read

Bibi Fatima (A.S) Kiigizo Chema Kwa Wanawake

Bibi Fatimah (a.s.) ni mwanamke anayezingatiwa kuwa ni mwanamke wa kutolea mfano katika dini ya kiislamu, na pia ni kiigizo chema kwa kila mwanamke anayetafuta mafanikio katika maisha yake. Bibi Fatimah binti Muhammad (s.a.w.w) ndiye mwanamke bora ulimwenguni aliyezaliwa na kupata malezi katika nyumba iliyokuwa ikishuka ndani yake Wahyi kutoka mbinguni.

Si hivyo tu bali Bibi Fatimah alihitimu mafunzo ya Uislamu katika madrasa ya Utume, na kutokana na mafunzo hayo aliweza kufikia daraja ya juu na tukufu. Katika kuthibitisha ubora wa Bibi Fatimah, Mtume (s.a.w.w) amepata kusema, "Hakika Mwenyezi Mungu huwa radhi kwa radhi ya Fatimah, na huchukia kutokana na kuchukia kwa Fatimah."1

Kwa ajili ya daraja kubwa aliyonayo Bibi Fatimah katika Umma wa Nabii Muhammad (s.a.w.w) imekuwa ni wajibu kwa kila mwanamke duniani kuiga mwenendo wa Bibi huyu katika maisha yake, ajing'arishe kwa nuru yake nzuri na afuate nyayo zake ambazo zitamuelekeza kwenye mafanikio na utukufu. Hakika Bibi Fatimah (a.s), ni mfano wa kila utukufu na kila jema. Mwanamke yeyote atafanikiwa iwapo ataamua kufuata mwenendo wa Bibi Fatmah (a.s.), na kinyume chake ni kuwa, kila mwanamke ataangamia iwapo ataamua kujichagulia mwenendo wake au kuiga usiyokuwa mwenendo wa Bibi Fatimah. Pia Fatimah (a.s.) alikuwa Mchaji Mungu na mwenye kutekeleza vilivyo maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Pia ile maana nzima ya Hijabu aliifahamu vema na kuitekeleza kama ilivyoamriwa na Mwenyezi Mungu.

Hivyo utekelezaji wake katika maamrisho ya Mwenyezi Mungu ulikuwa wa hali ya juu, kwani hakupata kutoka nje ila huwa amevaa vazi la kumsitiri mwili wake wote tangu kichwani hadi miguuni. Isitoshe alikuwa akiichukia mno tabia ya wanawake kutoka majumbani mwao bila kujisitiri kisheria. Bibi Fatimah alichukizwa na tabia hiyo kwa sababu Mwenyezi Mungu pia anaichukia tabia ya kutokujisitiri na hasa kwa kuwa kukosa sitara ya kishera kwa wanawake ni ufunguo wa kuyaendea maovu na ni miongoni mwa vitangulizi vinavyosababisha watu kuteleza, bali wanaaanguka kabisa.

Sasa hivi tunawaletea baadhi ya mafundisho kuhusu Hijabu na tutaona pia utukufu wa Bibi Fatimah katika mafunzo hayo.

Ni Kitu Gani Kilicho Bora Kwa Mwanamke?

Inasimuliwa katika historia kwamba, Mtume (s.a.w.w) siku moja aliwauliza Masahaba suali lifuatalo: "Je! ni kitu gani kilicho bora kwa mwanamke?" Masahaba walinyamaza kwa kuwa jibu la mkato na sahihi hawakulifahamu, ikawa kama kwamba akili zao zinahangaika baina ya kuwa kilicho bora kwa mwanamke ni mali, uzuri wake, kuolewa au kitu gani? Kipindi chote hiki Bibi Fatimah alikwisha lisikia swali hilo, na baada ya kimya cha kukosekana jibu, Bibi Fatimah alimtuma mtu aende kwa Mtume (s.a.w.w) akatoe jibu sahihi la swali hili nalo ilikuwa: "Kilicho bora kwa mwanamke ni yeye mwanamke asimuone mwanaume na mwanaume naye asimuone mwanamke."2

Baada ya jibu la bibi Fatimah Masahaba walikuwa wakisubiri jibu la Mtume atasema nini kuhusu jawabu alilotoa Binti yake. Mtume (s.a.w.w) akasema "Amesema kweli Fatimah." Na akaongeza kusema, "Fatimah ni sehemu iliyotokana na mwili wangu." Maana ya maneno ya Mtume yalimaanisha kwamba hilo ndilo jawabu sahihi na hiyo ndiyo imani.

Kutokana na jawabu hili, Bwana Mtume (s.a.w.w.) akawa ameitangazia dunia nzima kwamba: Utu, heshima, utukufu, na wema wa mwanamke unapatikana ndani ya Hijabu, na kinyume chake ni uovu na shari, isitoshe hasara humfika mwanamke anapoitupa Hijabu.

Mazungumzo Ya Kustaajabisha

Historia inaendelea kutufahamisha kwamba Bibi Fatimah (a.s.) alikuwa amekaa na baba yake ambaye ndiye Mtume (s.a.w.w), mara alibisha hodi Sahaba Abdalla ibn Ummi Maktum ambaye alikuwa kipofu. Kabla Sahaba huyu hajaingia Bibi Fatimah (a.s.) alisimama akaondoka mahali hapo. Baada ya kwisha mazungumzo baina ya Mtume na Sahaba huyu, Sahaba Abdallah ibn Ummi Maktum aliondoka. Bibi Fatima alirudi na akaendelea kuzungumza na Mtume (s.a.w.w.) Bwana Mtume (s.a.w).wakamuuliza Binti yake sababu ya kuondoka wakati alipoingia Sahaba Abdallah ibn Ummi Maktum hali kuwa anafahamu kabisa kwamba yule ni kipofu haoni3

Bibi Fatimah alijibu kama ifuatavyo."Ikiwa yeye hanioni basi mimi namuona na yeye ananusa harufu ya wanawake.

" Mtume (s.a.w.w) alifurahishwa mno na jawabu la Binti yake ambalo linaonyesha kipimo cha Uchamungu na utukufu unaotoka kwa Binti yake Mwenye hekima. Isitoshe kwa jawabu hilo, Bwana Mtume hakumlaumu binti yake kutokana na mkazo huu mkali unaohusu Hijabu, bali furaha ya Mtume iliendelea kwa upeo mkubwa na akaunga mkono kwa dhati kabisa kisha akasema: "Nashuhudia kwamba wewe ni sehemu iliyotokana nami"4

Tukio Muhimu Ndani Ya Msikiti Wa Mtume (S.A.W.W.)

Siku moja Bibi Fatimah (a.s.) alitaka kutoa mhadhara ndani ya msikiti wa Mtume (s.a.w.w). Kabla ya kuanza kuhadhiri alitengenezewa sitara humo Msikitini, akakaa yeye na Waumini wengine wakike upande mmoja na Waumini wanaume wa Kiansari na Muhajirina nao wakakaa upande wa pili. Sitara hii aliyotengenezewa Bibi Fatimah (a.s) ilikuwa ina maana nyingi ndani yake.

Kwanza ilikuwa ni kutekeleza sheria inayohusu Hijabu katika sura ya kuweka kizuizi, ambapo pande mbili hizo zilitenganishwa. Pili, hali hiyo ilikuwa ni kuonesha kutokuukubali kwa vitendo mchanganyiko wa wanaume na wanawake, jambo ambalo maadui wa Uislamu wanatumia kila mbinu kulihalalisha kwa kulitolea hoja batili.

Sasa nakutazama ewe dada yangu wa kiislamu, nikitarajia umeiona mifano hii mitatu inayohusu maisha ya Bibi Fatimah (a.s.) ambaye ni mwanamke bora kuliko wanawake wote duniani, na ni mwanamke anayestahiki kuigwa katika Uislamu. Inafaa uige na ujifunze kwake ili upate kupambika kwa umbile la kike ( yaani kuwa na haya) na utukufu, kadhalika ifanye nafsi yako iwe ya mwanamke Mchamungu mwenye kushika mafunzo ya kiislamu na hukmu za Qur'an. Ewe dada wa kiislamu hebu shikamana na mafunzo ya kiislamu ambayo Mwenyezi Mungu amekupa ili ufanikiwe duniani na akhera. Mafunzo haya yatakupandisha kwenye daraja tukufu la wenye imani na mafanikio. Fahamu kwamba hutafanikiwa isipokuwa uwe umeshikamana na kuyatumia mafunzo hayo kwa kuyatekeleza maishani mwako.

Kujiheshimu Ndiyo Pambo La Mwanamke.

Bwana Mtume (s.a.w.w) amesema, "Kujiheshimu ndiyo pambo la Mwanamke." 5

Hapana shaka kwamba pambo limegawanyika sehemu mbili: Pambo lisilo halisi na pambo halisi. Ama pambo lisilo halisi ni lile ambalo linaloonekana wazi, na ni lenye kubakia kwa muda maalum, kisha hutoweka bila hata ya kumuongezea kitu muhusika katika utu wake. Ama lile pambo halisi, ni lile ambalo hubakia muda wote na pia humfanya mwanamke aupate ule utu wake kamili na kumfikisha kwenye daraja ya ukamilifu. Ukweli usiokuwa na shaka ni kuwa, pambo halisi ndilo lenye umuhimu mno kuliko lile jingine, bali ndilo lengo analopaswa kulishughulikia kila mtu. Endapo mtu atakosa kuwa na fungu fulani katika pambo hili halisi, basi pia huwa hana faida yoyote ndani ya lile pambo la dhahiri.

Hapana shaka kwamba kujiheshimu ndilo pambo pekee linalomfaa mwanamke kama alivyosema Bwana Mtume (s.a.w.w). Pambo hilo humjengea mwanamke utu, heshima na utukufu hapa duniani na kesho akhera. Ama madawa ya kujirembesha, manukato na mengineyo miongoni mwa mapambo, yote hayo ni mapambo ya nje tu na hayana maana yoyote khususan mwanamke mwenyewe atakapokuwa si Mchajimungu: Mwenyezi Mungu apishe mbali.

Hijabu ndiyo alama pekee inayoweza kutambulisha Uchaji Mungu wa mwanamke na pia heshima yake na utu wake. Wakati huo huo tabia ya kutokuwa na Hijabu huchafua heshima ya mwanamke na kuacha maswali chungu nzima kuhusu Uchaji Mungu wake na kujiheshimu kwake kwa jumla.

Yote haya yanakuja kwa sababu yeye mwenyewe kauweka mwili wake kuwa maonesho mbele ya maelfu ya watu siku zote. Kutokana na hali kama hiyo, hata huwezi kutambua ni mikono mingapi iliyowahi kuushika mwili wake kwa kuuacha wazi na kutokujisitiri kwa mujibu wa sheria!!

Hivi unadhani watu wa kale na hata wa leo hii, nyoyo zao zitasal imika vipi katika mazingira hayo ya wanawake kuicha wazi miili yao? Kamwe hawatasalimika kabisa, kwani wanawake wanapoiacha wazi miili yao ni jambo linalopelekea tuhuma mbaya kwa wanawake. Imam Ali (a.s.) anasema : "Yeyote mwenye kuiweka nafsi yake mahala penye tuhuma mbaya, basi asimlaumu mtu atakaye mdhania vibaya." 6

Hapana shaka kwamba, mwanamke asiyekuwa na Hijabu huwa anaidhuru nafsi yake mwenyewe kwa sababu. Kwanza, huwa anapata hasara mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Pili, heshima yake ndani ya jamii huwa inaporomoka.

Hasara anayoipata mwanamke huyo mbele ya Mwenyezi Mungu inakuja kwa sababu mwanamke huyo huwa amekwenda kinyume na kanuni za mbinguni na kukosa utiifu kwa Mwenyezi Mungu. Baadaye tutaeleza adhabu za huko akhera atakazozipata mwanamke asiyejali kujisitiri kwa mujibu wa sheria ya KiIslamu.

Ama hasara atakayoipata mwanamke kutoka na na heshima yake kuporomoka ndani ya jamii, hali hiyo inasababishwa na yeye mwenyewe kutokana na tabia yake ya kuyaacha wazi maungo yake yaonekane kwa kila mtu, hali ambayo humuingiza ndani ya kila aina ya uovu na ufisadi na hatimaye akadhalilika vibaya.

Na tukirejea kwa mwanamke mwenye kujisitiri kwa mujibu wa sheria ya kiislamu, huyu hupata faida za aina mbili kwa pamoja:

Faida aipatayo mbele ya Mwenyezi Mungu ni kwamba, yeye huwa ni mwanamke mtukufu mbele ya Mwenyezi Mungu na Malaika wake pamoja na Mawalii wa Mwenyezi Mungu. Utukufu huu anaupata kwa kuwa amemtii Mola wake, ametekeleza maamrisho yake na ameyasitri maungo ambayo Mwenyezi Mungu ameamrishsa yasitiriwe. Na kwa ajili hii basi, mwanamke kama huyu kamwe hatonyanyua unyayo wake bali rehma za Mwenyezi Mungu huwa ziko pamoja naye, pia radhi za Mwenyezi Mungu humbatana naye, na wakati huo huo Malaika wa Mwenyezi Mungu wanamuombea msamaha. Mwenyezi Mungu anasema: "Kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora na ni chenye kubakia." 7

Ama faida atakayoipata ndani ya jamii, ni pale mwanamke huyo anapokuwa ni mwenye kuheshimiwa na kutukuzwa, yote haya anayapata kwa kuwa yeye amejipamba kwa pambo la kujiheshimu na kuuhifadhi utu wake, kisha akausitiri uzuri huo aliopewa na Mwenyezi Mungu.

Majadiliano Na Msichana Wa Kikristo.

Msichana mmoja wa Kikristo alikwenda kwa mwanachuoni wa kiIslamu na kumwambia. "Mimi nimefahamu mambo mengi kuhusu Uislamu na kwa hakika dini hii imenishangaza sana kwa kanuni zake na miongozo yake, na nimeupenda Uislamu kwa mapenzi ya kweli.

Lakini kanuni moja tu kwangu mimi imekuwa ni kikwazo kuingia katika Uislamu. Nimewauliza watu wengi kuhusu kanuni hiyo, mpaka sasa sijapata jawabu la kunitosheleza.

Iwapo wewe Sheikh utaweza kunibainishia hekima iliyomo ndani ya kanuni hii, basi nakuthibitishia kuwa nitaingia katika Uislamu."

Yule Mwanachuoni akasema, "Ni ipi kanuni hiyo?" Msichana akajibu. "Kanuni ya kuvaa Hijabu, ni kwa nini Uislamu haumuachi mwanamke akatoka nje apendavyo kama ilivyo kwa wanaume?" Mwanachuoni yule wa kiislamu akasema, "Je umepata kumuona sonara ameweka dhahabu na johari nyinginezo katika sanduku la kioo, kisha akalifunga sanduku hilo kwa kufuli? Msichana akajibu, "Ndiyo." Sheikh huyu akamwambia tena yule msichana, "Je, ni kwanini sonara hakuziacha johari hizo zikawa zinashikwa na kila mtu ajaye kutaka kununua? Kwa nini amezihifadhi ndani ya sanduku la kioo lililofungwa?" Msichana akasema: "Amefanya hivyo ili azilinde johari zake kutokana na wezi na mikono yenye khiyana." Yule Mwanachuoni akamwambia msichana: "Hii ndiyo hekima ya Hijabu, fahamu kwamba mwanamke ni johari ya thamani ambayo ni lazima kuilinda kutokana na waovu na wahaini.

Pia ni wajibu kumhifadhi mwanamke kutokana na macho ya watu waovu ndani ya kitu ambacho kitamsitiri barabara kama inavyolindwa lulu katika kola lake, ili asije akaangukia mikononi mwa watu hao na kumgeuza kuwa ngawira yao." Hakuna njia bora isipokuwa Hijabu, hicho ndiyo kizuwizi na ni mlinzi wa mwanamke. Kwa hakika mwanamke mwenye Hijabu huwa salama kutokana na shari. kwa kuwa mwili wake umesitirika, na mapambo yake nayo hayaonekani mbele ya kila mtu.

Hali ya kuvaa Hijabu inawafanya watu wasimtamani mwanamke huyo kwa kuwa hakuna wakionacho cha kuwafanya wamtamani. Kutokana na hali hiyo huwa wanamuepuka, wala hakiwageuzi kitu chochote cha kuwafanya wamuangalie mwanamke huyo, bali humuogopa na kumuheshimu. Mwisho wa yote watu humuogopa na kumpa heshima yake kama anavyostahiki. Yote hayo yatapatikana kwa ajili ya kuvaa Hijabu, na hali hii inamaanisha kwamba, Hijabu ndiyo mlinzi wako na ni hifadhi ya heshima, na utukufu wako. Ewe msichana huu ndio upande mmoja wa falsafa ya Hijabu."

Baada ya maelezo hayo ya Sheikh, msichana yule wa Kikristo alionesha furaha na akaridhishwa na maelezo ya Sheikh kisha akasema, "Sasa nimetosheka na falsafa iliyomo ndani ya kanuni hii ya kiislamu, na pia nimefahamu hekima iliyomo na ninapendezwa kuingia katika Uislamu." Baada ya hapo msichana akatoa Shahada mbili na akawa Muislamu. Majadiliano haya mazuri ya kidini yanatubainishia kwamba Uislamu unakusudia kuihifadhi hehsima na utukufu wa mwanamke, pia Uislamu unataka kuilinda jamii. Na kwa sababu hizo basi, Uislamu umewajibisha Hijabu kama sharti la msingi kuweza kutimiza malengo hayo.

Tofauti Ya Mwanamke Mwenye Hijabu Na Asiye Na Hijabu.

Mmoja wa marafiki zangu alinisimulia tukio la kufurahisha lililomtokea Muumini mmoja wa kiislamu. Tukio hili lilikuwa kama ifuatavyo. Siku moja Muumini huyo alikuwa akitembea pamoja na mkewe aliyekuwa kavaa Hijabu. Matembezi hayo yalimfikisha katika moja ya bustani zinazotembelewa na watu wa aina tofauti.

Ghafla Muumini huyo alijiwa na mtu fulani ambaye naye alikuwa na mkewe. Mke wa mtu huyu hakuwa amevaa vazi la Hijabu na hivyo basi kwa dharau na kejeli alimwambia yule Muumini. "Kwa nini umemvalisha mkeo Hijabu, kwa nini hukumuacha akatoka bila Hijabu kama jinsi alivyo mke wangu? Hijabu ina faida gani?" Jawabu alilotoa Muumini yule lilikuwa la kushangaza na la kishujaa. Alimwambia. "Je unafahamu tofauti ya mwanamke mwenye Hijabu na asiyekuwa na Hijabu? Bwana yule mwenye kejeli akasema "Nini tofauti yake?" Yule Muumini akajibu kwa njia ya kuuliza, je, kuna tofauti gani baina ya taxi na gari ambalo mtu hulitumia yeye binafsi? Yaani kwa matumizi yake pekee yake." Bwana yule akajibu akasema, "Taxi hutumiwa na kila mtu, wakati ambapo gari maalum linamuhusu mwenyewe peke yake. Hii ndiyo tofauti iliyopo." Basi yule Muumini akasema, "Hali hiyo ndio iliyopo baina ya mwanamke aliyevaa Hijabu na yule asiye na Hijabu.

Mwanamke asiye na Hijabu ni sawa na taxi ambayo kila mtu anaweza kuikodisha na kuitumia. Mwili wa mwanamke huyo huwa wazi na kuonesha mapambo yake na uzuri wake, na kuwafanya watu wavutike kutokana naye, jambo ambalo linaweza kusababisha kutendewa maovu, kama ambavyo mara kwa mara hali hii inavyowapata wanawake wa aina hii. Ama mwanamke aliyevaa Hijabu yeye ni bibi aliyemtukufu, ni maalum kwa ajili ya mumewe, mapambo yake na uzuri wake havionekani kwa kila mtu. Pia watu wenye nyoyo chafu na dhaifu hawamuangalii, na uso wake na mapambo yake havikutani na macho yenye khiana, kwa kuwa amehifadhiwa ndani ya Hijabu. Kwa hiyo utukufu wa mwanamke huyu na mwili wake vimo ndani ya hifadhi bora, pia bibi huyu hupendwa na kupendeza mbele ya mumewe na kumfanya mume kuwa na imani na mkewe, kwa sababu ya hifadhi hiyo inayomkinga kuwa na mahusiano na watu wengine kwa njia mbaya." Baada ya maelezo yaliyotolewa na yule Muumini wa kiIslamu, bwana yule mwenye kejeli aliona haya na akaanza kumwambia yule Muumini, "Najuta kwa kukuudhi, kwani maneno yako ni ukweli mtupu, na mifano uliyonipa ni sawa kabisa naomba samahani kwa haya niliyokutamkia na pia natubia kwa Mwenyezi Mungu kwa kitendo nilichokitenda na sasa. Kabla bwana huyu hajamaliza kujieleza mkewe alimkatiza na kusema. "Naam, naapa maneno haya aliyosema bwana huyu ni sawa na mfano aliotoa ni mzuri sana, kwani kabla ya leo nilikuwa sijasikia mawaidha kama haya. Mfano huu umeniingia moyoni nami pia natubia kwa Mwenyezi Mungu."

Baadaye yule mume akarudia kukamilisha usemi wake akasema, "Na mimi sasa naiamini Hijabu na kuanzia leo mke wangu ataingia katika uwanja mtukufu kwa kuvaa Hijabu. Kamwe sikubali mke wangu atoke bila Hijabu, kwani ndiyo vazi la amani na imani. Nafsi yangu haipendi kabisa kumuona mke wangu akidhihiri mbele za watu kama kwamba yeye ni kwa ajili ya kila mtu."

Ni Lipi Lengo La Wanaopinga Hijabu?

Baada ya kuusoma Uislamu kwa undani, maadui wa Uislamu wameandaa mikakati ya kuuangamiza Uislamu na Waislamu kidogo kidogo, bila Waislamu kuigundua hali hii isipokuwa wachache. Na miongoni mwa mikakati yao ya kishetani katika kutilia mkazo kuiondoa Hijabu, wametumia na bado wanatumia kila njia za kuvutia na madai batili kutimiza lengo lao hilo. Kuna mambo mengi machafu wanayoyaeneza katika jamii ya Waislamu, chini ya kiza kinene chenye ibara zinazovutia na kampeni ambazo matokeo yake ni mabaya. Kwa kutumia mbinu za kimaendeleo na utaalamu, wamefaulu kuwapotosha Waislamu, na wakasambaza uovu mwingi. Kwa madai hayo hayo ya maendeleo na kupigania uhuru na haki za binadamu, uchafu wao umeenea ndani ya jamii zetu za kiislamu. Kwa hakika wamefaulu kuzinyang'anya jamii zetu maumbile ya kuwa na haya na heshima. Ibara hizi zimewahadaa Waislamu wengi, wake kwa waume.

Masikini Waislamu hawa wamekuwa wafuasi wa itikadi hizi zenye sumu kali inayovuja kuelekea kwenye maovu na maangamio. Wanawake wa kiislamu na mabinti wa kiislamu wanafanya upinzani hadharani dhidi ya vazi hili la kiislamu. Wametoka katika nyumba ya utukufu na imani na kuingia katika nyumba ya kiza na upotovu. Wanawake wetu na wasichana wetu wameathiriwa na mavazi ya Kiyahudi na Kikristo yatokayo kwa wapinzani wa kimagharibi na makafiri wa mashariki. Maadui na wavamizi hawa wamefanikisha kwa kiasi kikubwa lengo lao, kwa kuwa sasa hivi jamii ya kiislamu imekwisha tumbukia na kuzama katika dimbwi la matendo machafu. Jamiii ya kiislamu ambayo asili yake ni adilifu na yenye muruwa, leo imegeuka na kushika bendera ya maovu ya kila aina.

Matukio ya kubaka,8 kupora, udanganyifu, dhulma, kutoa mimba na mengineyo, yameivamia jamii yetu tukufu. Watu hawa wa Ulaya magharibi na mashariki yake, hawali wakashiba wala hawalali wakapata usingizi, ila mpaka watimize lengo lao la kutuachisha utamaduni wetu wa kiislamu.

Ni wazi kabisa kwamba watu hao wanaomtaka mwanamke wa kiislamu avue Hijabu lengo lao wanataka wamuone mwanamke huyu anafanya ufisadi kwa kumlazimisha akae uchi. Nia yao ni kumuangamiza na kuipotosha jamii kwa jumla. Kumtaka mwanamke asivae Hijabu ni kumuondolea heshima yake na uchamungu wake.

Ewe msomaji wangu, iwapo utataka kuyafahamu vizuri maneno yangu, muulize mzee yeyote katika wazee wa makamo na mababu ambao bado wanayo kumbukumbu ya hali ya mambo ilivyokuwa hapo zamani. Waulize kwa kusema, "Hivi maovu haya yaliyopo sasa hivi ya kuwavunjia heshima wanawake na kuwabaka, na watu kudhulumia, mambo haya yakulikuwepo hapo zamani kabla ya miaka ishirini au thelathini iliyopita?" Watakujibu kwa nguvu zao zote, kwa kusema, Hapana kabisa hayakuwako."

Sasa yametoka wapi mambo haya maovu na matukio ya kuhuzunisha? Watakuambia, "Hali hii imetokana na mambo mengi, miongoni mwake ni wanawake wenyewe kutembea mabarabarani bila sitara ya kisheria."

Hili ndilo jibu sahihi kwa matatizo kama haya ya ubakaji ambayo takwimu zake zinaongezeka kila siku. Iwapo utataka uhakika zaidi, waulize wakazi wa miji michache ambayo wakazi wake bado wanashikamana na sheria za kiislamu na imani zao zingali hai na uwaambie, "Hivi katika miji yenu kuna matukio maovu ya kubaka na unyang'anyi kama inavyotokea katika miji mikubwa?" Bila shaka watakujibu hapana. Sababu kubwa ya kutokuwepo maovu kwa wingi katika sehemu hizo, ni kwa kuwa jamii bado inauheshimu na kuulinda Uislamu na kanuni zake zenye hekima.

Maovu mengi zaidi yanajitokeza katika miji au sehemu ambazo zinadai kuwa zimeendelea. Miji hiyo imehusika kwa kiwango kikubwa na ongezeko la maovu ambayo yanakithiri kwa kasi ya kutisha, licha ya serikali zao kutoa adhabu kali kwa wanaohusika kila wanapobainika na kukamatwa.9

Hali hii inaonyesha wazi kwamba kanuni peke yake hazitoshelezi, wala hazinufaishi katika kuirekebisha jamii, bali kinachotakiwa ni kuing'oa mizizi ya maovu kwanza, ili maovu hayo yapate kunyauka yenyewe. Kwa kawaida kila kitu kina asili yake, na asili ya maovu yaliyozikumba jamii zetu sasa hivi, ni hizi picha za video wanazooneshwa vijana wetu, picha ambazo huwa zinaonesha hali ya maumbile ya siri, isitoshe huonesha pia matendo ya jinsiya baina ya mke na mume bila kuona aibu wala huzuni kuuchezea na kuudhalilisha uanadamu ambao ni kitu cha thamani, kutokana na kuwa na uwezo wa kutambua nini cha kufanya na nini si cha kufanya. Kitu kingine kinachochangia ni nchi zetu zinaporuhusu uingizaji wa magazeti na majarida yanayochapisha picha zinazoonesha sehemu za siri na kisha magazeti hayo na majarida yanasambazwa katika jamii. Maadam asili ya maovu bado ipo kama mifano ya picha za video na majarida tuliyoyataja hapo kabla, basi maovu na matukio machafu yataendelea kutokea siku hadi siku, na kamwe hayataondoka kwa kutegemea kanuni hizi za kidunia.

Ni Yupi Mwanamke Bora

Sasa napenda kutoa mifano miwili ya wanawake wawili ambao kila mmoja anao mwelekeo wake na mwenendo tofauti na mwenzake, lakini wote wanaishi katika jamii moja. Wa kwanza ni yule mwanamke mwenye kuvaa Hijabu ambayo ni sitara ya imani na ni vazi la kiislamu, tena ni vazi la heshima na humpa utukufu mvaji.

Kwa kuvaa Hijabu, mwanamke huyu atakuwa amepata radhi za Mola wake na kupata utukufu wa watu wa peponi. Kwa vazi hili mwanamke huyu huvutia mvuto wa ucha Mungu na heshima. Pia dalili za utulivu hujitokeza kwa mwanamke huyu na dhana njema kwake hutawala fikra za kila amuonaye. Amtazamapo mwenye kumtazama, huwa ni shida kutambua, je, mwanamke huyu ni msichana au ni mtu mzima? Sura yake ikoje nzuri au la? Hutatizika wanaomuangalia. Matokeo yake watu humuangalia kwa jicho la heshima, hakuna awezaye kumkabili kwa maneno chafu au maudhi, kwani anafahamu wazi kwamba mwanamke huyo ameshikamana na dini yake na anaheshimu utu wake. Isitoshe mwanamke kama huyu huwa amejitenga na matendo ya aibu na kujiepusha na wanawake wasio na sitara, na kwa ajili hiyo hayuko tayari kuidhalilisha nafsi yake.

Huo ndiyo mfano wa mwanamke mmoja na namna alivyojiweka katika jamii yake. Kwa upande wa yule mwanamke wa pili, ni yule asiyejali kujisitiri uso wake amevua vazi la la stara, hana aibu wala haya. Kwa maana hiyo ameing'oa imani yake, kwa sababu Mtume anasema: "Mtu kuwa na haya ni sehemu ya imani, na mtu asiye na haya hana imani." Kwa mwenendo wake mwanamke huyu, huwa ni mpinzani mkubwa wa muongozo wa Qur'an na huwa anajidhalilisha kwa kuonesha mapambo yakem, kama walivyokuwa wakionesha mapambo yao wanawake wa zama za kijahiliya kabla ya kuja Uislamu. Isitoshe kwa mwanamke huyu, hali aliyo nayo huwa amejifananisha na wanawake wa Kiyahudi na Kikristo, na huwa yuko mbali na heshima yake na utu wake. Kutokana na kuudhihirisha mwili wake na uso wke na mikono yake, pia kifua chake na sehemu nyingine katika maumbile ya kike. Watu waovu na wenye tamaa huyaona wazi wazi maumbile yake na hapo tayari anakuwa mfano wa bidhaa zilizotandazwa sokoni, kwani kila mtu ana uhuru wa kuziangalia bila mipaka.

Matokeo ya uovu wa mwanamke huyu, ni kupata usumbufu toka kwa wahuni ambapo hatimaye wanaweza kumtendea matendo machafu yanayoweza kumharibia tohara yake. Na iwapo itafikia hali ya kuharibiwa tohara yake, basi atakuwa amepoteza heshima yake na utu wake katika jamii. Hii ni kwa sababu ameacha kuulinda mwili wake ndani ya vazi la kisheria.

Baada ya kuwa mmefahamu namna za wanawake hawa wawili sasa tuwe pamoja kaitka kulinganisha hali zao kati yao na tujiulize masuali yafuatayo.
1.Je ni yupi mwanamke bora baina yao?
2.Yupi kati yao ni mtulivu na anayevutia,
3.Mwenye kujilinda au yule anayeuacha wazi mwili wake?
4.Ni yupi mwenye kuheshimika kati yao, mwenye Hijabu au yule asiye na Hijabu?

Bila shaka, mwanamke mwenye Hijabu na ucha Mungu ni bora na ni mtukufu tena ni mwenye thamani kuliko yule mwingine.

Kipindupindu Ndani Ya Jamii

Miongoni mwa maradhi yanayoua haraka ni kipindupindu kwa mujibu wa taarifa ambazo huwa zinatolewa baada ya maradhi hayo kuingia katika kijiji au mji. Kila yanapodhihiri maradhi haya, hutangazwa hali ya hatari katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kuwekwa karantini. Kama ilivyo katika kuzuia kipindupindu kisienee katika mji au kijiji, na fisadi nyingine ni hivyo hivyo. Sasa basi mtazamo wa Uislamu katika kuitazama jamii ni mtazamo wenye hekima kubwa, na ni mtazamo ambao lengo lake ni kujenga jamii nzuri na safi isiyokuwa na maovu ndani yake. Miongoni mwa mambo yanayoweza kudhibiti amani na ubora wa jamii ni mavazi. Siyo kweli kwamba kila vazi linaweza kukidhi haja hii, bali Hijabu pekee ndiyo jawabu, kwa sharti ya kuwa mvaaji aivae kwa kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu na siyo kinyume chake.10

Hijabu humlinda mwanamke kutokana na ufasiki na inamzuia kukhalifu maumbile yake aliyopangiwa kuishi ndani yake. Kwa kanuni hii ya Hijabu, Uislamu unakuwa umeisalimisha jamii na kuilinda isije ikajikuta imeteleza na kuvamiwa na maovu. Hali halisi inayojitokeza katika malengo ya msingi kuhusu kanuni hii ya Hijabu, ni kuitakasa jamii na kuisafisha, pindi wanawake watakapofuata sheria ya kuvaa Hijabu. Kinyume chake haitawezekana kabisa kudai kwamba jamii yetu ni safi, wakati wanawake zetu wanatembea bila kujali ni nguo gani wamevaa, kwa kuwa suala la mavazi kwa wanawake linataka litazamwe kwa mapana na marefu isiwe mradi kuvaa tu. Ni mara ngapi tunashuhudia mambo ya aibu na ya kuhuzunisha wanafanyiwa wanawake? Hivyo uchafu unasambaa haraka na kuleta madhara kwa wingi, kama kipindupindu kilichoingia mjini au kijijini. Na kwa ajili hiyo karantini inahitajika kuwekwa na kufuatwa kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu.

Uislamu kwa upande wake unataka kukata na kung'oa mizizi ya fitina na maovu kwa kutumia njia mbali mbali ikiwemo kusisitiza vazi la Hijabu. Pia Uislamu kwa nafsi yake unapinga kwa nguvu uovu na kila jambo linalokuwa ni sababu ya kueneza uchafu ndani ya jamii, miongoni mwa sababu hizo ni mwanamke kutokuwa na Hijabu ambayo ni vazi la kisheria.

Kukosekana Sitara Kunaleta Maovu.

Miongoni mwa maovu na athari mbaya katika jamii, ni wanawake kuacha kuisitiri miili yao ipasavyo, kitu ambacho kimesababisha vijana wetu wa kiume kuteleza na kujikuta wanafanya mambo machafu bila kukusudia. Imam Ali ibn Musa Ar-ridha anasema, "…….Imeharamishwa kuangalia nywele za wanawake, kwani katika kuziangalia nywele hizo kunasababisha kuamsha hisia za wanaume ambazo huwafanya waingie katika maovu na mambo yasiyo halali na yasiyopendeza."11 Hapana shaka kwamba, mwanamke anayetoka nyumbani mwake na kwenda sokoni bila kujali ni vazi gani alilovaa, hajali kama limemsitiri vizuri au hapana, ni wazi kabisa huko njiani ataonekana kwa watu wa aina mbali mbali wakiwemo vijana ambao ndiyo kwanza wanaingia katika rika la ujana na nafsi zao bado hazijaweza kujimiliki kuhusu suala la kijinsiya. Hali kama hii ni lazima itaamsha hisia za kimaumbile za vijana hao kutokana na jinsi mwanamke huyo atakavyokuwa amevaa na umbile lake linavyoonekana kwa jumla pindi atakapopita mbele yao. Hisia hizi za kimaumbile ni lazima ziamke kwa kuwa ndivyo ilivyo hali halisi. Kwa hali hii basi nafsi za vijana hawa kwa tabia ya maumbile ya mwanaadamu huanza kuhangaika kutafuta njia za kuyatosheleza maumbile yao.

Suala la kujiuliza hapa ni je, vijana hawa watafanya nini? Ikiwa wao sio watu walioshikamana na mafunzo ya dini wala hawafuati miongozo ya kiislamu, basi watajaribu kutosheleza hamu zao kwa njia ya siri ambayo ni kujitoa manii jambo ambalo ni hasara na aibu. Ama wengine hufanya baya zaidi ambalo ni kinyume cha utaratibu aliotuwekea Mwenyezi Mungu, hawa hufanya liwati. Kundi jingine wao huamua kuzini na katika huko kuzini huwa wanatumia kila njia kufanikisha azma yao hiyo, ikiwa ni kwa hila au hata kwa nguvu ambayo ni kubaka wanawake mitaani. Matokeo ya ubakaji ni kuvunja heshima za watu na kuwadhalilisha wanawake.

Pamoja na matendo haya kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu, pia yanasababisha maradhi hatari na vifo vya ghafla.12

Inakadiriwa kwamba idadi ya hospitali zinazo shughulikia maradhi ya uasherati peke yake inafikia hospitali mia sita hamsini.

Hesabu hii ni kwa nchi ya Marekani peke yake. Chanzo cha balaa lote hili ni kwa wale wanawake wasiojali kutenganisha maumbile yao na ya wanaume mpaka wakawa wanaona miili yao haistahiki kulindwa na kupewa hadhi ya pekee. Lakini kila mwanamke asiyezingatia suala la mavazi kisheria ni lazima atambue kwamba, yeye ni mshiriki mkubwa anayesababisha madhambi na misiba hii, na anayo sehemu yake ya adhabu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Yote yaliyotajwa hapa sasa hivi, yanatokana na vijana ambao wao siyo watu wa dini wala hawashikamani na Uislamu. Kwa upande wa pili inawezekana vijana hao wakawa ni watu wa dini na wanaambatana na mafunzo ya kiislamu na sheria zake, basi vijana hao huzuia hisia zao zisivuke mipaka ya Mwenyezi Mungu na hupambana na matamanio ya nafsi zao na kumlaani shetani asije akawahadaa. Vijana hawa huvumilia kero ya maumbile na kubeba mzigo mzito ambao hawakutarajia kuubeba. Kwa mara nyingine tena mwanamke au wanawake wasiojali sheria ya mavazi kama Mwenyezi Mungu alivyoamrisha, wanabeba uzito wa taabu na maudhi yanayowapata watu hawa wa dini.

Kutokuvaa Hijabu Na Madhambi Ya Ubakaji

Miongoni mwa athari mbaya zinazosababishwa na tabia ya wanawake ya kutokuvaa Hijabu ni yale makosa ya jinai ya kuwabaka wanawake na kuwaingilia kwa nguvu bila hiyari yao. Ni jambo lisilofichikana pindi mwanamke anapouacha wazi mwili wake na mapambo yake, hali hiyo huamsha hisia za kijinsia kwa wanaume. Kwa hakika ni juu ya mwanamke mwenyewe kuulinda mwili wake, mapambo yake na utu wake kutokana na hatari hiyo inayoweza kumkabili.

Hapana shaka kwamba, macho ya vijana wasiokuwa na msimamo wa dini, pindi wanpomuangalia mwanamke ni sawa na macho ya mbwa mwitu anapomuangalia kondoo. Pia tunaweza kuyalinganisha macho hayo na macho ya paka anapomuona panya, au tuseme yanafanana na macho ya mnyama mkali wa porini, anapomuona mnyama mwingine au kitu kimngine ambacho kinamfaa kwa chakula. Siyo ajabu kabisa kwa mazingira kama haya kumkuta mwanamke amenasa ndani ya mtego aliojitegea mwenyewe kutokana na tabia ya kujitangaza mbele ya watu waovu.

Tabia hii ya ubakaji mara nyingi inatokea katika sura ya kutisha huko kwenye nchi za magharibi ambazo zimeporomoka mno katika suala zima la maadili. Katika ripoti moja kati ya matoleo ya gazeti la The Gurdian la nchini Uingereza iliandikwa kwamba: "Takwimu za polisi zinaonesha kuwa, makosa ya jinai ya kubaka yanaongezeka mwaka hadi mwaka. Katika mji wa Washington peke yake kila baada ya dakika kumi na tano huwa kuna tukio la kubaka, na katika mji mkuu wa Uingereza (London) yalitokea matukio 2095 ya kubaka wanawake na wasichana mnamo mwaka wa 1970 peke yake."13 Haya ni machache katika mengi ambayo tungeweza kukuorodheshea.

Na miongoni mwa matukio ya kubaka kutokana na wanawake kutokujali kujisitiri kwa mujibu wa sheria na maumbile yao, mimi nimesikia kwamba, kuna rais fulani anayeongoza nchi moja miongoni mwa nchi za Kiarabu, yeye hufanya ziara za mara kwa mara kuvitembelea vyuo vikuu akitafuta mabinti katika vyuo hivyo na kuwachagua wale wazuri na wanaopendeza. Kisha humtoa nje ya msitari binti anayemuona kuwa atamfaa. Baada ya muda mfupi askari wa usalama wa taifa huwa wanakwenda nyumbani kwa binti huyo na kumweleza baba yake kwamba rais wa jamhuri anamtaka binti yake akakeshe naye katika usiku wa siku hiyo!!

Hali kama hii husababisha msiba mkubwa kwa baba, mama, binti huyu na hata familia nzima huingia ndani ya mtihani huu. Msiba huu huwagubika watu hawa kwa sababu wanafahamu wazi kwamba rais huyu ataishi na binti yao kwa usiku huo mmoja tu!! Sasa je, watu hawa watalikataa ombi la rais? Na je, inawezekana kwa watu hawa kuuepuka unyanyasaji unaowasubiri kutoka kwa rais wao? Basi je, matokeo ya jambo hili yatakuwaje? Hapana jambo jingine litakalotokea hapo isipokuwa msichana itamlazimu kuuendea uovu kwa miguu yake mwenyewe. Ataifuata fedheha na aibu hiyo kubwa bila kupenda, na kisha atarudi nyumbani hali ya kuwa amekwishapata hasara ya kuvunjika kwa heshima yake na utu wake pia kagubikwa na kiza la ulimwengu machoni mwake.

Ewe msomaji mpendwa, hapana shaka kwamba watu wanaosoma au kusikia unyanyasaji huu, utawaona wanamlaani na kumshtumu rais huyu muovu. Lakini hebu tufikiri kidogo juu ya misingi inayosababisha mateso haya na tujiulize swali lifuatalo: Je! Ni nani mwenye makosa? Hivi kweli mwenye makosa siyo yule baba ambaye toka hapo mwanzo alimruhusu binti yake atoke ndani hali ya kuwa maungo yake yako wazi na uzuri wake unaonekana kwa kila mtu? Lau binti huyo angekuwa ni mwenye kujisitiri, hivi unadhani yule rais mpumbavu angelimtamani na kumfanya kuwa kiwindo chake? Ni baba ndiyo mwenye kustahili lawama tangu ile siku aliponunua television (ambayo ni adui mkubwa muovu aliyemo ndani) ili kuistarehesha familia yake kwa kuangalia vipndi viitwavyo kuwa ni vya watu walioendelea!! Baba huyo huyo ndiyo mwenye lawama siku zile alipokuwa akiichukua familia yake kwa ajili ya kwenda sinema kuangalia filamu za watu walio uchi. Na mama pia anastahili lawama… Je ! Siyo yeye yule ambaye alikuwa akizifumua nywele za binti yake na kumpamba utadhani siku hiyo ndiyo siku ya harusi yake na kisha akamwacha kwenda shuleni akiwa katika mazingira kama hayo?

Ni huyo mama aliyekuwa akimchagulia binti yake asiyejuwa kitu mavazi mafupi yanayobana mwilini ambayo hayamsitiri inavyopasa? Binti naye anapaswa kulaumiwa kutokana na matokeo hayo yenye kiza kinene cha majonzi kwa kuwa ni yeye mwenyewe ndiye aliyechagua tabia ya kuuweka wazi mwili wake, na pia akachagua kupita njia ngumu iliyojaa miba na mawe. Naam, watu hawa ndiyo tabaka la mwanzo la kulaumiwa, na baada ya hapo ndio mnapaswa kumlaani rais yule!!

Kutokuvaa Hijabu Na Madhambi Ya Utoaji Mimba

Ni vema pia kutaja mambo mengine ambayo yanaletwa na makosa ya jamii inapokuwa imepuuza na kuacha Hijabu. Yapo mengi, lakini yanayotajwa ndani ya kijitabu hiki ndiyo ya msingi. Suala la kutoa au kuharibu mimba ni miongoni mwa athari mbaya ziletwazo na ukosefu wa sitara bora ya kisheria kwa wanawake. Ni mara nyingi inatokea kwa wanawake wasio na Hijabu kuvunjiwa heshima zao na utu wao.

Mwanamke asiyekuwa na sitara bora pindi anapodhihiri mbele ya vijana wenye dhiki ya kukidhi haja zao za kijinsia, hapana shaka vijana hao hushindwa kuyazuwia matamanio yao na hapo ndipo huamua kumbaka. Hapo mwanamke huwa anajikuta ametumbukia mikononi mwao bila hiyari, na huenda ikatokea bahati mbaya mwanamke huyo anaweza kubeba mimba haramu ambayo hakuitarajia. Kutokana na uovu huu aliofanyiwa hulazimika kuitoa au kuiharibu mimba hiyo. Leo hii katika anga la dunia yetu matukio kama haya ni mengi mno. Yako wazi kila mahali na hasa nchi za Ulaya Magharibi na zile zote zinazojaribu kuiga ustaraabu wa magharibi.

Tarehe 28 Februari mwaka 1972. jarida la An Nahaar la Lebanon lilichapisha katika ukurasa wake wa makala maalum kama ifuatavyo. "Katika mji wa London idadi ya utoaji mimba imeongezeka kutoka wanawake hamsini elfu mwaka 1969 hadi kufikia wanawake themanini na tatu elfu mwaka 1970 na idadi inayokaribia laki mbili mwaka 1971. Na huko Ufaransa hali hii imeongezeka na kufikia kutolewa mimba arobaini na sita hadi mia moja arobaini na tatu katika kila mimba mia mbili wanazobeba wanawake kwa mwaka. Ama huko Urusi, kuna mimba zipatazo milioni sita zinazotolewa kila mwaka.14

Kwa hakika takwimu na taarifa hizi zinatisha, na yote haya ni matokeo ya tabia ya wanawake kuyaonesha wazi maumbile yao na uzuri wao mbele ya kila mtu. Hakuna njia ya kuzuwia madhambi haya isipokuwa vazi la Hijabu iwapo litavaliwa kwa mujibu wa sheria na kutunza mipaka ya dini.

Kutokuvaa Hijabu Na Uharibifu Wa Ndoa

Tangu utamaduni wa kutovaa Hijabu ulipokuwa umeenea baina ya wanawake, yapo matatizo mengi yamezuka katika ndoa, na idadi ya matatizo haya inaongezeka siku hadi siku.

Tatizo hili la ndoa wakati mwingine huwa mume ndiyo sababu kubwa inayochangia uharibifu wa ndoa yake. Hasa pale mume huyu anapochukua fursa ya kutoka yeye na mkewe kwenda kwenye sherehe au mahafali mbali mbali zilizo na mchanganyiko wa wanaume na wanawake au kumpeleka mkewe katika majumba ya starehe na sinema. Wakati mwingine mume huyu hupata akaleta nyumbani kwake wageni wanaume na mkewe akaja kuwapokea kwa tabasamu zuri na kupeana nao mikono na chungu nzima ya makaribisho mengine ambayo mke wa bwana huyu huwafanyia wageni wa mumewe, ikiwa ni pamoja nakuwaletea matunda na vyakula vingine mbali mbali. Yote haya yanafanyika bila ya mume huyu kukumbuka kwamba wageni hao ni wanaume na jinsi yao kimaumbile inatofautiana na maumbile ya mkewe, pia pande mbili hizi hazina uhusiano wa kisheria.

Katika kipindi cha kubakia hapo, wageni hawa huendelea kupata kila aina ya makaribisho yasiyokuwa na mipaka ya kisheria. Kutokana na hali kama hii mara ghafla mume huyu humkuta mkewe amekwishaanzisha uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa marafiki zake hao. Hapa ndipo mume huyu huzusha ugomvi na mkewe na kuwasha moto wa volkano dhidi yake, pamoja na ukweli ulio wazi kwamba, yeye ndiyo sababu iliyoleta huzuni hii kubwa na msiba ndani ya nyumba yao. Mume huyu anasahau kwamba, yeye ndiye aliyekuwa kiongozi na muandalizi wa njia ya mkewe kulifikia giza hili na dhambi hii kubwa.

Baada ya tatizo kama hili baina ya mke na mume, hapo hujitokeza moja katika mambo mawili. Ama mume huyu aendelee kubaki na mkewe huyu muovu katika hali ya maisha ya dhiki yatakayokuwa yakiumiza roho yake na kuiadhibu nafsi yake, na kutokuaminiana tena na mkewe. Au pengine aende mahakamani ili akapate kufungua madai dhidi ya mkewe na kudai fursa ya kutoa talaka. Na mara nyingi talaka ndiyo uamuzi ambao mume huuchagua ili atatue tatizo hili. Lakini uamuzi huu unakuja baada ya kutokea fedheha, aibu na unyonge mkubwa katika familia hii. Na mwisho huu mbaya huleta matokeo ya kusikitisha, kwani familia hii hubomoka na maisha mazuri ya ndoa ya wawili hawa huvunjika.

Zaidi ya hapo msiba mkubwa hubaki kwa watoto ambao huwa bado wanahitajia kuwa na mama yao. Kuishi mbali na mama, watoto hawa hukosa huruma na upole wa mama yao, pia hukosa malezi mazuri na mwelekeo mwema. Hapo ndipo mahali ambapo hujitokeza fundo la moyo kwa watoto hawa na kujihisi kuwa na upungufu katika jamii wanayoishi. Watoto hawa hubadilika taratibu katika tabia zao na hatimaye hutokea wakajiunga katika magenge au makundi yenye mielekeo mibaya na kujikuta wamo miongoni mwa wezi na majambazi.15

Mengi ya matukio ya aina hii yamekuwa yakitokea katika nchi zisizo za Kiislamu. Katika moja ya makala zake, gazeti la Kisovieti liitwalo Pravda liliandika kama ifuatavyo: "Asilimia themanini ya makosa ya uvunjaji sheria yafanywayo na vijana wenye umri wa kukaribia balehe (miaka kumi mpaka kumi na tano) yanatokana na kuvunjika kwa familia." Pia likaendelea kueleza gazeti hilo kwamba: "Katika kila matatizo tisa yanayohusu ndoa, moja katika matatizo hayo, matokeo yake huwa mume na mke kupeana talaka." Pravda likaendelea kutoa sababu za matatizo hayo kwa kusema: "Sababu za msingi zinazochangia kuleta hali hii, ni kuharibika kwa mwenendo wa jamii kutokana na ulevi wa kupindukia.16

Sasa basi, ukweli uliopo ni kwamba matokeo ya yote haya yanakuja kutokana na uovu unaosababishwa na kutokujisitiri wanawake kama sheria inavyowataka. Uislamu kwa upande wake haukuharamisha bila mantiki mavazi yasiyowafunika wanawake kwa mujibu wa sheria, isipokuwa ni kwa lengo la kuzuwia maovu haya, na pia haukufaradhisha vazi la Hijabu kwa mwanamke isipokuwa ni kwa nia ya kumuepusha mwanamke asifikwe na maovu haya na mengine mfano wa haya. Kwa hiyo Uislamu unawalazimisha wanawake kuvaa Hijabu ambalo ndilo vazi rasimi kisheria ili kuzuia kuzuka kwa maovu kama yalivyotangulia kuelezwa.

Magazeti na vyombo vingine vya khabari kila mara vinatuarifu habari mbali mbali zinazohusu matatizo ya ndoa na khiyana zinazofanyika baina ya mke na mume, na hali hii husababisha watu kupeana talaka na pengine ikasababisha kutokea mauaji. kila unapofanyika uchunguzi, Sababu za msingi zinarudi kwenye upuuzaji wa Hijabu kwa ile maana yake halisi iliyokusudiwa na Uislamu. Ni mara nyingi tunasoma magazetini au kusikia redioni kwamba mtu kamuacha mkewe na wanawe kwa ajili ya msichana asiye na Hijabu ambaye kakutana naye ofisini au katika mabustani ya mapumziko na au mahali pengine. Au ni mara ngapi tumesikia na pengine kuona mke anamuacha mume wake ili tu akaolewe na kijana aliyekutana naye sinema au pwani wakati wa kuogelea?

Kuna gazeti moja liliandika kama ifuatavyo: "Mtu mmoja alimuua rafiki yake ili amchukue mkewe ambaye alikuwa akijidhihirisha wazi mbele ya bwana huyo bila Hijabu wala aibu. Gazeti liliendelea kueleza kwamba, kuna mwanamke mwingine ambaye yeye alimuua mumewe kwa msaada wa huyo mpenzi wake na kisha wakamkatakata viungo vyake na kuvitupa ndani ya mfereji wa maji machafu. Bibi huyu alifanya madhambi haya ili tu aolewe na huyo bwana mpya." Pia kulitolewa habari na gazeti moja la Kiarabu ambalo liliandika tukio moja miongoni mwa matukio yanayosababisha ndoa za watu kuvunjika, hasa mijini ndiko kwenye matukio mengi ya aina hii. Tukio hilo kwa hakika lilikuwa la kuhuzunisha sana, na cha kuhuzunisha zaidi ni kwa kuwa lilitokea katika moja ya nchi za Kiislamu, lau lingekuwa limetokea katika nchi za magharbi, hali hii ingekuwa ni mahala pake kwa kuwa nchi hizo ndiyo vituo vya kila aina ya maovu, kama vile zinaa na uchafu mwingineo. Lakini ni vipi leo mambo haya yanatokea hata katika nchi takatifu za Kiislamu ambazo hapo kabla zilikuwa zimetakasika kutokana na uchafu huo?

Hapana shaka, hayo ni matokeo ya wanawake kuuwacha utamaduni wao wa Kiislamu katika suala la mavazi, pia mienendo ya Waislamu imebadilika na wameshawishika na utamaduni mbaya wa kimagharibi. Kutokana na kupotea kwa Waislamu na kuacha mwelekeo na utamaduni wao, sasa hivi imekuwa kazi ngumu kuyaepuka maovu na balaa hizi isipokuwa njia pekee ni kurudia utamaduni wetu kama alivyotuamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w.w).

Ewe msomaji mpendwa, hebu kaa tayari nikusimulie hicho kisa ili ujionee mwenyewe umuhimu wa Hijabu kwa maana yake kamili na pia ubaya wa kuacha Hijabu: "Naam, wanamichezo wa nchi fulani walitoa mwaliko wa kimichezo kwa mmoja wa wanamichezo mashuhuri wa nchi fulani. Kwa bahati nzuri mwanamichezo mualikwa aliukubali mualiko huo na kufanya safari kuelekea huko akifuatana na mkewe ambaye hakuwa amevaa Hijabu, na kwa sura binti huyo alikuwa kaumbika.

Walipofika uwanja wa ndege wa nchi aliyoalikwa mwanamichezo huyu na mkewe, kwa pamoja walilakiwa na wenyeji wao ambao nao ni wanamichezo. Mwanamichezo huyu mgeni alisalimiana na wenyeji wake kisha akamtambulisha mkewe kwa wenyeji hao nao wakampa mikono mkewe huyu, kitendo ambacho Uislamu umekiharamisha. Wanamichezo hawa wenyeji walionyesha furaha kubwa sana na tabasamu kwa mke wa rafiki yao kiasi kwamba mmoja wao alimtamani mke wa mgeni wao na akafikiria lau angemuoa yeye. Isitoshe alifikiria pia njia za kumuwezesha kutimiza azma yake hiyo. Mwisho wa yote alitumia kila ujanja na mbinu za kishetani za kumhadaa bibi yule na akapata fursa ya kukaa naye faragha. Hapo alimuuliza thamani ya mahari aliyopewa alipoolewa na mumewe, na bila kusita mwanamke yule alitaja thamani ile, k.m. dinari alfu moja. Bwana yule aliendelea kusema: 'Mimi nitakupa dinari elfu tatu kwa sababu uzuri wako unastahiki hivyo, siyo thamani aliyokupa mumeo ni ndogo mno na kwa kweli amekudhulumu.' Kisha akamuuliza mumeo ana kazi gani afanyayo zaidi ya michezo? Yule mama akajibu: 'Mume wangu ni karani katika wizara fulani.' Bwana yule aligutuka na kusema 'Aah!!! Hii ni dhuluma kubwa uliyofanyiwa, hivi kweli pamoja na uzuri wote ulionao unakuwa mke wa karani? Haiwezekani kabisa, wewe thamani yako ni kubwa mno. Napenda kukufahamisha kwamba, mimi ni mhandisi na ninayo shahada ya udaktari na nimemaliza Chuo Kikuu, nataka kukuoa lakini kwanza mumeo huyu akuache.' Na mwisho yule bwana alimuhadaa mke wa rafiki yao na wakaafikiana afanye kila hila adai talaka toka kwa mumewe naye atamuowa. Yote haya wakati yanafanyika masikini mume yule hana habari anandelea na michezo.

Ziyara hiyo ilipokwisha bwana yule na mkewe wakarudi nyumbani kwao. Baada ya safari yao bwana huyu akaanza kuona mabadiliko ya tabia ndani ya nyumba yake. Tabia ya mkewe ikawa si nzuri tena, wakati hapo zamani alikuwa akiliona tabasamu la mkewe ambalo lilikuwa likimsahaulisha taabu ya kutwa nzima kazini, leo ni kinyume chake. Baadaye alimuuliza mkewe sababu ya mabadiliko haya. Mke akajibu, 'Wewe umenidanganya.' Mume akasema, 'Nimekudanganya nini?' Mke akasema, 'Umenioa kwa mahari ndogo ambayo mimi sikustahiki, yuko mtu ambaye anaweza kunioa kwa mahari inayonistahiki na sasa nipe talaka yangu.' Mume huyu akili zilimruka baada ya kusikia majibu ya mkewe. Alipigwa na butwaa la majonzi ambalo yeye ndiye aliyeliandaa siku aliposafiri na mkewe asiye na sitara na kumtambulisha kwa watu wasio maharimu wake. Hata hivyo bwana huyu alijaribu kumpa rai mkewe abadili uamuzi wake, lakini jitihada zake zilishindikana na baadaye akamwacha mkewe kwa uchungu mkubwa hali akiwa bado anampenda. Na yule bibi baada tu ya kuachwa, alisafiri hadi kwa yule bwana aliyemuhadaa akiwa na ushahidi wa talaka mkononi ili akatimize lengo lake la kuolewa upya."

Fikiria ewe msomaji, hili ni tukio katika matukio mengi yanayoharibu ndoa za watu. Hebu tafuta sababu yake, hutapata isipokuwa ni kwa sababu bibi yule alikuwa hakusitiriwa Kiislamu, na lau angekuwa kavaa Hijabu inayositiri maungo yake na uzuri wake, je bibi huyu angetumbukia katika mtego huu? Je, mume huyu naye angeingia katika machungu ya kumwacha mkewe hali ya kuwa bado anampenda kutokana tu uovu aliouandaa mwenyewe kwa kumwacha mkewe bila ya kuwa na sitara ya Kiislamu? Lakini taabu hii na machungu haya aliyataka mwenyewe kwa kutomlea mkewe ndani ya malezi ya Kiislamu. Na haya ndiyo malipo ya mtu anayekwenda kinyume na kanuni za Kiislamu na hukmu za Qur-an.

Wakati huo huo tunajiuliza, hivi kweli mke huyu baada ya kuachwa na yule mume wa kwanza, je ndoa ile kwa huyu mume wa pili ilidumu?

Jawabu la swali hili linasema kuwa: "Mara nyingi ndoa za aina hi huwa hazidumu isipokuwa chache tu miongoni mwa hizo, kwa sababu mume wa aina hii huwa hamuowi mwanamke kwa lengo la kujenga maisha ya ndoa kwa maana ya mke na mume, bali huwa anaowa ili tu atosheleze matamanio yake ya kijinsiya na kuyashibisha matamanio yake ya kinyama. Matokeo yake ni kwamba bibi yule aliachwa na kurudi kwenye mji wao hali ya kuwa ni mwenye huzuni na majonzi tele. Alipata hasara ya kumpoteza mumewe wa kwanza ambaye alikuwa akiishi naye kwa kila aina ya mapenzi na huruma.

Ewe msomaji mpendwa, hili ni tukio moja tu kati ya maelfu ya matukio ya hiyana za ndoa za watu. Lakini hebu fanya uchunguzi juu ya sababu zinazosababisha hali hii. Huwezi kupata sababu isipokuwa ni ile tabia ya wanawake kujidhihirisha na kuyaacha wazi maungo yao. Lau mwanamke yule angelikuwa na Hijabu, akausitiri uzuri wake ipasavyo, hivi kweli angenaswa katika mtego huu? Na je, lau yule mume angejikuta ameanguka ndani ya machungu yale ambayo kwa hakika yeye mwenyewe ndiye aliyeyaandaa? Hapana shaka kwamba haya ndiyo malipo ya mtu yeyote anayekwenda kinyume na kanuni za Uislamu na hukmu za Qur'an.

Nafasi Ya Sinema Na Picha Za Video Katika Uharibifu Wa Jamii.

Sinema na picha za video zinachangia kwa kiwango kikubwa katika kuharibu mwelekeo sahihi na wa kweli kwa vijana kutokana na kuonesha filamu zinazohusu mambo ambayo ni ya siri baina ya mke na mume. Isitoshe sinema hizi huonesha maumbile ya shemu hizi mbili za siri wazi wazi kiasi kwamba, hupanda mbegu mbaya kifikra kati ya wasichana na wavulana. Si hivyo tu bali sinema hizi zinawaondolea vijana wetu aibu machoni mwao na kuwapokonya imani, kisha kuwaingiza kwenye matendo maovu na machafu ambayo yanawafanya wasahau utamaduni wao wa Kiislamu na kuwafanya waige wanayoyaona humo.

Ni mara nyingi sinema na picha za video zimekuwa zikitumiwa kupotosha jamii zetu, kwa kuonesha miili iliyo uchi ya wanawake.

Wacheza sinema huthubutu kudhihiri mbele ya watazamaji kwa kitendo ambacho kwa kweli ni aibu na ni fedheha kwa mwanadamu kukitenda hadharani, na hiyo ni tabia ya kinyama kabisa. Kwa hali hiyo basi, sinema zinatangaza uchafu huu wazi wazi na kuupigia kampeni huu kama kwamba ni kitendo kizuri. Mwenyezi Mungu anajua sana idadi ya maovu haya na matukio yanayotokea kutokana na jamii zetu kuendelea kuoneshwa filamu hizi chafu. Katika kuonesha madhara ya filamu hizi, kuna kijana mmoja wa kiume alikwenda kuangalia filamu zinazohusu mapenzi kati ya mume na mke. Baada ya kuangalia onesho hilo ambalo liliyateka mawazo yake na alirudi nyumbani kwao haraka sana. Alipofika tu alimkamata dada yake aliyekuwa kalala na kumtenda kitendo kichafu huku akiigiza namna ya kitendo hicho kama alivyoona katika filamu. Kitendo hiki kilisababisha maumivu makali kwa nduguye huyu aliyekuwa mdogo kwa umri, maumivu ambayo baadaye yalisababisha kifo cha msichana huyu.17

Bila shaka ndugu msomaji kwa mfano huu mmoja tu, unaona ni jinsi gani sinema zimekuwa ni nyenzo kubwa ya kueneza uchafu ndani ya jamii zetu. Kwa hiyo basi, sinema hizi ni vituo vikubwa wanavyovitumia wakoloni wa magharibi katika kuwavua Hijabu mabinti zetu na hatimaye kuwasukumiza kwenye shimo la maovu. Vile vile vituo wanavyotumia kugeuza vijana wetu kuwa watumwa wa matamanio yanayohusu mambo ya jinsiya na kuwafanya kuwa wasomi wa maraha na upuuzi huo. Sasa hivi imefikia mahali ambapo vijana wetu hakuna wanachokiwaza isipokuwa starehe tu, hawafikirii tena suala la maendeleo au utalaamu wa aina mbali mbali.

Hizi ni siasa za mataifa hayo makubwa, na lengo lao ni kuona vijana wetu na mataifa yetu hayajikwamui kiuchumi wala kisiasa, ili maendeleo ya viwanda, uchumi na elimu viendelee kuwa chini ya milki yao. Kamwe hawataridhika mpaka watuone sisi Waislammu tunabakia katika unyonge na udhalili, tukiendelea kuwategemea wao kwa kila mambo makubwa na hata madogo, na wao waendelee kuwa watawala wetu. Kwa hakika wametunyooshea panga zao mbele ya nyuso zetu na wametufanya kuwa ni vinyago vyao na wanatuchezea na kututumia namna wapendavyo.

Mpaka hapa mimi nauona umuhimu wa kuelekeza tena usemi wangu kwa Waislamu wote wanaohisi wajibu na jukumu katika dini. Mimi nawaambia kwamba, "Zipigeni vita sana sana hizi sinema za X18 na wawakemee watu wasiziangalie. Si hivyo tu bali wanapaswa kuwatahadharisha watu, kwani kujiingiza katika mambo hayo licha ya kuwa ni kumuasi Mwenyezi Mungu, bali hali hii inatumikia maslahi ya maadui wa Uislamu na kuharibu mwenendo wa vijana wa Kiislamu kwa kutumia kigezo cha utaalamu na maendeleo.

Madhara Ya Kuchanganyika Wanaume Na Wanawake.

Mchanganyiko unaokusudiwa hapa ni ule wa kukaa pamoja wanaume na wanawake wakawa wanatazamana ana kwa ana bila kuwepo kizuizi baina yao kitakacho tenganisha pande mbili hizi.

Kutokana na maumbile ya wanaadamu yalivyo, sheria ya KiIslamu haikubaliani na kitendo hiki cha kuchanganyika wanawake na wanaume, na hapana shaka kwamba Mwenyezi Mungu anachukizwa na jambo hili. Kwa nini basi jambo hili liwe baya?

1. Ni kuvunja moja katika sheria za Kiislamu (Hijabu) na ni kukaribisha maovu katika jamii.

2. Jambo hili huandaa na kurahisisha njia za kupatikana mahusiano ya kijinsiya baina ya pande mbili hizi kinyume na utaratibu uliowekwa kisheria.

3. Jambo hili huwa ndiyo chanzo na sababu ya kuharibu familia na kuzitenganisha na ni kivutio kikubwa cha maovu ndani ya jamii.

4. Jambo hili linasababisha misiba na majonzi, pia linaleta uharibifu mkubwa kati ya pande mbili husika.

Kwa hiyo mchanganyiko kati ya wanaume na wanawake ni kirusi chenye maradhi hatari yanayotishia usalama na mwenendo wa familia, kiasi kwamba tunaweza kuyafananisha na maradhi ya kansa ambayo mgonjwa huwa hapati nafuu isipokuwa kwa kuikata shemu iliyopatwa na ugonjwa huo na kukiondoa kiini cha ugonjwa. Katika nchi au jamii zilizoruhusu mchanganyiko huu, hapana shaka kwamba zimechangia sehemu kubwa ya ongezeko la maovu na kufikia idadi inayotisha hasa katika mashule na vyuo vikuu ambako wasichana na wavulana wanachangaywa pamoja utadhani ni viumbe wenye jinsi ya moja. Matokeo ya mchanganyiko huu ni kugeuka kwa mashule haya na vyuo hivi kuwa vituo vya mafunzo ya uhuni na mambo machafu ambapo lengo lake lilikuwa ni kupafanya kuwa mahali pa kujifunza elimu. Yote haya yanakuja kwa sababu ya kukosekana kwa sitara au kizuwizi cha kuzitenganisha jinsiya hizi mbili.

Katika ripoti moja iliyotolewa na Jaji mmoja wa Kimarekani anasema: "Asilimia 45% ya wasichana wanaosoma katika shule za mchanganyiko hupoteza bikra zao kabla ya kutoka shuleni, na asilimia hii huzidi kadri wasichana wanavyoendelea katika masomo ya juu." Huko Uingereza wasichana wamekuwa wakiandaliwa kutembea na vidonge vya kuzuwiya mimba, na kwamba asilimia 80% ya wasichana hutembea na vidonge hivyo katika mikoba yao. Hii ni dalili ya wazi inayotuonesha kwamba, wasichana hao huwa wako tayari wakati wowote ule kutenda kitendo kichafu kwa kuwa kinga wanayo. Wasichana hawa wanayafanya haya kukwepa matokeo mazito yanayoweza kuwakuta ndani ya uchafu huo wanaoutenda19. Lakini je hivi kweli ni sahihi kumuacha msichana akawa katika mazingira kama haya ndani ya jamii hasa ya Kiislamu?

Baada ya maelezo haya bila shaka ina dhihiri wazi hekima kubwa iliyomo katika Uislamu katika kupiga marufuku michanganyiko baina ya wanaume na wanawake. Hapana shaka kabisa kwamba, Uislamu lengo lake ni kutaka kuiepusha jamii kutokana na hatari tulizozitaja hapo kabla. Ndiyo maana umeharamisha mchanganyiko kati ya wanaume na wanawake katika sehemu zote, kama vile mashuleni, vyuoni, katika sehemu za sherehe, na kwa ujumla popote katika jamii mchanganyiko kati ya wanaume na wanawake hauruhusiwi.

Yote haya makusudio ni kuihifadhi jamii kutokana na maovu yanayozaliwa na michanganyiko. Na ama hali ya mikusanyiko ya wanaume na wanawake tunayoiona katika msimu wa Hija na katika maeneo matakatifu na pia ndani ya kumbi za Huseiniyyah, mikusanyiko kama hiyo haikuharamishwa hasa kwa kuwa wanawake wanaohudhuria ndani ya maeneo hayo huwa wako katika hali ya kujisitri kama sheria inavyowataka wajisitri.

Uislamu Siyo Dini Ya Nadharia.

Mara nyingi tunasoma katika baadhi ya magazeti kwamba, baadhi ya watu waliohadaika na wasiojuwa chochote kuhusu Uislamu, eti wanajaribu kutoa fikra zao katika kukosoa baadhi ya kanuni za sheria ya Kiislamu. Miongoni mwa kanuni ambazo wamekuwa wakijaribu kuzikosoa kwa kutumia kalamu zao ni hili vazi la Hijabu. Waandikapo husema: "Mimi sioni umuhimu wa Hijabu, kwani Hijabu katika maoni yangu sio lazima kwa kuwa inarudisha nyuma maendeleo." Au hupata wakasema kuwa: "Kuna ubaya gani wanaume na wanawake kuchanganyika pamoja?" Na mengine mengi wanasema lakini kifupi ni hayo. Sisi tunawajibika kuwaambia watu hawa na wengine mfano wa hao kwamba: "Ninyi ni kina nani? Ninyi ni kina nani hasa mpaka mnathubutu kutoa maoni yenu dhidi ya desturi na mila ya Mbinguni? Na mna utukufu gani mbele ya maamuzi ya MwenyeziMungu na sheria nzima ya Kiislamu? Na je Uislamu ni dini ya fikra za kinadharia mpaka mumediriki kuusemea kwamba mimi naona kadhaa, au mtazamo wangu katika sheria ya Kiislamu naona hivi au vile.? Kisha nawauliza hawa wanaosema maneno haya: "Je, ninyi kweli ni Waislamu? Ikiwa wao ni Waislamu wanawajibika kuwa watiifu katika maamrisho ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake, pia washikamane na sheria za Kiislamu ambazo miongoni mwake ni Hijabu. Na kama ninyi siyo Waislamu basi, hamna haki ya kuingilia mambo ya Kiislamu, wala hamna haki ya kutoa maoni yenu potofu mbele ya Umma wa Kiislamu.

Mpaka hapa ndugu msomaji nashangazwa na ujeuri wa watu hawa dhidi ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na ni kwa misingi gani viumbe hawa dhaifu wamejasirika na kufikia kiasi cha kukosoa hukmu na kanuni za Mwenyezi Mungu? Je wanasahau kwamba Mwenyezi Mungu anasema katika Sura Al-Maidah katika

وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنْزَلَ اللَّهُ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ

Aya tatu mfululizo: "Na wale wasiyohukumu ( kwa sheria) aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu basi watu hao ni makafiri, madhalimu, mafasiki.20

Watu hawa mbele ya Mwenyezi Mungu watabeba mzigo mzito kwa makosa yao ya kuhamasisha watu kuvunja amri za Mwenyezi Mungu na kutenda machafu yaliyo katazwa. Malipo (adhabu) yao pia ni mazito kutokana na maneno yao hayo, kwa adhabu kali watakayoadhibiwa kutokana na wao kuunga mkono maasi na kuyatia nguvu yatendwe.

Mimi naamini kuwa, watu hawa hawasemi kutoka katika nafsi zao, bali wao wanatumwa na maadui wa Uislamu wanaoupiga vita Uislamu kupitia nyuma ya pazia. Lengo lao ni kuiangamiza maana nzima ya Uiislamu, na kisha kuwapotosha wasichana na wavulana wa Kiislamu. Jambo la kusikitisha na kuhuzunisha ni kwamba, kauli kama hizi zimekuwa zikirudiwa mara kwa mara na katika nyakati tofauti, ima ndani ya magazeti na majarida na au katika mikutano mbali mbali. Kuna lugha nyingi zinazotumika katika kampeni hii ikiwemo lugha ya Kiarabu ambayo inawaunganisha Waislamu wa dunia nzima kama lugha ya dini yao.

Yote haya ndugu Waislamu, ni majaribio ya makusudi kabisa yenye lengo la kuivuruga na kuipoteza jamii takatifu ya Kiislamu. Kinachotakiwa kwa Waislamu wenye uchungu na dini yao ni kunyanyuka na kuyapinga magazeti haya kwa kuwa yenyewe ndiyo sauti ya vita vya kuutokomeza Uislamu na Waislamu. Kwa hakika wajibu wa kisheria unamtaka kila Mwislamu kupambana na majaribio haya hatari kwa uwezo wake wote kinadharia na kivitendo, hadi lengo la maadui hawa lisitimizwe katika nchi zetu tukufu za Kiislamu na jamii za Kiislamu popote zilipo duniani.

Kadhalika kukabiliana na maadui hawa dhidi ya njama zao za kutaka kugeuza nchi zetu kuwa ni mapori ya wanyama kufuatia mila zao wanazokusudia kuturithisha.Watu hawa madhalimu, katika nchi zao wamebadilika kutoka katika mila ya wanaadamu na wamekuwa na tabia za wanyama, kiasi kwamba mwanamke na mwanaume wanakidhi matamanio yao mabarabarani kama wafanyavyo wanyama bila kuwa na hisiya zozote za kuona haya wala kuogopa kwamba wao ni viumbe teule na watakatifu kwa kuumbwa kwao kama wanaadamu.

Vipi Wamefaulu Kutupotosha ?

Sasa tuangalie namna gani watu hawa wamefanikiwa kutupotosha, kwa kuwavua binti zetu na wake zetu mavazi ya Kiislamu. Pia ni kwa vipi wamefaulu kututeka kwa kupitia anuani ya kutetea uhuru wa mwanamke. Ili kupata ufumbuzi wa suala hili hatuna budi kufanya ziyara ya uchunguzi katika nchi za magharibi na kuiangalia jamii yao, na ni vema pia kufuatilia magazeti yao na majarida ili tuyaone mazingira mabaya wanayoishi wanawake wasio na Hijabu huko kwao. Kwa watu wa magharibi mambo hayaishii kwenye kukosa Hijabu na kutembea kichwa wazi na miundi nje basi. Bali hali yao inakwenda mbele zaidi kiasi kwamba kifua nacho huwa wazi, na wanawake hao kadhalika huvaa nguo nyepesi inayodhihirisha rangi ya mwili hadi kufikia kufanana na mtu aliye uchi kabisa.

Matokeo ya mavazi haya ni umalaya au kutekwa nyara na baadaye kubebeshwa mimba za haramu kisha kuingia katika kufanya mauaji pindi wanapotaka kuzitoa mimba hizo. Linalojitokeza hapa ni kudhulumu kiumbe hicho kinachotolewa kwa nguvu au muhusika kukumbwa na kifo wakati wa zoezi hilo.

Hali hii ndiyo iliyoko kwenye nchi zinazoitwa zimeendelea. Nchi zetu za Kiislamu na Waislamu kwa jumla kwa sasa wanakabiliwa na tishio la hatari hii inayokuja kwa kasi ya ajabu kutoka kwenye hizo nchi za mashariki na magharibi. Kinachotakiwa kwa Waislamu ni kuwa na tahadhari kubwa na kuikabili kasi hii ya hatari inayokuja kutoka katika nchi hizo za mashariki na magharibi. Kwa hakika wameeneza uovu wao katika jamii yetu chini ya kivuli cha utaalamu na elimu.

Idadi kubwa ya makosa ya jinai yanayotokea katika nchi zinazodaiwa kuwa zimeendelea ni mengi mno, ukilinganisha na matukio kama hayo yanayotokea katika nchi zetu za Kiislamu. Tofauti hii ni kwa sababu Uislamu unahimiza na kutilia mkazo watu wawe na maadili mema, tabia nzuri na waepukane na kila tabia chafu. Pamoja na hali hii ambayo kwa kiasi fulani inaonesha tofauti baina ya nchi za Kiislamu na hizo za magharibi, Ni lazima kwa Waislamu kuchukua tahadhari, wasihadaike na hali waliyonayo, kwani hatari inakuja na shari zinaandaliwa dhidi yao, na ni wajibu wa kila Mwislamu kuwa na tahadhari. Yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayotendeka katika nchi ambazo ndizo zinazoongoza katika kupiga vita utamaduni wa Kiislamu.

1. Nchini Uingereza peke yake karibu filamu 10 zinazohusu mambo machafu hukamilika kutengenezwa kila wiki na kutumwa nchi za nje. Kwa hali hii basi kila mwaka filamu zisizopungua 500 hutengenezwa nchini Uingereza na zote ni za kuonesha mambo ya aibu tupu na uchafu ambao jamii yetu inapotea na kuangamia kutokana na yaliyomo ndani ya filamu hizi.

2. Mwaka 1961 polisi wa Uingereza walijaribu kuwaangamiza wanawake wapatao laki moja, ambao kazi yao ilikuwa umalaya na machafu mengineyo, lakini baadaye walitangaza kushindwa kwa jaribio hilo.21

3. Mjini Rome kuna majumba yapatayo mia tano ya malaya, humo ndani mna maelfu ya wanawake ambao kazi yao ni kusubiri wanaume22

Gazeti la " The Gurdian" liliandika kwamba takwimu za polisi zinaonesha kuwa, makosa ya jinai ya kubaka yanaongezeka mwaka hadi mwaka. Katika mji wa Washington peke yake kila baada ya dakika kumi na tano huwa kuna tukio la kubaka.

Na katika mji mkuu wa Ungereza (London) yalitokea matukio 2095 ya kubaka wanawake na wasichana mwaka 1970 peke yake. Haya ni machache katika mengi ambayo tungeweza kukuorodheshea.

Ewe Dada Wa Kiislamu

Ewe dada wa kiislamu nakuomba uyafanyie mazingatio baadhi ya mafunzo ya Kiislamu ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu amekupangia ili uweze kufanikiwa duniani na akhera. Mafunzo hayo ni mafunzo mema yatakayo kupandisha daraja ya ubora, imani, na utukufu. Na sina shaka kwamba utafanikiwa na kupata kheri nyingi mno, lakini sharti uyatumie na kushikamana nayo maishani mwako.

Hijabu kabla ya mambo mengine: Hijabu pekee ndiyo kinga yako ya kuaminika ambayo itakulinda kutokana na maovu na waovu, na ni hifadhi madhubuti dhidi ya kila aina ya uchafu na wahusikao na uchafu huo.

Vazi la Hijabu ewe dada wa Kiislamu, ni ujumbe rasmi wa Mwenyezi Mungu kwako, basi mtii Mola wako na tekeleza amri yake. Hakika Hijabu ni kwa faida yako na umewekewa kwa ajili ya kulinda hadhi yako wewe mwenyewe. Dada mpendwa, Muumba wako ni mpole kwako naye anakwambia katika Qur-an,

وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ

"Na wala msioneshe mapambo yenu kama walivyokuwa wakionyesha mapambo yao wanawake wa zama za jahiliya."Q. 33:33

Na anasema tena Muumba wako:

وَقُلْ لِلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ

"Wanawake wateremshe (vizuri) shungi zao hadi vifuani mwao na wala wasioneshe mapambo yao." 24:31

Maelekezo ya Mola wako ndiyo haya, ole wako ukiyapa mgongo utaangamia duniani na akhera.

Dada mpendwa, ufunguo bora wenye thamani kubwa utakaoweza kufungua milango ya dini yako, dunia yako na heshima yako umo ndani ya Hijabu, hebu jitahidi kufuata amri ya Mola wako ili uupate ufunguo huo. Pia fahamu kwamba uzuri wako, thamani yako na heshima yako vimo ndani ya Hijabu. Ole wako kama utaiacha Hijabu, basi uzuri wako na heshima yako vitaporomoka. Ningependa pia ufahamu kwamba, njia ya wewe kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kuingia peponi imo ndani ya Hijabu. Kwa hiyo radhi za Mola wako na pepo utavikosa iwapo utaitupa Hijabu. Kadhalika dada mpendwa fahamu kwamba, njia inayoelekea kwenye ghadhabu za Mwenyezi Mungu na motoni inapitia kwenye kuvua Hijabu na kutoitekeleza. Basi ole wako usijeanguka ndani ya kina kirefu cha moto wa Jahanam.

Imamu Ali (a.s.) amesema: "Mwanamke ni kama mmea mzuri wenye harufu nzuri, na wala siyo kama nyenzo." Basi ni juu yako ewe dada ujifahamu thamani yako. Usiruhusu mwili wako na mapambo yako yachezewe na kila mtu, isipokuwa mumeo tu. Katika kumsifu mwanamke mchamungu, Bwana Mtume (s.a.w.w.) anasema: "Mwanamke mchamungu ni yule anayejihifadhi na kujisitiri mbele ya wanaume wengine, lakini huuacha wazi mwili wake anapokuwa faragha na mumewe, husikiliza ni kitu gani akitakacho23 mumewe, ni mtiifu kwa mumewe, na wakikaa faragha humpa akitakacho."

Dada yangu katika Uislamu, angalia sana usije ukawa mfano wa bidhaa zilizotandazwa sokoni, au bidhaa za dukani kila mmoja huangalia na kuzikamata kamata apendavyo.24

Usitumie vifaa vya kujirembesha na manukato ila unapokuwa nyumbani mwako na nduguzo wanaokuhusu kisheria. Tahadhari tena tahadhari sana na tabia ya kujirembesha kisha ukatoka barabarani, jambo hili ni hatari unaweza ukafanyiwa maovu, pia litakusababishia ghadhabu na laana za Mwenyezi Mungu. Bwana Mtume (s.a.w.w.) amesema:"Usijifananishe na wanaume katika mavazi na mambo mengine, bali bakia katika maisha na maumbile yako ya kike." Bwana Mtume (s.a.w).w amesema: "Mwenyezi Mungu awalaani wanawake wanaojifananisha na wanaume (katika mavavi na mengineyo) na awalaani pia wanaume wanaojifananisha na wanawake."25 Ewe dada mpendwa, usipeane mkono na mwanamume asiye kuhusu, japo kuwa yeye ni miongoni mwa jamaa zako, kama watoto wa ami zako au watoto wa mjomba. Iwapo mwanaume atanyoosha mkono wake kwako mwambie: "Dini yangu na Mola wangu ananizuia kupeana nawe mkono.

Usimuogope mtu ikiwa atachukia au kukasirika kwani radhi ya Mwenyezi Mungu ni bora kuliko radhi za watu. Na kuogopa kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu ni bora kuliko kukasirikiwa na watu. Imesimuliwa ya kwamba Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume Isa (a.s.): "Ewe Isa iwapo Mimi nitakukasirikia, basi hapana radhi ya mtu yeyote itakayokunufaisha, na iwapo mimi nitakuridhia hapana ghadhabu ya mtu yeyote itakayokudhuru."26

Usione haya kuvaa Hijabu, bali shikamana nayo kila inapokuwa. Ni lazima popote pale japo iwe ni katika jamii isiyovaa Hijabu, au hata kama umo ndani ya shule au chuo ambacho wengi wao hawana Hijabu wala hawataki kuvaa. Inakupasa uwe na msimamo wa dini yako sawa sawa kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'an:

فَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ وَمَنْ تَابَ مَعَكَ وَلَا تَطْغَوْا

"Uwe imara (na msimamo) kama ulivyoamrishwa. 11:112

Mwenyezi Mungu amesema tena:

إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنْتُمْ تُوعَدُونَ

"Hakika wale waliosema Mola wetu ni Allah kisha wakawa na msimamo (katika dini yao) huteremkiwa na malaika (wakati wa kutoka roho zao na wakawaambia) msiogope wala msihuzunike na furahini kwa pepo mliyokuwa mkiahidiwa."
41:30

Usijali kelele za wapinzani, sawa sawa wakiwa ni wanawake au wanaume, bali waambie kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

قَالَ إِنْ تَسْخَرُوا مِنَّا فَإِنَّا نَسْخَرُ مِنْكُمْ كَمَا تَسْخَرُونَ

"Ikiwa ninyi mnatukejeli basi na sisi tutawakejeli kama mnavyotukejeli." Hud:38

Hapana shaka kwamba tabia ya wapinzani wa sheria za Mwenyezi Mungu siku zote imejaa kejeli na dharau dhidi ya Waumini na Watu Watakatifu. Yote hayo wanayafanya kwani wao hawana utu, na wala hawana dalili wala hoja ya kutetea upinzani na upotofu wao. Na kwa ajli hiyo basi wao hutegemea zaidi njia za kutukatisha tamaa ili tu wapate kufanikisha maovu na maasi yao. Hapana shaka kwamba njia hizi za upinzani ulioshindwa dhidi yetu, ndizo hizo hizo walizokuwa wakizitumia kupambana na Mitume wa Mwenyezi Mungu na watu wema na waumini tangu hapo zamani katika historia ya ulimwengu. Mwenyezi Mungu anasema:

وَمَا يَأْتِيهِمْ مِنْ رَسُولٍ إِلَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ

"Na hapana Mtume yeyote aliyewafikia isipokuwa wao walimfanyia kejeli." Al-Hijr: 15:11

Na anasema tena Mwenyezi Mungu:


إِنَّ الَّذِينَ أَجْرَمُوا كَانُوا مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا يَضْحَكُونَ


{29}
.
وَإِذَا مَرُّوا بِهِمْ يَتَغَامَزُونَ
"Hakika wenye kutenda maovu walikuwa wakiwacheka walioamini. Na wanapopita karibu yao wanakonyezana." 83:29-30

وَإِذَا رَأَوْهُمْ قَالُوا إِنَّ هَٰؤُلَاءِ لَضَالُّونَ

"Na pindi wanapowaona husema kuwa hakika hawa wamepotea. 83:32

Ewe dada yangu katika Uislamu, je unafahamu kwamba mwenda wazimu hujiona kuwa yeye pekee ndiye mwenye akili na wengine wote ni wenda wazimu, wakati ukweli hauko hivyo?27

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

فَالْيَوْمَ الَّذِينَ آمَنُوا مِنَ الْكُفَّارِ يَضْحَكُونَ

"Basi leo Walioamini watawacheka wale waliokufuru." 83:34

Hapana shaka kwamba, iko siku Mwenyezi Mungu na waumini watawakejeli wapinzani hawa wanaozicheza shere sheria na kanuni za Mwenyezi Mungu.

Mwenyzi Mungu anasema:

اللَّهُ مِنْهُمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

"Mwenyezi Mungu atawalipa kejeli zao na watapata adhabu kali." 9:79

Anasema Mwenyezi Mungu:

فَحَاقَ بِالَّذِينَ سَخِرُوا مِنْهُمْ مَا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ

"Yakawazunguka wale waliyofanya mzaha miongoni mwao, yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha." 6:10

Mwenyezi Mungu anasema tena:

تَلْفَحُ وُجُوهَهُمُ النَّارُ وَهُمْ فِيهَا كَالِحُونَ {104}

أَلَمْ تَكُنْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَكُنْتُمْ بِهَا تُكَذِّبُونَ {105}

قَالُوا رَبَّنَا غَلَبَتْ عَلَيْنَا شِقْوَتُنَا وَكُنَّا قَوْمًا ضَالِّينَ {106}

"Moto utababua nyuso zao nao watakuwa humo wenye kukenya (meno yao kwa adhabu). (Waambie) Je hamkusomewawa Aya zangu na ninyi mkazipinga? Watasema: Mola wetu! Uovu wetu ulituzidi na tukawa ni watu wenye kupotea." 23:104-106

Maneno haya ya Mwenezi mungu yanaonesha namna watakavyokiri watu hao wenye kejeli kwamba wao katika ulimwengu huu walikuwa waovu, wenye kupoteana kutangatanga. Lakini Mwenyezi Mungu atawajibu kwa jawabu kali:
"Atasema (kuwaambia watu hao) Dhalilikeni humo motoni na wala msinisemeshe. (Kumbukeni kwamba) Bila shaka kulikuwa na kundi katika waja wangu likisema: Mola wetu tumeamini basi utusamehe na utuhurumie kwani wewe ndiwe Mbora wa wanaohurumia. Lakini ninyi mliwafanyia mzaha hata wakakusahaulisheni kunikumbuka na mlikuwa mkiwacheka.

إِنِّي جَزَيْتُهُمُ الْيَوْمَ بِمَا صَبَرُوا أَنَّهُمْ هُمُ الْفَائِزُونَ

Hakika leo nimewalipa (wema) kwa sababu ya kusubiri kwao, bila shaka hao ndiyo wenye kufuzu." 23:111

Kwa hiyo jione mwenye fahari kwa kuvaa Hijabu, kwani umo katika hali ya kuonesha utiifu wako kwa Allah (s.w.t), na unapata thawabu kila hatua yako moja utembeayo.

وَمَا عِنْدَ اللَّهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ

Kilichoko kwa Allah (s.w.t.) ni bora na ni chenye kudumu Basi Je, Hamfahamu?” 28:60.”

وَرِضْوَانٌ مِنَ اللَّهِ أَكْبَرُ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

Na radhi za Mwenyezi Mungu ni kubwa.” 9:72

Kinyume chake katika thawabu ni, yule mwanamke asiye na Hijabu, kwa kuwa anapata madhambi kwa kila hatua yake moja anayotembea. Wapo wanawake wasemao: "Mimi najiamini nafsi yangu siwezi kufanya maasi na maovu, hivyo sioni sababu ya kunilazimisha kuvaa Hijabu." Jawabu la fikra kama hii ni hili lifuatalo. Kwanza: ni lazima ifahamike kwamba vazi la Hijabu ni jambo la wajibu juu yako kwa mujibu wa sheria kati hali yoyote ile iwayo, sawa sawa ukiwa unajiamini au la. Pili: Kujiamini peke yake hakutoshi kwa sababu.

وَمَا أُبَرِّئُ نَفْسِي ۚ إِنَّ النَّفْسَ لَأَمَّارَةٌ بِالسُّوءِ إِلَّا مَا رَحِمَ رَبِّي ۚ إِنَّ رَبِّي غَفُورٌ رَحِيمٌ

“Hapana shaka kwamba nafsi ni yenye kuchochea maovu isipokuwa ambayo Mola wangu ameirehemu.” 12:53

Kuna wasichana wengi wameteleza na wakajikuta wameingia ndani ya maovu kwa sabau ya kuacha Hijabu.

Tatu: Kuishi bila sitara ya Kiislamu kunasababisha kuamsha hisia za kimaumbile kwa wanaume wanaokutazama, pia inaweza kuwa sababu ya kukufanyia uchafu bila wewe kutarajia. Je! hili haliwezekani? Hali kama hii ikikufika, huko kujiamini kwako kutakusaidia na au kunaweza kuizuwia hali kama hii isitokee? Ewe msichana na mwanamke wa Kiislamu, usihadaike na fikra potofu, maadui wa Uislamu ndiyo hao hao maadui wa mwanamke, wanaipiga vita Hijabu kwa njia nyingi. Huna budi kuzinduka na kuepuka kampeni hizo sizizo na hekima. Wala usidanganyike na mitego yao iliyomo ndani ya mtizamo wao. Kwa kukuzindua ni kwamba: maneno wayasemayo huenda yakawa yanavutia hasa yanapokuja kwa lugha ya kutaka eti kukukomboa. Maneno yao haya ni sawa na asali tamu lakini ina sumu ukiila itakudhuru. Angalia iwapo utahadaika utakuwa umeiuza nafsi yako na dini yako kwa maadui wa Mwenyezi Mungu, pia fahamu ya kwamba utakuwa umeshawauzia kwa thamani ya kukuangamiza wewe mwenyewe.

Hebu jitahidi kuwa Mwislamu kwa ulimi wako na vitendo vyako. Wachana na nyendo za kiulaya, kwani miongoni mwa malengo yao ni kumtumia mwanamke kama chombo cha kutangaza biashara hali ya kuwa hana sitara. Jilinde kwa Mwenyezi Mungu akuepushe na nyendo zao ambazo nia yake ni kuichafua jamii ya Kiislamu na kuiangamiza. Fahamu ewe dada mpendwa kwamba, maendeleo na uungawana kwa mwanamke ni kuwa na sitara inayokubaliana na mazingira na hali yake kama mwanamke. Dada wa Kiislamu, utamaduni na uhuru wa kweli unapatikana ndani ya Uislamu na kanuni zake toka mbinguni.

Elewa pia kwamba, uovu na fedheha vitakupata iwapo utakwenda kinyume na kanuni za Kiislamu. Ni wajibu wako kutangaza na kuelimisha hekima ya Hijabu na falsafa yake kwa nduguzo, jamaa na marafiki. Kazi hii ifanye popote, ikiwa nyumbani, shuleni, chuoni, ofisini na sehemu nyinginezo unazoweza kufanya hivyo katika muda wote wa uhai wako. Kufanya tabligh siyo kazi ya wanaume peke yao, bali na wanawake inawahusu kikamilifu. Mtume (s.a.w.w.) anasema: "Kila mmoja wenu ni mchungaji na ataulizwa kuhusu uchungaji wake aliokabidhiwa."

Historia inatuonesha kwamba Bibi Fatma (a.s.) alikuwa akifafanua mambo yanayohusu sheria kwa wanawake wa Madina. Bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib alikuwa akifundisha tafsiri ya Qur'an kwa wanawake wa mji wa Al-Kufah huko Iraq. Fahamu ya kwamba Mwenyezi Mungu atakulipa thawabu nyingi kwa kila msichana au mwanake atakayefuata nasaha yako ya kuvaa Hijabu na akaongoka kupitia mkononi mwako.

Imesimuliwa ndani ya hadithi kwamba, Mwenyezi mungu alimpelekea ufunuo Nabii Musa (a.s.) akamwambia: "Ewe Musa ikiwa utamrejesha mlangoni kwangu mtu amabaye ni mwenye kuniasi au ukamrejesha uwanjani kwangu mtu aliyepotea, ni bora mno jambo hilo kwako kuliko ibada ya miaka mia moja ambayo mchana utakuwa umefunga saumu na ukasimama usiku ukisali."28

Hapana shaka kwamba mwanamke asiyevaaa Hijabu ni muasi anayeziasi kanauni zitokazo mbinguni. Basi mtu kama huyu akirudi kwenye uwanja wa Mwenyezi Mungu kisha akashikamana na Hijabu kutokana na juhudi zako na maelekezo yako, hapana shaka utapata malipo yaliyomo ndani ya hadithi iliyotajwa hapo juu. Kwa hakika hayo ni malipo makubwa mno na ni thawabu nyingi. Hivyo basi ifanye nafsi yako iwe miongoni mwa watu wa tabligh hasa kuhusu Hijabu na elekeza tabligh yako baina ya wasichana wenzio na wanawake wenzio.

Usikatae kuolewa: Dada mpendwa endapo atakuja mtu kukuposa, tafadhali chunguza vitu muhimu na vya msingi. Vitu hivyo ni kama vile Dini yake na tabia yake. Iwapo mtu huyu kakamilika sawasawa kwa sifa mbili hizi usibabaike baina ya kuolewa au hapana. Kwani Dini na tabia ndiyo msingi wa mafanikio ya maisha yako ya ndoa. Usichunguze shahada yake au jinsi yake (utaifa) wala usiangalie suala la mahari kwamba ni kiasi gani anachotoa. Pia nakusihi acha visingizio vya eti mpaka nikamilishe masomo yangu ili nipate shahada ya juu, na sababu zingine zisizokuwa na maana ambazo huenda zikakusababishia kuharibikiwa na Mwenyezi Mungu hatakuridhia. Mtume (s.a.w.w.) anasema: "Atakapokujieni mtu ambaye mwenendo wake na dini yake vinakuridhisheni, basi muozeni mtu huyo, na iwapo hamtamuozesha mtasababisha fitina na uchafu duniani."

Kuolewa ni sawa na kiota cha dhahabu ambacho ukikipata utatulia na kustarehe ndani yake, na ukweli ulivyo kitakulinda na kuyadhibiti maumbile yako. Mwenyezi Mungu hakumuumba mwanamke ili aishi maisha ya ujane na upweke, bali amemuumba aishi na mume bega kwa bega ili wajenge familia na jamii bora katika kuendeleza kizazi cha wanaadamu.

Kwa maelezo haya elewa jambo jingine muhimu nalo ni kuwa: Kuchelewa kuolewa ni makosa na ni hatari, chukua tahadhari ya jambo hili. "Mtume (s.a.w).w. anasema: "Enyi watu! Jibril amenijia kutoka kwa Allah (s.w.t) akaniambia, hakika wasichana bikra ni sawa na matunda yaliyomo mtini, matunda hayo yakishawiva na yakachelewa kuchumwa jua litayaharibu, upepo nao ukivuma utayaangushwa chini, hiyo ndiyo hali ya wasichana bikra wakisha vunja ungo hakuna dawa nyingine kwao isipokuwa ni kupata mume (waolewe) na kama hawakuolewa basi hawatasalimika na dhambi, kwani wao ni wanaadamu."

Baada ya Mtume kumaliza kusema maneno haya, alisimama mtu fulani akasema: 'Tumuoze nani basi?' Mtume akajibu: 'Wanaume wanaostahiki kuwaowa.' Yule mtu akauliza ni kina nani hao? Mtume akajibu: 'Waumini baadhi yao ni stahiki kwa baadhi nyingine.' Akakariri mara mbili."29 Ama ikiwa mchumba atakayekuja ni muasi wa Dini yake au kuna kitu kibaya katika tabia yake, kwa mfano asiyeswali, mlevi na mengineyo, huyu mkatae wala usitishike kwa mali yake au cheo chake. Maisha ya upweke ni bora kuliko kuishi na Mume muasi wa Mungu au mwenye tabia mbaya, japo awe na mali au cheo kikubwa. Ewe dada yangu wa Kiislamu, muombe Mwenyezi Mungu akukadirie upate mume mwema ambaye ni muumini aliyekusanya sifa za uzuri wa sura, Dini na tabia njema, kwani Yeye Mwenyezi Mungu anasema:

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ

"Niombeni nami nitakujibuni maombi yenu." 40-60

Ewe Mume Mwema.

Jukumu lako ewe mume kuhusu suala la ndoa ni muhimu sana mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani unawajibika kutengeneza na kurekebisha mwenendo na tabia ya mkeo.

Mwenyezi Mungu amekufanya uwe msimamizi wa mkeo na kiongozi wake. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنْفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ

"Wanaume ni walinzi juu ya wanawake kwa sababu Allah amewafadhilisha baadhi yao kuliko wengine na kwa sababu ya mali zao walizozitoa." 4:34

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنْفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ

Na Mwenyezi Mungu anasema: "Enyi mlioamini jiokoeni nafsi zenu na watu wenu kutokana na moto ambao kuni zake ni watu na mawe" 66:6

Na ili uweze kutekeleza wajibu wako kisheria na majukumu yako ya dini kama alivyoamuru Allah s.w.t na Mtume Wake, ni lazima uambatanishe mafunzo na maelekezo ya Kiislamu kwa vitendo kama ifuatavyo.

Hijabu liwe ni jambo la mwanzo: Unalazimika kumuamuru mkeo avae Hijabu kama alikuwa havai, na pia umuoneshe dalili za kutosheleza na kukinaisha kuhusu Hijabu. Hii ni kwa sababu atakapovaa awe anafahamu na kuelewa umuhimu wa kanuni hii ya Kiislamu. Endapo utashindwa kumkinaisha kimaelezo basi fuatana naye hadi kwa Sheikh ambaye ataweza kumfahamisha kwa maelezo yatakayoonesha umuhimu wa falsafa inayopatikana katika Hijabu. Na ikiwa kuna njia nyignine ya kumfahamisha kama vile kumtafutia vitabu ajisomee yeye mwenyewe ni bora kumpatia.

Imam Ali (a.s.) anasema kumuusia mwanawe Muhammad AlHanafiyya: "Umuhimu wa Hijabu ni kitu bora kwako na kwao wanawake, ili muondokane na shaka. Kutoka nje (kwa matembezi ya kawaida) na wanawake siyo jambo baya kuliko wewe kuja na mgeni mwanaume asiyeaminika nyumbani mwako kisha ukamtambulisha kwao (wanawake) na iwapo utaweza kutowatambulisha wake zako kwa yeyote basi fanya hivyo."30

Imam Ali anamaanisha kwamba, mume asimtambulishe mkewe kwa wanaume wasiomuhusu mkewe, kwa kuwa jambo hili husababisha fitna.

Jambo la pili: Tahadhari na sherehe zenye mchanganyiko: Ewe mume mwema, epukana na mahafali na sherehe zenye mchanganyiko wa wanaume na wanawake. Usimpeleke mkeo sehemu hizo, muepushe mbali kabisa na mikesha ya nyimbo na magoma. Kumpeleka mkeo, katika majumba ya sinema kunachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu mwenendo wa mkeo na pia hali hii itasaidia kumfanya asiwe na aibu na heshima yake itatoweka.

Mume anayempeleka mkewe sehemu zenye sherehe zenye mchanganyiko wa wanawake na wanaume, au anayemuingiza mkewe katika majumba ya sinema, mume huyu ni haini wa kwanza dhidi ya mkewe. Yeye ndiye dhalimu atakayekuwa mfundishaji wa mwelekeo mbaya wa mkewe.

Dhoruba la uovu atakalolianzisha mume huyu dhidi ya mkewe, bila shaka litaanza kumpiga yeye mwenyewe, ili ayaone matunda ya kazi yake hiyo mbaya. Dhoruba hili si jingine, bali ni pale mkewe atakapofanya hiyana ya kuanzisha uhusiano na watu wengine. Hivyo ni wajibu wako wewe mume kumuepusha mkeo kutokana na maeneo ya uovu na mengineyo machafu. Asiyakaribie maeneo hayo licha ya kwenda ili uishi kwa amani na nafsi iliyotulia.

Jambo la tatu: Usimtii mkeo: Inakulazimu uishi maisha ya muongozo wa dini ya Mwenyezi Mungu na hukumu zake na utahadhari na kila mwelekeo mbaya na wa kupotosha. Kwa kuwa utulivu wa nafsi yako hupatikana toka kwa mkeo, basi huenda akataka umfanyie jambo ambalo Mwenyezi Mungu kaliharamisha. Iwapo hali hii itajitokeaza kwa mkeo, jaribu kumuleza kwa upana hukmu ya Mwenyezi Mungu kuhusu ombi lake hilo ili atambue ubaya wa jambo hilo. Haifai kabisa kumtii mkeo (hata mtu mwingine) katika mambo ya kumuasi Mwenyezi Mungu s.w.t kwani hapana twaa ya kumtii kiumbe katika kumuasi Muumba.

Hivi sasa soma hadithi ifuatayo: Mtume (s.a.w).w anasema: "Mwenye kumtii mkewe Mwenyezi Mungu atamuingiza motoni mtu huyo. Mtume (s.a.w).w. akaulizwa huko kumtii mke ni namna gani? Mtume akasema: Mke kuomba ruhusa kwa mumewe kwenda kwenye starehe na michezo hali ya kuwa kavaa nguo nyepesi (na mume akatoa ruhusa)."31

Kwa hiyo basi, usimruhusu mkeo kuhudhuria sherehe au harusi zenye mchanganyiko na usimkubalie kuvaa mavazi mepesi mbele ya wanaume wengine kwa kuwa yote haya hayamridhishi Mwenyezi Mungu.

Jambo la nne: Kuwa na wivu kwa mkeo: Huna budi ewe mume kuwa na wivu kwa mkeo, kwani imekuja hadithi kutoka kwa Imam Jaafar Sadiq (as) kwamba: "Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ana wivu na anampenda kila mwenye wivu, na kwa wivu wake Allah (s.w.t) amekataza maovu yafanywayo dhahiri na yale yafanywayo kwa siri.”32 Kwa ajili hiyo basi ni lazima umuhifadhi mkeo na binti zako kitabia, pia mavazi ili msijefikwa na balaa na ghadhabu za Allah (s.w.t). Amesema Imam Jaafar (a.s.) kwamba: "Pepo imeharamishwa kwa mtu duyuuth (asiye na wivu)." Na amesema tena Imam Jaafar (a.s.) "Watu wa aina tatu Mwenyezi Mungu hatawasemesha siku ya kiama wala hatawatakasa 1. Sheikh (mwanachuoni) mzinifu. 2 Duyuuth (asiye na wivu) 3. Mwanamke anayemlaza mwanamume mwingine kwenye kitanda cha mumewe."33

Na katika kuonesha kuwa una wivu, ni kutomwacha mkeo au mmoja kati ya watu wa nyumba yako, wakiwemo mabinti zako wakatoka nje hali ya kuwa wamejitia manukato na madawa ya kujirembesha na mapambo mengine. Hapana shaka kwamba jambo hilo huwa linatishia heshima yako na yao ndani ya jamii, na matokeo ya hali hiyo ni mabaya mno. Mtume (s.a.w.w.) amesema: "Mwanaume yeyote atakayemwacha mkewe ajipambe na kisha mwanamke huyo akatoka nyumbani mwake akiwa katika hali hiyo, basi mume huyo atakuwa ni duyuuth (hana wivu).

Na ikiwa mke huyu atatoka nyumbani mwake hali kajipamba na kutia manukato na mumewe akawa radhi, mumewe atajengewe nyumba ndani ya moto kwa kila hatua moja atakayotembea mkewe.34 Bwana Mtume ((s.a.w).w.) anasema kuwa: "Aina kumi za watu hawataingia peponi mpaka kwanza watubie:. Miongoni mwa hao kumi Bwana Mtume alimtaja Duyuth, na akaulizwa, ni nani huyo Duyuth? Akasema ni yule mwanaume asiyekuwa na wivu kwa mkewe.35

Imetokea zaidi ya mara moja, kwangu mimi kumuona mtu anakula chakula ndani ya mgahawa au hoteli hali ya kuwa na mkewe na watu wengine wakiwa wanamuangalia mtu huyo na mkewe. Cha ajabu ni kwamba bwana huyo anapokuwa katka mazingira hayo anakuwa yuko huru bila wasiwasi kabisa. Hajali kama kuna sitara yoyote au hapana, na wala hana hata habari juu ya kuwa mkewe kavaa Hijabu au hapana. Kama ambavyo sasa hivi iko wazi kabisa kule kuwako kwa mabustani na maeneo ya matembezi yanayotembelewa na watu wengi wake kwa waume. Kwa hakika jambo hili bila kificho ni jambo baya mno linalohatarisha usalama wa jamii. Kuna Mkurugenzi wa mgahawa mmoja aliniambia kuwa: "Wako baadhi ya watu wanakataa kula chakula ndani ya vyumba maalum vilivyotengwa kwa ajili ya watu wenye familia, na wanaona ni bora wale chakula mahali pa wazi hali ya kuwa wamefuatana na familia zao!" Kama hali ni hii, uko wapi basi wivu wa wanaume kwa wake zao enyi Waislamu?

Mfundishe mkeo Surat An-Nur. Inapendekezwa kwako ewe mume kumfundisha mkeo surat Annur na tafsiri yake, kwa kuwa ndani yake mna Aya nyingi zinazozungumzia mas'ala ya wanawake.

Aya hizo zimedhibiti mambo mengi ambayo yanamlazimu mwanamke ayafahamu ili aishi maisha bora ya Kiislamu na awe mbali na maovu. Mtume wa Mwenyezi Mungu anasema: "Wafundisheni wanawake surat An-nur kwani ndani yake mna mawaidha mengi (kwa wanawake).36

Usimuweke mkeo katika chumba cha barabarani. Bwana Mtume (s.a.w).w.amekataza kuwaweka wawnawake katika vyumba vya barabarani akasema: "Musiwaweke wanawake katika vyumba vya barabarani." Makusudio halisi ya hadithi hii ya Bwana Mtume (s.a.w.w.) ni kuwaonya wanaume juu ya kuwaweka wake zao katika vyumba vinavyotazamana na barabara.

Zaidi ya hapo ni lazima tufahamu hata vyumba vinavyotazamana na masoko na maeneo mengine yenye msongamano wa watu ni hatari kuwaweka wanawake ndani ya vyumba hivyo. Imekuja katika hadithi kwamba, miongoni mwa hatua ambazo Imam Mahdi (a.s.) atazichukua katika kurekebisha hali ya Umma pindi dola yake itakaposimama, ni kuondosha madirisha yanayoelekea barabarani.37

Pengine utajiuliza kwamba ni ipi hekima ya jambo hilo? Jawabu lake ni hili lifuatalo: Hapana shaka kwamba madirisha yanayotazama barabarani ni kichocheo kikubwa katika kuleta uharibifu ndani ya ndoa za watu na pia kuvuruga familia. Na sababu yake ni kwamba dirisha hilo huwa ni nyenzo ya kumfanya mtu aone ni kitu gani kilichomo ndani ya chumba na hasa katika majengo ya ghorofa kadhaa. Majengo haya huwa yanaonesha kila kilichomo ndani ya chumba hicho kwa wapita njia na hata watu wanaoshi mkabala na majengo hayo.

Sasa basi uharibifu wa familia na ndoa za watu unaweza kuja kutoka katika moja ya pande mbili, yaani upande wa mwanamke aliyemo ndani ya jengo hilo au yule mwanaume mpita njia. Kwa mfano mwanamke ikitokezea akachungulia njiani kwa kupitia dirishani na kwa bahati mbaya mmoja kati ya wapita njia akimuona na moyo wake ukaingia namna fulani ya kumpenda huyo mwanamke, basi hapo ndipo unapoanzia ule msiba wa maovu. Na pengine mwanaume naye anaweza kuwa amesimama dirishani na mara akamuona mwanamke kwenye ghorofa lililoko mkabala na ghorofa analoishi yeye, basi kutokana na mazingira ambayo hayapingiki ni kuwa bila ya shaka mwanamke huyo atakuwa hakujisitri kwa kutambua kuwa yumo ndani mwake. Katika hali kama hii tunataraji matokeo gani baina ya wawili hawa ikiwa hawatamuogopa Mwenyezi Mungu? Hapana shaka kwamba Bwana Mtume (s.a.w.w.) amesema kuwa:

"Yeyote atakayechungulia ndani ya nyumba ya jirani yake kisha akaona tupu ya mwanaume au nywele za mwanamke au akaona sehemu yoyote ya mwili wa mwanamke, basi Mwenyezi Mungu atakuwa na haki ya kumuingiza motoni mtu huyo pamoja na wanafiki ambao walikuwa wakifuatilia tupu za wanawake hapa duniani na wala Mwenyezi Mungu hatamtoa ulimwenguni mpaka kwanza amfedheheshe na audhihrishe wazi utupu wake huko akhera.38

Hekima inatwambia kwamba: "Kinga ni bora kuliko tiba." Hali inajieleza wazi kwamba, ni mara nyingi tiba imekuwa ni jambo lisilo na mafanikio, wakati ambapo kinga imekuwa ni dhamana yenye nguvu. Kwa hakika miongoni mwa mambo yanayohuzunisha ni kuona kwamba jamii kwa jumla inaishi nje ya mafunzo haya ya Kiislamu yenye ulinzi madhubuti.

Utamuona mwanamke anatoka barazani hali ya kuwa kavaa nguo zinazostahili kuvaliwa ndani, kisha katika hali kama hiyo anaanika nguo kwenye kamba. Au utamkuta mwanamke anachungulia njiani katika hali ile ile huku akiwa amejisahau kwamba kwa kufanya hivyo anajiletea msiba na huzuni yeye binafsi na familia yake. Basi ni juu yako ewe mume mwema uzindukane na ushikamane na mafunzo bora ya Kiislamu, na pia uyatumie ndani ya maisha yako ya ndoa na familia yako kwa jumla mpaka ifikie hali ya maisha yako na familia yako kuwa maisha mema yenye kuepukana na fedheha za duniani na udhalili wa huko akhera.

Mafunzo ya Kiislamu. Ndugu Mwislamu pokea baadhi ya mafundisho ya Kiislamu ambayo Mwenyezi Mungu ametuamrisha kuyatumia katika maisha yetu ya kijamii. Mafunzo haya yanalenga kumhifadhi mtu kutokana na uovu pia kumlinda asiteleze na kuingia makosani.

Kwanza: Usimuangalie mke asiyekuhusu.39 Kumtazama mwanamke asiyekuhusu ndiyo hatua ya kwanza kuelekea kwenye uharibifu wa tabia na ndiyo ufunguo wa shari na kutelezesha watu. Katika kumtazama mara moja hutokea ukavutika na kuongeza mtizamo wa pili, na hatimaye watatu na mwisho husababisha nia mbaya katika nafsi.

Mshairi mmoja anasema: Kutazama ndiyo hatua ya mwanzo, tabasamu hufuatia, kisha salamu. Kinachofuata ni mazungumzo, na hatimaye ahadi hufungwa na mwisho wa yote kitendo hutimia.

Kwa sababu kama hizi, Uislamu kwa kutaka kukata mizizi ya fitina umekataza jambo hili.

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameharamisha kumtazama mke asiyekuhusu, na akaonya kwa onyo kali. Isitoshe Mwenyezi Mungu amewaamuru Waumini wa kiume wainamishe macho yao wasiwatazame wanawake wasiowahusu Akasema:

قُلْ لِلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ

"Waambie Waumini wanaume wainamishe (chini) macho yao na wazilinde tupu zao, kwani kufanya hivyo kuna utakaso kwa ajili yao. Na hakika Mwenyezi Mungu anafahamu wanayotenda."40

Hapana shaka kwamba tabia ya kibinaadamu ni tabia inayopelekea mvuto baina ya jinsiya mbili hizi , yaani ya kiume na ile ya kike kwa sababu tu ya kila mmoja kumtazama mwenzake. Kwa hiyo basi, ni lazima tabia hii iwekewe mipaka kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu, vinginevyo matokeo ya maisha ya jamii ya wanaadamu yataingia ndani ya ufisadi na matokeo ya ufisadi huo ni mabaya. Imam Jaafar As-sadiq (as) amesema: "Kuangalia kwa kukazaia macho kunapanda mbegu ya matamanio ndani ya moyo, na kwa hakika inatosha kuwa ni fitna kwa mwenye kuangalia namna hiyo." Hapana41 shaka kwamba kuangalia huko kulikoharamishwa na sheria, ndiko kunakoandaa maovu hapa duniani, na kwa ajili hii kumekuja maonyo ndani ya hadithi kama ifuatavyo: "Kuangalia ni mjumbe wa uzinifu.

"Hadithi hii inatufunza kwamba, mwanzo wa uzinifu hupatikana kwa njia ya kuangalia kulikoharamishwa na sheria. Jambo hili liko wazi kwa kuwa, uzinifu haupatikani ila baada ya mwanaume kumkazia macho mwanamke, na ndiyo maana tukaambiwa ndani ya ile hadithi iliyotangulia hapo kabla kwamba:

"Kuangalia kulikoharamishwa ni mjumbe wa uzinifu." Kwa maelezo haya ndugu msomaji, wala hakuna haja ya kuuliza juu ya athari mbaya zinazojitokeza kutokana na uzinifu ikiwemo maradhi mabaya yanayosababishwa na tendo hilo chafu. Isitoshe hali hiyo, bali kuna uharibifu mkubwa mno ndani ya jamii. Na kila ukichunguza utakuta kuwa uzinifu ndiyo chanzo cha misiba hii, na ambayo chimbuko lake ni kumuangalia mwanamke asiyekuhusu kwa mujibu wa sheria. Nabii Yahya ibn Zakariyya (a.s.) aliulizwa kuhusu chanzo cha uzinifu akasema: "Ni kumuangalia (mwanamke asiyekuhusu) na nyimbo." Siyo jambo la ajabu kuwa, sheria imekuja kuyakataza kwa mkazo sana mambo haya, na wala siyo jambo la kushangaza kuwa, huko akhera kutakuwa na adhabu kali na ngumu kwa watendao matendo haya. Imekuja ndani ya hadithi tukufu ya Mtume (s.a.w.w.) kwamba: "Mtu yeyote atakayeyajaza macho yake kwa kumuangalia mwanamke ambaye ni haramu kwake, Mwenyezi Mungu atayajaza macho yake siku ya kiama kwa misumari ya moto na ataendelea kuyajaza moto macho hayo mpaka watu wote waishe kuhukumiwa ndipo naye aamuriwe kuingia motoni." 42

Hadithi nyingine nayo inasema kuwa: "Yeyote mwenye kuyajaza macho yake kwa kuanglia vitu vilivyoharamishwa, Mwenyezi Mungu atayajaza macho yake siku ya kiyama kwa misumari ya moto, isipokuwa kama atatubia." 43

Miongoni mwa athari za kuwaangalia wanawake wasiyokuhusu ni kujiadhibu wewe mwenyewe nafsi yako na kujisababishia mawazo mengi bila sababu ya msingi. Imam Ali (a.s.) anasema:

"Yeyote mwenye kuliachilia jicho lake (likawaangalia wanawake wasiomhusu) mtu huyo hujisababishia majonzi mengi."44 Na kasema tena Imam Ali (a.s): "Mtu yeyote ambaye macho yake ni yenye kuangalia kwa kufuatilia (wanawake wasiomhusu au mambo ya haramu) mtu kama huyu majuto yake huwa ni ya kudumu." 45 Mtu anayeishi maisha yanayoruhusu macho yake kuangalia kila anayemtaka na anachokitaka, hapana shaka kwamba mtu huyu huishi maisha yenye majonzi mengi na huiadhibu nafsi yake mwenyewe, na huwa mwenye mawazo yasiyo na kikomo. Yote haya yatampata kwa sababu moyo wake utakuwa umefungwa kwa huyo aliyemuona na akamtamani kisha asimpate. Akili yake ataishughulisha akifikiria namna ya kumpata, na huwenda akakosa raha na hata usingizi.

Hadithi hii iliyotaja hatari za kuangalia, na kisha kumsababishia taabu na majuto mwenye tabia hiyo, inahusisha mambo mengi ambayo haipaswi kuyaangalia, lakini moja wapo na muhimu ni hili la kuwaangalia wanawake wasiokuhusu, bali tunaweza kusema kuwa hilo ndilo makusudio. Na kwa ajili hiyo basi Imam Jaafar (a.s.) akibainisha hatari za kumuangalia mwanamke asiyekuhusu anasema: "Kumtazama mwanamke asiyekuhusu ni mshale wenye sumu miongoni mwa mishale ya iblisi, na ni mara nyingi kumtazama mwanamke asiyekuhsu limekuwa ni jambo lenye kuleta majuto ya muda mrefu.46"

Ewe ndugu yangu bila shaka unafahamu jinsi mshale unavyoweza kuingia mwilini na kupasua mishipa iliyoko mwilini. Hebu fikiria namna mshale usiokuwa na sumu unavyoweza kuleta madhara pindi uingiapo mwilini, sasa je itakuwaje hali ya mshale wenye sumu ukiingia mwilini?

Bila shaka madhara yake ni makubwa zaidi ambayo yanaweza kupelekea mauaji kwa mtu. Hali ni kama hiyo kwa mtu mwenye tabia ya kuangalia wanawake wasiomhusu, kwani kuangalia huko ni sawa na mshale wenye sumu, mshale huo hujitengenezea njia mpaka ndani ya moyo ili kumnyima mtu huyo raha na utulivu na kumuachia majuto ya muda mrefu. Ewe ndugu yangu mpendwa! Ili uweze kujitakasa na kuwa mbali na mawindo ya shetani, napenda kukufahamisha pia kwamba Uislamu unachukizwa na tabia ya kuwaangalia wanawake. Mimi naamini kwama kuna baadhi ya watu wasiofuata mafundisho ya dini wanapokutana na wanawake, wakishakupishana nao basi huwaangalia nyuma hali ya kuwa wanatizama kwa mtazamo wa kutaka kufahamu namna wanawake hao walivyo au wanavyotembea, pia maumbo yao. Kwa hakika hii ni tabia mbaya mno haifai kabisa. Inasimuliwa kwamba Abu Basir alimuuliza Imam Jaafar (a.s.) "Ni vipi mtu anapomwangalia mwanamke kwa nyuma? "Imam a.s. akajibu kwa kusema: "Hivi mmoja wenu anapenda mkewe au jamaa yake wa kike aangaliwe namna hiyo?" Abu Basir akajibu: "Hapana." Imam akasema: "Basi waridhie watu kwa kile unachokiridhia kwa ajili ya nafsi yako." 47

Kuna kisa kimoja kinamuhusu Mtume Musa (a.s.) katika tafsiri ya neno la Mwenyezi Mungu akimnukuu Binti ya Mtume Shuaibu (a.s.) aliposema:

قَالَتْ إِحْدَاهُمَا يَا أَبَتِ اسْتَأْجِرْهُ ۖ إِنَّ خَيْرَ مَنِ اسْتَأْجَرْتَ الْقَوِيُّ الْأَمِينُ

"Ewe Baba muajiri huyu, hakika mbora uwezaye kumuajiri ni mtu mwenye nguvu tena mwaminifu.48

Nabii Shuaibu alipoyasikia maneno ya Binti yake alimuuliza akasema: "Huyu Musa ni mwenye nguvu na hii ni kwa sababu umemuona akilinyanyua jiwe kwenye kisima, sasa je, huu uaminifu wake umeufahamu vipi?" Yule Binti akajibu kwa kusema: "Ewe Baba mimi nilikuwa natembea mbele yake, mara Musa akaniambia, tembea nyuma yangu na iwapo nitapotea njia basi wewe utanielekeza, kwani sisi ni watu tusiyowaangalia wanawake kwa nyuma.49

Katika tafsiri ya neno la Mwenyezi Mungu lisemalo kuwa: "Waambie Waumini wanaume wainamimshe macho yao." Imamu Muhammad Al Baqir (a.s.) anasema: "Kijana mmoja wa Kiansari alikutana na mwanamke fulani katika vichochoro ya mji wa Madina, na huyu kijana akamkazia macho yule mwanamke. Walipopishana kijana huyu akageuza shingo yake na akaendelea kumuangalia yule mwanamke huku anakwenda hali ya kuwa kageuza shingo yake akimuangalia. Basi ghafla alijikuta amejigonga ukutani na damu zikaanza kumchuruzika. Kijana yule kuona hivyo akasema: Ni lazima niende kwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu nikamueleze juu ya kisa hiki. Kijana yule alipofika mbele ya Mtume (s.a.w.w) hali damu zikiendelea kumtoka, Mtume alimuuliza umepatwa na nini? Yule kijana akasimulia yaliyomfika, na mara Malaika Jibril (a.s.) alishuka akiwa na Aya inayowaamuru Waumini wanaume wainamishe macho yao." 50

Kipo kisa kingine kinasimuliwa kuhusu hali kama hizi na kinasema kuwa: "Kuna mtu mmoja ambaye kazi yake ilikuwa kuteka maji na kupeleka ndani ya nyumba ya Sonara fulani kwa muda wa miaka thelathini.

Bila shaka kuna wakati yule hakuwako nyumbani kwa mke wa sonara alikuwa akija kumfungulia mlango yule mchota maji ili apate kumimina maji mahala panapostahili. Kipindi chote hiki yule mchota maji hakuwahi kufanya hiyana yoyote dhidi ya mke wa sonara japo kumuangalia kwa jicho la hiyana.

Siku moja wakati yule mama anamfumngulia mlango yule mchota maji, mara ghafla aliunyoosha mkono wake na kumvuta yule mama na akambusu!! Kwa bahati nzuri mwanamke huyu aliuvuta mkono wake kwa nguvu kisha akapiga makelele na hapo hapo akamfukuza yule mchota maji kutoka mule ndani. Baadaye huyu mama alianza kufikiria huku akishangazwa na hali ile iliyojitokeza. Imekuwaje mchota maji yule kufanya hiyana ile baada ya kuwa muaminifu kwa muda wa miaka thelathini?!! Mumewe aliporudi nyumbani mkewe akamuuliza: 'Je leo kuna jambo gani limetokea huko dukani kwako?' Yule mume akajibu kwa kusema: 'Leo kuna mwanamke alikuja dukani kwangu kununua bangili, basi nilipomfunua mikono yake ili apate kuvaa bangili zile, nilimshika mkono wake kisha nikambusu.'!! Basi pale pale mkewe alipiga makelele akasema: 'Allahu Akbaru!' 51 Baada ya hapo alimsimulia mumewe mambo yaliyotendwa na yule mchota maji."

Naam chochote atakachokifanya mtu kuwafanyia wenziwe na wake wa wenzake, basi na yeye yatamfika hivyo kwa mkewe, mama yake, dada yake na binti yake. Ndani ya hadithul Qudsi inasemwa kuwa: "Vile uwatendeavyo wenzako, basi na wewe utatendewa hivyo hivyo." Maana yake ni kwamba: Iwapo utawatendea wema wenzako basi na wewe utatendewa wema, na iwapo wewe utawatendea ubaya wenzako fahamu wazi kuwa na wewe utatendewa ubaya.52

Ewe msomaji mpendwa: Narudia tena kuzungumzia suala la kumuangalia mwanamke asiyekuhusu na ninasema: Hapana shaka kwamba Uislamu ni dini yenye mafunzo yanayokuhamasisha kutenda mema, na wakati huo huo inayo mafunzo ya kukuonya usiyaendee maovu. Ndiyo maana utaiona Qur'an Tukufu pindi Mwenyezi Mungu anapoitaja pepo na neema zake, hapo hapo hufuatisha kuelezea habari za moto na adhabu zake. Yote haya lengo lake ni kumfanya mtu awe katika mazingira ya kutumainia neema na thawabu, na pia awe na khofu ya moto na adhabu kwa upande wa pili. Hivi punde tu umesoma baadhi ya hadithi tukufu zilizosimulia kuhusu adhabu za kumuangalia mwanamke asiyekuhusu na pia matokeo mabaya yanayoletwa na tabia hiyo mbaya.

Hivi sasa umefika wakati wa kuzungumzia hadithi zinazoelezea malipo mema aliyoyaandaa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ajili ya wale watakaojiepusha na mambo ya haramu. Kadhalika hadithi hizo zitaelezea athari njema zinazopatikana kutokana na tabia njema za kujiepusha na mambo aliyoyakataza Mwenyezi Mungu.

Bwana Mtume (s.a.w).w anasema: "Kuyatazama mapambo ya wanawake wasiokuhusu ni mshale miongoni mwa mishale ya ibilisi iliyo na sumu, atakayeliacha jambo hilo kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu (s.w.t) basi Mwenyezi Mungu atamuonjesha ladha ya ibada itakayomfurahisha.53

"Katika hadithi nyingine Mtume (s.a.w.w) anasema: "Kumtazama mwanamke asiyekuhusu ni mshale miongoni mwa mishale ya ibilisi iliyo na sumu, atakaye acha jambo hilo kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu (s.w.t) basi Mwenyezi Mungu atampa mtu huyo imani ambayo furaha ya imani hiyo ataihisi moyoni mwake."54

Bwana Mtume anaendelea kutufunza anasema kwamba: "Yainamisheni macho yenu, kwa kufanya hivyo mtaona maajabu (makubwa).55

Hapana shaka kwamba Mwenyezi Mungu humfunika mtu huyo kwa wingi wa baraka kutokana na kitendo chake cha kuinamisha macho na kutowaangalia wanawake wasiomhusu. Imam Ja'far Sadiq (a.s) anasema: "Mwenye kumuangalia mwanamke asiyemhusu kisha akanyanyua macho yake juu au akayafumba (ili tu asimuone mwanamke huyo), Mwenyezi Mungu humuozesha mtu huyo mwanamke wa peponi kabla hajarudisha macho yake chini."56 Anasema tena Imam Ja'far (a.s): "Hawezi mtu yeyote kujihifadhi isipokuwa kwa kuyainamisha macho yake, kwani macho hayatainamishwa kutokana na mambo aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu, isipokuwa ndani ya moyo wa mtu huyo huwa kumetangulia kuuona utukufu wa Mwenyezi Mungu."57 Sasa hivi kumebakia kitu cha mwisho ambacho ni: Je! Ni namna gani basi mtu anaweza kuepukana na jambo hili la haramu, wakati sote tunafahamu kwamba, gonjwa hili la kansa ya wanawake kuvaa nusu Hijabu na kutokujisitiri kwa mujibu wa sheria limeenea? Na kwa bahati mbaya sana hata katika nchi zetu za Kiislamu gonjwa hili limo. Hivi kweli kwa hali tuliyonayo mtu anaweza tena kuinamisha macho yake na ni vipi ataiona njia?

Jawabu la suali hili ni kama ifuatavyo: Sina shaka umesoma baadhi ya Aya na hadithi tulizozitaja. Kinachotakiwa ni kuinamisha macho siyo kuyafumba, na hii ndiyo maana iliyokusudiwa, yaani uangalie chini.

Anachopaswa mtu kukifanya wakati anapomuona mwanamke asiyemhusu, haraka sana ateremshe macho yake chini au aangalie upande mwingine. Kwa hakika Mwenyezi Mungu hawezi kupoteza malipo yake.

1. Usimpe mkono mwanamke asiyekuhusu: Ndugu Mwislamu, Mwenyezi Mungu ameharamisha kumpa mkono mwanamke asiyekuhusu. Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema: "Yeyote atakayepeana mkono na mwanamke asiyemhusu mtu huyo hujiingiza katika ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na anayedumisha uhusiano (wa kimapenzi) na mwanamke asiyekuwa mkewe, atafungwa kwa mnyororo wa moto pamoja na shetani kisha wasukumizwe motoni.58

2. Usimtanie mwanamke asiyekuwa mkeo: Miongoni mwa mambo ambayo Mwenyezi Mungu amekukataza na kukuharamishia ewe ndugu Mwislamu, ni kufanya utani na mwanamke asiyekuhusu kisheria, kwani jambo hili mara nyingi hukaribisha uovu na pia husaidia kwa kiasi kikubwa kuamsha hisia za maumbile zilizokuwa zimejificha katika pande mbili hizi. Bwana Mtume (s.a.w.w) anasema: "Yeyote anayemtani mwanamke asiye na milki naye (asiyekuwa mkewe) Mwenyezi Mungu atamfunga mtu huyo miaka alfu moja (huko akhera) kwa kila neno moja alilomsemesha mwanamke huyo."

3. Usichelewe kuoa: Ndugu yangu Mwislamu, kuoa ni jambo la lazima kwa Mwislamu anapofikia umri wa kubalehe.

    a. Ni lazima Mwislamu aoe ili ailinde dini yake, na ndiyo jambo la kwanza apasalo kufahamu.

    b. Jambo la pili: Pindi atakapooa atapata radhi za Mwenye Mungu Mtukufu.

    c. Na jambo la tatu: Atakuwa amehifadhi nafsi yake kutokana na mambo ya haramu. Kwa hakika Mwenyezi Mungu amemuumba mtu na akamuwekea matamanio ya kijinsiya, na akayafanya kuwa ndiyo matamanio yenye nguvu kuliko mengine yote. Kwa matamanio hayo Mwenyezi Mungu akafanya kuwa ndiyo njia ya kukidumisha kizazi cha wanaadamu, na akafanya kuoa ndiyo njia ya pekee kuyatosheleza matamanio haya. Kwa hiyo kuoa ndiyo njia nzuri na tukufu na ndiyo ufumbuzi wa pekee uliopo kisheria kuhusu tatizo hili la kijinsiya.

Ukweli ulivyo ni kwamba, kuchelewa kuoa kunamfanya mtu akumbwe na mambo mawili.
1. Kwanza: Katika kushindana na matamanio yake kutamfanya aiumize nafsi yake na kupata taabu kubwa ya kuvumilia katika muda huo.

2. Pili: Huenda hatimaye akaingia katika haramu ikiwa ni pamoja na njia isiyo ya kawaida katika kuyatosheleza matamanio yake, au akajikuta anafanya mambo machafu zaidi ambayo ni kinyume na maumbile. Au huenda akafanya uzinifu na matokeo yake ni kuvunja heshima yake au heshima za watu wengine. Na kutokana na hali halisi ilivyo, kila jambo moja katika hayo lina hatari kubwa kwa mtu yeye mwenyewe na heshima yake na utu wake. Kwani kuzuia matamanio na kuyadhibiti kunasababisha kuiadhibu roho na matokeo yake huleta athari mbaya mwilini na hasa katika akili.

Hali hii husababisha kuingia katika dhambi na hatimaye mtu ndipo hujikuta akifanya ambalo hakulitarajia, hapo utu wake huporomoka na mwisho hupata akahukumiwa kwa kosa la jinai na kuingia gerezani na kuishi humo sawa na wezi na wanyang'anyi.

Basi Nini Ufumbuzi Wa Tatizo Hili?

Ufumbuzi wa tatizo hili ni kuoa, kitu ambacho Uislamu unakitanguliza mbele na hata akili inakubaliana kabisa na ukweli huu, kwa kuwa kuoa ndiyo dawa pekee ya kutibu maumbile haya. Kuoa kunatimiza furaha ya kiroho kwa mtu na kuiliwaza nafsi na kuyapamba mazingira na tabia ya mtu. Kwa jumla ladha ya maisha na starehe vimo ndani ya ndoa, na kwa upande mwingine kuoa kunazuia mtu kuyaingia maovu na madhambi. Zaidi ya hapo ni kwamba, Mwenyezi Mungu hakumuumba mtu ili aishi maisha ya ujane na upweke, bali amemuumba aishi na mkewe aliye Muumini bega kwa bega ili wajenge familia na jamii bora hasa katika malezi ya watoto. Kwa hakika ujane ni miongoni mwa mambo yanayomchukiza Mwenyezi Mungu, pia Uislamu unapinga kwa nguvu zake zote jambo hili na hata Mawalii wa Mwenyezi Mungu wanachukizwa na ujane. Bwana Mtume (s.a.w.w) anasema: "Waovu miongoni mwenu ni wajane, (wasiyooa au kuolewe) nao ni ndugu wa shetani."59 Na akasema tena: "Watu wengi wa motoni ni wale wajane ( wasiyooa au kuolewa)."60

Imesimuliwa kutoka kwa al-Ukaaf al-Hilali anasema: "Nilikwenda kwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) akaniambia 'ewe U'kaafu unaye mke?' Nikamwambia, Hapana sina mke. Mtume akaniambia: 'Je unaye mjakazi?' Nikasema: Hapana sina. Bwana Mtume akasema: 'Je wewe ni mzima na mwenye uwezo (yaani unao uwezo wa mali na unalimudu tendo la ndoa)?

'Nikamjibu: Ndiyo tena namshukuru Mwenyezi Mungu. Bwana, Mtume akasema: 'Ikiwa unayamudu hayo na hujaowa, basi kwa kweli wewe ni miongoni mwa ndugu wa mashetani, au basi utakuwa miongoni mwa mapadri wa Kikristo na kama si hivyo, fanya kama wanavyofanya Waislamu kwani miongoni mwa mila zetu ni kuowa.' Mtume aliendelea kunionya na kusisitiza suala la kuowa mpaka akafikia hatua ya kuniambia: 'Ole wako ewe U'kaafu, owa hakika wewe ni miongoni mwa waovu ( ikiwa hukuowa).' Nikamwambia Bwana Mtume: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu niozeshe kabla sijaondoka hapa." Bwana Mtume akamuozesha Bwana huyo kabla hajaondoka.61

Na katika kulitilia mkazo suala la kuoa na kuhimiza watu waowe, Bwana Mtume (s.a.w.w) anasema: "Hakuna jengo bora lililojengwa katika Uislamu na likawa linapendeza mbele ya Mwenyezi Mungu na likapata utukufu kuliko kuoana."

Na akasema tena: "Kijana yeyote anayeowa katika umri wake wa mwanzo katika ujana, shetani huchukia na kusema: Lo nimepata hasara theluthi mbili za dini yake kijana huyu amezikinga kutokana na uovu wangu." Kisha Mtume akamuusia kijana wa aina hii akasema: Na amuogope Mola wake kijana huyu katika theluthi iliyobaki." 62

Makusudio ya maelezo haya ni kuonesha kwamba kuoa kunahifadhi theluthi mbili ya dini, kwa hiyo mtu anatakiwa awe mchamungu katika theluthi iliyobakia. Na kama hali ni hii, umuhimu wa kuoa katika maisha ya mtu ni jambo ambalo linayo nafasi ya pekee na tukufu, na pia mwanaadamu anatakiwa alipatie nafasi kubwa ya kulitekeleza katika mipango yake.

Tukamilishe mazungumzo juu ya kuowa kwa hadithi ya Mtume (s.a.w).w. inayosema kuwa: "Rakaa mbili anazoswali mtu aliyeowa, ni bora zaidi kuliko rakaa sabini anazoswali mtu asiyeowa."63

Makazi Ya Mwanamke Asiyejisitiri.

Ni yapi makazi ya mwanamke asiyevaa Hijabu wala hajisitiri Kiislamu huko akhera?

Sote tunafahamu kwamba, Mwenyezi Mungu ameweka adhabu kali kwa wale wanaokiuka maamrisho yake na wanaamua kuyaingia mambo ya haramu. Je ni adhabu gani atakayoadhibiwa mwanamke asiyejisitiri kwa vazi la Kiislamu na akaona ni bora kuutembeza mwili wake wazi kinyume na sheria inavyomtaka avae? Jawabu lake ni kama ifuatavyo: Kwa mwanamke asiyejsitiri hujisababishia laana na kujiweka mbali na rehma na radhi za Muumba wake. Pia hujiingiza mwenyewe katika unyonge na adhabu za Mwenyezi Mungu. Bwana Mtume (s.a.w.w) anasema: "Katika zama za mwisho watakuja watu katika umati wangu ambao wanawake zao nusu wamevaa na nusu wako uchi. vichwani watasuka mafundo ya nywele na kuyaacha wazi bila kuyafunika.
Basi sikilizeni (niwaambieni) kuweni wenye kuwalaani wanawake hao kwa kuwa wamekwisha kulaaniwa, wala hawataipata harufu ya pepo na iko mbali nao kwa masafa ya mwendo wa miaka mitano."64 Naye Imam Ali (a.s.) amesema: "Katika zama za mwisho kitapokuwa kiama kimekaribia, watatokea wanawake watakaokuwa wakitembea uchi bila kujisitiri kisheria.

Wanawake wa aina hii watakuwa wametoka katika dini na wataingia katika fitna, watapenda starehe na mambo ya fahari na watahalalisha mambo ya haramu. Wanawake hawa malipo yao ni kuingia motoni, basi angalieni sana kipindi hicho ni kibaya kuliko vyote."

Kuna hadithi nyingine kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w.) inayoelezea adhabu za wanawake wasiojisitiri kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Hadithi hii tunainakili kwa kifupi. Imam Ali (a.s.) anasema: "Mimi na Fatma (a.s.) tuliingia nyumbani kwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu tukamkuta analia sana. Nikamwambia ni kitu gani kinakuliza? Mtume akasema: 'Ewe Ali, usiku niliopelekwa mbinguni niliwaona wanawake katika umati wangu wakiadhibiwa vikali. Nilihuzunishwa na hali yao hiyo na nikalia kutokana na adhabu kali wanayoadhibiwa.' Kisha Bwana Mtume (s.a.w).w akaanza kueleza aliyoyaona katika usiku huo wa Miraji akasema

'Nilimuona mwanamke amefungwa kwa nywele zake kwenye moto na ubongo wake unatokota. Na nikamuona mwanamke mwingine amening'inizwa kwa ulimi wake huku moto ukimiminwa kooni mwake. Pia nikamuona mwanamke anakula nyama ya mwili wake hali yakuwa chini yake panawaka moto mkali, na mwingine amefungwa mikono yake na miguu kwa pamoja, kisha amezungukwa na mojoka mengi na nge wanamuuma. Pia nilimuona mwanamke kiziwi tena kipofu halafu hawezi kusema akiwa ndani ya moto ubongo wake unavuja kupitia puani, mwili umeenea vidonda mithili ya mgonjwa wa ukoma. Na kuna mwanamke mwingine anakatwa nyama za mwili wake kwa mikasi.

Bibi Fatma (a.s.) akasema kumwambia baba yake: 'Baba hebu nifahamishe ni matendo gani waliyoyatenda wanawake hao hapa duniyani?' Mtume (s.a.w.w.) akajibu: 'Ewe Binti yangu, ama yule aliyekuwa amefungwa kwa nywele zake, yeye alikuwa hafuniki kichwa chake mbele ya wanaume wasiomhusu. Na yule aliyening'inizwa kwa ulimi wake alikuwa akimkera na kumuudhi mumewe. Ama aliyekuwa akila nyama ya mwili wake, huyo alikuwa akiupamba mwili wake kwa ajili ya watu wamuone. Na yule mwanamke aliyefungwa mikono na miguu kwa pamoja na akawa anaumwa na majoka na nge, huyu alikuwa mchafu hana udhu nguo zake chafu na alikuwa hakogi janaba wala hedhi na alikuwa akipuuza kuswali. Ama yule kipofu, kiziwi na hawezi kusema alikuwa akizaa watoto wa zinaa ( nje ya ndoa) na kisha humpachikia mumewe na kudai kwamba ni watoto wa mumewe. Na huyu wa mwisho ambaye alikuwa akikatwa nyama za mwili wake kwa mikasi, alikuwa Malaya, akiitoa nafsi yake kwa kila mwanaume.”65 Kwa hiyo imetudhihirikia wazi katika hadithi hii aina mbali mbali za mateso na adhabu alizoziandaa Mwenyezi Mungu kwa wanawake wasiozingatia kanuni ya Hijabu kwa maana zake zote.

Miongoni mwa adhabu hizo ni kufungwa kwa nywele zake nwanamke na kutokota ubongo baada ya kupata adhabu ya moto unaowaka pande zake zote. Kwa hivyo basi, ina maana kila mwanamke atakayeshindwa kusitiri mwili wake na akauacha wazi kwa kila mtu, hapana budi ataadhibiwa kwa adhabu kali inayoumiza, kama zilizotajwa ndani ya hadithi.

Lakini ikiwa mwanamke mwenye sifa hizi zilizotajwa katika hadithi atatubia kwa Mwenyezi Mungu na kuacha kabisa makosa hayo aliyokuwa akiyatenda, kisha akavaa kama sheria ya Kiislamu inavyomtaka avae kwa ukamilifu, bila shaka Mwenyezi Mungu atakubali toba yake na atamsamehe. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:

وَهُوَ الَّذِي يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَعْفُو عَنِ السَّيِّئَاتِ وَيَعْلَمُ مَا تَفْعَلُونَ

"Ni yeye Mwenyezi Mungu ambaye anakubali toba za waja wake (wanapotubia) na anasamehe makosa na anafahamu mnayoyatenda"66

وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِمَنْ تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ

Na anasema tena Mwenyezi Mungu (s.w.t.): "Nami kwa hakika ni mwingi wa kusamehe kwa yule anayetubia na akaamini na kutenda mema kisha akaoongoka67

Hijabu Isiyokamilika: Kuna baadhi ya dada zetu ambao utwaona wamavaa Hijabu, lakini Hijabu yao hiyo siyo kamilifu kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Kina dada hao utawaona wamejistiri sehemu fulani tu ya kichwa, na au sehemu fulani ya mwili na halafu sehemu nyingine za mwili ziko wazi mbele ya kila mtu. Wakati mwingine wanaweza kujisitiri vizuri kichwa chote, lakini utaona mikono au miundi iko wazi au ikawa haikusitiriwa ipasavyo.

Kwa hakika Hijabu kama hi moja kwa moja ni Hijabu isiyokamilika ni Hijabu pungufu isiyoweza kutimiza lengo la Hijabu linalokusudiwa. Wakati huo huo, uvaaji kama huo si uvaaji ulioko juu ya msingi wa kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu.

Hali kama hii ya uvaaji usiokamili iliwahi kutokea katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w), ambapo walikuwako wanawake ambao hujistiri sehemu ya kichwa na kuacha sehemu nyingine bila kuisitiri ikiwa ni pamoja na masikio. Tendo kama hili Mtume (s.a.w.w) alilikemea na akawaamuru wanawake wajisitiri kikamilifu kwa mujibu wa sheria. Kumbuka ndugu msomaji ile hadithi ya Mtume aliposema: "Nusu wamevaa na nusu wako uchi." Hadithi hii inamaanisha kwamba, wanawake watakuwa wanajisitri sehemu ya maungo yao na sehemu nyingine hawajisitiri. Kama hali ndiyo hii tuliyonayo, lengo la Mtume (s.a.w.w) ni kuwafahamisha wanawake wanaovaa hivyo kwamba wasidhani kuwa wamevaa Hijabu, bali inawapasa watambue kwamba uvaaji huo siyo kamili na haukubaliki kisheria.

Neno La Mwisho

Wasomaji wapendwa imetudhihirikia katika yale tuliyoyataja ndani ya kitabu hiki kwamba, Hijabu ni vazi la Kiislamu na siyo fashion,68 na ni kanuni iliyojaa hekima nyingi. Hijabu inalinda heshima ya mwanamke na inaitakasa familia na jamii nzima.

Zaidi ya hapo ni amri ya kidini na hukumu ya sheria za Kiislamu, Mwenyezi Mungu ameithibitisha na kuitaja ndani ya Qur'an Tukufu. Naye Bwana Mtume (s.a.w.w) na watu wa nyumba yake wamesisitiza na kuitilia mkazo sheria hii. Kinyume cha maagizo haya na faida zilizomo ndani ya Hijabu, tayari tumekwishakuona wazi kwamba jamii huwa inaharibika na mwanamke kuangamia na ndipo familia inapotengana.

Zaidi ya hapo kutokuchunga mipaka ya mavazi, hasa Hijabu kwa wanawake ni uasi wa amri ya Mwenyezi Mungu, na maamuzi yake pia ni kinyume na maslahi ya wengi. Kwa hiyo ni wajibu wetu sote kufanya kila linalowezekana ili kuona sheria hii inafanya kazi na kuieneza baina ya wanawake waliomo katika jamii zetu, majumbani, mashuleni, maofisini na kila mahali. Kwa kufanya hivyo, tutapata radhi za Mwenyezi Mungu, pia huu utakuwa ni wema kwa ajili ya nafsi zetu hapa duniani na kesho akhera.

Habari Motomoto

1. AlAzhar Yasema: Wanawake Wa Kiislamu Walioko Ufaransa Wanaweza Kuvua Hijab Kama Wakilazimishwa

Cairo, Desemba 30, 2003 (IslamOnline, net):

Imamu Mkuu wa Al-Azhar Sheikh Mohammad Sayed Tantawi siku ya jumanne, Desemba 30, 2003 alisema kwamba: Wanawake wa kiislamu wanaoishi Ufaransa wanaweza kuvua Hijab zao kama wakilazimishwa kwa shida, alikuwa akirejea kusudio la sheria ya kupiga marufuku Hijab katika shule za serikali.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari na waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy (aliyekuwa anaizuru Misir), Tantawi alisisitiza kwamba Hijab "ni sharti la kiMungu kwa mwanamke wa kiislamu… Hakuna Mwislamu yeyote, awe yeye ni mtawala au mtawaliwa, awezaye kulipinga hilo."

Lakini alihoji kwamba Ufaransa wana haki ya kupiga marufuku Hijab katika shule za serikali, akaongeza kwamba chombo chochote cha kiislamu au nchi ya kiislamu haina haki ya kulipinga hilo, kwa sababu Ufaransa sio nchi ya kiislamu.

"Hijab ni wajibu kama mwanamke anayeishi katika nchi ya kiIslamu. Kama anaishi katika nchi isiyo ya kiislamu, kama Ufaransa, ambayo watawala wake wanataka kufuata sheria inayopinga Hijab, ni haki yao," alisema Imamu mkuu huyu wa AlAzhar, mwachuoni aliyeteuliwa na serikali.

Alisema kwamba iwapo mwanamke wa kiislamu atafuata sheria za nchi isiyo ya kiislamu (kwa kuvua Hijab yake), basi Uislamu humchukulia kama aliyelazimishwa kwa shida.

Sheikh Tantawi alitetea maoni yake hayo kwa kusoma Aya Tukufu, ambayo inasema:
"Mmeharamishwa (kula) nyama mfu na damu na nyama ya nguruwe, na kilichosomewa jina lisilo la Mwenyezi Mungu…Lakini mwenye kusongeka kwa njaa, pasipo kuelekea kwenye dhambi, wala kupituka mipaka basi Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe mwenye kurehemu."

"Nasisitiza na kukazia: Ni haki yao na siwezi kuipinga… sisi, kama nchi ya kiislamu, hatuwezi kumruhusu mtu yeyote kuingilia katika mambo yetu ya ndani," alisema akisherehesha juu ya upigaji marufuku wa Ufaransa ulio na majadala.

"Mimi mwenyewe, katika wadhifa wangu kama Imamu Mkuu wa Al-Azhar, siwaruhusu watu wasio Waislamu kuingilia katika mambo yetu ya ndani, na kwa mantiki hiyo hiyo, siwezi nikaruhusu nafsi yangu kuingilia katika mambo ya ndani ya nchi isiyo ya kiislamu," aliongeza Sheikh Tantawi.

Rais wa Ufaransa Jacques Chirac siku ya jumatano, 17 Desemba, 2003 aliunga mkono kusudio juu ya utungaji mpya wa sheria ya kupiga marufuku uvaaji wa Hijab katika shule za serikali.

Waziri wa sheria wa zamani wa Ufaransa, Bernard Stasi, ambaye aliongoza kamati ya serikali juu ya mazingira ya kilimwengu na dini, alipendekeza mapema katika mwezi huo kuwekwa sheria ya kupiga marufuku Hijab, misalaba mikubwa na vikofia vya kiYahudi.

Hatua hiyo iliyopendekezwa, imepangwa kuwakilishwa mbele ya Bunge la Ufaransa mwezi Februari 2004, na inatarajiwa kuanza kutumika katika mwezi wa Septemba 2004.

{Kwa mujibu wa fatwa za wanachuoni wengi pamoja na Mkuu wa Mamlaka kubwa ya ulimwengu wa Waislamu-Mashi'a, Ayatollah Mkuu Sayyid Seestani (HA): hairuhusiwi kwa msichana wa kiIslamu kuvua Hijab yake Shuleni, na kama akilazimishwa kuvua, basi asihudhurie Shuleni hapo.]69

2. Kujifunika Kichwa Na Uhuru Wa Dini

Nchi kadhaa za Ulaya zinachochea sheria za kupiga marufuku au kuzuia uvaaji wa mitandio ya kichwa kwa wanawake wa kiislamu. Sheria hizo huzua maswali kwenye misingi ya kuvumiliana na usawa katika jamii ambayo hupigania mfumo wa kutambua mawazo, misimamo mbali mbali na uhuru wa dini.

Hivi sasa Ufaransa inafikiria kupiga marufuku uvaaji wa Hijab (shela) mashuleni, wakati ambapo katika nchi ya Ujerumani, majimbo mawili yamependekeza itungwe sheria ambayo itapiga marufuku moja kwa moja uvaaji wa ushungi (Hijab) katika taasisi za elimu.

Makala hii inazungumzia suala la Hijab, adabu ya kufunika kichwa kwa wanawake wa kiislamu, na vile vile na desituri za Wayahudi na Wakristo za uvaaji wa shela na ushungi.

Hijab na shela?

Baadhi ya watu katika nchi za Magharibi (yaani, Ulaya na Amerika) hufikiria adabu ya kufunika kichwa inayofuatwa na wanawake wa kiislamu kama alama kubwa ya ukandamizaji wa wanawake na utumwa. Je, ni kweli kwamba hakuna desturi zinazo fanana katika mila za Mayahudi-Wakristo?

Hebu ngoja tuiweke rikodi hii sawasawa. Kwa mujibu wa Rabbi Dr. Menachem M. Brayer (Profesa wa Biblical Literature, Yeshiva University) katika kitabu chake, 'The Jewish woman in Rabbinic Literature,’ ilikuwa ni desturi ya wanawake wa Kiyahudi kutoka nje wakiwa na shungi (nguo ilyofunika kichwa), ambayo wakati mwingine, hufunika hata uso wote na kuachilia jicho moja tu nje.70

Anawanukuu baadhi ya Marabbi wa zamani wakisema, "Haifanani kwa mabinti wa Israeli kutembea bila kufunika vichwa" na "Laana iwe juu ya mwanaume ambaye anaruhusu nywele za mkewe zionekane…mwanamke ambaye anaonesha nywele zake kwa ajili ya kujirembesha huleta ufukara."sheria za Kiyahudi hukataza usomaji wa dua za kuomba baraka au maombi (yoyote) mbele ya mwanamke aliyeolewa akiwa kichwa wazi, kwa vile kutokufunikwa kwa nywele za mwanamke huchukuliwa kama 'uchi'.71

Dr. Brayer vile vile anataja kwamba ,"wakati wa kipindi cha utawala wa Marabi (wanachuoni wa dini ya Kiyahudi) kushindwa kwa mwanamke wa Kiyahudi kufunika kichwa kulichukuliwa kama tusi kwa heshima yake. Akiwa hakufunika kichwa chake anaweza kupigwa faini ya zuzim mia nne kwa kosa hili." Dr. Brayer vile vile anaelezea kwamba shela ya mwanamke wa Kiyahudi haikuchukuliwa wakati wote kama alama ya adabu. Wakati mwingine, shela huashiria hali ya ubora na anasa kuliko adabu. Shela huupa utu heshima na ubora wa wanawake watukufu. Vile vile huwakilisha kutokuwezekana njia yeyote ya kumuendea mwanamke kama miliki ya mume iliyotakaswa.72

Shela huonesha kujiheshimu kwa mwanamke na hadhi ya kijamii katika jamii. Wanawake wa daraja za chini mara kwa mara huvaa shela ili kutoa picha ya daraja la juu. Ukweli kwamba shela ilikuwa ni alama ya utukufu, ilikuwa ndio sababu ya makahaba kutokuruhusiwa kufunika nywele zao katika jamii ya Kiyahudi ya zamani. Hata hivyo, makahaba mara kwa mara walivaa mitandio maalum ili waonekane wa heshima.73 Wanawake wa Kiyahudi huko Ulaya waliendelea kuvaa shela mpaka karne ya kumi na tisa wakati maisha yao yalipokuwa yameingiliana zaidi na utamaduni wa kisekula ulioyazunguka. Shinikizo la nje la maisha ya Kizungu katika karne ya kumi na tisa liliwalazimisha wengi wao kutoka nje vichwa wazi. Baadhi ya wanawake wa Kiyahudi waliona inafaa zaidi kubadilisha shela yao ya asili kwa kuvaa wigi (nywele za bandia) kama muundo mwingine wa kufunika nywele. Leo, wanawake wachamungu zaidi wa Kiyahudi hawafuniki nywele zao isipokuwa katika Hekalu.74 Baadhi yao, kama vile madhehebu za Hasidic bado wanaendelea kutumia wigi.75

Vipi kuhusu mila ya Ukristo? Inajulikana sana kwamba watawa wa Kanisa Katoliki wamekuwa wakifunika vichwa vyao kwa mamia ya miaka sasa, lakini hiyo sio mwisho. Mt. Paulo katika agano jipya ameandika maelezo ya kuvutia sana kuhusu shela:

Lakini nataka mjue ya kuwa kichwa cha kila mwanaume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanaume, na kichwa cha Kristo ni Mungu. Kila mwanamume asalipo, au anapohutubu, naye amefunika kichwa yuaabisha kichwa chake. Bali kila mwanamke asalipo, au anapohutubu, bila kufunika kichwa, yuaabisha kichwa chake: kwa maana ni sawa sawa na yule asiye nyolewa. Maana mwanamke asipofunikwa na akatwe nywele.

Au ikiwa ni aibu mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa, na afunikwe. Kwa maana kweli haimpasi mwanamume kufunika kichwa, kwa sababu yeye ni mfano wa utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume. Maana mwanamume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanamume. Kwa hiyo imempasa mwanamke awe dalili ya kumilikiwa kichwani, kwa ajili ya malaika. 1Wakorintho 11:3-10

Mantiki ya Paulo ya kuwavisha wanawake shela ni kwamba, shela huwakilisha alama ya utawala wa mwanaume, ambaye ni mfano na utukufu wa Mungu juu ya mwanamke, ambaye ameumbwa kutokana na mwanaume na kwa ajili ya mwanaume. Mt. Tertullian katika tasnifu yake mashuhuri, 'On the veiling virgins' ('Juu ya kuwavisha wanawali shela), anaandika hivi: "Wanawake vijana, mnavaa shela zenu nje mitaani, hivyo ni lazima mzivae mkiwa kanisani, mnazivaa mkiwa pamoja na wageni, basi zivaeni mkiwa pamoja na kaka zenu...

"Miongoni mwa sheria za kanisa Katoliki za sasa, kuna sheria inayowataka wanawake kufunika vichwa vyao wakiwa kanisani.76

Baadhi ya madhehebu ya Kikristo kama vile Amish na Mennonites kwa mfano, wanawavalisha wanawake wao shela hadi sasa. Sababu ya kuvaa shela, kama inayotolewa na viongozi wa Kanisa ni kwamba, "Kufunika kichwa ni alama ya mwanamke kuwajibika kwa mwanaume na Mungu," ambayo ni mantiki ile ile iliyotolewa na Mt. Paulo katika Agano Jipya.77

Kutokana na ushahidi wote huo hapo juu, ni wazi kwamba Uislamu haukubuni ushungi. Hata hivyo, Uislamu umeuthibitisha.

Qur'an inawahimiza wanaume waumini na wanawake waumini kuangusha macho yao chini na kulinda tupu zao, na kisha huhimiza wanawake waumini kuteremsha shungi zao ili kufunika shingo na kifua:

"Waambie waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, hili ni takaso kwao, bila shaka Mwenyezi Mungu anazo habari za yale wanayoyafanya. Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, na wasioneshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au watoto wa kaka zao, au watoto wa dada zao, au wanawake wenzao, au wale waliomilikiwa na mikono yao, au wafuasi wanaume wasio na matamanio (kwa wanawake) au watoto ambao hawajajua siri za wanawake. Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha. Na tubieni nyote kwa Mwenyezi Mungu enyi wenye kuamini ili mpate kufaulu." Qur'an...24:30-31

Qur'an iko wazi kabisa kwamba shela ni muhimu kwa ajili ya adabu, lakini kwa nini adabu ni muhimu? Qur'an bado iko wazi:

Ewe Nabii! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wake wa waumini: Wateremshe juu yao shungi zao. Kufanya hivyo inaelekea zaidi wajulikane na wasiudhiwe, na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu. Qur'an...33:59

Hii ndiyo nukta yote, adabu imeamriwa ili kuwakinga wanawake kutokana na usumbufu au kwa lugha nyepesi, adabu ni kinga. Hivyo, dhumuni pekee la Hijab katika Uslamu ni kinga.

Hijab, tofauti na shela ya mila ya Kikristo,sio alama ya mamlaka ya mwanaume juu ya mwanamke, wala sio alama ya mwanamke kuwajibika kwa mwanaume. Hijab, tofauti na shela iliyoko katika mila ya Kiyahudi, sio alama ya anasa na ubora wa baadhi ya wanawake watukufu walioolewa. Katika Uislamu Hijab ni alama ya adabu ambayo hulinda salama uadilifu binafsi wa mwanamke. Qur'an inasisitiza kwa nguvu sana kuhifadhi heshima ya mwanamke, na kuwahukumu wanaume kuadhibiwa vikali kama kwa uwongo wanashutumu wanawake kwa uchafu:

Na wale wanaowasingizia wanawake waaminifu kisha hawaleti mashahidi wanne, basi wapigeni mijeledi themanini na msiwakubalie ushahidi wao kabisa, na hao ndio mafasiki.
Qur'an 24:4

Baadhi ya watu, hususan katika nchi za magharibi, wamezowea kudhihaki hoja yote ya adabu kwa ajili ya kinga. Hoja yao ni kwamba, kinga bora ni uenezaji wa elimu, tabia za kistaarabu na kujizuia. Tungesema: Vema, lakini haitoshi. Kama ustaarabu ni kinga ya kutosha, basi kwa nini wanawake katika Amerika ya Kaskazini hawathubutu kutembea peke yao katika mitaa yenye giza au hata kukatisha sehemu iliyotupu ya kuegeshea magari? Kama elimu ni ufumbuzi, basi kwa nini vyuo vikuu vyetu vina 'huduma ya kusindikizwa nyumbani' kwa wanafuzi wa kike katika kampasi (eneo la chuo)? Kama kujizuia ni ufumbuzi, basi kwa nini taarifa za unyanyasaji wa kijinsia katika sehemu za kazi huripotiwa kwenye vyombo vya habari kila siku? Mfano wa wale walioshutumiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia, katika miaka michache iliyopita, ni pamoja na: Mabaharia maofisa, Mameneja, Maprofesa wa vyuo vikuu, Maseneta, Mahakimu wa Mahakama Kuu, na Rais wa Amerika! (Clinton).

Ifuatayo ni takwimu iliyochapishwa katika kipeperushi kilichotolewa na mkuu wa kitengo cha wanawake katika Queen's University ya Canada:

Nchini Canada mwanamke anashambuliwa kijinsia kila baada ya dakika 6, mwanamke mmoja katika wanawake watatu nchini Canada atakuwa ameshambuliwa kijinsia wakati fulani katika maisha yake. Mwanamke mmoja katika wanawake wanne wako katika hatari ya kubakwa au kujaribiwa kubakwa katika maisha yake. Mwanamke mmoja mmoja katika wanawake wanane watakuwa wameshambuliwa kijinsia wakati wakuhudhuria vyuo au vyuo vikuu, na utafiti umegundua kwamba wanaume 60% wenye umri wa kwenda chuo kikuu wamesema wangeweza kufanya shambulio la kijinsia kama watakuwa na uhakika kwamba hawatashikwa.

Kukabiliana na ushambuliaji wa wanawake, mabadiliko makali ya msingi katika muundo na utamaduni wa maisha ya jamii ni ya muhimu kabisa. Utamaduni wa adabu ni wenye kuhitajika sana, adabu katika mavazi, katika kuongea, na katika tabia za wote wanaume na wanawake, vinginevyo takwimu za kutisha huelekea kuongezeka , na kwa bahati mbaya mwanamke peke yake ndiye mwenye kulipa gharama hiyo. Kwa hakika, tunateseka, lakini kama alivyosema K. Gibran:"...kwa mtu ambaye anapigwa ngumi sio sawa sawa na yule ambaye anazihesabu."78

Jamii kama ya Kifaransa ambayo inawafukuza wasichana kutoka mashuleni kwa sababu ya mavazi yao ya adabu, mwishowe inajidhuru yenyewe.

Ni moja ya kejeli kubwa ya dunia yetu ya leo kwamba ushungi ule ule uanaoheshimiwa kama alama ya 'utukufu' wakati ukivaliwa na watawa wa Kanisa Katoliki, unakejiliwa na kushutumiwa kama alama ya 'ukandamizaji wa wanawake' wakati ukivaliwa na wanawake wa kiislamu kwa madhumuni ya adabu na kinga.

Wasala Llahu ala Sayyidina wa Nabiyyina Muhammadin wa Alihittaahiriina. Wal hamdulilahi Rabbil-alamin.

Mwandishi: Muhammad Ibrahim Kaadhim Al-Qaz-wini.

Mtarjumi: Msabah Sha'ban Mapinda.
27 Muharram 1412 -9 August, 1991

 • 1. Mustadrak Alhakim juz 3 uk , Al isabah ya Ibn Hajar Al asqalani juz 4 uk.
 • 2. Hapana shaka makusudio yaliyomo ndani ya jawabu la bibi Fatimah (a.s.) ni kwamba, wawili hawa yaani mwanamke na mwanaume ni wale wasiokuwa na uhsiano wa kisheria. Watu wenye uhusiano kisheria ni kama hawa wafuatao: Mama, dada, shangazi na au Baba, kaka, mjomba na wengine ambao wametajwa katika vitabu vinavyohusika na sheria. Ama mume na mke, wawili hawa uhusiano kati yao hauna haja ya kutolewa maelezo. Mtarjumi.
 • 3. Ni vyema ikaeleweka wazi kwamba Bwana Mtume (s.a.w).w alimuuliza Binti yake suali hilo hali ya kuwa yeye mwenyewe anajua wazi kuwa Sahaba yule alikuwa haoni, lakini lengo la Bwana Mtume (s.a.w) kuuliza suali hilo alitaka aone namna Binti yake atakavyo toa jawabu la suali hilo ili historia ipate kusajili mazungumzo haya ya kiimani na ubakie kuwa ni mfano mzuri wa kuigwa siku zote.
 • 4. Mustadrak Al-Wasail Kitabun-Nikah. Biharul-An-Waar juz 104 uk 38.
 • 5. Kalimatur-Rasuli uk 110 cha Sayyid Shirazi.
 • 6. Al-kafi juz uk 152. Miongoni mwa dhana mbaya atakayodhaniwa mwanamke asiyejali sitara ya kisheria ni kuwa, wakati wote huonekana yuko tayari kufanya ufisadi. Kama si hivyo, amtazamaye hushawishika kumtendea uovu. Mtarjumi.
 • 7. Qur'an 42:36
 • 8. Kwa asili mia kubwa wakazi wengi wa visiwa vya Unguja na Pemba, pwani ya Kenya inayojumuisha Mombasa, Lamu n.k, Visiwa vya Ngazija na miji mingi ya Tanganyika (Tanzania bara) kwa kipindi kirefu imekuwa ni miji ya amani na utulivu. Mazingira haya mazuri yalijengeka kutokana na wakazi hao kuwa ni wafuasi wa dini ya kiislamu iliyowajenga katika maadili mema ya kiislamu. Ni ukweli usiyopingika kwamba hapo zamani hapakuwa na matukio ya kuwavunjia heshima wanawake kama tunavyoyashuhudia mambo hayo leo hii ndani ya miji yetu. Misamiati ya kufadhaika na kubaka haikuwako hapo zamani. Utoaji mimba na kutupa watoto ni mambo mageni kwetu hayakuwako. Ujambazi, utapeli na kutokuaminiana ni misamiati mipya. Lakini haya yote ni mipango ya maadui wa dini ya kiislamu, na kwa bahati mbaya Waislamu wamehadaika na mbinu za kikafiri na kujikuta wanapoteza dini yao na hata hiyo dunia waliyopambiwa imewatupa mkono hawana nayo asilani. Msiba uliyoje kwa Umma wa Kiislamu!! Mtarjumi.
 • 9. Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimekumbwa kwa kiasi kikubwa na matatizo ya mmomonyoko wa maadili, na zinatungwa sheria kali kila leo ili labda? itawezekana kurekebisha hali hii, lakini bila mafanikio. Tunachokiona ni ongezeko la maovu ambayo yanatendeka wazi wazi na kila mtu anayashuhudia wakiwemo hao wanaokaa na kutunga sheria hizo kwa matumaini ya kukomesha maovu. Hakuna njia inayoweza kukomesha hali hiyo isipokuwa ni kushikamana na mafunzo bora ya kiislamu. Ni muhimu kwa viongozi wetu wakatambua mambo yanayochangia uharibifu wa mwenendo wa jamii na kuhakikisha kuwa wanaing'oa mizizi yake. Mtarjumi.
 • 10. Kuna baadhi ya watu wanajaribu kulitia dosari vazi la Hijabu kuwa eti ni vazi linalovaliwa ili kuficha maovu ya hao wanovaa. Upo ukweli fulani kuhusu madai haya, lakini upotoshaji huu wa vazi la Hijabu usiwe miongoni mwa sababu za kuwakatisha tamaa wanawake wa kiIslamu wanaovaa Hijabu kwa kumtii Mola wao, kwani ni mara ngapi watu wanautumia usiku kwa mambo maovu wakati Mwenyezi Mungu ameuweka kuwa ni kipindi cha mapumziko baada ya kazi za kutwa nzima? Kwa hiyo matumizi mabaya ya kitu kizuri hayawi ni sababu ya kukifanya kitu hicho kuwa kibaya. Mtarjumi
 • 11. Biharul Anwaar juz 6 uk 130. Kilichokusudiwa hapa bila shaka ni nywele za mwanamke ambaye si maharim wako wala siyo mkeo. Ikiwa nywele tu zinatosha kumuingiza mwanaume ndani ya madhambi, basi ikoje hali ya watu leo hii kwa namna wanawake wa kileo wanavyovaa.? Je! Ni kwa kiasi gani wanatuingiza katika madhambi? Leo hii siyo nywele tu bali vifua vya wanawake vinaonekana kwa kila mtu na maungo mengi yanakashifiwa na kila mtu. Hivi kweli kwa hali kama hii vijana wetu watasalimika na maovu? Pia hao kina dada nao watamlaumu nani watakapovunjiwa heshima? Mtarjumi.
 • 12. Asili ya yote hayo ni mwanamke au wanawake ambao kwa makusudi kabisa wanaamua kuvaa nguo ambazo zitahatarisha usalama wao na usalama wa jamii yote. Kuhatarisha usalama wao na wa jamii peke yake haitoshi, bali waelewe kwamba wanasababisha vijana wetu wa kiume kuchuma madhambi makubwa, na wakati mwingine kuwaharibia maisha yao ya baadaye kwa kufungwa jela kutokana na hatia ya kubaka. Madhara mengine yaletwayo na matukio ya zinaa na liwati ni pamoja na kuambukizwa maradhi hatari kama vile kisonono, kaswende, na leo ukimwi. Maradhi haya hatari yameleta huzuni na misiba inayotisha katika ulimwengu. Mtarjumi.
 • 13. Majallatud-Dastuur Lebanon
 • 14. Jarida la An Nahar la Lebanon tar 28/2/1972.
 • 15. Hapa kwetu Tanzania uko msamiati usemao: "Watoto wa mitaani." Lakini ukifanya uchunguzi utakuta kwamba msamiati huu umeundika kutokana na matatizo ya kuvunjika kwa ndoa bila ya sababu za msingi, pia madhara yatokanayo na? ?kukosekana kwa uaminifu ndani ya ndoa za watu ni sehemu kubwa sana inayozalisha watoto wa mitaani. Pamoja na hali hiyo kuna mambo mengine k.m. umasikini. Kwa hakika kila mtu anapaswa kuwa muaminifu katika ndoa yake si kwa maslahi yake tu bali akiangalie kizazi chake kisije kuishia mitaani na kudhurika kwa mambo mengi yaliyoko huko. Mtarjumi.
 • 16. Gazeti la Al Ahram linalochapishwa mjini Cairo Misri la Tar 26 April 1966 likinukuu kutoka gazeti la Pravda
 • 17. Jarida la An nahar la Lebanon toleo la 1311
 • 18. Sinema za X ni zile sinema ambazo mara nyingi zinajihusisha kuonesha matendo ambayo hayapaswi kuonekana hadharani na khususan huwa ni matendo ambayo hufanywa kwa siri baina ya mke na mume, tena kwa mujibu wa sheria yaani wawe ni mke na mume waliyoowana. Lakini kutokana na wanaadamu kuzama ndani ya maasi dhidi ya Muumba wao na hasa wazungu, matendo haya sasa yamebadilishwa na kuwa mambo yanayofanyika waziwazi, siyo kwenye sinema peke yake bali hata picha za Camera na zinafanywa kuwa ni biashara motomoto. Tuseme nini kwa namna watu wasivyokuwa na aibu sasa hivi, kwani wamekubali kuacha ubinaadamu na kuchagua maumbile ya wanyama wasiyostahi kufanya lolote na popote pale. Mtarjumi.
 • 19. Kitabu Qadhaya Az ziwaj wal Usrah
 • 20. Suratul Maidah Aya No 44, 45 na 47.
 • 21. Hapa kwetu Tanzania Serikali imejaribu mara kadhaa kuwaondoa mitaani wasichana na wanawake wanaofanya umalaya hadharani, lakini bila mafanikio. Kuna wakati sisi tunajiuliza hivi kweli serikali imedhamiria kupiga vita tabia hizi chafu au la? Swali hili linakuja pale tunapoyaona na kuyasikia makongamano mbali mbali ambayo yanahusu kuitahadharisha jamii kutokana na ugonjwa hatari wa ukimwi.

  Hivi ni kweli tutaweza kupambana na janga hili kwa mikutano na semina zisizokwisha wakati mitaa yetu kila inapofika jioni wasichana wetu na wanawake wetu wanatoka barabarani wakisubiri wanaume? Pamoja na hali hiyo, mavazi wanayovaa wanawake na wasichana hao pindi wanapofuatilia mawindo yao, ni mavazi hatari ambayo bila kuuliza ni kichocheo kikubwa kwa wanaume kunasa katika mtego huo.

  Binafsi yangu ninaingiwa na mashaka makubwa juu ya lengo na madhumuni ya semina, mikutano pamoja na mabango yanayoitahadhrisha jamii kuhusu janga la ukimwi. Haiwezekani kabisa kuupiga vita UKIMWI wakati vyanzo vyake viko huru ikiwemo kuwahamasisha Watanzania kuwa wazinifu kwa kuwaambia wavae kondom. Hapana shaka sote tunafahamu kwamba, njia kuu ya maambukizo ya ugonjwa huu ni uzinifu. Hivyo basi, ni wazi kwamba kwa utaratibu huu hatuwezi kushinda vita dhidi ya UKIMWI.

 • 22. Majumba hayo kwa hapa kwetu yanajulikana kwa jina la madanguro. Imani yangu ni kwamba madanguro hayo yanajulikana fika, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa na jamii au vyombo husika kuyaondosha majumba hayo ili kuisalimisha jamii yetu kutokana na tabia hizi za kinyama. Je, huku nako sikuupalilia UKIMWI uzidi kushamiri katika jamii yetu? Iko wapi hapa dhamira ya kupiga vita UKIMWI? Mtarjumi.
 • 23. Al Kafi juz 5 uk 324.
 • 24. Makusudio ya usemi huu ni kwamba: "Mwanamke muovu ni yule ambaye mwili wake hauna hifadhi popote pale, ndani au nje, akiwa na mumewe au hata mbele ya wanaume wengine." Kwa hiyo mwanamke huyo ni sawa na bidhaa iliyoko sokoni au dukani inatafuta na au inangojea wanunuzi waione. Endapo wataipenda watainunua na wasipoipenda wataiacha. Na kawaida ilivyo ni kwamba, bidhaa inapokuwa sokoni au dukani, basi wanunuzi wana uhuru mkubwa katika kuchagua bidhaa wanayoitaka na hapo ndipo mtu huikamata bidhaa hiyo na kuigeuza kila upande ili tu aone kama itamfaa au la. Bwana Mtume ((s.a.w).w.) anamtahadharisha mwanamke asiwe ni kiumbe kinachokamatwa na kila mtu kama bidhaa iliyoko sokoni, ni lazima aulinde uwanamke wake na utu wake. Mtarjum
 • 25. Al Kafi juz 5 uk 552
 • 26. Al Kafi juz 8 uk 138
 • 27. Huu ni mfano mzuri sana kwa hao wanaopinga sheria na muongozo wa Mwenyezi Mungu
 • 28. Biharul Anwar juz 2 uk 4.
 • 29. Al kafi juz 5 uk 337, Biharul Anwar juz 103 uk 371.
 • 30. Nahjul Balaghah
 • 31. Al Kafi juz 5 uk 517.
 • 32. Al Kafi cha Shaikh Al islam Al Kulaini juz 5 uk 535
 • 33. Al Kafi juz 5 uk 537
 • 34. Biharul An war juz 103 uk 249
 • 35. Al mawaidhatu Al adadiyyah uk223.
 • 36. Alkafi juz 5 uk 516.
 • 37. Biharul An waar juz 52 uk 339
 • 38. Biharul An war juz 104 uk 38/ Iqabul-A'maal cha Sheikh Saduq
 • 39. Jambo hili kwa upande wa pili, haipaswi kwa mwanamke kumuangalia mwanaume asiyemuhusu. Na inaposemwa kuwa mke asiyekuhsu makusudio ni wale wanawake ambao kisheria unaweza kuwaoa, au kwa lugha fupi wasiyo Maharimu wako. Ili kuwafahamu zaidi unaweza kurejea Qur'an sura ya nne Aya 23 mpaka 24
 • 40. Qur'an 24 : 30
 • 41. Bila ya shaka kinachokusudiwa hapa Ni kuwa: Ima muangaliaji atakuwa ni mwanaume kamuangalia mwanamke kwa kumkazia macho, au mwanamke kumuangalia mwanaume kwa kumakazia macho. Sote tunafahamu vilivyo matokeo ya hali hii na namna inavyosababisha uharibifu katika jamii. Lakini ni nani yuko tayari kuiepuka tabia hii? Hakuna ila wachache.
 • 42. I'qabul A'maal cha As Saduq
 • 43. Lialaail Akhbar juz 5 uk 195.
 • 44. Kitabu Al Kafi juz 8 Khutbatul Wasilah
 • 45. Kitabu Jamiul Akhbar uk 93. Tabia ya kumuangalia kila mwanamke apitaye au umuonaye kwanza: Ni tabia mbaya mno, na hapana shaka sote tunakubaliana kwamba mtu mwenye tabia hii huwa na majuto kila wakati kwa sababu hutamani kila akionacho na kwa hakika siyo rahisi kukipata kila anachokitamani. Kutokana na kutokuwepo uwezekano wa kupata kila anachokitamani, matokeo yake mtu huyo hubakia kuwa ni mwenye majuto na majonzi yasiyokwisha. Ni kwa nini hasa mtu ajiadhibu kiasi hiki wakati Mwenyezi Mungu ametupatia fursa ya kuoa mke zaidi ya mmoja? Siyo siri kwamba wanawake ni wengi mno kuliko idadi ya wanaume. Kwa hiyo oa badala ya kubakia unajiadhibu hapa duniani kwa majuto yasiyokwisha na kesho akhera unasubiriwa na adhabu kali kutokana na wewe kuyajaza macho yako kwa misumari ya motoni. Mtarjumi
 • 46. Biharul Anwar juz 104 uk 40
 • 47. Lialil Akhbar juz 5 uk 196.
 • 48. Qur'an 28: 26.
 • 49. Lialil Akhbar juz 5 uk 196
 • 50. Al Kafi juz 5 uk 521
 • 51. Maana yake: Mungu ni Mkubwa. Tamko hili licha ya kuwa ni utajo wa Mwenyezi Mungu, pia hutumika kama tamko la kuonesha mshangao au kustushwa na kitu fulani kilichotokea bila kutarajia.
 • 52. Lialil Akhbar juz 5
 • 53. Mustadrak Al wasail juz 2 uk 554
 • 54. Biharul An waar juz 104 uk 42
 • 55. Biharul An waar juz 104 uk 30
 • 56. Safinatul Bihari juz 2
 • 57. Biharul Anwaar juz 104 uk 41
 • 58. Biharul Anwaar juz 103
 • 59. Mustadrak al Wasail Kitabun Nikah
 • 60. Wasailus Shia juz 7 uk 8
 • 61. Mustadrak al Wasail Kitabun Nikah.
 • 62. Mustadrak al Wasail Kitabun Nikah.
 • 63. Wasailus Shia juz 7 uk 6
 • 64. Musnad Ahmad, Hayatul Hayawan cha Ad Dumair.
 • 65. Biharul Anwaar juz 103 uk 245
 • 66. Qur'an 42: 25
 • 67. Qur'an 20:82
 • 68. Fashion/Mtindo: Kwa kawaida mtindo ni kitu ambacho hupita na kuja kingine badala yake, lakini siyo Hijabu, kwani yenyewe ni vazi la mwanamke kisheria na anapaswa kulivaa wakati wote anapokuwa ndani ya mazingira husika kama ilivyokwisha kuelezwa kitabuni. Mtarjumi
 • 69. Msimamo unaopaswa kuoneshwa na Waislamu ndiyo huu. Hatuko tayari kumfurahisha Jacques Chirac wa Ufaransa na wakati huo huo tumchukize Mwenyezi Mungu
 • 70. Menavhem M. Brayer, Mwanamke wa Kiyahudi katika fasihi ya ki-Rabbi: A Psychosocial Perspective (Hoboken, n.J: Ktav Publishing House, 1986) uk. 239
 • 71. Ibid., uk. 316-317. vile vile tazama Swidler, op. cit., uk. 121-123.
 • 72. Ibid., uk. 139
 • 73. Susan W. Schneider, Jewish and Female (New York: Simon & Schuster, 1984) uk.237
 • 74. Ibid., uk. 238-239
 • 75. Alexandra Wright, "Judaism", in Holm and Bowker, op. cit., uk. 128-129
 • 76. Clara M. Henning, "Cannon Law and the Battle of exes" in Rosemary R. Ruether, ed., Religion and Sexism: Images of woman in Jewish and Christian Trraditions (new York: Simon and Schuster, 1974) uk. 272
 • 77. Donald B.Kraybill, The riddle of the Amish Culture (Baltimore: Johns Hopkins University Press, 1989) uk. 56.
 • 78. Khalil Gibran, Thoughts and Meditations (New York: Babtam Books, 1960) uk. 28.