Table of Contents

(5). Bahlul Na Faqihi

Faqihi mashuhuri kutoka Khurasan alifika Baghdad, alialikwa na Harun Rashid katika Baraza lake na akimkalisha ubavuni mwake.

Wakati alipokuwa akizungumza na Harun, alitokezea Bahlul ambaye naye alikaribishwa aketi karibu nao. Huyo mtu alimwona Bahlul yu kama mwehu na hivyo alimwambia Harun: "Nimestaajabishwa na heshima na mapenzi yako Khalifa, kwa kuwa unawastahi hata watu waliwehuka hadi kuwakaribisha karibu nawe?"

Alipoyasikia hayo Bahlul, alielewa kuwa alikuwa akisemwa yeye tu na hapo akajikaza akamwambia: "Kwa nini waringia ilimu yako hiyo kidogo, usinidharau kwa udhahiri wangu bali jitayarishe kwa mabishano ili nami nimdhihirishie Khalifa kuwa wewe haujui lolote!"

"Mimi nimesikia kuwa wewe u - mwehu na hivyo siwezi kubishana na wehu!" Aliyasema huyo Faqihi.

Hapo Bahlul alimjibu akiwa ameghadhabika, "Mimi ninaukubalia uwehu wangu lakini wewe unakataa kuukubalia ujahili wako na kutokuwa na ilimu kamili."

Harun alipoyasikia hayo, alijaribu kumtuliza Bahlul, lakini ilishindikana huku akidai kuingia mabishano na huyo Faqihi, iwapo anajiamini kwa ilimu kamili."

Basi Harun alimgeukia huyo Faqihi na kumwambia: "Je kuna kipingamizi gani katika kumwuuliza maswali?"

Hapo huyo Faqihi alijibu: "Mimi nipo tayari kubishana naye iwapo atakubaliana na shuruti langu moja nalo ni, iwapo ataweza kunijibu basi nitampa Dinar elfu moja za dhahabu na akishindwa itambidi anilipe hivyo."

Bahlul alimjibu: "Kwa kweli mimi huwa sina mali za kidunia na wala sina Dinar wala dhahabu, lakini nipo tayari kuwa mtumwa wake iwapo nitashindwa kumjibu, na iwapo nitamjibu basi nipatiwe hizo Dinar elfu moja za dhahabu ambazo nitazigawa miongoni mwa mafukara."

Kwa hayo, huyo mtu alianza kumuuliza swali hivi: "Katika nyumba moja yupo mwanamke aliyeketi na mume wake halali kisheria na humo humo wapo watu wawili ambao mmoja wao anasali na mwingine yupo katika hali ya saumu. Ghafla anatokezea mtu kutokea nje na kuingia ndani ya nyumba hiyo. Kutokezea huku kwa mtu huyo, wale bibi na bwana wanakuwa haramu baina yao na sala na saumu za wale wawili zinakuwa batili. Je unaweza kuniambia huyo mtu aliyotokezea ni nani?"

Bahlul bila ya kusita anamjibu: "Huyo mtu aliyeingia nyumbani kwa ghafla alikuwa ndiye bwana wa kwanza wa yule bibi kwani alikwenda safari na baada ya muda mrefu kupita, ilijulikana kuwa amefariki na hivyo huyo mwanamke akaolewa na bwana wa pili (aliyekuwa nyumbani) baada ya kupokea idhini ya hakimu sharia. Wale watu wawili walikuwa wamelipwa kwa ajili ya kusali na kufunga saumu zilizo za qadhaa za bwana wake aliyesadikiwa amekufa safarini.

Na kurejea kwake kutoka safari ndefu aliyosadikiwa amekufa, imebatilisha ndoa ya mke wake na yule bwana kwani yu hai bado, vile vile saumu na sala pia zinabatilika kwani kumsalia mtu aliye hai pia ni batili."

Kwa hayo, Harun na wanabaraza wake wote walivutiwa na majibu ya Bahlul na walimsifu sana.

Baada ya hapo, ilikuwa ni zamu ya Bahlul kuuliza swali: "Je niulize?" " Uliza tu!" alijibiwa.

Bahlul aliuliza: "Iwapo ninayo kasiki moja ya siki (vinegar) na nyingine ya urojo wa sukari, na kwa ajili ya kutengeneza Sikanjabin (kinywaji cha Siki) nimeweka ili kuchanganya katika kasiki ya tatu na hapo tunakuja kumkuta panya amefia humo. Je unaweza kutuambia kuwa huyo panya alitokea kasiki ya Siki au Urojo wa Sukari?

Hapo huyo mtu alijaribu kwa uwezo wake wote kumjibu Bahlul, lakini alishindwa.

Kwa kuona hali hiyo, Harun alimwambia Bahlul "sasa wewe mwenyewe tujibu hayo."

Bahlul alimwambia Harun: "Nitafanya hivyo iwapo huyu mtu atakiri kutoelewa majibu yake."

Kwa masikitiko na aibu kubwa huyo Faqihi alikubali kushindwa kwake kwa kuling'amua hilo fumbo.

Alianza Bahlul kulijibu: "itabidi sisi kumtoa huyo panya na kumwosha vizuri kwa maji safi halafu tupasue tumbo lake na humo iwapo tutakuta siki au urojo wa sukari, basi itatubidi tumwage kile kitakachothibitika kuwamo tumboni mwake."

Wote waliokuwa wamehudhuria, walifurahishwa mno na majibu ya Bahlul na Faqihi alilazimika kutoa Dinar elfu moja za dhahabu ambazo Bahlul alizigawa miongoni mwa mafuqara wa Baghdad.