Table of Contents

(34). Bahlul Na Sheikh Junaid

Siku moja Sheikh Junaid Baghdadi alitoka nje ya mji wa Baghdad ili kutembea na kutazama mandhari nzuri. Kwa kuwa alikuwa ni Sheikh hodari na maarufu, alifuatwa na wafuasi wake. Sheikh aliwauliza hali ya Bahlul, wao wakamjibu." Yeye ni mtu mwenda wazimu, je unayo kazi gani naye?"

Sheikh aliwajibu: "Niitieni kwani ninayo kazi naye."
Basi watu walitoka kumtafuta Bahlul, walimkuta upweke. Sheikh alifika mbele ya Bahlul.

Sheikh alipomwendea na kumkaribia Bahlul, alikuta ameweka tufali chini ya kichwa akiwa katika hali ya kuwaza. Sheikh alimtolea salaam naye akajibu na akauliza: "Je wewe ni nani?"

Sheikh alimjibu: "Mimi ni Junaid Baghdad."
Bahlul alimwuliza: "Si wewe ndiye Abul Qasini?"
"Naam!" akajibiwa.
Bahlul akamwambia: "Je ni wewe mwenyewe Sheikh Baghdad ambaye unawafunza watu ilimu ya kiroho?"

Sheikh akajibu: "Naam!"
Bahlul akamwuliza: Je wewe wajua namna ya kula chakula chako?"

Sheikh alimjibu: "Mimi husema Bismillah, na hula kile kilicho mbele yangu, huchukua matonge madogo madogo na huweka upande wa mdomo wangu, hutafuna pole pole, huwa sitazami matonge ya wengine. Wakati wa kula huwa ninamkumbuka Mwenyezi Mungu na kila tonge nilalo husema Alhamdulillah na hunawa mikono kabla na baada ya kula."

Kwa kusikia hayo, Bahlul aliinuka aksimama na kwa kukasirika alisema: "Loh! Wewe wataka kuwaongoza viumbe ambapo hadi sasa hata haujui vile ule chakula chako" akasema hayo na akajiondokea.

Wafuasi wa Sheikh wakasema: "Ewe Sheikh! Huyu mtu ni mwehu!"

Sheikh akawajibu: "huyu ni mwendawazimu lakini yupo hofari katika kazi zake. Inatubidi tumsikilize kwa makini kwani huwa anasema maneno sahihi." Naye akaondoka kumfuata Bahlul, akisema "Ninayo kazi naye."

Bahlul alipotokezea katika upweke, aliketi. Sheikh alimwendea. Bahlul aliuliza: "Je wewe ni nani?"

Sheikh alijibu:
"Sheikh Baghdad ambaye hajui hata kula chakula."

Bahlul alimwambia:
"Iwapo wewe hujui kula chakula,basi je unajua namna ya kuzungumza?"

Sheikh alimjibu: "Naam!"
Bahlul alimwuliza: "Je unazungumzaje?"
Yeye alimjibu:"Huwa ninazungumza kwa sauti ya chini, wala sizungumzi pasipo hitajika na wala sizungumzi kupita kiasi. Huzungumza kiasi cha uwezo wa wasikilizaji kunielewa."

Huwalingania watu dini ya allah s.w.t. na Mtume s.a.w.w. Huwa sizungumzi kiasi cha kuchukiwa na wasikilizaji. Huwa mwangalifu ya yale yaliyo dhahiri na bitini." Kwa kifupi, alielezea taratibu zote zihusianazo na mazungumzo.

Bahlul alisema: "Loh! Acha kula usivyojua, hata kuzungumza pia haujui?" Na mara hii tena akaondoka zake baada ya kuyasema hayo.

Wafuasi wa Sheikh walisema: "Ewe Sheikh, je umeona kuwa huyu ni mwenda wazimu tu, sasa waweza kutegemea nini kutoka kwa mwendawazimu huyu?"

Sheikh Junaid akawaambia "Nina kazi naye. Nyinyi hamuwezi kujua."

Tena alimfuata Bahlul, naye akamwuliza: "Mbona unapenda kunifuata niendako, je unanitakia nini? Wewe hujui namna ya kula chakula na wala namna ya kuzungumza, sasa jee wajua namna ya kulala?

Naye akamjibu: "Naam"
Bahlul akamwuliza: "Je ualalaje?"
Sheikh alimjibu: "Baada ya sala ya Isha' na kumaliza shghuli zangu, huanza kuvaa mavazi yaliyotoharika." Alielezea taratibu na desturi zote azijuazo za kulala.

Hapo Bahlul akamwambia: "Mimi nimeshaelewa kuwa wewe hata desturi ya kulala pia haujui."

Na Bahlul alipotaka kuondoka tu, Junaid alimshika na kumwambia: "Ewe Bahlul! Mimi hayo masuala matatu siyajui, naomba kwa jina la Mwenyezi Mungu unifundishe!"

Bahlul alimwambia: "Mimi nimekuwa nikijitenga nawe kwa sababu wewe ulidai kuwa unajua vyote. Lakini kwa kuwa umekiri mwenyewe kuwa haujui, basi sikiliza "haya yote uliyoyazungumza wewe ni maswala ya matawi tu kwani misingi ni kuwa kila tonge lako liwe tonge halali kwani iwapo utatekeleza desturi zote za kula ambapo tonge lenyewe ni haramu basi hakutakufaidia chochote bali kutaongezea kiza moyoni mwako."

Junaid akasema: "Mwenyezi Mungu akujalie malipo mema!" Akaendelea Bahlul: "Katika kuzungumza, kwanza kabisa moyo na nia zinatakiwa ziwe safi na mazungumzo yenyewe yanatakiwa yawe ka ajili ya furaha za Allah s.w.t. Iwapo utazungumza ufidhuli au upuuzi basi kutakuletea madhara tu kwa hivyo, ukimya utakuwa wenye manufaa. Vile vile ulivyozungumzia desturi za kulala pia ni matawi tu."

"Misingi yake ni kuwa unapojitarisha kulala, ni lazima moyo wako usiwe na bughudha, kisasi na husuda dhidi ya Waislamu. Usiwe na tamaa ya mali ya dunia, na unapotaka kulala umkumbuke Allah s.w.t."

Junaid aliubusu mkono wa Bahlul na akamwombea dua njema. Wafuasi walikuwepo hapo wakidhani Bahlul yu mwenda wazimu, walishangaa kuona busara zake.

Kwa hivyo, imetufundisha kuwa iwapo usipojua kitu usiwe na aibu ya kuulizia vile Sheikh Junaid alivyojifunza kwa Bahlul.