Table of Contents

(35). Bahlul Na Qadhi

Mtu mmoja alinuia kwenda Hijja msimu huo. Kwa kuwa alikuwa na watoto wadogo wadogo, hivyo alichukua Ashrafi elfu moja akaziweka kwa Qadhi kama amana katika ofisi ya serikali, na akasema: "Iwapo nitakufa huko huko, basi fedha hizi utazisimamia wewe na utakuwa na uwezo wa kuwapatia kiasi chochote utakacho familia yangu amana yangu!

Baada ya kutoka Ofisini mwa Qadhi, aliondoka kwenda Hijja. Alifariki bado akiwa safarini. Watoto wake walipokua na kupata fahamu, walimwendea Qadhi kudai amana ya baba yao. Naye Qadhi akawajibu: "Kwa mujibu wa wasiya wa baba yao aliyoitoa mbele ya watu, mimi ninao uwezo wa kuwapa kiasi nikitakacho mimi. Kwa hivyo nitawapa Ashrafi mia moja tu!"

Watoto hao walianza kuleta vurugu. Hivyo Qadhi aliwaita wale wote waliokuwako wakati akipokea Ashrafi na kuwauliza: "Je mlikuwapo siku ile ambapo baba watoto hawa aliponiachia amana ya Ashrafi elfu moja na kuniambia kuwa niwape tu kiasi nitakacho mimi."

Wale wote waliitikia kuwa hayo ndivyo yalivyokuwa.
Kwa hivyo Qadhi alisema: "Basi mimi sintawapeni zaidi ya Dinar mia moja."

Wale watoto walijuta mno na walianza kuwaambia watu lakini hakuna mtu aliyeweza kupata ufumbuzi kwani lilikuwa swala la sharia. Pole pole na Bahlul akaja akapata habari. Akawachukua wale watoto hadi kwa Qadhi, na kumwambia: "Je kwanini hauwapatii haki yao mayatima hawa?"

Qadhi akamjibu: "Ulikuwa ni wasia wa baba yao kuwa niwape kiasi nitakacho mimi, hivyo sitawapa zaidi ya dinar mia moja."

Hapo Bahlul alimnasa Qadhi na akamwambia: "Ewe Qadhi! Wewe unataka Dinar mia tisa na kwa mujibu wa kauli yako, marehemu alikwambia uwape watoto wake kile kiasi utakacho wewe, na hivyo ni Dinar mia tisa ndizo uwape hawa!"

Qadhi alishindwa mbinu za kuwababaisha wale watoto na hivyo alilazimika kuwapa wale mayatima Dinar mia tisa.