Table of Contents

(48). Bahlul Azuru Makaburi

Bahlul alikuwa akipendelea zaidi kukaa makaburini. Siku moja alipokuwa makaburini, Harun Rashid alifika hapo akienda mawindoni. Alipomfikia Bahlul alimwuliza: "Je Bahlul, wafanya kitu gani hapa?"

Bahlul alimjibu: "Mimi nimekuja kuwaona wale watu ambao hawawasengenyi watu na wasiotarajia chochote na ambao hawawezi kunidhuru chochote."

Harun alisema: "Je wewe waweza kuniambia kuhusu Qiyama, Sirati na maswali yatakayoulizwa kuhusu hii Dunia?"

Bahlul alimwambia: "Waambie wahudumu wako wawashe moto na kuweka kikaangio cha mkate juu ili ipate moto."

Ilipopata moto, Bahlul alisema: "Ewe Harun! Mimi nitasimama juu ya kikaangio hiki nitajitayarisha na nitakutajia kile nilichokula na kile nilichovaa."

Harun alikubali hayo.
Bahlul alisimama juu ya kikaangio kilichopata moto na kwa upesi upesi akaanza kusema: "Bahlul, kilalio, mkate wa mtama na siki!" na alipomaliza, aliteremka chini huku miguu yake haikuungua hata kidogo.

Ilipofika zamu ya Harun Rashid, alianza kujitaarufisha kwa mujibu wa matakwa yake, na kabla haja maliza kujitaarufisha, miguu yake ikaaungua na kumfanya aanguke chini. Alikuwa akijitaarufisha tu na wala hakuanza kuongelea yale aliyokula au kuvaa.

Hapo ndipo Bahlul aliposema: "Ewe Harun! Maswali ya Qiyama yatakuwa hivi hivi. Wale wote watakaokuwa waja wema wa Mwenyezi Mungu, wenye kukinai na wasio na tamaa ya dunia ndio watu watakao pata raha kwa kupita haraka maswali na majibu ama wale wenye kupenda dunia na starehe zake, basi wao watabakia juu ya mtihani huo kwa muda mrefu pamoja na udhia wote."