Table of Contents

(27). Ubora Na Sifa Za Imam Ali A.S.

Siku moja Bahlul alimtembelea Harun Rashid, aliyekuwa ametulia kwake. Alimwuliza Bahlul: "Je ni ali a.s. yu bora kuliko Abbass, mjomba wake mtume s.a.w.w. au je Abbass ni bora kuliko Ali?"

Bahlul alimjibu: "Iwapo utanihakikishia usalama wa maisha yangu ndiyo nitakaposema yaliyo ya kweli."

Harun alijibu: "Ndiyo unayo amani."
Bahlul alisema: "Baada ya Mtume s.a.w.w. Ali a.s. alikuwa ni mbora kuliko Waislamu wote, kwani Ali a.s. alikuwa ni shakhsiya ambayo ilikuwanayo sifa za kila aina. Imani yake madhubuti ya Islam haina swali. Ushujaa wake katika vita vya kuinusuru Islam haina mfano. Yeye hakujitolea mhanga pekee yake katika kuinusuru Islam bali hata ukoo wake mzima ulijitolea mhanga. Katika vita vyote vya Kiislam vya kujihami, yeye daima amekuwa mstari wa mbele na kamwe hakuupa mgongo au kukimbia kwa kuwacha uwanja wa vita. Na wakati Ali a.s. alipoulizwa: "Je kwa nini hautazami nyuma wakati wa mapambano kwani unaweza kushambuliwa na maadui kwa nyuma?"

Ali a.s. aliwajibu: "Kupigana kwangu ni kwa ajili ya vita vya Allah s.w.t. Huwa sina woga wa aina yoyote na wala tamaa yoyote, kwani hujitolea kikamilifu kwa ajili yake Allah s.w.t. Iwapo nitauawa basi itakuwa ni kwa amri yake allah s.w.t. na katika njia yake. Je kutakuwa na upendo mwingine wowote zaidi ya kuuawa katika njia ya allah s.w.t.? ama kama nitauawa hivyo basi mtu ataajiliwa kukaa pamoja na wale watenda haqi!"

Zaidi ya hayo, wakati Ali a.s. alipokuwa Khalifa wa Waislamu yeye kamwe hakupumzika kwani alikuwa akishughulika usiku na mchana.

Yeye kamwe hakukubali mbadhirifu au utumiaji ovyo wa dola ya Umma na kamwe haqi za waombaji na masikini hazikupuuzwa au kusahauliwa.

Siku moja Aqil, ndugu yake, alimjia akiomba apatiwe mali kutoka hazina ya Umma lakini aliaibika kuomba hivyo kwani alimkuta Khalifa alivyokuwa akiishi, pamoja na hayo Imam Ali a.s. alimkatalia katakata.

Yeye daima alikuwa Khalifa aliyeongoza kwa haki na uadilifu na kamwe hakuwateua magavana ambao walikuwa wadhalimu na wala hakuwavumilia. Mfano Ibn Abbas, wakati alipokuwa Gavana wa Basra, alitumia wakati mmoja kiasi cha fedha kutoka hazina ya Umma, Ali a.s. alimtaka arejeshe haraka sana na alimkanya vikali mno.

Vile vile alimpatia tarehe ya kurejesha hizo fedha, lakini Ibn Abbas alishindwa kurejesha, hivyo Ali a.s. alimwamrisha afike kufa badala yake alikwenda Makka ili aweze kupata amani, kwani alitambua wazi wazi kuwa Ali a.s. alikuwa ni mtu afuataye sheria na kanuni kwani yu mtu mwenye msimamo thabiti.

Harun Rashid alipoyasikia hayo, alishikwa na aibu na hivyo akataka kumwulimiza roho Bahlul, aliuliza swali: "Je pamoja na kuwa na sifa zote hizo bora, kwanini aliuawa?"

Bahlul alimjibu:
"Wengi wa wale walio juu ya njia ya haki wamekuwa wakiuawa. Hata Mitume ya Allah s.w.t. pia imekuwa wakiuawa katika zama zao."