Table of Contents

(54). Bahlul Na Mafuvu Ya Kale

Siku moja Bahlul alikuwa amekaa makaburini akiwa na fimbo ndefu, huku akichunguza mafuvu mengi ya vichwa vya zamani yaliyokuwa yametawanyika hapa na pale. Harun Rashid alipita hapo na kumwona Bahlul akichunguza mafuvu hayo, Alisema: "Ewe Bahlul! Wafanya nini?"

Bahlul alimjibu: "Najaribu kutambua kama mafuvu haya ya vichwa ni ya wafalme au ni ya mafukara, kwani yote nayaona sawa!"
"Na hiyo fimbo ni ya nini?" aliuliza Harun.
"Naipimia ardhi." alijibu Bahlul.
Alianza Harun kwa kudhihaki: "Je unapima ardhi, hoja gani?"
Bahlul alimjibu: "Ewe Harun! Urefu wa mikono mitatu kwangu mimi ijapokuwa mimi ni masikini ni sawa na mikono mitatu kwangu kwako wewe ijapokuwa una fahari na mali!" (Yaani wote wanaingia katika kaburi la vipimo sawa hakuna ubaguzi wa tajiri kupewa pana au masikini kupewa finyo!)