Table of Contents

(9). Harun Rashid Amkasirikia Bahlul

Harun alimwajiri jasusi makhususi kwa ajili ya kuchunguza na kuripoti kwake juu ya imani na akida sahihi za Bahlul. Baada ya siku chache huyo jasusi alikamilisha uchunguzi wake na kuripoti kwa Khalifa kuwa Bahlul alikuwa ni mpenzi wa Ahl-al-Bayt ya mtume (s.a.w.w.) na alikuwa mfuasi wa Imam Musa al-Kadhim (a.s.).

Harun alimwita Bahlul na kumwambia: "Ewe Bahlul! Mimi nimepata habari za kuaminika kuwa wewe ni mmojawapo wa wapenzi na wafuasi wakubwa wa Musa ibn Jaafar na hivyo unafanya kila jitihada za kudhihirisha na hivyo umejidhihirisha u - mwehu ambapo sivyo ulivyo!"

Bahlul alimjibu: "Iwapo hivyo ndivyo ilivyo, je utanifanya nini?"

Kwa majibu hayo, Harun alighadhibika mno na kumwamuru Masrur, mfanyakazi wake, amvue nguo Bahlul akalishwe juu ya punda na kuzungushwa mjini na hatimaye kukatwa kichwa mbele yake Harun.

Masrur, alitekeleza vile alivyoamrishwa na hatimaye kumleta mbele ya Harun katika hali hiyo ili aweze kuuawa.

Mara, hapo akatokezea Jaafer Barmaki ambaye kwa kuiona hali hiyo ya Bahlul alimwuliza sababu ya hali yake hiyo:
"Ewe Bahlul! Je umetenda kosa gani?"
Bahlul alimjibu: "Kwa kuwa mimi nimesema ukweli, kwa hivyo Khalifa akanizawadia mavazi yenye thamani."

Harun Rashid, Jaafar, na wote waliokuwepo walichekeshwa mno kwa majibu ya Bahlul, na papo hapo Harun alimsamehe Bahlul na kutoa amri ya kufunguliwa na apewe mavazi mapya na mazuri.

Lakini Bahlul hakukubali hayo bali yeye alichukua kifurushi cha nguo zake kuukuu na kuondoka.