Table of Contents

(50). Bahlul Aenda Bafuni

Siku moja Bahlul alikwenda bafuni (bafu za kulipia fedha ) na huko wahudumu hawakumjali ipasavyo bali walimdharau tu. Lakini yeye alioga na alipotoka nje akaenda moja kwa moja kwa mwenye mali, akampa Dinar kumi.

Wahudumu walipoona hayo, walijuta mno kwani wangalipatapo chochote kama bakhshishi yao.

Juma lililofuatia, tena alikwenda bafuni kuoga. Safari hii wahudumu walimkaribisha vyema na kumpa kila aina ya huduma ipasavyo. Alipomaliza kuoga, aliwapa wahudumu Dinar moja tu. Hao walimwuliza kwa hasira: "Loh! Juma lililopita bila ya huduma zozote ulilipa Dinar kumi na leo vipi baada ya huduma zote hizo unatoa Dinar moja tu.?"

Bahlul aliwajibu: "Malipo ya leo nilikuwa nimeshalipa wiki iliyopita, hivyo ninatoa Dinar moja tu ili mjue, muwe daima mukikwahudumia wateja wenu vile iwapasavyo bila ya kuweka tamaa mbele."