Table of Contents

(14). Bahlul Amsihi Harun.

Harun Rashid alikuwa akipita njia moja na alimkuta Bahlul akicheza mbio na watoto, hapo alimpigia sauti ya kumwita.

Bahlul alipofika alisema: "Je una kazi gani?"
Harun alimwambia, "Nataka nasiha zako!"

Hapo Bahlul alimwambia: "Tazama kwa makini mno majumba ya Wafalme yaliyokuwa ya fahari na sasa yalivyo na vile vile makaburi yao. Hayo pia yanatosha kukutanabahisha. Wewe waelewa vyema kabisa vile wafalme hao walivyokuwa wakiishi katika majumba hayo kwa starehe na fakhari na kiburi chao, lakini leo walipo (makaburini mwao) hawana la kufanya ila wao wanajuta kwa yale waliyoyafanya wakiwa na uwezo. Uelewe vyema kabisa kuwa nasi pia karibuni tutaungana nao." (tutakufa).

Kwa hayo, Harun alitetemeka, na hakusita kuuliza: "Sasa, je nifanyeje ili mola aniwie radhi?"

Bahlul alimjibu, "Watendee matendo mema viumbe vya Mwenyezi Mungu kwa hayo utaweza kupata radhi yake Mwenyezi Mungu."
Harun aliuliza, "Je ni kama matendo gani?"

Bahlul alimjibu: "Utawale kwa haki na uadilifu. Chochote kile ukionacho kibaya kwako ndivyo hivyo hivyo kiwe kwa ajili ya wengineo. Kilio cha aliyedhulumiwa na maombi yake uyasikilize vyema na kuyajibu kwa utukufu na uyafanyie uchunguzi kwa makini na utoe maamuzi na hukumu zako kwa haki na uadilifu."

Harun alisema: "Hongera ewe Bahlul! Kwa hakika umenipatia nasiha nzuri mno. Mimi natoa hukumu kuwa deni zako zote zilipwe."

Bahlul alimjibu: "Deni haliwezi kamwe kulipa deni. Chochote kile ulichonacho wewe ni mali ya Umma,uwarejeshee mali yao. Usinifanyie hisani kwa mali iliyodhulumiwa."
Harun alimwambia: "Fanya ombi lako lingine."

Bahlul alimjibu: "Ombi langu ni kuwa wewe ujaribu kutimiza nasiha zangu, lakini nasikitika mno kuona kuwa roho na nafsi yako imeshakuwa ngumu kutokana na tamaa na starehe za dunia na hivyo nasiha zangu hazitakuathiri chochote."

Kwa hayo, Bahlul akipeperusha kifimbo chake na kusema: "Sogea, kwani farasi wangu hupiga teke pia." Kwa maneno hayo, alijiondokea na safari yake.