read

Somo La Kumi Na Mbili: Sifa Za Imam Ali (A.S.) Na Mwonekano Wake

Urafiki

Laiti kama si mafuriko makubwa ya urafiki wa kweli na huruma iliy- ojaa na kumwagika ndani ya nafsi yake basi Ali (a.s.) asingechagua urafiki penye uadui. Kwa ajili hiyo wanahabari waaminifu kuanzia wafuasi wake hadi adui zake wamepokea kuwa: Pindi Zubayri na Talha walipong’ang’ania kumpiga vita, wakakataa kumtii huku wakimtuhumu katika tukio mashuhuri la vita vya ngamia (Jamal) Ali (a.s.) aliwaendea akiwa hajajiandaa kwa vita, hana ngao wala silaha huku akiwaonyesha amani aliyodhamiria, kisha akanadi:

“Ewe Zubayri! Njoo kwangu”. Zubayri akatoka akiwa amejiandaa kwa vita akiwa na silaha. Aisha alipomsikia Ali (a.s.) akapiga kelele akisema: “Eee vita.”

Alipiga ukulele huo kwa kuwa kwa uchache alikuwa hana shaka kuwa hakuna kipingamizi isipokuwa ni Zubayri kuuawa, kwani anayepambana na Ali (a.s.) bila kizuizi huuawa hata kama atakuwa ni shujaa mkubwa wa namna yoyote ile au akawa na ujuzi wa juu wa kivita wa kiwango chochote kile.

Lililomshangaza sana Aisha na waliomzunguka ni wao kumwona Ali bin Abu Talib (a.s.) akimkumbatia Zubayri kwa muda mrefu, kwa kuwa sababu za mapenzi ya kweli haziishi ndani ya moyo mkubwa kama huu. Imam Ali (a.s.) akaanza kumuuliza Zubayri kwa lugha ya urafiki wao wa zamani akisema:

“Jihurumie ewe Zubayri, hivi ni kitu gani kilichokutoa uje kunipiga vita?” Akajibu: “Damu ya Uthman.” Imam akasema: “Mwenyezi Mungu amuuwe aliyetuchonganisha kwa damu ya Uthman.”

Hapo Imam akaanza kumkumbusha ahadi zao, urafiki wao na siku za undugu wao wa zamani. Na huenda Ali (a.s.) alilia sehemu kama hii, lakini Zubayri aliendelea kumpiga vita Imam Ali (a.s.) mpaka Zubayri alipouawa huku kifo chake kikimkarahisha yule aliyemuuwa mwenye kujali upendo Ali bin Abu Talib (a.s.).1

Huruma Ya Ali (A.S.)

Imam Ali (a.s.) alisema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu laiti nikipewa mbingu saba na vyote vilivyo chini yake eti ili tu nimwasi Mwenyezi Mungu kwa kumnyang’anya mdudu chungu punje ya shairi, sitofanya, na hakika dunia yenu hii ni dhalili kwangu kuliko jani lililomo mdomoni mwa nzige.”2

Ali (a.s.) ndiye mwenye maagizo mazuri aliyoyatuma kwa Al-Ashtar An-Nakhaiy gavana wake wa Misri na watu wake. Ndani ya maagizo hayo amesema: “Usiwe mnyama mkali mwenye kushambulia unayetumia fursa kwa ajili ya kuwala wao. Kwani hakika wao wako katika makundi mawili: Ima ni ndugu yako katika dini au ni kiumbe mwenzako, hivyo wape msamaha wako kama unavyopenda upewe msamaha na Mwenyezi Mungu. Wala usijute kwa msamaha wowote utakaotoa, wala usijivune kwa adhabu yoyote utakayotoa.” Kisha akamwambia: “Jizuie kujilimbikizia.”3

Hakika ukali wa Ali (a.s.) katika kuzuwia kujilimbikizia ulikuwa ni sababu kubwa ambayo ilipelekea kutokea yaliyotokea kati yake na Muawiya na jamaa zake, kwani hakika hawa walitaka ufalme, mali na utajiri kwa ajili ya nafsi zao huku Ali (a.s.) akitaka hayo yote yawe kwa ajili ya raia wote.

Huruma iliwafikia watu wote akawasamehe dhidi ya yale wanayoya- tenda, hivyo watu wa Basra walimpiga vita, wakaupiga kwa mapanga uso wake na nyuso za wanae, wakamtukana na kumlaani, lakini alipowashinda hakuwauwa na akawa kawaingiza katika amani yake. Na aliusia kutendewa wema yule mwovu muuaji wa nafsi yake Ibnu Muljim.

Uadilifu Wa Ali (A.S.)

Si ajabu Ali (a.s.) kuwa mwadilifu kuliko watu wote bali ajabu ni kama hatokuwa hivyo. Kati ya mambo yanayoelezea uadilifu wake ni kuwa alikuta ngao yake kwa mkiristo mmoja wa kawaida, hivyo akampeleka kwa Kadhi ambaye jina lake ni Sharihu ili aweze kumhukumu na kumtolea maamuzi, hivyo waliposimama wote waw- ili mbele ya Kadhi, Imam Ali (a.s.) alisema: “Hakika ni ngao yangu sijaiuza wala sijaitoa zawadi.”

Hapo Kadhi akamuuliza yule mkiristo: “Unasemaje kuhusu aliyoyasema kiongozi wa waumini?” Akajibu: “Hakuna ngao isipokuwa ni ngao yangu, na kiongozi wa waumini kwangu si mwongo”. Hapa Kadhi Sharihu akamuelekea Ali (a.s.) na kumuuliza: “Je una mashahidi watakaothibitisha kuwa hii ni ngao yako?” Ali (a.s.) akatabasamu na kusema: “Sharihu umepatia, sina mashahidi.”

Hivyo Sharihu akahukumu kuwa ngao ni ya yule mkiristo na hapo akaichukua yule mkiristo na kuondoka huku kiongozi wa waumini akimtazama.

Isipokuwa baada ya hatua chache yule mkiristo akarudi huku akise- ma: “Hakika mimi nakiri kuwa haya ni maadili ya manabii, yaani kiongozi wa waumini ananipeleka kwa Kadhi ili ahukumiwe yeye!” Kisha akasema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu hakika ngao hii ni ngao yako ewe kiongozi wa waumini, na mimi nilisema uongo katika madai yangu.”

Baada ya muda watu walimwona mtu huyu akiwa pembeni mwa Imam Ali (a.s.) akiwa ni askari wake mwaminifu na komandoo wake mkubwa akipambana vikali katika vita vya Nahruwani dhidi ya waasi (Khawariji).4

Usia wa Imam Ali (a.s.) na barua zake kwa magavana wake, zote zinakaribia kulenga lengo moja nalo ni uadilifu, hivyo watu wote wa mbali na karibu hawakumkubali isipokuwa ni kwa sababu alikuwa ni kipimo cha uadilifu, kipimo ambacho hakikuelemea kwa mtu wa karibu wala hakikumpendelea mtawala, hakikuhukumu isipokuwa haki tupu.

Ama Uthman bin Affan ambaye alitawala dola kabla yake hakika aliachia huru mikono ya ndugu zake wa karibu, wasaidizi wake na swahiba zake wafanye watakavyo katika kila sekta ya vyeo na mali huku akiongozwa na mawazo mabaya ya siri, na hasa Mar’wan ndiye aliyemuathiri sana katika mawazo. Hivyo ilipofika dola mikononi mwa Imam Ali (a.s.) hakutaka chochote isipokuwa ni kuwafanyia uadilifu, akawavua utawala baadhi yao akawaondoa kwenye vyeo na kuwatenga dhidi ya ujilimbikiziaji wa mali huku akipambana na kila aliyetaka kugeuza dini kwa lengo la kujimiminia mali, vyeo na mamlaka nyumbani kwake kwa kuitoa dini kwenye msitari wake.

Mara kwa mara alikariri kauli yake nzuri masikioni mwa watu hawa akisema: “Mimi ninajua litakalowafaa na kunyoosha mapindo yenu, lakini haifai niwatengenezee hali zenu kwa kuiharibu
nafsi yangu.”5

Ukarimu Wa Imam Ali (A.S.)

Imam Ali (a.s.) alikuwa mkarimu sana na mwenye mkono mkunjufu kuliko watu wote, kwani alikuwa akifunga na inapofika wakati wa kuftari anachukua chakula chake na kumpa mtu huku akibaki na njaa, hivyo Aya hizi zikamshukia yeye na familia yake: “Na huwalisha chakula masikini na yatima na mfungwa hali ya kuwa wanakipenda.* Tunakulisheni kwa ajili ya radhi ya Mwenyezi Mungu tu, hatutaki kwenu malipo wala shukurani.”6

Wafasiri wamepokea kuwa alikuwa hamiliki isipokuwa dirhamu nne, hivyo akatoa sadaka dirhamu moja usiku na nyingine mchana, na dirhamu nyingine kwa siri na ya nne kwa dhahiri hapo ikateremshwa Aya: “Wale watoao mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhahiri, basi wana malipo yao kwa Mola wao, wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.”7

Imepokewa kuwa alikuwa akimwagilia maji mitende ya mayahudi huko Madina mpaka mkono wake unatoa uvimbe lakini apatapo malipo huyatoa sadaka huku akibakia na njaa akifunga jiwe juu ya tumbo lake.

Ukweli Na Nia Njema Ya Imam Ali (A.S.)

Alifikia kiwango cha juu cha nia njema, kiasi kwamba kutokana na nia hiyo njema akapoteza utawala wa dola, na laiti kama katika hali fulani angebadili nia yake njema basi asingepata adui, wala rafiki zake wasingegeuka adui dhidi yake.

Kuna kipindi maswahaba wakubwa muhajirina walijikusanya kwake kwa lengo la kutaka kumkinaisha kwa kumpa njia ya kumwondoa Muawiya, amuundie jambo la ghafla litakalommaliza, lakini aliwakatalia wote akijiepusha dhidi ya njama hiyo.

Baada ya Imam Ali (a.s.) kupewa kiapo cha utii cha kuongoza dola alikuja Al-Mughira bin Shu’bah ambaye alijulikana kwa ujanja, njama na mitego, akamwambia Ali (a.s.):

“Hakika wewe una haki ya kutiiwa na kunasihiwa, na mawazo ya leo huzaa yatakayokuja kesho, na upotovu wa leo hupoteza yaliyotakiwa kesho, hivyo mwache Ibnu Amir katika kazi yake, na Muawiya katika kazi yake na watumishi wengine katika kazi zao ili watakapokutii na askari wao wakakupa kiapo cha utii basi ndipo ubadili utakayembadili na umwache unayemtaka.” Imam akanyamaza kwa muda kisha akatangaza kuikataa njama hiyo akisema:

“Sidanganyi katika dini yangu wala sifanyi la udhalili katika jambo langu.”8

Pindi njama na ujanja wa Muawiya ulipodhihiri Imam alitoa ibara ifuatayo ambayo inafaa kuwa mfano bora wa maadili mema ya hali ya juu, alisema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hakika Muawiya si mjanja kuliko mimi, lakini yeye anadanganya na kutenda maovu, hivyo laiti kama si kuchukia udanganyifu basi mimi ningekuwa mjanja kuliko wote.”9

Amehimiza kukazania nia njema katika hali yoyote ile akasema: “Alama ya imani ni kutanguliza ukweli japo unakudhuru, na kuuacha uwongo japo unakunufaisha.”10

Kujiamini Kwa Imam Ali (A.S.)

Sifa zote hizi nzuri ziliungana na sifa nyingine ya kupendeza ya kuji- amini, ambayo Imam alifahamika kwayo. Bali kujiamini ni kitu kinachoshikamana na sifa hizi, hivyo Imam anatenda huku akiwa na matumaini na uzuri wa matendo yake, huku akidhihirisha haki wazi wazi, kiasi kwamba hata shujaa wa Bara la Uarabu Amru bin Abdul Wuddi hakumzuia kudhihirisha haki huku Mtume (s.a.w.w.) na maswahaba wakimtahadharisha dhidi ya Amru. Hiyo ni dalili inayoonyesha kujiamini kwake na ushujaa wake mbele ya haki, vitu ambavyo vilijaa ndani ya nafsi yake.

Mara nyingi amekuwa akitoka kuelekea kwenye swala bila ya kusindikizwa na mtu atakayezuia hatari za maadui mpaka Ibnu Muljimu alipomkuta na kumpiga kwa upanga wenye sumu. Je, huu si ushahidi juu ya kujiamini kwake mbele ya haki, kujiamini ambako kunaendesha viungo vyake vyote na mwenendo wake wote.

Kutokana na kujiamini huku kuzuri ndio maana anamwambia swahaba wake na gavana wake huko Madina Sahlu bin Hunayfa Al-Answariy kuwa: “Ama baada, zimenifikia habari kuwa watu kati ya wale waliokuwa kabla yako wanakwenda kwa Muawiya kwa siri, hivyo usihuzunike kwa idadi yao itakayokupita wala kwa mchango wao utakaokutoka, kwani naapa kwa Mwenyezi Mungu wao hawa- jakimbia toka kwenye ujeuri wala hawajajiunga na uadilifu.”11

Muhtasari

Huruma ya kutekeleza ahadi ni huruma ya kina kwa Imam Ali (a.s.), huruma ambayo ilikuwa imejenga moyo wake huku ikidhihirika katika matendo na mienendo yake, hiyo ni hata mbele ya adui yake.
Akitarajia kuwaongoza waliopotea na kuwarudisha katika njia sahihi wale waliokengeuka.

Ama kuhusu uadilifu ni kuwa laiti kama ungejitokeza kwa mtu basi angekuwa ni Ali bin Abu Talib (a.s.) na wala si mwingine, kwani alikuwa ni nguvu kali ya kutekeleza uadilifu kwa watu wote. Alikuwa ni mjuzi anayemjua mwanadamu, jamii na kanuni za Mwenyezi Mungu, hivyo kidole chake hakikuacha haki na uadilifu kwa maana yote ya uadilifu na vipengele vyake vyote katika maisha.

Kila kitu katika utu wa Imam Ali (a.s.) kimekamilika na chenye muundo mmoja, kwani hatupati tofauti yoyote katika sifa zake na mwonekano halisi wa utu wake, hivyo akastahiki kuwa alama kati ya alama za utukufu wa Mwenyezi Mungu na mfano bora kwa wanadamu wote katika kumtii Mwenyezi Mungu, na kujenga imani ya Mwenyezi Mungu, kifikira, kimwenendo na kihuruma, hivyo yeye ni mfano mwema wa mtawala shupavu na mtawaliwa mwaminifu mtiifu, na yeye ni sura halisi ya nia njema, utiifu, ibada na nguvu ya haki.

Imam Ali (a.s.) alikuwa mkarimu sana kuliko watu wote huku akiwa na mkono mkunjufu. Alikuwa na ukarimu wa hali ya juu huku akijitofautisha kwa kuwa na moyo salama usiokuwa na chuki hata kwa maadui zake, hivyo hakuridhia jambo mbadala lichukue nafasi ya ukweli, kikauli au kivitendo.

Sifa zote hizi ziliungana na sifa ya kujiamini mbele ya haki kwa kiwango cha juu.

Mwana wa Abu Talib alijitofautisha na wengine kwa jihadi iliyoende lea katika vipindi vyote vya maisha yake yote huku akiwa na maadili bora na mtazamo wa ndani wa makini uliyonyooka, akiwa na ubainifu safi na utambuzi wa haraka na nguvu za kupambana, hivyo akawa ni kiongozi bora na mfano wa juu baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) katika kila sifa bora.

Maswali

1. Toa taswira halisi ya urafiki wa Imam Ali (a.s.)?
2. Toa maneno matatu yanayothibitisha na kutoa sura halisi ya huru- ma ya Imam Ali (a.s.)?
3. Ni mahusiano yapi yaliyopo kati ya uadilifu na Imam Ali (a.s.)?
4. Japokuwa Imam Ali (a.s.) alikuwa hana kitu lakini kwa nini alikuwa mkarimu kuliko watu wote?
5. Ni uhusiano upi uliyopo kati ya ukweli wa Imam Ali (a.s.) na ukun- jufu wa nia yake?
6. Toa taswira mbili zinazoonyesha jinsi Imam Ali (a.s.) alivyojiamini kwa kiwango cha hali ya juu?

 • 1. Murujud-Dhahab, Juz. 2, Uk. 370. Qadatuna, Juz. 2 Uk 176.
 • 2. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 224.
 • 3. Nahjul-Balaghah, barua ya 53.
 • 4. Tarikhul-Khulafai, Uk. 184. Al-Kamil fi Tarikh, Juz. 3 Uk. 401.
 • 5. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 69,
 • 6. Al-Insan: 8-9.
 • 7. Al-Baqarah: 274.
 • 8. Murujud-Dhahab, Juz. 2 Uk. 364-365.
 • 9. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 200.
 • 10. Nahjul-Balaghah, hekima ya 458.
 • 11. Nahjul-Balaghah, barua ya 70.