read

Somo La Kumi Na Moja: Sifa Za Imam Ali (A.S.) Na Mwonekano Wake

Kuifuata Haki

Shakhsia ya Imam Ali (a.s.) ilikuwa na alama dhahiri ambayo ndio makusanyikio ya sifa zake zote na mazalisho ya ukamilifu wake wote, nayo ni kuifuata haki vyovyote itakavyokuwa na popote itakapokuwepo. Kufuata kwake haki kulipatikana tangu kipindi cha mwanzo cha uhai wake kwa kutii amri za Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.) bila mipaka.

Pia kujitokeza kwake daima katika kupambana kwa ajili ya malengo ya utume na uongozi uliotakasika, kumfuata nabii kiongozi kwa ukamilifu na kujijenga kiukamilifu kwa ajili ya amri zote za uongozi huu uliyonyooka.

Hivyo kwa ajili hii akastahiki kuwa khalifa wa Mtume (s.a.w.w.), naibu mtekelezaji, na mwaminifu mwenye moyo mkunjufu katika kutimiza malengo ya Mtume (s.a.w.w.) na makusudio ya utume, kwani sifa zote nzuri za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) zilipatikana vizuri kwa Imam Ali (a.s.).

Ibada Yake

Imam Ali (a.s.) amesema: “Hakika kuna watu wanamwabudu Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kutamani, hakika hiyo ni ibada ya wafanya biashara. Na hakika kuna watu wanamwabudu Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuogopa, hakika hiyo ni ibada ya mtumwa. Na kuna watu wanamwabudu Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kumshukuru, hakika hiyo ni ibada ya watu huru.”1

Ibnu Abul-Hadid Al-Muutaziliy amesifia ibada ya Imam Ali (a.s.) kwa kusema: “Alikuwa ni mfanya ibada sana, mwenye kuswali na kufunga kuliko watu wote. Watu wamejifunza Swala za usiku, kushikamana na nyuradi na swala za Sunna kutoka kwake.

Unasemaje kuhusu mtu ambaye kutokana na kuhifadhi uradi wake amefikia kutandikiwa busati la ngozi usiku katikati ya vita siku ya usiku wa Hariri, akavuta uradi wake huku mishale ikidondoka mikononi mwake na mingine ikipita juu ya masikio yake kulia na kushoto lakini hatetemeshwi na hayo, wala hasimami mpaka amalize jukumu lake. Unasemaje kuhusu mtu ambaye kutokana na kurefusha sijida yake bapa lake la uso lilikuwa na sugu kama sugu za ngamia.?”

Ukifuatilia dua zake na minong’ono yake ukaelewa yaliyomo ndani, kuanzia jinsi anavyomtukuza Mwenyezi Mungu na kumtakasa, mpaka anavyonyenyekea kwa ajili ya haiba na utukufu wa Mwenyezi Mungu huku akimfuata kwa unyenyekevu, utajua ni jinsi gani alivyozungukwa na ikhlasi na utafahamu ni ndani ya moyo upi zimetoka dua hizo na ni kupitia ulimi gani imepatikana minong’ono hiyo.

Utawa Wake

Harun bin Antranti amepokea kutoka kwa baba yake kuwa alisema: “Niliingia kwa Imam Ali (a.s.) huko Al-Khawranaqi, yalikuwa majira ya masika nikamkuta kajifunika kitambaa chakavu. Nikamuuliza: Ewe kiongozi wa waumini, hakika Mwenyezi Mungu amekuwekea wewe na familia yako fungu katika mali hii, kisha wewe unajifanyia hivyo? Akajibu: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu, sikupata chochote toka kwenu, wala sina chochote isipokuwa kipande hiki cha kitambaa ambacho nilikuwa nacho toka Madina.”2

Imam Ali (a.s.) alisikika akisema juu ya mimbari: “Ni nani atakayenunua upanga wangu huu? Laiti ningekuwa na thamani ya kununulia shuka basi nisingeuuza.” Hapo akasimama mtu na kusema: “Nakupa thamani ya shuka hivi sasa.”3

Mmoja wao akamletea Ali (a.s.) chakula kitamu kizuri lakini Ali (a.s.) hakukila, akakitazama na kusema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu ewe chakula una harufu nzuri, rangi ya kupendeza na ladha nzuri, lakini sipendi kuizoweza nafsi yangu mambo ambayo haijayazowea.”4

Mashuhuri ni kuwa Ali (a.s.) hakupandanisha tofali juu ya tofali wala nguzo juu ya nguzo. Alikataa kuishi ndani ya kasri la utawala ambalo lilikuwa limeandaliwa kwa ajili yake huko mji wa Kufa. Ibnu Abul- Hadid ameelezea utawa wa Imam Ali (a.s.) akasema: “Katu hakushiba chakula, na alikuwa mgumu wa kula na kuvaa, alikuwa akisema: “Msiyafanye matumbo yenu kuwa makaburi ya wanyama.”5

Msamaha Na Upole Wake

Ibnu Abul-Hadid amesema: “Ama kuhusu upole na msamaha, alikuwa mpole sana anapokosewa na msamehevu sana dhidi ya mwenye kosa. Lilidhihirika hilo siku ya vita vya ngamia (Jamal), kwani alimshinda Mar’wan bin Al-Hakam ambaye alikuwa ndiye adui yake mkubwa na mwenye chuki sana dhidi ya Ali lakini Ali alisamehe.6

Watu wa Basra walimpiga vita wakaupiga uso wake na nyuso za wanawe kwa mapanga huku wakimkashifu, lakini alipowashinda hakuwauwa, bali akanadi msemaji wake katikati ya vikosi vya jeshi lake: “Sikilizeni, anayekimbia hafuatwi, aliye majeruhi hashambuliwi, aliyetekwa hauwawi, na yeyote atakayetupa silaha chini basi amesalimika. Pia atakayejiunga na askari wa Imam naye kasalimika”. Hakuchukua mizigo yao wala hakuteka watoto wao, wala hakuchukua chochote katika mali yao huku laiti angetaka kufanya hivyo angefanya lakini yeye aliacha kufanya hivyo ili atoe msamaha.

Pindi jeshi la Muawiya lilipomiliki na kuzingira pande zote za mto Furati, viongozi wa Sham waliamrisha jeshi kwa kusema: “Wauweni kwa kiu kama walivyomuuwa Uthman bin Affan kwa kiu.” Hapo Ali (a.s.) na maswahaba zake waliliomba jeshi liwaachie wanywe maji. Askari wakajibu: “Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu hapana, hatuwezi kuwapa hata tone moja la maji mpaka mfe kwa kiu kama alivyokufa mwana wa Affan.”

Imam Ali (a.s.) alipoona hakuna njia isipokuwa kifo aliwaongoza maswahaba zake na kuwashambulia askari wa Muawiya mashambulizi mazito mpaka akawaondoa toka kwenye vituo vyao, hivyo baada ya mauaji mazito ambayo yalidondosha vichwa na mikono mingi, Imam Ali (a.s.) alimiliki maji dhidi yao, na hapo askari wa Muawiya wakawa jangwani hawana maji.
Maswahaba na wafuasi wake wakamwambia: “Ewe kiongozi wa waumini wanyime maji kama walivyokunyima, wala usiwanyweshe hata tone moja, waue kwa upanga wa kiu na uwashike kwa mikono wala hauna haja ya kuendelea na vita.” Akajibu: “Hapana, naapa kwa Mwenyezi Mungu siwalipi mfano wa kitendo chao, waachieni baadha ya sehemu za kunywea maji, kwani ukali wa upanga unatosha.”

Hakika kitendo hiki ukikilinganisha na upole na usamehevu ni uzuri wa hali ya juu, na ukikilinganisha na dini na uchamungu basi hakuna budi mfano wa hili lifanywe na mtu kama yeye (a.s.).”7

Ushujaa Na Ushupavu Wa Imam (A.S.)

Ibnu Abul-Hadid amezungumzia ushujaa wa Imam Ali (a.s.) akasema: “Hakika yeye aliwasahulisha watu kumbukumbu ya ushujaa wa wale waliyokuwa kabla yake. Msimamo wake vitani ni mashuhuri, hutolewa mfano mpaka siku ya Kiyama. Yeye ni shujaa ambaye katu hakukimbia wala hakutetereka dhidi ya maadui Wala hakuna aliyechomoza kupambana naye isipokuwa alimuuwa. Katu hakupiga pigo la kwanza kisha akahitajia la pili. Imepokewa ndani ya hadithi kuwa: Mapigo yake yalikuwa ni moja.8

Pindi Ali (a.s.) alipomwomba Muawiya achomoze kwenye mpam- bano ili watu wapumzike na vita kwa kuuawa mmoja wao, Amru alimwambia Muawiya: “Hakika kakufanyia uadilifu.” Hapo Muawiya akasema: “Hujawahi kunidanganya tangu uanze kuninasihi isipokuwa leo, yaani unaniamrisha niende kupambana na Abul Hasan ilihali wewe unajua fika kuwa ni shujaa asiyezuilika, naona unatamani utawala wa Sham baada yangu.”9

Waarabu walikuwa wakijifaharisha wasimamapo kupambana naye vitani, hivyo dada wa Amru bin Abdul Waddi alipokuwa akimlilia kaka yake alisema: “Laiti aliyemuuwa Amru angekuwa si huyu aliye- muuwa, basi ningelia milele maadamu bado nipo duniani. Lakini aliyemuuwa ni mtu asiyekuwa na mfano, na baba yake alikuwa akimwita: ‘Wa pekee asiye na mfano.”10

Ibnu Qutayba amesema: “Katu hakupambana na mtu isipokuwa alimshinda,11 na yeye ndiye aliyeng’oa mlango wa Khaybari kisha likakusanyika kundi la watu ili waweze kuugeuza mlango huo hawakuweza kuugeuza. Na yeye ndiye aliyeng’oa sanamu la Hubal toka juu ya Al-Kaaba, sanamu ambalo lilikuwa kubwa sana lakini akaling’oa na kulitupa aridhini. Na yeye ndiye aliyeng’oa jabali kubwa kwa mkono wake zama za utawala wake yakatoka maji chini yake, hiyo ilikuwa ni baada ya jeshi zima kushindwa kung’oa jabali hilo.”12

Kujizuwia Dhidi Ya Dhulma Na Ujeuri

Imam Ali (a.s.) pamoja na nguvu zake zote zisizo na mfano na ushu- jaa wake wa pekee lakini alikuwa akijizuia kutokufanya dhulma na ujeuri vyovyote vile itakavyokuwa. Wanahistoria wote wamesema kuwa Ali (a.s.) alikuwa haanzi vita isipokuwa pale atakaposhambuli- wa. Alikuwa akiharakisha kusawazisha mambo kati yake na adui kupitia njia za amani ambazo zitazuwia umwagaji damu, hali hii ni hata kama mtu ataharakisha kumfanyia uadui. Hivyo mara nyingi alikuwa akikariri masikioni mwa mwanae Hasan kuwa: “Msiombe kupambana.”13

Kwa kuwa kauli ya Imam haitoki isipokuwa kutoka kwenye madini safi basi mara zote alikuwa akitekeleza huu usia wake, hivyo alijizuwia kupigana isipokuwa pale alipolazimishwa. Kwa ajili hiyo pindi majeshi ya waasi (Khawariji) yalipoanza kujiandaa ili kumpiga na akatokea mtu mmoja kumnasihi Imam kuwa aanze kuwashambulia kabla hawajamshambulia, Imam alimjibu kwa kusema: “Siwapigi mpaka watakaponipiga.”14

Muhtasari

Pindi tunaposoma kurasa za utu wa Imam Ali (a.s.) hakika tunakuwa tumeashiria kiasi tu kidogo kinachofikiriwa na akili zetu katika kufa- hamu nafasi ya Imam huyu maasumu. Kwani akili imeshindwa kujua utukufu wa mwanadamu huyu, hivyo baadhi zikavuka mipaka na kujikuta zimemshirikisha Mwenyezi Mungu, na nyingine zikapun- guza hivyo zikamchukia na kujikuta zimeritadi.

Imam Ali (a.s.) alikuwa mchamungu sana wala hakuna yeyote aliyemshinda kwa ibada, lakini yeye aliweka mfano bora wa uhusiano wa mja na muumba wake hivyo akatekeleza ibada kwa kiwango bora zaidi. Akatekeleza ibada ndani ya mwenendo wake wa kila siku, na mfumo wake wa malezi ambao unamjenga mwanadamu mchamungu na kumtengenezea ustaarabu wa kipekee wa kiislamu.

Imam Ali (a.s.) aliishi huku akiwa kajitenga mbali na ladha zote za dunia hii ya mpito, hilo ni kwa sababu aliijua vizuri dunia na akajua vizuri namna ya kujitenga nayo, hivyo akazidiriki neema za Mwenyezi Mungu ambazo hazilingani na neema nyingine yoyote ile.

Imam Ali (a.s.) alimtendea kila adui yake kwa heshima na adabu, kwa akili na imani, akitarajia kutengeneza umma na kuondoa uharibifu, huku akitaka kuamsha dhamira zilizo ndani ya nafsi zenye maradhi, hivyo akasamehe na kuwa mpole huku akijisahaulisha mabaya aliyotendewa, akasahau kulipiza kisasi japokuwa kulipiza huko ni haki yake.

Historia haijamfahamu mtu shujaa mwenye kuitetea imani ya Mwenyezi Mungu kama Imam Ali (a.s.). Hakika alikuwa jasiri shujaa mwenye yakini asiyetetereka, shupavu asiyelainika, mwenye moyo usiojua khofu, hivyo akaupa ulimwengu wote sura dhahiri ya ukomandoo na ushujaa katika medani za kivita na katika kutekeleza jukumu gumu.

Kajizuia kufanya uadui ilikuwa ni msingi kati ya misingi ya mfumo wa Imam Ali (a.s.) katika maisha yake.

Maswali

1. Ni sifa zipi muhimu zilizompamba Imam Ali (a.s.)?
2. Elezea jinsi utu wa Imam Ali (a.s.) ulivyopatikana kutokana na kuishi kwake na Mtume (s.a.w.w.)?
Na ni athari zipi zilizopatikana katika mahusiano hayo?
3. Elezea jinsi zilivyokuwa ibada kwa Imam Ali (a.s.)?
4. Kwa nini Imam Ali (a.s.) alikuwa akijiepusha na dunia japokuwa ana haki ya kuitumia?
5. Ni kitu gani kilichomtofautisha Imam Ali (a.s.) na wengine wenye kujitenga na dunia?
6. Toa mifano halisi miwili inayoonyesha msamaha na upole wa Iman Ali (a.s) ?

 • 1. Nahjul-Balaghah, semi fupi 237.
 • 2. Hilyatul-Awliyai, Uk. 82. Al-Kamil fi Tarikh, Juz. 2, Uk. 442.
 • 3. Al-Manaqib cha Al-Khawarazmi, Uk. 69. Kashful-Ghummah, Juz. 1, Uk. 232.
 • 4. Tadhkiratul-Khuwas, Uk. 115.
 • 5. Shar’hu Nahjul-Balaghah, Juz.1 Uk. 26.
 • 6. Shar’hu Nahjul-Balaghah, Juz.1, Uk. 22.
 • 7. Shar’hu Nahjul-Balaghah, Juz.1, Uk. 23.
 • 8. Shar’hu Nahjul-Balaghah, Juz.1 Uk. 20, uhakiki wa Muhammad Abul Fadhli Ibrahim.
 • 9. Shar’hu Nahjul-Balaghah, Juz.1 Uk. 20, uhakiki wa Muhammad Abul Fadhli Ibrahim.
 • 10. Ni miongoni mwa beti ambazo kazitaja mwandishi wa kamusi Lisanul- Arab, Juz. 8, Uk 395.
 • 11. Al-Maarif, Uk. 210.
 • 12. Shar’hu Nahjul-Balaghah, Juz.1, Uk. 21.
 • 13. Nahjul-Balaghah, hekima ya 233.
 • 14. Tazama kitabu Abqariyatul-Imam Ali cha Abbas Mahmud Al-Aqqad, Uk. 18.