Bibi Khadija Bint Khuwailid

Toka enzi za kunawiri mwangaza kwa walimwengu, Bibi Khadija alikuwa ni miongoni mwa mashujaa wa kidini waliojitolea wao wenyewe na hata mali zao ili kuunusuru na kuutumikia Uislamu kidhati.

Kinyume cha wadhaniavyo wasiojuwa kwamba dini ni ya waume tu, Bibi huyo aliudhihirishia ulimwengu mzima jinsi wanawake walivyo na fungu kubwa la kuutumikia Uislamu.

Ndiye Bibi wa pekee wa Mtume (s.a.w.) zama za uhai wake, ndiye wa kwanza kabisa kumwamini Mtume (s.a.w.) wakati uadui na masingizio ya Makureishi yalipokuwa yamekomaa na kufikia kilele cha udhia kwa Mtume (s.a.w.).

Msaidizi mkuu na wa pekee kati ya wanawake wote wa Hijazi alikuwa Bibi huyu ambaye kamwe hata kwa pepeso la jicho hakudhamiria kujiunga na kundi la jamaa zake katika kumkaidi Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Pamoja na utajiri wake aliokuwa nao ambao ulikuwa wa daraja ya kwanza, kamwe mali yake haikumghafilisha na yatosha tu kuwa ushahidi wa hili kule kuwa kwake mtu wa kwanza kusali nyuma ya Mtume licha ya kuwepo waume. Akishirikiana na Amiye mumewe (Abu Talib), Bibi Khadija alijaribu kwa uwezo wake wote kupinga miongozi na maasi ya Makureishi ambao lengo lao hasa likiwa ni kummaliza Muhammad (s.a.w.).

Daraja ya mwisho aliyoifikia kabla ya kuuondokea kwake huu ulimwengu, ni kule kubashiriwa pepo na kuwa miongoni mwa wanawake watakatifu ambao ni wanne tu (Wa kwanza wao akiwa yeye, wa pili mwanaye Fatimatuz Zahraa, wa tatu, Asia binti Mazahim ambaye ni mkewe Firauni, na wanne wao ni Bibi Mariam binti Imran, mamake Nabii Isa (s.a.).

Bibi huyu - Khadija - kafariki mwezi huu wa Ramadhani tarehe 10 mwaka wa tatu kabla ya Mtume kuhama Madina. Na hivyo basi alizikwa katika Mji Mtakatifu wa Makkah.