Table of Contents

(44). Kumwelimisha Punda?

Mtawala wa Kufa aliletewa Punda mmoja mzuri sana kama zawadi. Watu waliokuwapo katika Baraza walianza kumsifu huyo punda, mara mmoja miongoni mwa waliokuwepo, alisema: "Ehee! Mimi nitamuelimisha Punda huyu, hivyo nipo tayari kuwa mwalimu wake."

Mtawala alipoyasikia hayo, alisema kwa furaha: "Maneno hayo aliyoyasema lazima uyatimize na hivyo ukifanikiwa nitakuzawadia utajiri mkubwa na lau utashindwa, basi nitatoa amri ya kuuawa."

Huyo mtu alijutia mzaha wake . Pasi na lingine la kusema au kufanya, aliomba apatiwe kipindi fulani ili aweze kutekeleza hayo. Mtawala alimpa siku kumi tu.

Mtu huyo alimchukua yule Punda akamleta nyumbani mwake. Kwa kweli alikuwa amezongwa na mawazo na kutaabika mno kwani alikuwa haelewi ni lipi la kufanya. Hatimaye alimwacha Punda nyumbani na yeye akaondoka kwenda sokoni. Hapo njiani alikutana na Bahlul na kwa kuwa alikuwa akimjua Bahlul busara zake, hivyo hakusita kumuomba msaada wake katika swala mushkeli kama hilo.

Bahlul alimwambia: "Ndiyo, naam! Mimi ninayo mbinu humo. Utafanikiwa iwapo utatekeleza vile nikuambiavyo."

Bahlul alimwambia: "Usimpe chakula chochote kwa siku nzima. Chukua kitabu kimoja uweke ndani mwake uwele kidogo, na hivyo ndivyo umlishe huyo Punda, kwani atakuwa akila kutoka kitabuni. Na hivyo utekeleze kwa siku zote. Na ikifika siku ya kumi, usimpe chochote, abakie na njaa kali. Hapo ndipo umlete mbele ya mtawala na mbele ya watu wote ukiweke kitabu hicho mbele ya punda bila chalula chochote ndani yake."

Huyo mtu alifanya hivyo hivyo kama alivyoelekezwa na Bahlul. Ilipowadia siku ya kumi, alimwendea Mtawala pamoja na kitabu na Punda na mbele ya wote akamuachia mbele yake Punda kile kitabu. Kwa kuwa punda alikuwa na njaa kali mno, hivyo alianza kufunua kila ukurasa wa kitabu hicho katika kutafuta chakula kama vile alivyokuwa amezoea. Huyo punda alipofikia ukurasa wa mwisho, akaelewa kuwa chakula chake hakikuwapo, na hivyo alianza kulia kwa sauti kubwa akitaka kuwaelezea wote kuwa alichokuwa akitaka ni chakula kwani alikuwa na njaa kali mno, lakini waliokuwapo hapo walidhani kuwa punda analilia kitabu kingine kwani amekimaliza hicho. Kwa kuyaona hayo, Mtawala huyo alijua kuwa kwa kwel i punda amesomeshwa na hivyo anajua kusoma kitabu.

Mtawala alitimiza ahadi yake kwa kumpatia zawadi nono yule mtu hivyo Bahlul alimsaidia asiadhibiwe kwa kuuawa.