Table of Contents

(51). Bahlul Na Mzozo Wa Kuku

Siku moja mfanyabiashara mmoja kutoka Bara Hindi alileta mali huko Baghdad na alipofika wakati wa njiani alibakia pamoja na msafara, na aliagiza chakula kwa mpishi mmoja, aliletewa kuku na mayai machache yaliyochemshwa. Baada ya kulala alipoamka alikuta msafara umeishaondoka na hivyo hakuweza kumlipa mpishi fedha za kuku na mayai.

Baada ya mwaka mmoja kupita ikatokea kuwapo papo hapo, aliagiza chakula cha jioni. Mpishi alimletea vile vile yaani kuku na mayai machache yaliyochemshwa. Kulipokucha alimwita mpishi, na kumwambia: "Mimi unanidai deni la mwaka jana la kuku na mayai machache. Naomba unipatie hisabu hiyo na ya leo ili niweze kukulipa kwa pamoja."

Mpishi, baada ya kupiga mahesabu yake kwa makini, alimwambia mfanyabiashara amlipe Dinar elf moja. Mfanyabiashara huyo aliposikia chakula cha jioni kugharimu Dinar elfu moja, alichukia na kusema: "Mimi nadhani kuwa wewe umewehuka kwa kudai Dinar elfu moja za kuku mawili na mayai machache."

Mpishi alimjibu: "Loh! Unathubutu kuniambia mwehu huku mimi nimepiga mahesabu yangu kwa uangalifu ili nisije kukudai zaidi hata chembe kidogo?"

Mfanyabiashara akasema: "Mimi nashukuru mno lakini umefikiaje kiasi hiki cha madai?"

Mpishi akamjibu: "Tafadhali zingatia kwa makini kabisa nikuambiayo. Gharama hiyo ninayokudai imetokana na wewe kula kuku na mayai sita hapo mwaka jana.

Iwapo kuku huyo angalikuwa hai basi mayai hayo angalilalia na hivyo angaliangua vifaranga. Na kila kifaranga angalitaga mayai kama hayo na vifaranga. Kwa hivyo, mimi ningalimiliki maelfu ya mayai na vifaranga, lakini yote hayo, nimekuachia wewe waniambia kuwa mimi ni mwendawazimu!"

Wasafiri wote katika msafara walivutiwa na ugomvi huo, nao walifanya kila jitihada katika kuwanyamazisha na kuwasuluhisha lakini ilishindikana. Hatimaye ilifikiwa kuchukua hatua za kwenda mbele ili kupatia ufumbuzi wa maswala hayo.

Mshauri alipoelezwa habari kwa ukamilifu, alitoa uamzi: "Ewe mfanyabiashara! Unatakiwa kumlipa mpishi huyu Dinar elfu moja."

Kwa hayo, mfanyabiashara alihangaika na kubabaika kwani hakuelewa lipi la kufanya. Mmoja wa wasafiri, alikuwa ni rafiki yake Bahlul na alitambua kuwa ufumbuzi wa haki unaweza tu kutolewa na Bahlul. Basi aliwaambia: "Enyi wenzangu! Kutoka hapa hadi Baghdad si mbali na hivyo nitawaletea Qadhi wa Baghdad ili tupate hukumu yake katika swala hili. "Aliondoka mbio akimtafuta Bahlul, na alimkuta katika msikiti mmoja ambapo alimwelezea habari zote.

Alirudi pamoja na Bahlul hadi msafara huo. Walipoukaribia ule msafara, Bahlul alimwambia yule mtu "Wewe tangulia, nami ninakufuata kwa miguu na vile vile uwaambia kuwa mimi nitafika baada ya nusu saa hivyo wanisubiri. Qadhi ameahidi, atafika tu!"

Huyo mtu aliwaambia hivyo hivyo,na watu wote walianza kupima kila dakika. Ilipofika nusu saa wakaona bado Qadhi hajafika, alifika baada ya saa moja na nusu na kila mmoja alisimama kutoa heshima zake. Aliketi na kuwaambia kuwa amekwisha pata habari za mgogoro wa mfanyabiashara na mpishi. Alisema: "Mimi naomba msamaha kwa kuchelewa kwani nilikuwa nikikoboa ngano, kwani ngano iliyokobolewa inaota vizuri zaidi na hivyo nilishughulishwa na hayo."

Wote waliokuwapo walianza kusema: "Huyu Qadhi ni mtu wa ajabu kwani anakoboa ngano kabla ya kupanda shambani."

Bahlul aliwajibu: "Kwani nini mumestaajaabishwa kwani kwenu hapa kuku aliyepikwa pia huweza kutaga mayai."

Mshauri alisema: "Qadhi huyu amesema yaliyo sahihi kwani kuku aliyepikwa hatoi vifaranga!"
Hatimaye, watu waliafikiana neno kwa kumpa fedha za kumridhisha yule mpishi. Nao wote wawili walikumbatiana kwa kufurahi.