili (mantiki).

Maisha ya kijamii ya mwanadamu mara zote yanabadilika. Kila karne ulimwengu unabadilika. Hapo ndio kuna siri ya mwanadamu kuwa mfalme wa viumbe vyote. Mwanadamu ni mtoto wa maumbile aliyekomaa na kustahili heshima. Amefikia hatua ambayo hahitaji muongozo wa moja kwa moja wa ile nguvu ya ajabu iitwayo silika.

Maumbile yanafahamu kuwa mwanadamu ni kiumbe aliyekomaa, na ndio maana yamemuacha huru. Yale ambayo wanyama wanayatekeleza kwa silika na kwa kufuata kanuni za maumbile ambazo hawawezi kuzivunja/kukiuka, wanaadamu wanatakiwa kuyatekeleza kwa kutumia akili na elimu na kwa kufuata sheria zilizopitishwa na zinazoonekana.

Mwanadamu akiwa ni mwamuzi wa mwisho wa majaaliwa yake mara zote anaweza kupotoka na kuiacha njia ya maendeleo, na hapa ndio kuna siri ya kuteleza kwake, vipingamizi vyake (anavyokumbana navyo) kupotoka na kushindwa kwake.

Kama tu ilivyo kuwa maendeleo yapo wazi kwake, halikadhalika njia ya kuelekea upotofu, ufisadi na kushindwa haijafungwa.

Wanaadamu wamefikia hatua ambayo kwa mujibu wa maneno ya Qur’ani wanaweza kubeba dhamana ambayo mbingu, ardhi na milima haviwezi kubeba; kwa maneno mengine, wanaweza kuishi maisha huru na wanaweza kuchukua majukumu ya kisheria, kitaalamu na mengineyo. Hii ndio sababu hawana kinga ya makosa, ubinafsi, ujinga na dhulma.

Pale Qur’ani inapouelezea uwezo huu wa ajabu wa binadamu, mara moja unamtaja kuwa ni ‘dhalimu na mjinga’.

Uwezo na sifa hizi mbili za mwanadamu, uwezo wa kuboreka (kuwa bora zaidi) na uwezo wa kupotoka havitenganishiki. Mwanadamu sio kama mnyama ambaye katika maisha yake ya kijamii, huwa haendi mbele wala nyuma, hageukii kulia wala kushoto. Lakini mwanadamu kwa upande wake, katika maisha yake wakati fulani huenda mbele na wakati fulani nyuma. Katika maisha ya wanadamu kama kuna mwendo na kasi, basi kuna kusimama na kupumzika pia. Kama kuna maendeleo na kubadilika kwenda katika hali bora zaidi basi kuna ufisadi na upotofu pia. Kama kuna haki na wema, basi kuna udhalimu na ushari pia. Kama elimu na busara vimedhihiri basi ujinga na matamanio duni yamedhihiri pia.

Inawezekana kwamba mabadiliko yanayotokea na hali mpya zinazoonekana vikawa ni vya kundi la pili (la mabaya).

Wasiotaka Kubadilishwa Na Waliopotoshwa.

Ni moja ya tabia za mwanadamu kwamba wakati fulani hufanya jambo kupita kiasi na wakati fulani hufanya jambo kwa kiasi kidogo zaidi kuliko inavyohitajika. Kama akichagua kundi la kati na kati hufanya jitihada kutofautisha kati ya mabadiliko ya aina sahihi na mabadiliko ya aina potofu. Hujaribu na hufanya jitihada kuusukuma muda mbele kwa msaada wa elimu na ubunifu wake na kujinasibisha na maendeleo huku akijaribu kuudhibiti upotofu na kuepuka kutangamana nao.

Lakini kwa bahati mbaya, si mara zote mwanadamu huchagua njia hii. Anaandamwa na magonjwa mawili ya hatari, ugonjwa wa kutotaka kubadilika na ugonjwa wa ujinga. Ugonjwa wa kwanza matokeo yake ni kubaki bila mabadiliko na kujiepusha na maendeleo na matokeo ya ugonjwa wa pili ni upotofu wa kuangamia.

Asiyetaka kubadilika huchukia kila jambo jipya na hawezi kuafikiana na kitu chochote isipokuwa cha zamani. Kwa upande wa pili, limbukeni huona kila kitu kipya kuwa ni cha kisasa na maendeleo na hukiaona kuwa ndio hitajio la wakati. Kwa yule asiyetaka mabadiliko (rigid) kila maendeleo mapya kwake anaona ni ufisadi na upotofu wakati limbukeni anaona mambo yote mapya bila kubagua yote yana maana kupanuka kwa utamaduni na elimu.

Asiyetaka mabadiliko hatofautishi kati ya pumba na kiini safi na kati ya njia na malengo. Kwa maoni yake kazi ya dini ni kuhifadhi yale yote ya kale na kuukuu hata kama hayatumiki. Anafikiri kuwa Qur’ani iliteremshwa ili kudhibiti mwendo wa wakati na kuibakiza hali ya dunia iwe vile vile siku zote.

Kwa mujibu wa mtazamo huu, mila za zamani na zilizopitwa na wakati, kama vile kuanza kusoma Qur’ani kuanzia mwisho, kuandikia kalamu za matete na wino wa kuchovya kunawia kwenye beseni la kituruki; kula kwa mikono, kutumia taa ya mafuta ya taa na kubakia bila ya kujua kusoma na kuandika ni mambo ya kidini ambayo lazima yahifadhiwe na kudumishwa.

Kwa upande mwingine limbukeni huelekeza macho yake yote nchi za Magharibi ili aweze kuiga mtindo wowote mpya utakaotokea na kila mila mpya. Huiita hali hii kuwa ni kisasa na jambo la lazima kufuatwa lililoletwa na wakati. Wote wawili, wasiotaka mabadiliko na waliopotoka (wajinga) wanaamini kuwa mila na desturi zote za zamani ni kanuni/matendo ya kidini, tofauti ni kuwa asiyetaka mabadiliko anataka kuzihifadhi wakati mjinga anaona kuwa dini ni sawa na kudorora (bila mabadiliko yoyote).

Katika karne chache zilizopita suala la migongano kati ya dini na sayansi limekuwa likibishaniwa sana miongini mwa watu wa nchi za Magharibi.

Wazo la migongano liliibuka kutokana na mambo mawili. Kwanza kanisa lilikuwa limezikubali baadhi ya dhana za kisayansi na kifalfasa kuwa ni imani za kidini, lakini maendeleo ya sayansi yakathibitisha uongo wa dhana hizo. Pili, sayansi imebadilisha muundo na hali za maisha.

Wale wasiotaka mabadiliko, ambao wana muonekano wa kushika dini, wanataka kuufanya muonekano wa nje wa maisha ya kimaada kuwa sehemu ya dini, kama tu, bila ulazima wowote walivyoyapa sura ya kidini baadhi ya masuala ya kifalsafa.

Limbukeni nao wanaamini kuwa dini imeamuru muundo fulani wa maisha ya kimaada, na kwa vile sayansi imeamuru kuwepo kwa mabadiliko katika muundo huu, dini inapaswa kutupiliwa mbali.

Kupinga mabadiliko kwa kundi moja, na ujinga wa kundi jingine, kumezua wazo la kubuni la mgogoro kati ya sayansi na dini.

Hadith Ya Mafumbo Katika Qur’ani

Uislamu ni dini ya kimaendeleo na inataka wafuasi wake waendelee. Qur’ani imetumia hadith ya mafumbo (yenye mafundisho) kuwashawishi Waislamu wasonge mbele, chini ya nuru ya Qur’ani. Inasema kuwa wafuasi wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni kama mbegu iliyopandwa katika ardhi. Kwanza matawi yake hutokeza kama majani laini ya mbegu. Kisha hukua na kuimarika sana kiasi cha kuweza kusimama katika kikonyo chake. Hakua haraka mno kiasi cha kuwashangaza sana wakulima.

Huu ni mfano wa jamii ambayo Qur’ani inaukusudia. Qur’ani inachokikusudia ni kukua. Qur’ani inataka kuweka msingi wa jamii ambayo mara zote itakuwa ikikua, ikiendelea na kupanuka.

Will Durant anasema hakuna dini iliyowataka wafuasi wake kuwa na nguvu kama Uislamu ulivyofanya. Historia ya Uislamu wa awali inaonyesha ni kiasi gani Uislamu ulivyo na nguvu ya kuijenga upya jamii na kuisukuma mbele kimaendeleo.

Uislamu unapingana na vyote viwili kutaka mabadiliko na ulimbukeni (ujinga) na unaviona vyote hivi viwili kuwa ni hatari. Uchakavu wa kiakili wa wasiotaka mabadiliko na kung’ang’ania kwao mila za zamani ambazo hazina uhusiano wowote na Uislamu, kumetoa kisingizio kwa limbukeni kuuona Uislamu kuwa unapingana na maisha ya kisasa (usasa).

Kwa upande mwingine kufuatana na kuiga mitindo mipya zaidi na namna za maisha za Magharibi kunakofanywa na limbukeni, imani yao kwamba kufuata utaratibu wa Kimagharibi kimwili na kiroho, kukubali kwao tabia, adabu na desturi za Magharibi, na kuiga kibubusa sheria za kiraia na kijamii kutoka katika nchi za Magharibi, kumetoa kisingizio kwa wasiotaka mabadiliko kukitazama kila kitu kipya kwa mashaka na kukiona kama tishio kwa dini yao, uhuru wao na kwa haiba ya kijamii ya jumuiya yao.

Kwa sasa, Uislamu unagharamikia makosa ya makundi yote mawili. Ung’ang’anizi wa wasiotaka mabadiliko umeacha uwanja wazi kwa limbukeni kufanya uharibifu na ujinga wa limbukeni umewafanya wasiotaka mabadiliko kuwa ving’ang’anizi zaidi katika imani zao.

Inashangaza kuona kuwa hawa wanaojiita wameelimika na kustaarabika ingawa kiuhalisia ni watu wajinga, wanafikiri kuwa muda ni maasumu (haubebi dhambi). Ukweli ni kuwa mabadiliko yote yanaletwa na watu, na mwanadamu sio maasumu hata kidogo (hajaepukana na madhambi). Sasa vipi inaweza kufikirika kuwa mabadiliko ya muda mara zote huwa hayana makosa na matatizo.

Kama ilivyo tu kuwa mwanadamu ana matakwa ya kupenda sayansi, maadili, sanaa na dini, na mara zote huchukua hatua mpya kwa maslahi ya wanadamu, pia ana baadhi ya tabia mbaya. Ni mbinafsi, mwenye uchu wa madaraka na mwenye kupenda raha. Anapenda fedha na unyonyaji kama tu alivyo na uwezo wa kugundua mambo mapya na kutafuta njia bora zaidi za kufanya mambo pia ana dhamana ya kutenda makosa. Lakini limbukeni na waliopotoka hawajui mambo hayo. Wanarudia mahadhi yale yale kuwa ulimwengu wa kisasa upo hivi na vile.

Kinachoshangaza zaidi ni kuwa wanalinganisha kanuni za maisha na vitu; kama vile viatu, kofia na gauni. Kwa vile vitu hivi hutafutwa na kuhitajika vinapokuwa vipya na kutupwa vinapochakaa, halikadhalika kwa mujibu wao, hali iwe hivyo hivyo kwa ukweli usiobadilika. Kwao, kizuri na kibaya havina maana zaidi ya kipya na cha zamani. Ukabaila ni mbaya kwa sababu tu ni mfumo wa zamani na umepitwa na wakati. Vinginevyo ulikuwa mzuri kabisa wakati unaanzishwa duniani kwa mara ya kwanza.

Halikadhalika unyonyaji wa wanawake ni mbaya tu kwa vile haupendwi na ulimwengu wa kisasa; vinginevyo hadi hivi majuzi, watu hawa hawa walikuwa hawampi mgao wa urithi. Walikuwa hawajaitambua haki yake ya kumiliki mali na walikuwa hawaheshimu ridhaa na maoni yake.

Kwa mujibu wa watu hawa, katika zama hizi, zikiwa ni zama za anga (kuruka na ndege n.k), kama ilivyokuwa tu haiwezekani kusafiri kwa punda na kuacha ndege, kuwasha kibatari na kuacha umeme, kushona nguo kwa mkono na kuandika kwa mkono huku ukiacha mashine kubwa za kisasa za kuchapishia, halikadhalika haiwezekani kuacha kwenda kwenye sherehe za muziki, sherehe ambazo watu wanavaa mavazi ya kuogelea, mialiko ya chakula cha usiku chenye nyama za kubanikwa, kutoshiriki katika vicheko vya ovyo, kutocheza karata, kutovaa visketi vifupu kwani vitu vyote hivi ni mitindo ya karne hii. Wanahofu kuwa wasiposhiriki katika mambo haya watarudi nyuma katika zama za kuendesha farasi.

Wanadai kuwa hizi ni zama za nyukilia, zama za sayansi, zama za miezi ya kubuni na zama za makombora ya masafa marefu. Hili ni jambo zuri! Sisi pia tunamshukuru Mungu kuwa tunaishi katika zama hizi na tunaomba kwamba tufurahie na kufaidika na sayansi na viwanda kwa kiwango cha juu kabisa. Lakini je, mambo yote haya yanasababishwa na sayansi tu? Je, hali zote za karne hii ni matokeo ya maendeleo ya kisasa ya sayansi? Je, sayansi inadai kuwa imedhibiti mambo yote hapa duniani?

Sayansi haijawahi kudai hivyo hata siku moja. Balaa la karne yetu ni kuwa kundi la wanasayansi kwa nia njema kabisa, huitumia sayansi kufanya ugunduzi mpya, lakini kundi jingine la wabinafsi na wenye uchu wa madaraka na wanaoabudu fedha huyatumia vibaya matunda ya jasho la wanasayansi ili kuyafikia malengo yao ya kiovu. Sayansi inalalamika kuwa inatumiwa vibaya na wanaadamu wakorofi na hii ndio bahati mbaya ya kizazi chetu.

Sayansi inasonga mbele katika fani za fizikia na inagundua sheria za mwanga na kuakisi na kundi la wakorofi na wabinafsi wanaitumia kutengenezea filamu za bluu (ngono) za uharibifu na uovu. Kemia inaendelea na kugundua tabia za vitu mbali mbali na michanganyiko yake.

Baadhi ya watu wanaamua kutumia ugunduzi huu kutengeneza madawa ya kulevya, heroin ambayo ni laana kwa wanaadamu. Sayansi iligundua chanzo kizuri cha nishati ndani ya atom, lakini kabla ya ugunduzi haujatumika kwa manufaa ya wanaadamu, wenye tamaa ya madaraka walifanya haraka kutengeneza bomu la atomiki, na kuwadondoshea watu wasio na hatia.

Mapokezi yalipoandaliwa, kwa ajili ya heshima ya Einstein, mwanasayansi mkubwa wa karne ya 20, yeye mwenyewe alipanda juu ya jukwaa na kusema, “Mnampa heshima mtu ambaye amechangia kwa namna fulani kutengenezwa kwa bomu la atomiki?”

Einsten mwenyewe hakutumia elimu yake kutengeneza bomu. Ni wengine waliotumia ugunduzi wake kwa lengo hili.

Matumizi ya heroin, mabomu ya atomiki na filamu za matusi (bluu) haviwezi kuhalalishwa eti kwa madai kuwa ni mambo ya karne hii.

Ikiwa ndege za kisasa kabisa za mabomu zinatumika kurushia mambomu bora kabisa kwa watu wa nchi nyingine, na watu walioelimika sana wanaajiriwa kufanya kazi hii, je, usasa huu unaweza kupuguza ushenzi wa kurithi wa tendo hili?