Table of Contents

(32). Swali Juu Ya Amin Na Ma'amun.

Siku moja bahlul alikuwa akienda kwa Harun na wakakutana njiani. Harun akamwambi: "Je wakwenda wapi?"

Bahlul akamjibu: "Kwako wewe!"
Harun akamwambia: "Mimi nakwenda shuleni kujua hali ya Amin na Ma'amun na maendeleo yao. Hivyo iwapo utapenda kuandamana nami, basi tufuatane pamoja."

Bahlul alikubali na hivyo walifika shuleni lakini wakakuta watoto hao wawili wametoka nje kidogo.

Harun alimwuliza mwalimu hali na tabia za watoto wawili hao.
Mwalimu alimjibu: "Amin ni mtoto wa kiongozi wa akina mama na Kiarabu, lakini ni mpumbavu na mwenye akili na fahamu ndogo, na kinyume chake ni Ma'amun ambaye ni hodari mwenye akili na mwerevu!

Harun alitamka: "Mimi si yaamini hayo!"
Mwalimu akachukua karatasi akaiweka chini ya zulia alipokuwa akikalia Ma'amun na akaliweka tufali chini ya zulia alilokuwa akilikalia amin. Baada ya muda mdogo tu, wote wawili walirejea darasani. Walipomwona tu baba yao, wote wawili walitoa heshima zao, na wakaketi nafasini kwao.

Ma'amun alipoketi, hakutulia, aliitazama dari na alitazama kushoto na kulia. Hapo mwalimu alimwuliza: "Ewe Ma'amun mbona unakodoa macho huku na huko? Je umekuwaje?"

Ma'amun alimjibu: "Baada ya kutoka darasani na kurejea nahisi kuwa hii ardhi imeinuka kiasi cha unene wa karatasi moja au dari la darasa limeteremka chini kiasi hicho. Yaani kwa kifupi, Zulia langu limeinuka kwa kiasi cha karatasi moja."

Papo hapo mwalimu alimwuliza Amin: "Je na wewe wahisi hivyo?"
Amin alimjibu: "La! Mimi sihisi chochote kile, nipo sawasawa."
Kwa kuyasikia hayo mwalimu alicheka na akawaambia watoke nje ya darasa na akamwambia Harun alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa maneno yake kuthibitika kweli mbele yake.

Hapo Khalifa alimwuliza: "Je nini sababu ya tofauti hizo?"
Bahlul akasema: "Ewe Khalifa! Iwapo utanipa ahadi ya amani na kusalimika kwangu kutokana na wewe mimi nitaweza kukujibu sababu zenyewe."

"Unayo amani na utasalimika, haya elezea yale uyajuayo kuhusu swala hili." Allimjibu Harun.

Hapo ndipo Bahlul alipoanza kuelezea kwa kinaganaga: "Uhodari na uwerevu wa watoto unatokana na sababu mbili - kwanza, wakati mwanamme na mwanamke wanapokutana kimwili pamoja na taratibu njema basi watoto wazaliwao huwa werevu, hodari na wakakamavu. Sababu ya pili, mwanamme na mwanamke wanapotokana na damu na ukoo tofauti basi watoto wao huwa wenye akili, werevu na wenye nguvu. Na vivyo hivyo ndivyo ilivyo katika mimea na wanyama, na hayo yameshakwisha kuthibitishwa, kwa mfano, iwapo kutapandikizwa tawi la tunda aina moja katika aina ya tunda lingine la jinsi hiyo hiyo, basi tunda jipya litakuwa tamu na lenye ladha nzuri kuliko tunda la mti wenyewe. Na iwapo kutakutanishwa kimwili kwa farasi na punda, basi kutazaliwa nyumbu ambaye atakuwa hodari na mwenye nguvu, mwepesi kuliko hao wazazi wake.

Kwa kifupi, kasoro aliyo nayo Amin katika kufikiri na fahamu ni kwa sababu ya Khalifa na Zubeidah wanatokana na damu na ukoo mmoja ambapo Ma'amun anaonekana mwerevu, hodari na mwenye akili ni kwa sababu mama yake mzazi ametokana na ukoo na damu tofauti na ile ya Khalifa, na tofauti yake ni kubwa!"

Khalifa kwa majibu hayo alicheka na kusema: "Mwehu atasema hayo hayo na wala hawezi kutegemewa kusema kingine cha akili." Lakini mwalimu aliyasadikisha maneno ya Bahlul moyoni mwake.