read

Dibaji

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kijitabu hiki ni tarjuma ya kijitabu kiitwacho Al-Hijab Saa'datun laa shiqaaun, kilichoandikwa na Sheikh Muhammad Ibrahim Al-Qazwini mwaka 1979. Ingawaje ni kiasi cha miaka ishirini na minne imepita tangu kilipoandikwa, maelezo na mafunzo yaliyomo yanaafikiana kabisa na hali iliyopo ndani ya jamii yetu leo hii. Mwandishi amejitahidi san kufafanua maana ya Hijabu, ikiwa ni pamoja na kuleta mifano mbali mbali na matukio ya kweli ili kuonesha umuhimu wa Hijabu katika maana inayokusudiwa na sheria ya Kiislamu.

Hoja zilizotumika ni madhubuti na zinakubalika iwapo tu uadilifu utatumika katika maamuzi, bila kujali zimesemwa na Uislamu au kinyume chake. Kijitabu hiki kimekuwa katika lugha ya Kiarabu kwa kipindi kirefu, na baadaye ikapendekezwa kifanyiwe tarjuma ya kiswahili, kwa matarajio ya kuwanufaisha watu wengi wa eneo la mashariki ya Afrika na kwingineko inakozungumzwa lugha ya Kiswahili. Kwa mara ya kwanza tarjuma ya kijtabu hiki ilifanywa mnamo mwaka 1991. Ndugu yetu Bwana Qurban Khaki alikuwa ni mtu wa kwanza kupendekeza tarjuma hiyo. Mwenyezi Mungu amlipe kila la kheri katika kuhudumia Uislamu na Waislamu.

Chapa uliyonayo mkononi sasa hivi ni chapa ya pili ya tarjuma ya kijitabu cha Al Hijab Saadatun laa Shiqaaun, ambacho kimechapishwa na Al Itra Foundation. Kama ile chapa ya kwanza katika kutarjum kijitabu hiki, tulichokizingatia zaidi ni maana aliyoikusudia mwandishi.

Hivyo basi tarjuma hii siyo neno kwa neno ingawaje safari hii mwandishi wa kijitabu hiki amejitahidi kufanya marekebisho ya kukiboresha kwa kuweka mambo mengi ndani ya chapa mpya iliyoko katika lugha ya Kiarabu. Isitoshe sisi wenyewe tumejaribu kufanya ufafanuzi katika maeneo kadhaa ya kijitabu hiki kutokana na umuhimu tuliouona, hasa kwa kuzingatia hali na mazingira tunayoishi hapa kwetu Tanzania na hata kwa majirani zetu wa eneo hili la mashariki ya Afrika.

Kijitabu hiki kimechapishwa mara kumi katika lugha ya Kiarabu kutokana na umuhimu wa maudhui ya Hijabu kwa umma wa Kiislamu na wanaadamu wote kwa jumla. Napenda kuitumia nafasi hii kumshukuru Dr Mohamed Kanju kwa msaada wake mkubwa wa kukipitia kijitabu hiki. Si hivyo tu bali namshukuru tena kwa mchango wake wa kututolea tarjuma za Habari moto moto tulizozinasa kutoka kwenye mtandao wa Inter Net wakati wa kumalizia tarjuma ya kitabu hiki. Habari hizo kwa umuhimu wake tumezitia mwishoni kitabuni humu kwa kuwa ni miongoni mwa njama za wapinzani wa Uislamu na Waislamu katika utekelezaji wa Sheria hii tukufu inayomtaka mwanamke wa kiIslamu avae Hijabu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie tuwe ni wenye kunufaika na miongozo iliyomo kitabuni humu, na tuonyeke kwa kila onyo lililomo.

Was-salaam Alaikum, Msabah S. Mapinda. Mtarjumi.
19/10/03.