Table of Contents

(4). Bahlul Amshauri Harun:

Siku moja Bahlul alimtembelea Harun al-Rashid, na aliombwa atoe nasiha.

Hapo Bahlul alianza:
"Ewe Harun! Iwapo wewe utakuwapo porini ukashikwa na kiu ya maji ambayo hayapatikani, huku ukikaribia kufa. Je utalipa kiasi gani kwa kiasi cha kikombe kimoja cha maji?"

"Sarafu za dhahabu (Dinar)!" alijibu Harun.

"Iwapo mwenye maji asiporidhia sarafu hizo, je utampa nini badala yake?" aliendelea kusema Bahlul.

"Nitampatia nusu ya dola yangu" alikatiza Harun kwa haraka.

"Naam, baada ya kumalizia kiu chako, ukashindwa kupata mkojo (ukaziba) nawe usiweze kujitibu, je utampa nini yule atakaye kutibu huo ugonjwa?" Alisema Bahlul.

"Nitampatia sehemu ya nusu ya dola yangu iliyobakia"Harun akanena katika hali ya bumbuwazi.

Basi hapo kwa kupumua, Bahlul alisema: "Ewe Harun! Usijivunie Ukhalifa wako ambao unajua uthamini wake ni sawa na kikombe cha maji na uponyaji wa ugonwa wako. Hivyo, ni kheri yako iwapo utawatendea watu wako kwa upole na haki!"