Table of Contents

(40). Bahlul Na Mwenye Nyumba

Siku moja Bahlul alikwenda Basara, na kwa kuwa kule hakuwa na mwenyeji hivyo aliweza kukodi chumba kimoja kwa siku kadhaa. Chumba hicho kilikuwa kikuu mno na kulipokuwa kukivuma upepo basi kulikuwapo na sauti.

Bahlul alimwendea mwenye nyumba, akamwambia: "Ewe bwana! Wewe umenipa chumba ambacho kinapovumiwa na upepo basi kuta na dari zake zinaanza kupiga sauti ambazo zinatishia maisha yangu kwani yapo hatarini."

Bwana nyumba alikuwa mcheshi alianza kusema katika kumjibu: "Hapana jambo lolote lililo baya. Wewe watambua vyema kabisa kuwa vitu vyote vinamtukuza Mola na Kumsifu na hivyo ndivyo chumba chako kinavyofanya."

Bahlul alimwambia: "Hayo ni kweli kabisa kwani kila kitu kinamtukuza Mola na hatimaye huangukia kusujudu pi, hivyo mimi nahofu kule kusujudu kwa chumba chako, hivyo itanibidi nihame haraka iwezekanavyo!" (Kusujudu akimaanishi kubomoka).