Table of Contents

(23). Bahlul Na Mwizi

Bahlul alikuwa akiishi katika nyumba iliyokuwa tupu. Mbele ya nyumba yake kulikuwa na duka la mshona viatu ambaye dirisha lake lilikuwa likifunguka mbele ya nyumba ya Bahlul alikusanya fedha kidogo na akazifukia ardhini na kila alipokuwa akipata dharura, alikuwa akifukua kiasi alichokuwa akikitaka na kufukia kiasi kilichobakia. Siku moja alipopata dharura ya fedha, alikwenda kufukua, na akakuta hakuna chochote shimoni, na hapo aling'amua kuwa fedha hizo zimeibiwa na mshona viatu tu kwani dirisha lake lilikuwa likifungukia mbele yake.

Basi yeye bila ya kuonyesha dalili zozote zile alikwenda dukani mwa mshona viatu na akaketi kimya, na alianza mazungumzo ya kila aina hadi mshona viatu akafurahi na kuvutiwa. Hapo ndipo Bahlul aliposema: "Ewe rafiki mpenzi! Hebu naomba unijumlishie hesabu yangu!"

Mshona viatu akasema: "Haya anza nami nitakujumlishia."
Bahlul alianza kutaja majumba mengi na pamoja na kila jumba alikuwa akiisemea na fedha.

Hadi kutaja na nyumba anamoishi kuwa ameficha kiasi fulani cha fedha. Mwishowe, mshona viatu akamwambia kuwa jumla ya sarafu alizozitaja ni dinar elfu mbili.

Bahlul akawaza kwa kitambo, na akaanza kusema: "Ewe rafiki mpenzi! Mimi na kuomba ushauri mmoja."

Mshona viatu akasema: "Ndiyo sema tu!"
"Mimi nafikiri kuwa dinar hizo elfu mbili nizilete hapo kwangu na kuzifukia shimoni."

Mshona viatu alimjibu "Loh! wazo zuri kabisa. Ndiyo, kusanya fedha zako zote kutoka kote ulikoficha na uzifukie hapo unapoishi."

"Kwa hakika mimi nasakiki maneno yako tu! Na nakwenda kuzichukua fedha zote zilipo ili nizifukie humu mwangu! "Alimjibu Bahlul. Baada ya kusema hayo Bahlul aliondoka.

Baada ya kuondoka kwake, yule mshona viatu akawaza kuwa itakuwa vyema iwapo hizo fedha kidogo alizoziiba akazirudishe mahala pake ili atakaporudi Bahlul kufukia zingine azikute zipo na hivyo asiingiwe na shaka ya kuibiwa. Hivyo ataweza kupata fedha zaidi kwa mara moja. Hivyo yeye alikwenda kurudisha zote alizokuwa ameziiba.

Baada ya masaa machache, Bahlul alirudi nyumbani mwake na akazikuta zile fedha zake zilizokuwa zimeibiwa na mshona viatu. Basi alizifukua zote na kumshukuru Mwenyezi Mungu, na aliacha nyumba hiyo akahamia mahali pengine. Mshona viatu alikuwa akimsubiri kwa hamu lakini hakuweza kumwona tena. Na baada ya kupita kipindi fulani, hivyo aliweza kung'amua kuwa Bahlul alimdanganya kwa hayo ili aweze kuzirudisha fedha zake!.