read

Uislamu Na Usasa – III

Hoja kuu ya wale ambao wanasema kuwa katika masuala ya haki za kifamilia tunapaswa kufuata mfumo wa Kimagharibi, ni kuwa muda umebadilika na mahitaji ya karne hii yanatutaka tufanye hivyo. Tunaonelea kuwa ni vizuri tuyaweke maoni yetu wazi juu ya nukta hii, kwa sababu bila kufanya hivyo, mjadala juu ya nukta yoyote hautakuwa kamili, ingawa kwa sababu ya uchache wa nafasi haiwezekani kulijadili suala hili kwa mitazamo yake yote, kifalsafa, kisheria, kijamii na kimaadili. Itatosheleza hapa kujadili nukta mbili tu.

Nukta ya kwanza ni kwamba kuafikiana kwayo na kukubaliana na mabadiliko ya wakati sio suala rahisi sana kama baadhi ya watu wasiojua wanavyofikiri. Mabadiliko yanayoletwa na wakati, wakati fulani huwa ni ya kurudisha maendeleo nyuma. Tunapaswa kwenda na mabadiliko ya wakati ya kimaendeleo na tunapaswa kuyapiga vita mabadiliko yanayoletwa na wakati ambayo ni ya kiharibifu. Ili kutofautisha aina hizi mbili za mabadiliko na kujua asili yake, tunapaswa kujua chanzo cha maendeleo (ugunduzi au mabadiliko) haya mapya na yameelekezwa katika mwelekeo gani. Tunapaswa kuangalia ni tabia gani za kibinadamu zimeyaleta (njema au mbaya) na ni matabaka gani ya watu yanatetea mambo haya mapya?

Tunapaswa kuangalia je yameletwa na tabia tukufu za mwanadamu au matamanio duni yanayofanana na wanyama, na kama yamekuja kama matokeo ya uchunguzi usio wa kibinafsi wa wanazuoni na wasomi, au yameletwa na matamanio duni ya wanaotumikia nafsi zao na tabia za kifisadi za jamii.

Mnyambuliko Wa Sheria Za Kiislamu

Nukta ya pili inayofaa kuwekwa wazi ni kuwa baadhi ya wasomi wa kiislamu wanaamini kuwa Uislamu una uwezo na sifa ambazo zinaupa uwezo wa kutumika zama zote. Kwa mujibu wa wasomi hawa, mafundisho ya Uislamu yanaafikiana na maendeleo ya wakati, kupanuka kwa utamaduni na matokeo ya mabadiliko haya.

Hebu tuangalie asili, sifa na uwezo huu ambao Uislamu unao. Kwa maneno mengine hebu tuangalie ni vifaa gani vimewekwa katika jengo hili la dini, na ikiwa vimeipa sifa ya kuafikiana na hali zote zinazobadilika, bila kuwa na haja ya kuacha baadhi ya mafundisho yake na bila mgogoro wowote kati ya mafundisho yake na hali yoyote inayojitokeza ya kupanuka kwa elimu na ustaarabu.

Ingawa suala hili lina sura ya kiufundi, ili kuondoa shaka shaka ya wale wanaotilia shaka ukweli huu kuwa Uislamu una sifa hii, tunalielezea kwa kifupi hapa.

Kwa undani zaidi juu ya suala hili, wasomaji wanaweza kusoma kitabu kiitwacho ‘Tanbihul Ummah’ cha hayati Ayatullah Naini au kitabu kingine kiitacho ‘Marjaiyyat Wal Imama’t cha mwanazuoni mkubwa wa zama hizi Allamah Tabatabai. Lakini vitabu vyote hivi vipo katika lugha ya kifursi.

Kuna nukta nyingi, ambazo zinaunda siri ya Uislamu kuwa na uwezo wa kuafikiana na kupanuka kwa elimu na ustaarabu, na uwezo wa kutumika kwa sheria zake thabiti na imara katika hali mbali mbali za maisha. Hapa tutataja baadhi yake.

Msisitizo Katika Roho Na Kutojali Sana Kiwiliwili.

Uislamu haujashughulikia maisha ya nje (kimwili) tu ambayo hutegemea kiwango cha maendeleo ya elimu ya mwanadamu. Mafundisho ya Uislamu hushughulikia roho pia na malengo ya maisha na hutoa njia bora kabisa ya kuyafikia malengo haya. Sayansi haijabadilisha roho na malengo ya maisha wala haijapendekeza njia yoyote nzuri zaidi, fupi zaidi na salama zaidi ya kuyafikia malengo haya. Imetoa tu njia bora zaidi na vifaa vya kukwamisha njia ya kuyafikia malengo haya.

Uislamu, kwa kuhifadhi malengo tu katika himaya yake na kuacha muundo na mbinu kwenye himaya ya sayansi na teknolojia, umeepuka migongano dhidi ya utamaduni na ustaarabu. Sio hivyo tu lakini pia kwa kuhimiza mambo yanayosaidia kupanuka kwa ustaarabu, yaani elimu, kazi, uchamungu, ridhaa, ujasiri na uvumilivu bila kukata tamaa, umejitolea kuwa kigezo kikuu cha kupanua ustaarabu.

Uislamu umeweka alama za barabarani katika njia yote ya maendeleo ya mwanadamu. Alama hizi kwa upande mmoja zinaonyesha njia na kituo cha mwisho na kwa upande wa pili zinaonyesha makorongo na sehemu za hatari. Sheria zote za Kiislamu ni alama za barabara, aidha za aina ya kwanza au ya pili.

Njia za maisha katika zama hutegemea juu ya kiwango cha elimu ya wanaadamu. Kwa kadri elimu ya watu inavyopanuka, ndivyo njia bora zaidi za kujipatia kipato zinavyotokea na moja kwa moja zinachukua nafasi ya zile njia duni (za zamani).

Mifumo ya nje na ya kimaada ya njia hizi (za kupatia riziki) haina utakatifu katika Uislamu, na Waislamu hawalazimiki kuzidumisha.

Uislamu haujasema kifaa hiki na kile kitumike kwa ushonaji, ususi, kilimo, usafiri, vita au kazi nyingine. Hivyo hapawezi kuwa mgogoro wowote kati ya sayansi na Uislamu, pindi kifaa kinapopitiwa na wakati, cha kisasa zaidi kinaweza kutumika badala yake. Uislamu haujaagiza kutumika kwa mtindo maalum ya viatu au nguo, wala haujapendekeza aina fulani ya ujenzi wa majengo. Halikadhalika hauhimizi juu ya mbinu fulani fulani za uzalishaji na ugavi.

Hii ni moja ya sifa hizo za Uislamu, ambazo zimeuwezesha kuweza kutumika katika maendeleo yote ya wakati.

Sheria Madhubuti Kwa Mahitaji Madhubuti

Na Sheria Zinazobadilika Kwa Mahitaji Yanayobadilika.

Sifa nyingine ya Uislamu, ambayo ina umuhimu mkubwa ni kuwa umeweka sheria madhubuti (zisizobadilika) kwa ajili ya mahitaji madhubuti (yasiyobadilika) na sheria zinazobadilika kwa mahitaji yanayobadilika. Mbali na mahitaji ya wanaadamu, mahitaji ya mtu mmoja mmoja na vikundi, yote yana asili ya kudumu. Hayabadiliki kwa mujibu wa wakati. Kanuni za mifumo inayotawala silika za binadamu na mahusiano ya kijamii hazibadiliki.

Tunazijua nadharia za ‘Maadili husianishi’ na ‘Uadilifu husianishi’ ambazo zina wafuasi wake, na tutatoa maoni yetu kuhusiana nao baadaye.

Sehemu nyingine ya mahitaji ya mwanadamu ni ile ya mahitaji yanayobadilika, na hii huhitaji sheria zinazobadilika. Uislamu ulishayaona mahitaji hayo na umeyaunganisha na kanuni fulani ambazo zina sheria ndogo zinazobadilika kila hali inapobadilika.

Kufafanua nukta hii hebu tuangalie mifano hii;

وَأَعِدُّوا لَهُمْ مَا اسْتَطَعْتُمْ

‘Andaeni majeshi kwa ajili yao (maadui)’ (Suratul Anfal 8:60.)

Wakati huo huo tunasoma hadith kadhaa za Mtume katika vitabu vya sheria za Kiislamu chini ya kichwa cha habari ‘Kuendesha farasi na kurusha mishale.’ Mtume aliwaelekeza Waislamu wajifunze kuendesha farasi na kurusha mishale na wawafundishe watoto wao pia. Haya yalikuwa ni sehemu ya mafunzo ya Kiislamu katika zama hizo.

Ni dhahiri kabisa hapa kuwa amri ya msingi ni ‘Kuandaa majeshi.’ Upinde na mshale, jambia na mkuki na farasi sio vya muhimu. Kilicho cha muhimu ni kuwa imara kijeshi dhidi ya maadui. Kuandaa majeshi ni amri ya kudumu ambayo imetokana na hitajio la kudumu.

Hata hivyo ulazima wa kupata ujuzi katika kuendesha farasi na kurusha mishale sio wa kudumu, na hubadilika kutokana na wakati. Kutokana na kubadilika kwa hali, ujuzi wa kufyatua risasi umechukua nafasi ya kurusha mishale.

Mfano mwingine ni sheria ya kijamii inayohusu kubadilishana mali, iliyotajwa katika Qur’ani. Uislamu umetambua kanuni ya umiliki wa mali wa mtu binafsi. Hata hivyo umiliki huu unaotambuliwa na Uislamu ni tofauti na ule uliopo katika nchi za kibepari. Tabia ya umiliki wa mali wa watu binafsi katika Uislamu ni kanuni ya kubadilishana.

Kwa utaratibu huu Uislamu umeweka sheria fulani. Mojawapo imeelezwa na Qur’ani Tukufu katika maneno haya

وَلَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُمْ بَيْنَكُمْ بِالْبَاطِلِ

‘Na msile mali zenu (kila mmoja kula za mwenzake) kwa batili’ (Suratul Baqarah, 2:188).

Kwa maneno mengine katika mauzo ya biashara, fedha isitoke mkono mmoja kwenda mwingine isipokuwa kwa kubadilishana na kitu kingine cha halali chenye kuwa na mamlaka ya mwisho juu ya mali hiyo.

Imelezwa na kufafanuliwa katika sheria ya Kiislamu mauzo na manunuzi ya vitu fulani yamekatazwa. Vitu hivyo ni pamoja na damu na kinyesi cha binadamu. Sababu ni kuwa vitu hivi havina thamani inayoviwezesha kuhesabika kuwa sehemu ya mali ya mwanadamu. Kanuni hii ni sawa ya mali ya mwanadamu. Kanuni hii ni sawa na ile iliyo katika Aya iliyonukuliwa hapo juu. Ubatili wa mauzo na manunuzi ya damu na kinyesi cha binaadamu ni sehemu au mfano tu wa matumizi ya kanuni hiyo. Hata kama hakuna ubadilishaji uliofanyika, (wa bidhaa au bidhaa kwa fedha) fedha au mali inayomilikiwa na mtu fulani haiwezi kufujwa au kuliwa bure.

Sheria inayokataza kula mali ya mtu mwingine bure (bila kufanya kazi) au kiwizi ni kanuni madhubuti na inatumika zama zote, na imetokana na hitajio la kudumu la jamii. Lakini kanuni kuwa damu na kinyesi cha binadamu havihesabiki kama mali na haviruhusiwi kuuzwa, inahuisiana na wakati na kiwango cha ustaarabu. Kanuni hii inaweza kubadilishwa kutokana na mabadiliko ya hali, maendeleo ya sayansi na viwanda na uwezekano wa kuzitumia bidhaa hizi katika namna sahihi na yenye manufaa.

Mfano mwingine; “Imam Ali (a.s) hakuwahi kuweka dawa kwenye nywele zake hata siku moja, ingawa zilikuwa zimekuwa za mvi katika miaka ya mwisho ya uhai wake. Siku moja mtu mmoja alimwambia, ‘Je Mtume hakuamrisha nywele za mvi ziwekwe dawa?”

Ali alijibu ‘Ndiyo aliamrisha’ Sasa kwa nini huweki dawa kwenye nywele zako? Yule mtu aliuliza. Ali akasema; “Katika wakati ule ambao Mtume alitoa maelekezo haya, idadi ya Waislamu ilikuwa ndogo na kulikuwa wazee wengi waliokuwa wakishiriki vitani. Mtume aliwaamrisha wazipake dawa ili kuficha umri wao halisi, kwani kama adui angeona kuwa anapambana na kundi la wazee tu, hamasa yake ingeongezeka. Kwa kuwa Uislamu umeenea dunia yote, hali imebadilika. Kila mtu yupo huru kupaka dawa nywele zake au kuacha.”

Kwa maoni ya Imamu Ali, maelekezo ya Mtume hayakuwa ya kudumu wala haikuwa sheria ya kudumu.
Uislamu unajali muonekano wa nje na roho ya ndani pia. Lakini unataka pumba kwa ajili ya punje yenyewe na unataka nguo kwa ajili ya mwili.

Suala La Kubadilisha Herufi

Katika siku za hivi karibuni hapa Iran kumekuwa na ubishani juu ya kubadlisha herufi. Suala hili linaweza kuangaliwa katika pande mbili kwa mtazamo wa kanuni za Kiislamu, na kwa sura mbili. Kwanza ni iwapo Uislamu unapendelea herufi fulani na kuzibagua nyingine. Je Uislamu unaziona herufi za sasa, ambazo ni za Kiarabu, kama zake, na herufi nyinginezo kama zile za kilatini zinazoonekana ni za kigeni? Uislamu ambao ni dini ya ulimwengu mzima unaziona herufi zote duniani kuwa ni sawa.

Sura ya pili ni kuwa kiasi gani kubadilika kwa herufi kutachanganya utamaduni wa Taifa la Kiislamu na watu wengine na kutakuwa na madhara gani kwa utamaduni wa taifa hili. Na zaidi ya hayo, katika karne 14 zilizopita, vitabu vya Kiislamu na kisayansi vilivyozalishwa na Irani vimeandikwa katika herufi za sasa (za kiarabu), je kubadilisha herufi si kutazifuta (haribu) kazi zote hizi? Swali jingine ni, ‘Ni akina nani wanaopendekeza mabadiliko haya, na ni akina nani watakaoyatekeleza? Maswali yote haya ni thabiti.’

Kuwategemea Wengine Ndio Kumekatazwa, Sio Kofia Ya Kizungu

Watu kama mimi mara nyingi wanakumbana na maswali, yanayoulizwa kwa dharau au kejeli. “Sheria ya Kiislamu inasemaje kuhusu kula ukiwa umesimama?’ Ni vipi kuhusu kula kwa kijiko au uma?’ Je kuvaa kofia ya kizungu kumekatazwa?’ Je kutumia lugha za kigeni kumekatazwa?’”

Katika kujibu maswali haya, tunasema kuwa Uislamu haujatoa maelekezo yoyote mahsusi juu ya hili. Uislamu haujawaelekeza wafuasi wake kula kwa mkono au kijiko. Ulichowaelekeza ni kuzingatia usafi. Uislamu haujaelekeza matumizi ya mitindo ya aina fulani ya viatu, kofia au nguo. Kwa mtazamo wa Uislamu lugha zote Kiingereza, Kijapani, Kifursi, zina hadhi sawa.

Hata hivyo, Uislamu unasema kitu fulani zaidi. Umesema kuwa imekatazwa mtu kupoteza utambulisho wake. Kuwaogopa wengine bila ulazima kumekatazwa, Kuwaiga wengine kumekatazwa, kuchekeshwa na kuvutiwa na wengine kama sungura anavyovutiwa na nyoka, kumekatazwa. Kumchukulia punda mgeni aliyekufa kuwa ni farasi kumekatazwa. Kuingiza nchini upotofu na ukosefu wa maadili kutoka nje, kwa madai ni mambo ya kisasa ya karne hii, kumekatazwa. Kuamini kuwa Waislamu wanapaswa kufuata mila na utamaduni wa Kimagharibi ndani na nje, kimwili na kiroho, kumekatazwa. Kwenda nchi ya Kimagharibi kwa siku chache na baada ya kurudi, unaanza kutamka maneno yetu kama wao (wazungu) kumekatazwa.

Muhimu Na Muhimu Zaidi.

Sura nyingine ya Uislamu inayoufanya uende na mahitaji ya wakati ni kukubaliana kwa mafundisho yake na akili/mantiki. Uislamu umetangaza kuwa sheria zake zimezingatia maslahi makubwa zaidi. Na wakati huo huo, Uislamu wenyewe umetoa madaraja mbali mbali ya umuhimu wa maslahi haya. Hii inarahisisha kazi ya wataalamu wa sheria za Kiislamu katika fani hizo ambapo maslahi tofauti yanaonekana kugongana.

Katika hali hizo, Uislamu umewaruhusu wataalamu wa sheria za Kiislamu kupima uzito wa maslahi tofauti, na kuzingatia mwongozo ambao Uislamu wenyewe umetoa, katika kuangalia ni maslahi gani hilo ni muhimu zaidi. Katika fani ya sheria za Kiislamu, hii huitwa suala la “muhimu na muhimu zaidi.” Kuna mifano mingi ambapo kanuni hii ya maslahi ya juu na ya juu zaidi imepata kutumika. Hata hivyo kwa sababu ya uchache wa nafasi, tunairuka sehemu hii

Sheria Yenye Haki Ya Turufu.

Sifa nyingine ya Uislamu ambayo imeipa dini hii uwezo wa kuhamishika na kutumika katika hali mbali mbali na imeifanya kuwa dini inayoishi na ya kudumu milele ni kuwa ndani yake kuna chombo cha sheria ambacho kazi yake ni kudhibiti na kurekebisha sheria nyingine. Mafakihi wanaziita kanuni hizi kuwa ni “ kanuni za kuongozea.”

Kanuni ya ‘Hakuna madhara’ na ‘Hakuna hasara’ kwamba sheria haitatumika pale ambapo inaweza kusababisha ugumu au madhara kwa maslahi ya mtu asiye na hatia, imeuenea (imeutawala) mfumo mzima wa kisheria. Lengo la kanuni hizi ni kudhibiti na kurekebisha sheria nyingine. Kwa kusema kweli Uislamu umezipa nguvu ya turufu kanuni hizi ambazo hubadilisha kanuni nyingine.

Madaraka Ya Mtawala

Kwa nyongeza kuna mfululizo mwingine wa kanuni za kuweka mambo katika mizania ambazo Mwenyezi Mungu ameipa dini hii ya mwisho. Ayatullah Na’ini na Allamah Tabatabai, juu ya hili, wametegemea madaraka ambayo Uislamu umeipa serikali ongofu ya Kiislamu.

Kanuni Ya Ijtihadi

Mshairi na mwanafalsafa wa Kipakistani anasema kuwa Ijtihadi (kuzalisha sheria kutoka vyanzo vyake vya asili) ni nguvu ya hamasa ya Uislamu. Yuko sawa kusema hivyo. Lakini kilicho muhimu zaidi ni kuwa Uislamu una sifa maalum ya kuruhusu Ijtihadi. Hakuna dini nyingine yenye sifa hii katika namna hii hii. Jengo la ndani la Uislamu limejengwa katika namna ambayo kwa msaada wa Ijtihadi, unaweza mara zote kwenda na mahitaji yanayobadilika katika maisha.

Abu Ali Ibn Sina (Avicenna) katika kitabu chake AlShifa, ameelezea haja ya Ijtihadi kuwa inatokana na kubadilika kila mara kwa mahitaji. Anasema kuwa hali za maisha mara zote zinabadilika. Matatizo mapya yanaibuka kila mara, lakini misingi ya Uislamu haibadiliki. Hivyo katika hali hii, lazima wawepo watu wanaojua sheria za kiislamu vizuri na mafundisho ya Kiislamu vizuri ili waweze kujibu maswali yote yanayoibuka katika kila zama na hivyo kukidhi mahitaji ya wakati.

Katiba ya Iran inaamuru kuwa pawepo chombo cha mujtahidi wasiopungua watano (wanazuoni wakubwa wa Theolojia wanaoweza kufanya ijtihadi) kitakachokuwa kikichunguza sheria zinazopitishwa na serikali kila wakati.

Lengo hapa ni kuwa watu hawa (mujtahidi) kwa vile sio wapinga mabadiliko wala hawapingi maendeleo ya kisasa, wala sio limbukeni wala hawawafuati wengine kibubusa, waangalie na kudhibiti mfumo wa sheria wa nchi.

Inapaswa kueleza kuwa ijtihad kwa namna halisi ina maana kubobea na inahitaji uelewa wa ndani sana wa misingi ya Uislamu na nguzo zake na elimu kubwa kabisa ya kanuni za fikihi ya Kiislamu, ambayo si kila mtu aliyesoma Uislamu kwa muda fulani anaweza kudai kuwa mujtahid.

Hapana shaka kuwa hii ni kazi ya umri mzima wa mtu ili kubobea katika kanuni na mafundisho ya Uislamu, na mbali na kipaji, nia na akili, inahitaji pia msaada wa Mungu.

Mbali na kubobea (kwenye mchepuo maalum) na Ijtihad, baadhi ya watu wanaweza kupata elimu na kufikia kiasi kwamba maoni yao yanaweza kuchukuliwa kuwa ni fatwa. Historia ya Uislamu inawataja watu hao ambao licha ya elimu yao kubwa na maadili yao ya hali ya juu walikuwa na hadhari kubwa, walipokuwa wakitoa maoni yao, juu ya masuala ya kisheria.