Table of Contents

(41). Khalifa Na Ulevi

Siku moja Bahlul alikwenda kwa Harun na akamkuta Khalifa akiwa katika hali ya kuleva vileo, kwa kuona hayo, Khalifa alitaka kuficha aibu yake isije ikatobolewa nje. Kwa hivyo, alianza kumwuliza Bahlul maswali: "Je kula zabibu ni haraam?"

Bahlul alimjibu: La, si haram."
Khalifa akauliza: "Baada ya kula zabibu, je mtu akinywa maji hukumu yake inakuwa vipi?"

Bahlul alimjibu: "Hakuna kitu!"
Khalifa aliuliza tena: "Iwapo baada ya kula zabibu na kunywa maji, mtu akakaa juani kwa kitambo, je hukumu yake nini?"

Bahlul akamjibu: "Hapo pia hapana kitu."
Hapo Khalifa akanena: "Iwapo Zabibu na maji yakiwekwa juani kwa kitambo, basi itakuwaje haramu?

Basi Bahlul naye pia alimjibu vivyo hivyo: "Iwapo utamwekea udongo kidogo juu ya kichwa cha mtu, jee itamdhuru?

Khalifa alimjibu: "La! Haitamdhuru."
Bahlul aliuliza tena: Iwapo udongo huo huo ukachanganywa na maji, likatengenezwa tofali na hilo tofali akapigwa nalo, je litamdhuru?"

Hapo Khalifa akajibu: "Bila shaka tofali litavunja kichwa chake."

Bahlul alimjibu: "Iwapo udongo ukichanganywa na maji unaweza kuvunja kichwa cha mtu na kuweza kumdhuru ndivyo vivyo hivyo zabibu na maji ikichanganywa itatengeneza kitu tofauti ambacho kimeharamishwa na sheria za Islam na kusema kuwa si toharifu. Kwa kunywa kinywaji hicho kinamletea mnywaji madhara mengi mno na hustahiki adhabu kali mno katika Islam."

Khalifa alistajabishwa mno kwa ufasaha wa Bahlul katika majina yake na papo hapo aliamrisha pombe zote ziondolewe pale.