Table of Contents

(13). Bahlul Amsihi Abdulla Mubarak

Siku moja Abdulla Mubarak alimwendea Bahlul kwa kutaka nasiha. Alipomfikia Bahlul, alimkuta kichwa wazi na miguu wazi akisema Allah! Allah..... Alimwendea na kumtolea salaam na Bahlul alimjibu.

Baadaye Abdulla alisema: "Ewe Sheikh! Naomba unipatie nasiha na naomba unionyeshe njia itakayonionyesha vile niishi maisha yangu pasi na madhambi kwani mimi ni mtu mwenye madhambi ambayo nafsi yangu potofu imenighalibu.Hivyo nionyeshe njia hiyo mwokovu."

Bahlul alimwambia Abdullah: "Mimi mwenyewe nimehangaika mno, sasa wawezaje kunitegemea? Iwapo ningelikuwa mwenye akili, basi watu wasingaliniita mwehu na wewe watambua kuwa maneno ya mwehu hayana athari yoyote yakuweza kukubaliwa na watu. Kwa hivyo, nakuomba umtafute mtu ambaye ni mwenye akili ili akushauri vyema."

Abdullah akasema: "Ewe Sheikh mara nyingi wehu wanatokezea kusema mengi yenye busara."

Kwa hayo Bahlul alinyamaza. Hapo tena Abdullah akaanza kumwomba kwa kumbembeleza. "Ewe Sheikh, tafadhali sana usinivunje moyo kwani nimekuja kwa matumaini makubwa."

Bahlul alimjibu: "Ewe Abdullah! Tafadhali sana kwanza kabisa kubali sharti zangu nne ili usiyageukie maneno ya mwehu, ndipo hapo nitakupa nasiha zangu ambazo zitakuokoa.

Abdullah akasema: "Je masharti hayo manne ni yapi ili niweze kuyakubali."

Bahlul akasema: "Sharti la kwanza ni lile, iwapo utatenda dhambi lolote lile, na kupinga hukumu ya Allah, basi uache kula riziki itokayo kwa Allah."

Abdullah akamwambia: "Nisipokula riziki ya Allah, je nitakula riziki ya nani?

Bahlul akasema: "Wewe ukiwa mtu mwenye akili umedai kuwa unafanya ibada ya Allah na kula riziki yake Allah na pepo hapo unafanya maasi ya kutozitii amri zake. Tafadhali sana jaribu kuamua mwenyewe iwapo hii ndio haki ya ibada?"

Abdallah akasema: "Ewe Sheikh wewe umesema kweli na yaliyo sahihi na sharti la pili ni ipi?"

Bahlul akasema: Sharti la pili ni kwamba, unapotenda dhambi lolote, basi jitoe katika milki ya Allah."

Abdullah akasema: "Ama kusema ukweli sharti hili la pili ni gumu kuliko hata lile la kwanza, kwani kila mahala pana ardhi ya Allah na utawala wake, sasa nitakwenda wapi?"

Bahlul alimwambia: "Kwa kweli hili ni jambo baya mno kwani wewe unakula riziki yake na kuishi katika milki yake na papo hapo unakana kutii kwa amri yake. Fanya maamuzi yako wewe mwenyewe kuwa hiyo ndiyo sharti ya ibada?"

Hapo Abdullah aliuliza: "Je sharti la tatu ni lipi?"
Bahlul alijibu: "Sharti la tatu ni kwamba iwapo wewe wataka kutenda madhambi yoyote, basi uende ujifiche mahala pale ambapo Allah hataweza kukuona, wala kuona hali yako, na hapo ndipo utende vile upendavyo."

"Sharti hilo ni gumu zaidi!" alisema Abdullah, kwani Allah anafahamu na kuona kila kitu, yupo kila mahala. Chochote kile akitendacho mja, Allah hukiona na kukielewa."

Bahlul alisema: "Wewe mwenyewe u - mtu mwenye akili. Inakubidi wewe uelewe kuwa Allah yupo kila mahala na kumwona kila mtu. Hivyo ni jambo la kustaajabisha ni kule kutumia riziki yake kuishi katika milki yake na vitendo wazi katika utawala wake ambavyo yeye anakuona na kufahamu. Baada ya yote hivyo unadai kufanya ibada yake.

Abdullah alisema: "Kwa hakika umesema ukweli kabisa. Na sharti la nne ni lipi?"

Bahlul alimwambia: "Wakati utakapoijiwa na Malakul Maut (Malaika atoae roho) ili kuitoa roho yako, basi umzuie asifanye hivyo hadi hapo utakapokuwa umekwisha agana na ndugu na rafiki zako wote na kuweza kutenda matendo mema ambayo yatakusaidia hapo baadaye."

Abdullah alijibu: "Lo! Sharti hili ni gumu zaidi kuliko masharti yote. Huyo Malakul Mauti hatanipa hata fursa ya kupumua!"

Hapo ndipo Bahlul alipomjibu: "Ewe mtu mwerevu! Wewe watambua vyema kabisa kuwa mauti hayana hila yoyote, na hauwezi kamwe kujitenga nayo na hautapatiwa muhula wowote ule. Na inawezekana pia ikatokea mauti katikati mwa hali ya madhambi na hautapata hata muhula wa kupumua kama vile Allah (s.w.t.) alivyosema.

Kwa hiyo ewe Abdullah! Pokea nasiha hata kwa mwehu na uamke kutoka usingizi wako!"

Jihadhari na ghururi na ulevi wako na uwazie akhera kwani safari yako ndefu ipo mbele yako na umri wako upo mdogo kabisa. Kazi ya leo usiiweke kesho kwani kesho hiyo labda hautaiona. Muda huu uliopo uthamini. Kazi za Aakhera usizicheleweshe kwani usichokitenda leo utakijutia hapo kesho na kujuta kwako hakutakufaidisha."

Abdullah alipoyasikia hayo alianza kuwaza huku akiwa amekiinamisha kichwa chake.

Mara Bahlul alianza kusema: "Ewe Abdullah! Wewe umenitaka nikusihi ili uweze kufaidika nayo kesho, sasa baada ya kuyasikia hayo mbona wainamisha kichwa chini?"

Siku ya Qiyama, katika uwanja wa Hisabu na Kitabu, utawajibu nini Malaika watakao kuhoji. Yeyote yule atakayekuwa na hisabu yake safi humu duniani, hatakuwa na khofu yoyote ile hapo Aakhera!

Hatimaye,Abdullah alikiinua kichwa chake na kusema: "Ewe Sheikh! Mimi nimeyasikia yote uliyoyazungumza. kwa moyo wangu wote na nimelikubali hili sharti la nne pia, naomba unisihi zaidi na kunifanya niwe mmoja wenu.

Bahlul alisema: "Ewe Abdullah! Mwanadamu afanyalo lolote inambidi aweke mbele maamrisho yake Allah s.w.t. na hata katika hali ya kusema au kusikiliza, kwani kwa kila hali yu mwumba wa Allah s.w.t."

Bahlul alikuwa ni mtu ameelimika kwa Imam Jaafer as-Sadiq a.s.